Friday, October 22, 2021

MJADALA BAINA IMAAM AL-ALBAANIY NA MSHEREHEKEAJI MAULIDI


Imaam Al-Albaaniy:
Je, kusherehekea Maulidi ya Nabiy ni khayr au shari?

Anayejadiliana na Imaam:
Ni khayr.

Imaam Al-Albaaniy:
Sawa. Lakini je, kwani khayr hii Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa hawaijui?

Anayejadiliana na Imaam:
Hapana!

Imaam Al-Albaaniy:
Sijaridhika na jibu lako hilo la “hapana,” bali unawajibika kuendelea kusema: “Haiwezekani kwamba ‘khayr’ hii (ya kusherehekea Maulidi), ikiwa ni khayr au vinginevyo, kuwa ifichike na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na hali sisi hatuujui Uislamu na Iymaan isipokuwa kutoka kwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Basi vipi tuijue sisi hiyo ‘khayr’ ambayo yeye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuijua! Haliwezekani hili!

Anayejadiliana na Imaam:
Kusimamisha Maulidi ni kuhuisha kumbukumbu zake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuheshimu.

Imaam Al-Albaaniy:
Falsafa hii tunaijua sisi, tunaisikia kutoka kwa watu wengi na tumeisoma katika vitabu vyao. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipowalingania watu, je, aliwalingania katika Uislamu wote au aliwalingania katika Tawhiyd? (kumpwekesha Allaah).

Anayejadiliana na Imaam:
At-Tawhiyd.

Imaam Al-Albaaniy:
Jambo la kwanza alilowalingania ni Tawhiyd. Kisha ikafaridhishwa Swalaah. Kisha Swiyaam (funga ya Ramadhwaan), kisha ikafaradhishwa Hajj, na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Basi nawe fuatia katika Sunnah hii ya Shariy’ah hatua kwa hatua.

Tumekubaliana sasa kuwa haiwezekani kwamba kuna ‘khayr’ ambayo hakuijua Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwani ‘khayr’ zote tumezijua kupitia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na uhakika huu hakuna wawili wanaoupinga wala hakuna kondoo wawili watakaopigana kwa pembe zao juu ya hili, na naitakidi kwamba yeyote atakayetilia shaka hili basi yeye si Muislamu. Na miongoni mwa Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayounga mkono kauli hii ni kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
مَا تَرَكْتُ شَيْئًا يُقَرِّبُكُم إلى اللهِ إلَّا وَأَمَرْتُكُم بِهِ
“Sikuacha jambo lolote linalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni kwalo.” [Atw-Twabaraaniy Isnaad yake ni Swahiyh. Rejea Swiffatu-Swalatin-Nabiy (3/942) ya Imaam Al-Albaaniy]

Basi ingelikuwa Maulidi ni ‘khayr’ na ingekuwa ni jambo linalotukurubisha kwa Allaah basi ingebidi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) atuelekeze nayo. Sawa au si sawa?
Mimi sitaki ukubaliane nami bila ya kukinaika kila herufi ninayotamka. Una uhuru kamili useme: “Tafadhali nukta hii sikukinaika nayo!”

Je, basi kuna lolote ambalo hukuridhika nalo nami au uko pamoja nami?

Anayejadiliana na Imaam:
Pamoja na wewe tamaam!

Imaam Al-Albaaniy:
Jazaaka Allaahu khayraa. Kwa hiyo ikiwa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Sikuacha jambo linalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni kwalo.”

Sisi tunawaambia wote wanaosema kuwa inafaa kusimamisha Maulidi: Maulidi haya ni ‘khayr’ kwa madai yenu. Basi ima Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelekeza kusherehekea Maulidi au hakutuelekeza nayo.
Wakijibu kuwa “Ametuelekeza kusherehekea Maulidi,” tunawaambia:
هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٦٤﴾
“Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli [An-Naml: 64]
Na wala hawatoweza kamwe kuipatia njia (dalili hiyo).
Nasi tumesoma vitabu vya 'Alawiy na vinginevyo visivyokuwa vya 'Alawi kuhusu Maulidi, na wala hawatumii dalili isipokuwa kusema tu kuwa “Maulidi ni bid’ah hasanah, bid’ah hasanah! (uzushi mzuri!).”

Basi wote wanaosherehekea Maulidi au wanaopinga sherehe hii wanakubaliana kwamba Maulidi haya hayakuweko katika zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala zama za Maswahaba watukufu wala zama za Maimaam Wanachuoni.
Lakini wanaojuzisha sherehe hii ya Maulidi husema: “Kwani kuna nini Maulidi na hali anatajwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumswalia na kadhaalika.”
Sisi tunasema: Ingelikuwa ni ‘khayr’ wangetutangulia kwa hayo (Maulidi).

Wewe unaijua Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ
“Watu bora kabisa ni karne yangu, kisha wanaowafuatia kisha wanawafuatia.”
nayo imo katika Asw-Swahihayn [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na karne ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndio ambayo wameishi humo Maswahaba, kisha waliowafuatia ambao ni At-Taabi’uwna, kisha ambao wamewafuatia nao ni Atbaa’ut-Taabi’iyna. Na hili pia hakuna kukhitilafiana kwalo.

Je, basi mnadhani kuwa kuna ‘khayr’ yoyote ambayo imewapita, katika yote mawili; elimu na ‘amali? Inawezekana hilo?

Anayejadiliana na Imaam:
Ama kuhusu elimu, ingelikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemwambia yeyote katika zama zake kwamba “dunia inazunguka…”

Imaam Al-Albaaniy:
Samahani! Nakuomba usipindishe maneno. Kwa vile nimekuuliza kuhusu mambo mawili; elimu na ‘amali. Na kwa hakika kupindisha kwako kumeninufaisha kwani mimi ninavyokusudia elimu, huwa nakusudia elimu ya Dini (shariy’ah) si ya utabibu. Mfano naweza kusema kuwa: “Daktari huyu ana ujuzi zaidi kuliko Ibn Siynaa katika zama zake kwa sababu (daktari huyu) ametokea katika karne za baadaye, na amefanya majaribio mengi mno ya uzoefu.” Lakini hii haina maana kuwa anasifika mbele ya Allaah wala haimtangulizi mbele ya karne zilizoshuhudiwa (katika Hadiyth ya juu kuhusu watu bora kabisa). Lakini anasifika katika elimu aliyoisomea na sisi tunazungumzia kuhusu elimu ya shariy’ah, baaraka Allaah fiyka. Basi unapaswa utanabahi kwa haya. Kwa hiyo ninapokuambia: “Je, unadhania kuwa tunaweza kuwa ni wajuzi zaidi?” Nikimaanisha ni elimu ya shariy’ah na si elimu ya majaribio kama jiografia au falaki au kemia au fizikia. Na chukulia mfano zama hizi; mtu amemkufuru Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lakini yeye ni mjuzi kabisa katika watu kwa elimu yake katika sayansi hii, je basi hiyo elimu yake itampelekea kuwa karibu na Allaah?

Anayejadiliana na Imaam:
Hapana.

Imaam Al-Albaaniy:
Kwa hiyo sisi hatuzungumzii elimu katika fani hizo, bali tunazungumiza elimu inayotukurubisha kwa Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa). Na hapo nyuma kidogo tumezungumza kuhusu kusherehekea Maulidi. Basi swali linarudi sasa na nataraji kuwa nitapata jibu la wazi bila ya kupindisha tena. Basi nauliza: “Je unaitakidi kwa akili na fahamu uliyopewa kwamba inawezekana sisi katika zama hizi tuwe wajuzi zaidi kuliko Maswahaba na At-Taabi’iyna (Waliofuatia) na Maimaam waliofanya juhudi katika elimu ya shariy-‘ah, na kwamba sisi tuwe ndio wepesi zaidi katika kufanya ya khayr ya kujikuribisha kwa Allaah kuliko hao Salafus-Swaalih (wema waliotangulia)?

Anayejadiliana na Imaam:
Unaposema “elimu ya shariy’ah” je, unakusudia elimu ya kufasiri Qur-aan?

Imaam Al-Albaaniy:
Wao wana elimu zaidi kuliko sisi katika kufasiri Qur-aan, na wana elimu zaidi kuliko sisi katika kufafanua Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na mwisho wana elimu zaidi kuliko sisi katika Shariy’ah nzima ya Kiislamu.

Anayejadiliana na Imaam:
Kuhusu Tafsiyr ya Qur-aan, labda kwa sasa ni zaidi kuliko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mfano Aayah katika Qur-aan:
وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ ۚ صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ ۚ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾
Na utaona majabali ukiyadhania yametulia thabiti nayo yanapita mpito wa mawingu. Utengenezaji wa Allaah Ambaye Ametengeneza kwa umahiri kila kitu. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyodhahiri na yaliyofichikana kwa yale myafanyayo. [An-Naml: 88]

Basi ingelikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika zama zake kwamba “ardhi inazunguka”, je, hivi ataamini yeyote? Hakuna ambaye angeamini!

Imaam Al-Albaaniy:
Hivyo wewe unatutaka sisi – na nasema haya bila ya kukulaumu – kurekodi dhidi yako kupindisha kwako tena maneno? Ee ndugu yangu! Mimi nauliza kwa ujumla na si sehemu tu ya swali! Sisi tunauliza swali la ujumla. Nani wenye ujuzi zaidi kuhusu Uislamu kwa ujumla?

Anayejadiliana na Imaam:
Bila shaka ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake.

Imaam Al-Albaaniy:
Hivi ndivyo tunavyotaka kwako baaraka Allaahu fiyka.
Ama kuhusu Tafsiyr unayoihojia, haina uhusiano na ‘amali, bali ina uhusiano na kutafakari na kufahamu. Kisha tulishazungumza nawe kuhusu Aayah iliyopitia na na tumekuthibitishia kwamba wale wanaonukuu Aayah hii kuwa ni dalili kwamba dunia inazunguka wamekosea kwa sababu Aayaah inakusudia Siku ya Qiyaamah:
يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ ﴿٤٨﴾
48. Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia na (viumbe wote) watahudhuria kwa Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika.” [Ibraahiym: 48]

Hata hivyo, sisi hatuko katika maudhui haya.

Nami kwa kukubaliana nawe kimjadala, basi huenda akaweko mtu katika wale waliokuja mwishoni ambaye ana utaalamu wa sayansi au utaalamu wa ki-ulimwengu kuliko Swahaba au Taabi’iy (mwanafunzi wa Swahaba) na kuendelea. Lakini haya hayana uhusiano na ‘amali njema. Kwa sababu mfano leo, makafiri wana utaalamu zaidi ya falaki na aina zake, lakini je, wananufaika nini kwayo? (kuhusiana na Allaah?) Si lolote! Basi sisi hatutaki sasa kutumbukia katika haya. Tunataka kuzungumzia kila jambo litakalotukurubisha kwa Allaah. Basi sisi sasa tunataka tuzungumzie kuhusu Maulidi ya Nabiy Mtukufu.

Na tumeshakubaliana kwamba kama ingelikuwa ni ‘khayr’, basi bila shaka Salafus-Swaalih (wema waliotangulia) na kiongozi wao ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wangekuwa na ujuzi nao zaidi kuliko sisi na wepesi zaidi kuyatenda kuliko sisi. Je, una shaka na hili?

Anayejadiliana na Imaam:
Hapana, hapana hakuna shaka kwa hilo!

Imaam Al-Albaaniy:
Basi usivuke mipaka ukachanganya haya na mambo ya elimu ya majaribio, kwani hayana uhusiano nayo katika kukurubisha kwa Allaah kwa ‘amali njema.

Maulidi hayakuweko zama za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kukubaliana sote. Kwa maana ‘khayr’ hii haikuweko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba na At-Taabi’iyn na Maimaam Mujtahidiyn. Vipi basi imefichika ‘khayr’ hii kwao?

Hakuna budi ila tuseme mojawapo kati ya mawili:

Waliijua ‘khayr’ hii kama tunavyoijua sisi; nao ni wajuzi zaidi yetu. Au hawakuijua. Sasa vipi basi sisi tumeijua?

Tukisema: Waliijua ‘khayr’ hii, na hii ni kauli iliyo karibu zaidi na bora zaidi kwa wale wanaosema Maulidi yanajuzu kusherehekewa, basi kwanini hawakuyafanyia kazi? Je, sisi tuko karibu zaidi kwa Allaah (kuliko wao)?

Kwanini asikosee mmoja wao hata mara moja; Swahaba au Taabi’iy au Mwanachuoni miongoni mwao au mfanya ‘ibaadah mno miongoni mwao (kwanini wasikosee) wakaifanyia kazi ‘khayr’ hii?

Je, inaingia akilini mwako kwamba ‘khayr’ hii haikufanywa kamwe na yeyote yule? Nao walikuwa ni mamilioni na ni wajuzi zaidi kuliko sisi na wema zaidi kuliko sisi na wako karibu zaidi na Allaah?

Hivyo wewe unajua kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
لاَ تَسُبُّوا أَصْحَابِي؛ فَإِنَّ أَحَدَكُمْ لَوْ أَنْفَقَ مِثْلَ أُحُدٍ ذَهَبًا مَا أَدْرَكَ مُدَّ أَحَدِهِمْ وَلاَ نَصِيفَهُ
“Msiwatukane Swahaaba wangu. Ninaapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya Allaah kugawa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao lao.“ [Al-Bukhaariy, Muslim]

Je, unaona upeo wa tofauti baina yetu na wao?

Kwa sababu wao wamefanya Jihaad katika njia ya Allaah (Ta’aalaa) pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakapokea elimu ikiwa mbichi safi mpya kutoka kwake moja kwa moja, bila ya kuwa kiungo kirefu baina yetu na baina yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Kama alivyoashiria (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maana hiyo katika Hadiyth Swahiyh:
((مَنْ أَحَبَّ أنْ يَقْرَأَ القرآنَ غَضًّا طَرِيًّا؛ فَلْيَقْرَأْهُ على قراءةِ ابنِ أمِّ عَبْدٍ)) يعني عبد الله بن مسعود
“Anayependa kuisoma Qur-aan mbichi safi mpya basi asome kwa Qiraa cha Ibn Ummi ‘Abd” (Yaani ‘Abdullaah bin Mas’uwd) [As-Silsilah Asw-Swahiyhah (5/379)].

Hawa Salafus-Swaalih (wema waliotangulia) na viongozi wao Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), haiwezekani sisi tuwadhanie kuwa hawakujua ‘khayr’ iliyowakurubisha kwa Allaah, na kwamba sisi ndio tuliyoijua ‘khayr’ hiyo! Na kama tukisema kuwa waliijua kama tunavyoijua basi ni mustahili kwetu kufikiria kuwa wameipuuza ‘khayr’ hiyo.

Huenda haya yamekuwekea wazi nukta ninayoizungumzia In Shaa Allaah?

Anayejadiliana na Imaam:
AlhamduliLLaah.

Imaam Al-Albaaniy:
Jazaaka Allaahu khayraa.
Kuna jambo jengine. Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zinazobainisha kuwa Uislamu umekamilika. Na nadhani kuwa ukweli huu wewe unautambua na unaamini na hakuna tofauti baina ya ‘Aalim na Twaalibul-‘Ilm (mwanafunzi) na mtu wa kawaida asiye msomi kuhusu kujua uhakika huu. Nao ni, Uislamu umekamilika na si kama dini ya ki-Yahudi au ki-Naswara kila siku kuna mageuzo na mabadiliko.

Na nakukumbusha mfano kauli ya Allaah (Ta'aalaa):
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الْإِسْلَامَ دِينًا
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nimekutimzieni Neema Zangu kwenu na Nimekuridhieni Uislamu kuwa ni Dini yenu)) [Al-Maaidah 5: 3]

Na sasa linakuja swali, nalo ni njia nyingine ya kubainisha kwamba kusherehekea Maulidi si jambo la khayr, hii mbali na yaliyotangulia kwamba ingelikuwa ni ‘khayr’ basi wangelitutangulia wao yaani: Salafus-Swaalih; walio na elimu zaidi yetu na wenye kufanya ‘ibaadah zaidi yetu.

Maulidi haya ya Nabiy ingelikuwa ni ‘khayr’ basi ni katika Uislamu. Tunasema: Je, hivi sisi sote tunaopinga kusimamisha Maulidi na wenye kuyajuzisha, je, sote tunakubaliana kama tulivyokubaliana nukta iliyotangulia kwamba sherehe hii haikuweko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Je, tuko bado katika kukubaliana huku (nukta hii ya pili?) kwamba sherehe hii, kama ni ‘khayr’ basi imo katika Uislamu na ikiwa si ‘khayr’ basi haimo katika Uislamu? Na siku ambayo Aayah hii imeteremshwa:
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu…
Siku iliyoteremshwa hakukuwa na sherehe ya Maulidi ya Nabiy. Kwa hiyo je, imo katika Dini katika uoni wako?

Tafadhali uwe mkweli nami. Wala usidhani kuwa mimi ni miongoni mwa Mashaykh wanaonyamazisha wanafunzi, bali hata watu wa kawaida kwa kuwaambia: “Nyamaza! Hujui! Huna elimu!” Hapana wewe uko na uhuru kamili kama kwamba unaongea na mtu kama wewe au chini yako kwa umri na elimu. Ikiwa hukukinaika sema: “Sikukinaika.”

Hivyo sasa, ikiwa Maulidi ni ‘khayr’ basi hayo ni katika Uislamu, na ikiwa si ya khayr basi sio katika Uislamu. Na tukikubalilana kwamba kusherehekea Maulidi hayakuweko pindi ilipoteremshwa Ayaah iliyotangulia, basi ni mantiki kusema kuwa si katika Uislamu.

Na nitathibitisha nnayoyasema kwa aliyoyasema Imaam wa makazi ya hijrah (Madiynah) Imaam Maalik bin Anas ambaye amesema:
“Atakayezusha bid’ah katika Uislamu…” (Tanabahi amesema: “bid’ah moja” wala hakusema bid’ah nyingi!) “…kisha akaiona kuwa ni nzuri basi amedai kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekhini risaalah (ujumbe).”

Na hili ni jambo khatari mno! Nini dalili ee Imaam (Maalik)?
Akasema Imaam Maalik: “Someni mkipenda kauli ya Allaah (Ta’aalaa):
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الْإِسْلَامَ دِينًا
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nimekutimzieni Neema Zangu kwenu na Nimekuridhieni Uislamu kuwa ni Diyn yenu)) [Al-Maaidah (5: 3]
"فمالم يكن يومئذٍ ديناً ؛ فلا يكون اليوم ديناً".
“Basi ambayo hayakuwa ni Dini siku hizo, hayawezi kuwa ni Dini leo.” (mwisho wa maneno yake Imaam Maalik)

Je, alisema lini haya Imaam Maalik? (Alisema) Katika karne ya pili baada ya hijrah ambayo ni mojawapo wa karne zilizoshuhudiwa kuwa ni karne bora. Sasa itakuwaje basi ikiwa ni karne ya kumi na nne (tuliyonayo sasa?)

Maneno haya (ya Imaam Maalik) yanapasa kuandikwa kwa dhahabu, lakini sisi tumeghafilika na kitabu cha Allaah (Ta’aalaa) na Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kauli za Maimaam ambao tunadai kuwa tunawafuata. Mbali kabisa mbali kabisa! Na tofauti baina yetu na wao katika kufuata ni kama tofauti ya Mashariki na Magharibi.

Huyo (Imaam Maalik) ni Imaam wa mji wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohajiri (Madiynah). Anasema kwa lugha safi sahihi kabisa ya Kiarabu: “Basi ambayo hayakuwa ni Dini siku hizo, hayawezi kuwa ni Dini leo.”
Leo kusherehekea mazazi ya Nabiy ni ya Dini na ingekuwa si hivyo, basi mjadala huu usingejiri baina ya ‘Ulamaa wanaoshikamana na Sunnah na kuihami (Dini) dhidi ya bid’ah. Itakuwaje yawe (Maulidi) katika Dini wakati hayakuweko wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala zama za Maswahaba wala zama za Taabi’iyna (waliofuatia Maswahaba) wala Taabi’iy Taabi’iyna (Waliofuatia baada ya Taabi’iyn)?

Imaam Maalik ni katika Atbaa’ut-Taabi’iyn na ni miongoni mwa waliotajwa katika Hadiyth:
((خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ)) متفق عليه
((Watu bora kabisa ni wa karne yangu, kisha ambao wanafuatia kisha ambao wanafuatia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Imaam Maalik amesema: “Basi ambayo hayakuwa ni Dini siku hizo, hayawezi kuwa ni Dini leo, na ummah wa mwisho hautatengemaa isipokuwa kwa kile kilichofanya ummah wa kwanza kutengamaa.”

Je, ummah wa mwanzo kabisa ulitengamaa (ulikaa sawa) kwa nini? Kwa kuzusha mapya katika Dini kwa kujikurubisha kwa Allaah (Ta’aalaa) mambo ambayo hakujikurubisha nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe ndiye aliyesema:
ما تَرَكْتُ شيئاً يُقَرِّبُكُمْ إِلَى اللهِ إلى وأَمَرْتُكُمْ به
“Sijaacha lolote litakalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni kwalo.”

Kwanini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakutuamrisha tusherehekee Maulidi yake? Swali hili lina jawabu:
Kuna sherehe ya kusherehekea Maulidi ya Nabiy yaliyowekewa shariy’ah kinyume na hizi sherehe za Maulidi haya (mnayoyafanya) ambayo hayakuamrishwa. Sherehe hii iliyoamrishwa ilikuweko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kinyume na yaliyokuwa hayakuamrishwa yakiwa na tofauti kubwa kabisa iliyoko baina ya sherehe mbili (hizi).

Tofauti ya kwanza: Ni kwamba sherehe iliyoamrishwa (tutaitaja) ni ‘ibaadah ambayo wamekubaliana Waislamu wote.

Tofauti ya pili: Sherehe iliyoamrishwa inakariri kila wiki mara moja, lakini hiyo yao ambayo haikuamrishwa inatokea mara moja tu kwa mwaka.

Hizi ni tofauti mbili baina ya sherehe mbili hizo. Kwamba ya kwanza ni ‘ibaadah, na inakariri kila wiki mara moja, kinyume na ya pili ambayo si ya kishariy'ah na si ‘ibaadah na wala haikariri kila wiki!

Na mimi sizungumzi kwa matamanio yangu ambayo Allaah Hakuteremshia dalili, bali nakutoleeni dalili kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo imehadithiwa katika Swahiyh Muslim (Rahimahu Allaah):
عنْ أَبِي قَتَادَةَ الْأَنْصَارِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ سُئِلَ عَنْ صَوْمِ الِاثْنَيْنِ فَقَالَ: ((فِيهِ وُلِدْتُ وَفِيهِ أُنْزِلَ عَلَيَّ)).
Kutoka kwa Abuu Qataadah Al-Answaariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu Swawm ya Jumatatu akasema: “Nimezaliwa siku hiyo na siku hiyo nimeteremshiwa (Qur-aan).” [Muslim]
Yanamaanisha nini maneno hayo?
Ni kama vile anasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
Utaniulizaje hivyo na hali Allaah Amenitoa siku hiyo kuwa na uhai na nikateremshiwa wahyi humo?
Yaani inawapasa mfunge Swawm siku ya Jumatatu kumshukuru Allaah (Ta’aalaa) kuniumba mimi siku hiyo na kuteremsha Wahyi kwangu siku hiyo.

Na hivyo ni sawa na Swawm ya Mayahudi siku ya ‘Aashuraa. Na huenda ukajua kuwa kabla ya kufaridhishwa Swawm ya Ramadhwaan, Swawm ya siku ya ‘Aashuraa ndio ilikuwa fardhi kwa Waislamu. Na kuna kauli nyengine za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alipohamia Madiynah aliwakuta Mayahudi wanafunga Swawm siku ya ‘Ashuraa. Akawauliza sababu yake wakamjibu: “Ni siku ambayo Allaah Alimuokoa Muwsaa kutokana na watu wa Fir’awn, hivyo tunafunga Swawm kumshukuru Allaah.” Hapo yeye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
“Sisi tuna haki zaidi juu ya Muwsaa kuliko nyinyi.”
Basi akafunga Swawm siku hiyo na akaamrisha watu, pia siku hiyo ikawa ni fardhi mpaka Allaah Alipoteremsha kauli Yake:
شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ ﴿١٨٥﴾
Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu (mwandamo wa) mwezi na afunge Swiyaam. [Al-Baqarah: 185]
Hapo ikawa Swawm ya ‘Aashuraa ni Sunnah ,na kukafutwa kuwajibika kwake.

Ushahidi wa haya ni kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliungana na Mayahudi kufunga Swawm siku ya ‘Aashuraa kama ni shukurani kwa Allaah (Ta’aalaa) kumuokoa Muwsaa ('Alayhis-Salaam) kutokana na Fir’awn. Hivyo mlango wa shukurani umefunguliwa kwetu kwa kufunga Swawm siku ya Jumatatu kwa sababu ni siku ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezaliwa na ni siku ambayo ameteremshiwa Wahyi.

Sasa nakuuliza: Je, hawa watu wanaosherehekea mazazi (yasiyokuweko katika shariy’ah) ambayo tunajua kuwa hayana khayr ndani yake - najua kuwa wengi ya watu hao hufunga Swawm Jumatatu kama wanavyofunga Swawm siku ya Alkhamiys - lakini je, Waislamu wengi wanafunga Swawm ya Jumatatu pekee?
Hapana! Hawafungi Swawm Jumatatu, lakini Waislamu wengi wanasherehekea mazazi ya Nabiy mara moja kwa mwaka. Je, hivi si kinyume na usahihi?
Hawa inawathubutikia kauli ya Allaah (Ta’aalaa) kwa Mayahudi:
أَتَسْتَبْدِلُونَ الَّذِي هُوَ أَدْنَىٰ بِالَّذِي هُوَ خَيْرٌ ۚ
“Je mnataka kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora? [Al-Baqarah: 61] (Kuchagua yaliyo duni na kuacha yaliyo bora)

Hiyo ndio khayr. Kufunga Swawm iliyokubalika kwa Waislamu wote; nayo ni Swawm ya Jumatatu, na juu ya hivyo Waislamu wengi hawafungi Swawm hiyo!

Kisha kwa ambao wanaifunga Swawm nao ni wachache. Je, wanajua siri ya Swawm hiyo?
Hapana hawajui!

Basi wako wapi Wanachuoni wanaotetea Maulidi?!
Kwanini hawawabainishii watu kuwa Swawm ya Jumatatu ni kusherehekea kulikoamrishwa kuwa ni Maulidi na wakahimiza kuifunga Swawm badala ya kutetea ambayo hayakuamrishwa? Na Amesadikisha Allaah (Ta’aalaa) Anaposema:
“Je mnataka kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora?
Na Amesadikisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
لَتَتَّبِعُنَّ سَنَنَ مَنْ قَبْلَكُمْ؛ شِبْرًا بِشِبْرٍ، وذِرَاعًا بِذِرَاعٍ؛ حَتَّى لَو دَخَلُوا جُحْرَ ضَبٍّ لَدَخَلْتُمُوهُ
“Mtafuata nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na katika riwaayah nyingine iliyo khatari:
حتى لو كان فيهم مَنْ يَأْتِي أُمَّهُ على قارعةِ الطريقِ لَكَانَ فيكم مَنْ يَفْعَلُ ذلك
“...hadi kwamba hata ingekuwa mmoja wao angejamiiana na mama yake katikati ya barabara, angekuweko mtu miongonii mwenu ambaye angefanya hivyo pia” [Al-Haakim ikiwa ni Hasan kama alivyoisahihisha Al-Bazzaar na Al-Albaaniy ameikubali katika Silsilah Asw-Swahiyhah (1348)]

Basi sisi (tunaosherehekea Maulidi) tunafuata mwendo wa Mayahudi, tukabadilisha ambayo ni ya (kuchagua yaliyo) duni kwa (kuacha) yaliyo khayr kama tulivyobadilisha (tukachagua) Maulidi ya Nabiy ambayo yanatokea mwaka mara na hayana dalili kwa (kuacha) ambayo yaliyo khayr nayo ni kusherehekea kila Jumatatu ambayo ni kusherehekea kulikoamrishwa kwa kuifunga Swawm, pamoja na kutanabahi siri yake humo kuwa unafunga Swawm kwa ajili ya kumshukuru Allaah (Ta’aalaa) kwa kumuumba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Akateremsha wahyi humo (siku hiyo).

Na nahitimisha maneno yangu kwa kutaja kauli ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
أَبَى اللهُ أنْ يَقْبَلَ توبةَ مبتدعٍ
“Allaah Amekataa kabisa kupokea tawbah ya mwenye kufanya bid’ah.” [Ibn Maajah na Imaam [Imaam Al-Albaaniy amesema ina udhaifu, lakini kuna Hadiyth ambayo ameisahihisha yenye maana kama hiyo iliyokusanywa na Abuu Imaam katika Taariykh Asbahaan (Uk. 259), Atw-Twabaraaniy katika Al-Awsatw (4360) na wengineo].

Na Allaah (Ta’aalaa) Anasema:
يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖوَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ
Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake. Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu. [Al-Maaidah: 67]

Anayejadiliana na Imaam:

Je, kusoma Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) si takrima kwake?

Imaam Al-Albaaniy:
Naam (endelea).

Anayejadiliana na Imaam:
Si mna thawabu ya khayr kutoka kwa Allaah?

Imaam Al-Albaaniy:
Yote ni khayr! Lakini hutofaidika chochote kutokana na swali hili. Kwa hiyo nakukatisha kwa swali: Je ,kuna yeyote aliyekuzuia kusoma Siyrah yake?
Kisha sasa nakuuliza swali: Ikiwa ni aina ya ‘ibaadah iliyoamrishwa lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuiwekea muda makhsusi wala hakuiwekea jinsi ya kuitekeleza; je, inajuzu kwetu kuiwekea wakati makhsusi au namna ya kuitekeleza? Je, unalo jibu?

Anayejadiliana na Imaam:
Hapana sina jibu.

Imaam Al-Albaaniy:
Allaah (Ta’aalaa) Anasema:
أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ
Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea idhini? [Ash-Shuwraa: 21]
Na Anasema pia Allaah (Ta’aalaa):
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣١﴾
Wamewafanya Wanavyuoni wao mafuqahaa wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miungu badala ya Allaah, na (pia wamemfanya) Al-Masiyh mwana wa Maryam (kuwa ni mungu); na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Ilaah (Allaah) Mmoja (Pekee). Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Utakasifu ni Wake! kutokana na yale yote wanayomshirkisha nayo. [At-Tawbah: 31]
‘Adiyy bin Haatim (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliposikia Aayah hii na alikuwa kabla ya kusilimu kwake, alipokuwa Mnaswara, ilikuwa ngumu kwake akasema: “Hatukuwa tukiwaabudu.” Hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
أَلْيَسَ يُحَرِّمُونَ مَا أَحَلَّ اللهُ فَتُحَرِّمُونَهُ وَيُحِلُّونَ مَا حَرَّمَ اللهُ فَتُحِلُّونَهُ؟
“Je, kwani hawakuwa wakiharamisha Aliyoyahalalisha Allaah nanyi mkayaharamisha, na wakahalalisha Aliyoyaharamisha Allaah nanyi mkayahalalisha?”
Akasema: Ndio.
Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Basi hiyo ndio kuwaabudu kwao.” [At-Tirmidhiy (3095) na ameipa daraja ya Hasan Imaam Al-Albaaniy]

Na hii inabainisha khatari ya kufanya bid’ah katika Dini ya Allaah (Ta’aalaa):

Mwisho wa Mjadala

************************

Imetolewa kutoka katika moja ya kanda za Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika Silsilat Al-Hudaa wan-Nuwr Kanda namba (1//94)




No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW