Wednesday, January 26, 2022

KWANINI WAKRISTO TUNAABUDU JUMAPILI NA HATUISHIKI SIKU YA SABATO?

 


SEHEMU YA TATU


SOMO:-KWANINI WAKRISTO

TUNAABUDU JUMAPILI


NA


HATUISHIKI SIKU YA SABATO?


[ Sehemu ya Tatu ]


〰〰〰〰〰〰〰〰〰〰


Ili iwe vyepesi kwetu kulielewa vizuri somo hili. Tutajifunza somo hili kwa kuligawa katika vipengele saba. Ambavyo ni:-


1⃣ ```MAANA YA NENO SABATO```


2⃣``` KWANINI WAKRISTO HATUISHIKI SIKU YA SABATO?```


3⃣ ```SABATO KIVULI CHA YESU KRISTO```


4⃣ ```AGIZO LA MUNGU KI-BIBLIA LA KUABUDU SIKU YA JUMAPILI.```


5⃣ ```SABABU ZA MSINGI KWA WAKRISTO KUABUDU JUMAPILI.```


6⃣ ```NI SIKU IPI HALALI YA KUABUDU?```


7⃣ ```KUSHIKA SIKU SIO TIKETI YA KWENDA MBINGUNI.```




Mstari muhimu wa kukumbuka


WAKOLOSAI 2:14,16-17:-"AKIISHA KUIFUTA ILE HATI ILIYOANDIKWA ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; AKAIONDOA ISIWEPO TENA, AKAIGONGOMEA MSALABANI. Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au KWA SABABU YA sikukuu au mwandamo wa mwezi, AU SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.


➖➖➖➖➖➖➖➖➖➖


HII NI SEHEMU YA TATU katika mfufulizo wa uchambuzi wa somo hili.


Katika sehemu ya pili tuliishia kujifunza kipengele cha pili. Hatuna muda kurudia yale tuliyokwisha kujifunza tayari. Kama hukuipata sehemu ya pili iliyotangulia itafute kwa bidii uisome. Leo tunapiga hatua kutokea pale tulipoishia.


2⃣ KIPENGELE CHA PILI


```KWANINI WAKRISTO HATUISHIKI SIKU YA SABATO?```.



Tuliishia kuona sababu ya pili inayotufanya wakristo tuishike siku ya sabato. Leo tunaendelea na sababu ya tatu:


```(3) MWANADAMU HAKUUMBWA ILI HAISHIKE SIKU YA SABATO```.


Hili ni la muhimu sana kulielewa juu ya ulazima wa kutokuishika siku ya sabato. Maana kuna watu wengine wameng'ang'ana kama kupe na siku ya sabato kanakwamba basi tusipoishika hiyi sabato hatuwezi kwenda mbinguni. Jambo ambalo siyo sahihi kabisa! Katika mafundisho ya Yesu kuhusu sabato, anatuonyesha kwamba ```HAKUNA ULAZIMA WOWOTE WA KUISHIKA SIKU YA SABATO```. Tunasoma juu ya hilo katika MARKO 2:23-28:-"Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato?......Akawaambia, SABATO ILIFANYIKA KWA AJILI YA MWANADAMU, SI MWANADAMU KWA AJILI YA SABATO. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.".


Ukisoma habari ya mistari hiyo yote kuanzia Mst wa 23-28. Utaona Wanafunzi wa Yesu walifanya jambo ambalo lilikuwa ni kuivunja sabato. Na mafarisayo walipomshitakia Yesu. Kimsingi Yesu hakukanusha kosa la wanafunzi wake la kuivunja siku ya sabato badala yake alijenga hoja za kuwatetea wanafunzi wake kwa kosa lao la kuivunja sabato hawana hatia. Kwa maana nyingine tungesema ```YESU ALITETEA NA KUHALALISHA SUALA LA KUVUNJWA KWA SABATO kwamba wanaofanya hivyo hawana hatia``` [ MATHAYO 12:1-8].


Na hoja kubwa aliyoisimamia Yesu kutufundisha ni kwamba sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu lakini mwanadamu hakuumbwa ili aje aishike sabato. Na kama mwanadamu hakuumbwa ili aishike sabato basi sio ajabu, kosa wala lazima kwake kutokuishika hiyo sabato. Na wanapaswa kuelewa kwamba Yesu mwenyewe ndiye Bwana wa sabato, maana yake Yeye ndiye aliyeifanya hiyo sabato kuwako, Yeye ni mkuu kuliko hiyo sabato. Na kama Bwana amesema wanaoivunja hiyo sabato hawana hatia! Basi Neno lake ndilo la mwisho la kufuatwa. Maana yeye aliyeitunga sheria anao uhalali pia wa kuibatilisha hiyo sheria. Ndicho akichomainisha Yesu hapo.


```MWANADAMU HAKUFANYWA/HAKUUMBWA ILI AISHIKE SABATO```. Kwa mfano ndiomaana tunaona baba yetu Adamu na Hawa hawakuambiwa kuishika sabato, nabii Henoko, Nuhu, Lutu, ibrahimu, Isaka na Yakobo, Yusufu na wengineo waliofuata. Hatuoni mahali popote walipoamuriwa na Mungu kuishika siku ya sabato. Lakini sheria/amri/agizo hili la kuishika siku ya sabato lilikuja kipindi tu cha torati au sheria ya Musa na sio kabla ya hapo [NEHEMIA 9:13-14]. Na wana wa Israeli walipewa sheria hiyo ya kuishika sabato kwa sababu maalumu kuu mbili. Ambazo ni:-


```(1) WALIKUWA WATUMWA KATIKA NCHI YA MISRI```.


Biblia inasema katika KUMBUKIMBU 5:14-15:-".........Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.".


Sababu ya kuamriwa kuishika sabato ilikuwa ni hiyo kwamba wanapopumzika siku ya sabato iwe ni alama ya kwao ya kukumbuka kwamba wao walikuwa watumwa katika mateso nchini misri. Na hivyo Mungu aliwaokoa. Hivyo Kupumzika siku ya sabato ilikuwa ni alama ya kukumbuka ukombozi wao wa kutolewa kwenye mateso nchini misri.


Adamu, Henoko, Nuhu, Lutu, Ibrahimu, Isaka na Yakobo n.k. hawakupewa amri ya kuishika siku ya sabato kwa sababu wao hawakuwahi kuwa watumwa katika nchi ya Misri. Na kwa mantiki hiyo hata sisi wakristo hatuna haja ya kuendelea kuishika sabato kwa sababu sisi hatukuwa watumwa Misri. Na kwa maana hiyo bado tupoishika sabato hatuna hatia.


```(2) ALIWAPA SABATO ILI ZIWE ISHARA KATI YAO ISRAELI NA MUNGU````


Hii ni sababu nyingine ya pili kwanini Israeli wao waliamuriwa kuishika siku ya sabato ILI IPATE KUWA ISHARA.

Biblia inasema katika EZEKIELI 20:10-12,20:-" Basi nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawaleta jangwani. Nikawapa amri zangu, na kuwaonyesha hukumu zangu, ambazo mwanadamu ataishi kwazo, kama akizitenda. Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye. Zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu."


Neno "ISHARA" maana yake inakuwa ni dalili au alama inayotoa maana fulani ya kitu/jambo.


Sabato kama Ishara kati ya Mungu na taifa la Israeli. Maana yake nini? Ni ```"Dalili au alama ya kukumbuka yenye uthibitisho wa Mungu kati yao ya kwamba Yeye ndiye aliyewatoa na kuwaokoa katika nchi ya Misri"```. Ili kwamba wanapopumzika na kuzishika sabato, basi iwe uthibitisho wa kukumbuka kwamba BWANA Mungu wao ndiye aliyewatoa katika nchi ya Misri, ili awe Mungu wao na wao wamtumikie yeye. Kwa kusudi la kwamba wasije wakashawika wakamuacha Mungu wao na kwenda kuitumikia miungu mingine wasiyoijua. Kwahiyo Mungu akawapa Ishara ya Sabato ili kuwakumbusha akijithibitisha kwao kuwa mimi ndimi Mungu wenu! Anasema katika

KUTOKA 29:45-46:-"Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao. Nao watanijua kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi BWANA Mungu wao.".

[ Pia soma KUTOKA 32:4; YOSHUA 24:1-25].


Swali. Sasa sisi wakristo wa makanisa ya leo tunapoishika sabato. Inakuwa na ishara gani kwetu ya kutukumbusha nini? Maana sisi hatukutolewa utumwani misri kwa jinsi ya mwili.

Suala kushika sabato ni desturi zao wayahudi ambazo hazituhusu wakristo wa mataifa kuzifuata [WAGALATIA 2:14].


```(4) YESU MWENYEWE HAKUTUPA KIELELEZO CHA KUISHIKA SIKU YA SABATO```.


Biblia inasema tumtazame Yesu na tena imetupasa kuenenda vile vile kama Yesu alivyoenenda [WAEBRANIA 12:2; 1YOHANA 2:6]. Na kwa maana hiyo hatunabudi kujifunza kwa Yesu alifanya nini kuhusu siku ya sabato. Je, Yesu aliishika sabato? Jibu ni hapana kwa herufi kubwa. Yesu kamwe hakuwahi kuishika sabato hata kidogo bali ```YESU KRISTO MWENYEWE ALIKUWA NI MVUNJAJI WA SABATO NAMBA 1```. Na nitalionyesha hili kwa kulithibitisha na kulifafanua kimaandiko. Utanielewa tu.


Kwanza ilitabiriwa katika unabii kwamba siku zinakuja ambapo MUNGU ATAZIKOMESHA SABATO ZOTE. Biblia inasema katika ```HOSEA 2:11:-"Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa."```

Unabii huo ulimzungumzia Yesu kristo mwenyewe ambaye alikuja kuutimiza kwa kuikomesha na kuiondoa sabato kabisa [ LUKA 24:44-45]. Na Yesu kristo mwenye aliivunja na kuikomesha sabato. Kwa mambo yafuatayo:-


```(i) Yesu alifanya kazi siku ya sabato ```.


Kisheria haikuruhusiwa kabisa kufanya KAZI YOYOTE Ile siku ya sabato. Haijalishi kwamba ni kazi njema au mbaya. Hakuna kufanya kazi yoyote siku ya sabato Ilikuwa ni kosa [ KUMBUKUMBU 5:12-14].

Lakini Yesu aliivunja sabato kinyume cha sheria kwa kisingizio cha kuifanya kazi njema akiwashutumu na wao mafarisayo waliomnyoshea vidole kwa wao pia kufanya lisilokuwa halali siku ya sabato. [ MATHAYO 12:9-14; LUKA 13:10-16]. Biblia inaendelea kueleza juu ya ukweli huo katika ```YOHANA 5:16-18:-"Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato. Akawajibu, Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, KWA KUWA HAKUIVUNJA SABATO TU, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu."```


Ni kweli Yesu alimuita Mungu Baba yake akijifanya kuwa sawa na Mungu na pia aliivunja sabato. Na hivyo ndiomaana walimuua msalabani kwa mtazamo wao. Ingawa kwa upande wa pili hawamkujua vizuri Yesu ni nani!


▪Na katika YOHANA 7:19-24. Utaona hapo kwamba Yesu anajenga hoja ya kujitetea kwake kwa kuivunja sabato. KAMA kwa kuwaelezea hivi:-"Wasimuhukumu yeye tu kwa kuivunja kwake sabato, kwa kuwa mbona na wao wanaivunja sabato kwa kumtahiri mtu siku ya sabato. Iweje wamuhukumu yeye ndiye mkosaji tu?"


AGIZO LA SHERIA ilikuwa ni kosa kumtahiri mtu siku ya sabato ilipaswa kuwa baada ya sabato [ WALAWI 12:1-3; LUKA 2:21].


```(ii) Yesu alikuwa kichocheo cha kusababisha watu wengine kuivunja Sabato```.


Kwa mfano:- Yesu aliijua vizuri sheria inasema nini. Lakini kwa makusudi kabisa baada ya kumponya mtu, Yesu alimwambia simama, JITWIKE GODORO LAKO UENDE. Jambo ambalo lilikuwa ni kosa kisheria kujitwika mzigo wowote siku ya sabato [ YEREMIA 17:19-24]. Lakini Yesu kwa makusudi akamwambia afanye lisilokuwa halali siku ya sabato. Kwa mantiki hiyo tunapata tafsiri ya kwamba kumbe Yesu mwenyewe alikuwa ni kichocheo cha kusababisha watu wengine waivunje sabato.


```(iii) Yesu aliwatetea watu waliyoivunja sabato kuwa walikuwa hawana hatia ````.


Ukisoma katika MATHAYO 12:1-8. Utaona wanafunzi wake Yesu waliingia mashambani siku ya sabato na kuanza kuvunja masuke. Jambo halikuwa halali kutendeka siku ya sabato kama Mungu alivyowaagiza katika sheria kuhusu sabato [ KUTOKA 23:10-13; KUTOKA 34:21]. Lakini kinyume chake Yesu alijenga hoja za kuwatetea hao walioivunja sabato hawakuwa na hatia.


Na ndiomaana mafarisayo waliyobobea katika Torati madai yao ya kumshutumu Yesu kuwa hakuishika sabato yalikuwa ni sahihi. YOHANA 9:16:-"Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato......."


Ni kweli Yesu kama tulivyofafanua hakuishika sabato ingawa kwa tendo hilo la kutokuishika kwake sabato walimdhania vibaya kwamba hakutoka kwa Mungu. Hawamkujua Yesu vizuri ni nani!


Watu wanaodai kwamba Yesu alikuwa akiishika sabato kwa kutumia andiko la LUKA 4:16. Ni wapotoshaji wa kweli. Andiko hilo halionyeshi chochote kwamba Yesu kwa kuingia kwake tu siku ya sabato alikuwa akiishika sabato. ```Swali la msingi ni kwamba Yesu aliingia siku ya sabato kufanya nini ilikuwa ni kuabudu?``` Jibu ni la! Yesu aliingia katika masinagogi yao siku ya sabato ```ILI KUWAFUNDISHA\KUWAHUBIRIA NENO ILI KUWATOA HUKO na ndiyo ilikuwa kusudio lake lake\target yake kubwa``` [ LUKA 4:16, 44; YOHANA 18:19-20; 8:12-24]. Na utaona wale waliokubali kumwamini na kumfuata Yesu waliitwa WANAFUNZI WA YESU na wale waliomkataa Yesu na kuendelea kushika sabato katika torati ya Musa, waliitwa WANAFUNZI WA MUSA. Biblia inasema katika

YOHANA 9:22,27-29:- " Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi (la washika sabato). Akawajibu, Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake? Basi wakamshutumu, wakasema, WEWE U MWANAFUNZI WAKE YULE; SISI TU WANAFUNZI WA MUSA. Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako."


Kwahiyo hapo kukatokea makundi mawili ya wanafunzi wa Yesu na wanafunzi wa Musa ambao ndio washika sabato. Kumbe ukiendelea kuishika sabato hujawa katika kundi la wanafunzi wa Yesu bali la wanafunzi wa Musa. Maana YESU KAMWE HAKUWAHI KUWA NA SIFA\VIGEZO VYA KUISHIKA SABATO. Huo ndio ukweli. Ndiomaana hata mafarisayo walimtenga na kuwa kinyume naye na wanafunzi wake.


Bwana Yesu kuingia kwake tu katika sinagogi lao siku ya sabato hicho sio kigezo cha kumainisha kwamba Yeye alikuwa ni mshika sabato. La hasha! Ni kwa mfano: Si kila mtu anayeingia kituo cha Polisi basi naye atakuwa ni Polisi. Au si kila mtu anayeingia hospitali basi na yeye atakuwa ni mgonjwa au ni dokta! Au si kila anayeingia ikulu na yeye ni Rais!

Au ingekuwepo nafas hata ya sisi kwenda kuhubiri injili ya Yesu ndani ya misikiti, hamainishi kwamba na sisi kuingia kwetu misikitini basi tutakuwa ni waislamu. Au hata hao wanaojiita wasabato wakitupa nafasi jumamosi ya kwenda kwao kuwahubiria neno, haimanishi kwamba kwa kuingia kwetu jumamosi kuwahubiria neno la Mungu, na sisi ni washika sabato! La hasha.

Tumeambiwa tukahubiri injili kila mahali na kwa kila kiumbe na kila aaminiye na kubatizwa ataokoka [ MARKO 16:15-16]. Kwahiyo Yesu naye ilikuwa desturi yake kuingia katika sinagogi lao siku ya sabato ILI KUWAHUBIRIA NENO WAOKOKE, ingawa hawa wasabato walimkataa Yesu na kumtoa nje, akawaacha akaondoka zake. Ukisoma katika ```LUKA 4:16-30, 44```. Utaona hayo niliyokueleza.



```(5) KATIKA MAFUNDISHO YA YESU/AGANO JIPYA HAKUNA MAHALI POPOTE TULIPOFUNDISHWA KUISHIKA SABATO.```


Mafundisho ya Yesu ni zaidi yale tu aliyoyasema Yesu mwenyewe, lakini linajumuishwa Agano lote jipya kwa ujumla wake kuwa ni mafundisho ya Yesu Kristo mwenyewe waliyoyanena mitume kwa kuongozwa na Roho wa Kristo [ WAGALATIA 1:11-12; 2PETRO 1:20-21].


Sasa katika mafundisho ya Yesu ndani ya Agano jipya. Hata pale alipotufundisha kuhusu AMRI KUMI, hakutufundisha au kutuelekeza kuishika sabato, bali tumefundishwa AMRI 9 KASORO AMRI YA 4 YA KUISHIKA SABATO. Hiyo imeondolewa na kufutwa katika Agano jipya. Lakini amri nyingine 9 zimeendelezwa kusisitizwa kwenye Agano jipya. Hebu tuone amri zote kumi zilizotajwa katika ```KUTOKA 20:1-17```. Ambazo ni:-


```(1)Usiwe na miungu mingine ila mimi```


➖Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [ MARKO 12:28-32; WAEFESO 4:6; MATHAYO 4:8-10].


```(2)Usijifanyie sanamu ya kuchonga kwa kuvishujudia wala kuvitumikia```


➖ Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [ MATHAYO 4:10; MATENDO 17:29; WARUMI 1:21-23,25; 1 WAKORINTHO 8:4-6; 1 WAKORINTHO 10:14; 1YOHANA 5:21; UFUNUO 21:8].


```(3)Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako```


➖ Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [YOHANA 17:6; 2TIMOTHEO 2:19; MATHAYO 5:33-37; YAKOBO 5:12].


```(4)Ikumbuke siku ya sabato uitakase```


❌ Amri hii imeondolewa na kufutwa katika Agano jipya. Haipo [ WAGALATIA 4:9-11; WAKOLOSAI 2:14, 16-17].


```(5) Waheshimu baba yako na mama yako```.


➖ Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [ MATHAYO 19:16-19; WAEFESO 6:1-3].


```(6) Usiue```


➖Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [ MATHAYO 5:21-26; MATHAYO 19:16-19; 1YOHANA 3:15].


```(7) Usizini```


➖Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [ MATHAYO 5:27-32; LUKA 16:17-18; MATHAYO 19:16-19; WAEBRANIA 13:4; UFUNUO 21:8].


```(8) Usiibe```


➖Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [MATHAYO 19:16-18; WARUMI 2:21; WAEFESO 4:28].


```(9) Usiseme uongo/ kumshuhudia jirani yako uongo```


➖ Amri hii katika Agano jipya umepitishwa [ MATHAYO 19:16-18; WAKOLOSAI 3:9; WAEFESO 4:25; 2TIMOTHEO 3:3; UFUNUO 21:8,27].


```(10)Usitamani nyumba ya jirani yako, mke wake na chochote alichonacho```


➖ Amri hii katika Agano jipya imepitishwa [ WAEFESO 5:3; WAKOLOSAI 3:5-6; 1WAKORINTHO 6:9-11; WARUMI 13:8-10].


La kumalizia hapa la kufahamu. Yesu aliposema katika "YOHANA 14:15:-" Mkinipenda, mtazishika amri zangu". Mstari huu hupotoshwa sana na kanisa la wasabato. Ni muhimu kuelewa kuna makundi mawili . Kuna ```(i) AMRI ZA MUSA alizopewa na Mungu``` [ YOSHUA 22:5; NEHEMIA 9:13-14]. Na

```(ii) AMRI ZA YESU alizotupa sisi```. Biblia inasema katika YOHANA 13:34:-" Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo".


Anasema hapo ```"AMRI MPYA Nawapa"```. Kwanini ametumia neno mpya? Ni mpya kwa sababu ni tofauti na zile za Musa. Kwa maana Yeye anatupa za kwake!

Katika amri za Yesu mpya alizotupa hakuna kuishika sabato. Amri tuliyopewa kuishika hapa ni UPENDO. Na zile amri zote nyingine zinajumuishwa tu katika neno hilo moja upendo [ WARUMI 13:8-10; 1YOHANA 3:23-24; 2YOHANA 1:4-6]. Na kwa maaana zaidi AMRI ZA YESU ni maneno yake yote alitotuagiza na kutufundisha au kutuamuru kuyatenda [ YOHANA 14:21,23-24]. Kubatiza, kuhubiri Injili, kutoa, kukesha katika kuomba n. k. Hizo ni amri za Yesu. Na kwa sababu Yesu hakutuagiza kuishika sabato. Hivyo basi kuishika sabato siyo amri ya Yesu katika Agano jipya.


Kwahiyo katika Agano jipya la Bwana wetu Yesu kristo tumeachiwa Amri 9 tulizoelekezwa kuzishika na sio siku ya sabato. Hiyo imefutwa, imeondolewa na kugongomewa pale msalabani. Huo ndio ukweli wa neno la Mungu linavyotufundisha.


Mpaka hapa tumeona juu ya uchambuzi wa sababu kuu tano ki-biblia zinazotufanya wakristo wote duniani kutokuishika siku ya sabato. Hivyo basi baada ya kuifahamu kweli, tangu sasa mtu asikutaabishe kuhusu sabato. Kaa kwenye kweli ya imani hii! Mafundisho na vitabu vyote vya vinavyotetea kuhusu sabato, puuzilia mbali.


Itaendeleaa sehemu ya nne.........!




Ukipenda kuwasiliana nami kwa ushauri , maombezi na mafundisho zaidi ya masomo ya neno la Mungu. Karibu :-


Mtumishi wa Mungu aliye hai.


MWL, REV:-ODRICK BRYSON


SIMU:- 0759 386 988; 0717 591 466


Email:- Odrick16@gmail.com.


Whatsapp group.


"KWELI YOTE YA NENO LA MUNGU ISIYOGOSHIWA"


[ 2 WAKORINTO 2:17 ]

Tar [240819] Rev:-Odrick Bryson.


No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW