Sunday, October 30, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA KUMI)


Kwenye somo letu lililo pita “Sehemu ya Tisa” tulijifunza kwanini Wakristo wanaabudu Jumapili, siku ya kwanza ya juma. Sasa tutajifunza kama kushika siku ya sabato kunaambatana na Torati yote ya Musa.
Maandiko matakatifu yanasema katika Yohana 1:17 “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”
Ndugu msomaji na watoto wa Mungu, ni jambo la msingi sana kufahamu kwamba, tunapotaja neno torati, tunamaanisha Amri kumi, sheria 613 na hukumu zake.

TORATI = AMRI KUMI + SHERIA 613 + HUKUMU ZAKE
Ningependa ufahamu kuwa katika nyakati za agano la kale “first dispensation”, ilikuwa, huwezi kuwa mkamilifu kwa kushika amri kumi tu bila kushika na sheria nyingine 613 na kuzitendea kazi hukumu zake. Mtu asiyetendea kazi yote yaliyoandikwa katika torati, alikuwa amelaaniwa;

UTHIBITISHO:

Galatia 3:10 tunasoma, “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika YOTE yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.”
Kumbe Mungu aliwaagiza wana wa Israeli washike torati yote na sio kushikilia siku moja to ya Jumamosi kama ambavyo Wasabato wa leo wanavyo fanya;

UTHIBITISHO:

Walawi 20:22 tunasoma, “Basi zishikeni amri zangu ZOTE, na hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi kuiketi isiwatapike.”

UTHIBITISHO:

Pia Kitabu cha Kutoka 35:10 Biblia inasema, “Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya haya YOTE ambayo Bwana ameagiza.”

Sasa basi, Wasabato wao wanang’ang’ania sheria ya kushika sabato na makatazo ya baadhi ya vyakula katika nyakati hizi za Agano jipya, Watu hawa ni wazi kabisa, hawapo kwenye fungamano la Agano Jipya, maana tumeona bayana kwamba, sheria hii, Bwana hakuipitisha, kwa kuwa ilikuwa ni ishara, iliyokuwa ikimuashiria Yeye kama (sabato) pumziko la kweli la kiroho (Wakolosai 2:16-17).
Hivyo kushika sabato ni kukataa sheria ya Kristo na kuikubali sheria ya Musa. Na sharti la sheria ya Musa (torati) ni kwamba, ni lazima mtu ashike Amri kumi zote, sheria nyingine 613 na hukumu zake.
Mfano; sheria ya kushika sabato ilikuwa na hukumu yake, pale ambapo mtu, alionekana kutoitimiza, yaani alipaswa kuuawa;

UTHIBTISHO:

Kutoka 31:14 tunasoma, “Basi mtaishika hiyo sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa, kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.”

UTHIBITISHO:Kitabu cha Kutoka 35:2 Biblia inasema, “Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo ATAUAWA.”

Kama Mungu alitoa agizo la kushika sabato, na pia akatoa agizo kuwa atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe; Je ni wasabato wangapi leo tunawaona wanafanya kazi Jumamosi, kama kuna usahihi wowote mbona hatuoni wakiitekeleza hukumu ya kuuana? maana ni agizo la Mungu mwenyewe.
Yakobo 2:10 inasema mtu akiishika sheria yote, akajikwaa katika neno moja tu, amekosa juu ya yote.

NDIO MAANA YESU ALIIVUNJA SABATO:    Wapendwa! hii ndiyo sababu iliyompelekea Bwana Yesu kuivunja sabato, baadhi ya sheria na hukumu zote; kwa kuwa ilikuwa ni huduma ya mauti (2 Wakorintho 3:7).

KWANINI WASABATO HAMSHIKI SHERIA 613 NA HUKUMU ZAKE?    Mtu anayeshika sheria ya sabato katika nyakati hizi za agano jipya, anapaswa kushika na amri tisa zote, pamoja na sheria 613 na hukumu zake, ambazo zote zimefafanuliwa kwenye vitabu vya Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la torati. Lakini kama Wayahudi walishindwa, sisi tutaweza wapi? Watoto wa Mungu, tusikubali kujitwisha mizigo ambayo Bwana wetu alikwisha itua, kwa nini tuendelee kukaa kwenye makosa yaliyofanyika katika agano la kwanza; 

UTHIBITISHO:Waebrania 9:15 tunasoma, “Kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya,ili, mauti ikiisha kufanyika, KWA KUKOMBOA MAKOSA YALIYOKUWA CHINI YA AGANO LA KWANZA, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.” Kazi ya torati (ikiwemo sheria ya sabato) ilikuwa ni kama kiongozi cha kutuleta kwa Bwana Yesu kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha Wagalatia 3:24-26 tunasoma, “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatumo tena chini ya kiongozi (torati-ikiwemo sabato).” Sabato ni kama kiongozi cha kutuleta kwa Kristo maana Yeye ndiye sabato mwenyewe (pumziko), sasa kwa vile Kristo amekuja, sasa hatupasWi kuing’ang’anisa sabato.


MADHARA YA KUSHIKA SHERIA YA SABATO:

1. Kushika sabato kuna mfanya mtu asiwe mwana funzi wa Yesu, bali mwanafunzi wa Musa, kwa kuwa torati ilikuja kwa mkono wa Musa na neema na kweli vilitolewa kwa mkono wa Yesu (Yohana 1:17).
2. Kushika siku ya sabato ni mafundisho manyonge na yenye upungufu, hivyo kumfanya mtu awe mwana wa Jehanamu mara mbili (Mathayo 23:15). Kitabu cha Wagalatia 4:9-10 Biblia inasema, “Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? MNASHIKA SIKU, na miezi, na nyakati, na miaka.”

3. Kushika sabato, kunamfanya mtu kuwa chini ya laana. Na hii ni kwa sababu sabato ni sheria iliyo katika torati; na tunaposema torati, tunamaanisha amri kumi, sheria 613 na hukumu zake. Na ilikwisha kuandikwa kuwa mtu asiyeshika torati yote ni amelaaniwa; Galatia 3:10 tunasoma, “Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika YOTE yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.” Kristo ndiye aliyetukomboa kutoka katika laana ya torati (Wagalatia 3:13), na ndiyo maana ukimwamini Bwana YESU, ni lazima ufuate sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2), na siyo sheria ya Musa. Kushika sabato (pumziko) siyo sheria ya Kristo, na Bwana Yesu na Baba yake waliipinga kama tunavyoweza kusoma katika Yohana 5:16-18, “Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwuudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato. AKAWAJIBU, BABA YANGU ANATENDA KAZI HATA SASA, NAMI NINATENDA KAZI. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa HAKUIVUNJA SABATO TU, bali pamoja na hayo, alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu.” Swali ni hili, huyu Yesu liyeshika sabato na kuwafundisha watu leo washike sabato ni Yesu yupi?
4. Kushika sabato kuna mfanya mtu awe mwilini; na mtu anayeufuata mwili ni ngumu sana kumpendeza Mungu (Warumi 8:8), kwa kuwa hatoweza kushinda dhambi. Na ndiyo maana utaona mtu anashika sabato, lakini bado haogopi kwenda kwa waganga wa kienyeji, haoni ni makosa kubishana, haoni dhambi kufanya uasherati na uzinzi. Kwake kuinadi sabato ndiyo injili, kuliko kumnadi Bwana Yesu.
5. Kushika sabato kunatengeneza ngome ya kifarisayo ndani ya mtu; na madhara ya ngome hii ni kwamba, hata kama mtu akisikia ukweli kutoka kwa Mungu mwenyewe, bado mtu huyo hawezi kuusikia wala kuufuata ukweli huo. Ufahamu wa mtu unafungwa hata nuru ya wokovu isimzukie (2 Wakorintho 4:4), hivyo moja kwa moja mtu anakuwa amekata tiketi ya kwenda Jehanam ya moto.
6. Kushika sabato kunamfanya mtu awe mnafiki. Mtu mnafiki huwa na kawaida ya kutangaza sheria na kuitilia mkazo, lakini yeye mwenyewe haitendei kazi. Luka 13:15 Biblia inasema, “Lakini Bwana akamjibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha?” Na ukweli ni kwamba hakuna mnafiki atakayeurithi ufalme wa Mungu.

Sasa baada ya kusoma na kuyafahamu madhara ya kushika Sabato, je, utaendelea kushika hiyo sabato na upatwe na madhara, au utajisalimisha kwa Yesu na kuwa huru?

Tumefika mwisho wa Sehemu ya KUMI, na sasa tutaenda SEHEMU YA KUMI NA MOJA
KUKOMESHWA KWA SABATO, JE, MUNGU ALIKOMESHA SABATO?

********** USIKOSE SEHEMU YA KUMI NA MOJA ***********
Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.



No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW