MOHAMMAD S.A.W MTUME WA WAISLMU, HAJAWAHI, SIYO , NA WALA HATAKUWA MTUME NA NABII WA KWELI
Nimesoma kwenye blog ya jamii forums na kuona Waislamu wakiwashawishi watu wengine wamuamini Mohammad kuwa naye ni miongoni mwa manabii na mitume wa Mungu aliye hai, jambo ambalo si kweli.Fuatilia…..
WAJUE MANABII WA UONGO
Na Mwalimu Daniel Mwankemwa
UTANGULIZI:
Suala linalohusu kuwajua manabii wa uongo , limekuwa linaleta shida sana kwa watu wengi, kwa sababu manabii hao wa uongo wanapokuja kwa watu kuleta ujumbe wao hudai “ tumetumwa na Mwenyezi Mungu kuleta ujumbe wake na hivyo kuwataka wanadamu kuupokea, kuuamini na kuufuata”. Inapotokea nabii amekuja kwa mtindo huo na akakutana na watu wasiojua kuwapambanua manabii na mitume kwa misingi ya Neno la Mungu, ndipo ukengeufu hutokea, na makundi ya aina mbalimbali ya imani za uongo hujitokeza.
Kwa hapa kwetu Tanzania,unaposoma katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Ibara ya 19 (i-iii) utakutana ma maelezo kuwa ,mfuasi wa dini yoyote anao uhuru wa kubadili dini yake ya awali na kujiunga na dini nyingine anayoona yeye kwake inamfaa. Lakini pamoja na uhuru huo si kila dini (njia) inafaa zingine zinaishia kwenye mauti ya milele.
Mith 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”. (Angalia pia Mith 16:25).
Miongoni mwa wanadamu wanaoitwa nabii na mtume, ni mtu aitwaye Muhammad s.a.w ibn Abdullah,ibn Abdu Mutallib, ambaye ni mtume na nabii katika dini ya Kiislamu.
Pengine wewe msomaji wa somo hili unaweza kushangaa ni kwa vipi sisi ambao si Waislamu bali Wakristo tuanze kuhoji habari za Muhammad s.a.w mtume wa Waislamu?. Jibu lake ni kwamba kitabu cha Qur’an kinachotumiwa na Waislamu kimetutaja sisi Wakristo mara 62 kikitutaka kuupokea ,kuuamini na hatimaye kuufuata ujumbe wa Muhammad s.a.w kwa madai ya kuwa yeye ni nabii na mtume wa mwisho hata kwetu Wakristo, aliyetumwa na Mungu.
Tunasoma hayo ndani ya Qur’an katika Suratul, Baqarah, (ng’ombe jike wa manjano), 2: 62 “Katika walioamini (Mitume ya zamani huko ) na Wayahudi na Wakristo na Wasabai, yoyote miongoni mwao atakayemwamini Mwenyezi Mungu (Sasa kama anavyosema Nabii Mohammed ) na akaamini siku ya mwisho na akafanya vitendo vizuri basi watapata thawabu zao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika”.
Kwetu sisi kama Wakristo japo katika aya hii tumetajwa , kuna swali ambalo tunajiuliza kuhusu unabii na utume wa Muhammad nalo ni hili “ HIVI MWENYEZI MUNGU ALISAHAU NINI KATIKA KAZI YAKE YOTE KAMILIFU YA KUMKOMBOA MWANADAMU KUTOKA KATIKA DHAMBI MPAKA AMLETE MUHAMMAD S.A.W?”.
Nabii ni mtu gani? Nabii ni mtu aliyeteuliwa rasmi kwa vigezo vya Kiungu ili kuleta ujumbe wa Mungu kwa wanadamu, kwa maneno mengine nabii ni msemaji wa siri za Mungu.
Nabii: Ni mtu ambaye ni msemaji wa Mungu (a mouthpiece of God) .Husimama kati ya Mungu na binadamu, mwenye jukumu la kupeleka ujumbe wa Mungu kwa watu. Nabii anapokuwa msemaji wa Mungu, huvuviwa na Roho wa Mungu, bila ujumbe wake kuwa na makosa. Nabii hujizuia kabisa utashi wake, nafsi yake,,na mawazo yake, anapokuwa anatoa ujumbe wa Kinabii toka kwa Mungu. Wakati mwingine Mungu mwenyewe hutia maneno yake vinywani mwao (Kum 18:18, Yer 1:9). Nabii ni mtumishi wa Mungu (Zekaria 1:6) na mjumbe wa Mungu 2 Nyak 36:15). Unabii wao umegawanyika katika makundi matatu: Unabii unaoelezea hatima ya Waisrael, Nabii zinazohusiana na ujio wa Masihi, na nabii zinazoelezea mambo yajayo (Eschatological prophets). Kwa hiyo Sheria na Manabii inahusiana na Torati (Pentateuch) yaani Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati. Na manabii ni vile vingine vyote visivyo kuwa Torati.
Kitabu cha nabii Amos 3:7 “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake”Neno nabii asili yake ni katika lugha ya Kiebrani na maana yake mwonaji. 1Sam 9:9 “ Hapo zamani katika Israel, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa mwonaji”.
Katika mstari huo hapo juu unatuonesha kuwa manabii wa kweli wa Mungu ni lazima chanzo cha ufunuo au ujumbe wao kiwe Mwenyezi Mungu mwenyewe (Roho Mtakatifu), au ndoto kutoka kwake, au maono kutoka kwake (Hes 12:6), au kupitia malaika watakatifu (Dan 8:15-21) . kinyume na hapo ni nabii wa uongo .
Tahadhari ya Bwana Yesu: Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani alituonya kuhusu kuwatambua manabii na mitume wa uongo kabla Muhammad hajazaliwa (amezaliwa 570 B.K), wala kabla Uislamu haujaanzishwa na Muhammad mwaka 610 B.K, wala kabla ya kuwepo kitabu kinachoitwa Qur’an. Tunayasoma maonyo hayo ya Bwana Yesu katika
Mathayo 7:15-16 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali, mtawatambua kwa matunda yao”.
Mathayo 24:11-13 “Na manabii wengi wa uongo watatokea na kuwadanganya wengi na kwasababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka”.
Mitume wa Bwana Yesu walisisitiza sana wakikazia kuhusu onyo la Yesu juu ya kuwajua manabii na mitume wa uongo .
1Yohana 4:1-3,15 “Wapenzi msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, ya kwamba zimetokana na Mungu kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja na sasa imekwisha kuwako duniani. 15 “ Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake naye ndani ya Mungu”
Vigezo hivi tulivyopewa na Biblia Takatifu kuwajua manabii na mitume wa uongo ni muhimu sana tukavichunguza katika maisha ya wale wanaoitwa nabii au mtume .
Nabii wa kweli hupata ufunuo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu:- 2Petro 1:20-21.” Mkijua neno hili kwanza,ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu.Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu;bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu,wakiongozwa na Roho Mtakatifu”.
1 Petro1:10-11 “Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta tafuta na kuchunguza chunguza ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi na wakati wa namna gani ulioonywa NA ROHO WA KRISTO ALIYEKUWA NDANI YAO ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaokuwako baada ya hayo…..” (maneno ya msisitizo kwa herufi kubwa ni ya mwandishi)
Ufunuo 19:10 “Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndiyo roho ya unabii”
Hivyo manabii walisema ndani yao wakiongozwa na Roho wa Kristo mwenyewe, kabla hajaja ulimwenguni katika mwili. Je Muhammad s.a.w ni miongoni mwao hata tuuamini ujumbe wake?
Muhammad hakujua kusoma wala kuandika
Qur’an 7:157
Ambao wanamfuata mtume nabii aliye ummy (asiyejua kusoma wala kuandika) na juu ya hivi atafundisha mafundisho hayo ya ajabu ya uislamu……….
Na ushahidi mwingine unapatikana katika kitabu cha Maisha ya nabii Muhammad uk 8 kilichoandikwa na Sheikh Abdallah Saleh Al-Farsy, tunasoma kama ifuatavyo katika kipengele cha kujifunza kwake;-
Habari ya kusoma haijakuwako katika nchi ya hijazi, hivyo mtume aliondokea kama Makureshi wengine bila ya kujua kusoma wala kusoma kilichoandikwa. Elimu yao ilikuwa kujifundisha mambo yanayohusu maisha yao ya kibedui, kama vita, kutunga mashairi ya kujisifu ushujaa wao na kutunga hotuba zinazoweza kuharakisha watu wapigane bila ya kufikiri.
Hivyo basi Muhammad katika maisha yake hakujua kusoma wala kuandika na ndivyo alivyoishi katika maisha yake yote.
Je Yesu alijua kusoma na kuandika? Luka 4:16-17. HOJA ya Waislamu wanasema katika Yoh 7:14 Yesu akiwa Yerusalemu watu wakashangaa kuwa amepataje elimu ambaye hakusoma? Ukweli ni kwamba Yerusalemu siko alikokulia Yesu. Yeye Yesu amekulia Nazareti ambako wanamfahamu kuwa anajua kusoma na ndiyo sababu alipewa chuo cha nabii Isaya ili akisome.
JINSI MUHAMMAD (S.A.W) ALIVYOPATA UTUME NA WAHYI (UFUNUO) WAKE
Ufunuo aliokuja nao Muhammad s.a.w , mtume wa Waislamu, ni tofauti sana na mitume wote walioishi kabla yake wanaotajwa ndani ya Biblia Takatifu. Tofauti yake ni kwamba manabii na mitume wote waliotajwa ndani ya Biblia Takatifu, wameandika watu mbalimbali wapatao 40 kwa miaka mingi sana inayokaribia 1500, lakini ufunuo wao ni wa aina moja (it has comformity). Ule unabii wa Agano la Kale umetimizwa katika Agano Jipya. Hii ni kwa sababu chanzo cha ufunuo huo ni kimoja, Roho Mtakatifu.
Lakini kwa upande wa Muhammad s.a.w , mtume wa Waislamu yeye chanzo cha ufunuo na hatimaye utume wake ni masuala yenye utata sana ambao hata wafuasi wa dini hiyo na wao hawajui kwa hakika ukweli ni upi.
Hebu tuangalie kwa ufupi utata huo.
Muhammad s.a.w alipotimiza umri wa miaka 38 alihama toka nyumbani kwake, akahamia katika mapango yaliyokuwa hapo karibu na mji wa Makka. Alipofikisha umri wa miaka 40 siku moja alitokewa na kiumbe ambacho Waislamu leo wanakiita Malaika Jibril.
Wahyi (ufunuo) uliokuja kwa Muhammad alisikia makengele,uso kuwa mwekundu,jasho kumtoka. Katika Bukhar, Hadithi na 2, Juzuu na 1,Al-Lu’lu Kitabu cha 3.Uk. Na.874 Hadithi na 1505 “Hadithi ya Aisha r.a mama wa waumini amesema, kuwa Al Harith ibn Hisham r.a alimuuliza mtume wa Allah s.a.w ‘ Ewe mtume wa Allah hivi wahyi (ufunuo) hukujia vipi?’ mtume wa Allah s.a.w akajibu, “ Wakati mwingine hunijia kama mlio wa kengele, na aina hiyo ndiyo ngumu zaidi kwangu, inaondolewa hali hiyo kwangu wakati tayari nimeshapata wahyi. Na nyakati nyengine malaika anakuja kwangu akiwa katika mfano wa mtu, kwa hiyo ananieleza na ninayazingatia aliyoyasema.” Aisha r.a alisema , Na hakika nilimwona unamshukia wahyi siku ya baridi kali na ilipomuondoka hali hiyo, paji lake la uso lilichuruzika jasho.”
Qurani 53:2 – 6 Suratul Najm (Nyota) “Kwamba mtu wenu huyu Nabii Muhamad (hakupotea kwa ujinga) na wala hakukosa (Na hali ya kuwa anajua). Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya (anayosema) ila ni wahyi (ufunuo) uliofunuliwa (kwake). Amemfundisha (malaika) mwenye nguvu sana. Mwenye uweza na yeye (huyu Jibril) akalingana sawa sawa.
Huyu malaika Jibril ndiye Waislamu wanasema alimtokea Muhammad kule pangoni na kwamba yeye huyo malaika Jibril ndiye Roho Mtakatifu. Tunaposoma ufafanuzi wa aya ya 2:87 ya Suratul Baqarah, uliyomo ndani ya Qur’an unasema “Kwa Waislamu Roho Mtakatifu ni Malaika Jibril si yule wanaodai Wakristo kuwa ni mmoja wa asili ya utatu (Trinity)”.
Jambo ninalopenda ulijue ni kwamba Waislamu wote hawakubahatika kupewa elimu ya Roho. Hii ni kuanzia mtume na nabii wao Muhammad . Tunasoma hayo katika Qur’an 3:7 “Yeye ndiye aliyekuteremshia kitabu (hiki Qur’an) ndani yake zimo aya Muhkam (nyepesi kufahamika) ambazo ndizo msingi (asili) wa kitabu (hiki) na ziko nyingine Mutashabihat (zinababaisha kama habari za akhera,za peponi na motoni na mengine ambayo yamekhusika na Roho).Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazo babaisha kwa kutaka kuwaharibu watu na kutaka kujua hakika yake vipi; na hakuna ajuaye hakika yake vipi ila Mwenyezi Mungu. Na wale waliozama katika ilimu husema:”Tumeziamini,zote zimetoka kwa Mola wetu.”Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili.”
Qur’an 17:85 Suratul Ban Israil (Wana wa Israeli). “Na wanakuuliza habari ya roho.Sema roho ni jambo lililohusika na Mola wangu (Mwenyezi Mungu),Nanyi hamkupewa katika ilimu (ujuzi) ila kidogo kabisa.(Nayo ni ilimu ya vitu visivyokhusika na roho”).
Hivyo katika Uislamu elimu ya Roho hawana kwa mujibu wa Qur’an. Hii ndiyo sababu mara nyingi wao hushughulikia sana mambo ya nje (externalistics) zaidi kuliko ya Rohoni k.m kutawadha na kupandisha maji puani wakiamini wamemtoa Shetani aliyekuwa ndani ya pua. Katika kitabu kiitwacho Al-Lu’lu’ wal-Marjan, Juzuu 1. Hadithi na 183 uk. 96 inasomeka hivi “Amesimulia Abu Huraira (r.a), Mtume (s.a.w) alisema, “Mmoja wenu anapoamka kutoka usingizini, basi atawadhe na apandishe maji puani na apenge mara tatu, kwa sababu Shetani alilala ndani ya tundu za pua yake”. (Bukhari, Hadithi, Na.516 Juzuu 4)
Baada ya kufahamu jinsi Waislamu wasivyokuwa na elimu ya Roho, ndipo tunapoanza kuhoji huyo malaika anayeitwa Jibril ni nani ? Je ni malaika wa Mungu wa Kweli YEHOVA?.
Biblia Takatifu inaeleza juu ya malaika walioasi mbinguni kisha wakafukuzwa na kutupwa huku chini. 1Petro 2:4 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachia “malaika waliokosa” bali aliwatupa shimoni akawatia katika vifungo vya giza walindwe hata ije siku ya hukumu”.
Kwa mafundisho haya ya Biblia yanatuonesha kuwa kuna kundi moja la malaika liliasi na likafukuzwa na hadi sasa kundi hilo linasubiri hukumu. Kundi hilo leo linaitwa Shetani,Majini au Mapepo wachafu.
Lakini tusomapo kitabu cha Qur’an , kitabu kilichokuja baadaye sana karne ya 7 (610 B.K) ,baada ya kitabu cha Biblia, ndani yake tunapata taarifa tofauti kuhusu malaika.
Qurani 32:13 Suratul As – Sajdah (Kusujudu) “Na tungalitaka tungempa kila mtu uwongofu wake (kwa lazima kama tulivyowapa malaika…”
Ufafanuzi wa aya ya 13 ulio ndani ya Qurani unasomeka hivi:.
“Angetaka Mwenyezi Mungu angemuumba binadamu kama malaika hawezi kufanya mabaya, maumbile yake ni kufanya mema tu; kwa hiyo halipwi kwa mema yake hayo kwani hayaonei taabu katika kuyafanya. Lakini binadamu ameumbwa kwa uweza wa yote mawili sawasawa na raha yake zaidi ni kufanya mabaya”
Aya hii na ufafanuzi wake, vinaeleza kuwa malaika wote wa Mungu wa Muhammad ni wema hakuna aliyekosa, na kuwa miongoni mwa malaika hao mmojawao ndiye aliyemtokea Muhammad na kumpa utume na ufunuo wa Qur’an. Sasa hebu tuchunguze kule pangoni alikokuweko Muhammad ili kupata utume alitokewa na kiumbe gani?. Tutaongozwa na vitabu vya dini ya Kiislamu.
Katika kitabu kiitwacho: Maisha Ya Nabii Muhammad s.a.w uk 16-17 kilichoandikwa na Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy, tunasoma kama ifuatavyo;-
Hata siku moja- katika mwezi wa Ramadhani mwezi 17, Jumatatu katika mwaka wa 40 ½ wa umri wake- mtume alimwona mtu kamsimamia mbele yake bila ya kumwona wapi katokea, akamwambia; “soma”. Mtume akamjibu; “Mimi sijui kusoma kwani sijapata kujifundisha kusoma.” Akaja akamkamata akambana, akamwambia tena; “soma,” Mtume akamjibu jawabu yake ileile. Hata mara ya tau akamwambia; “soma- Iqraa Bismi Rabbik.” Akamsomea sura hiyo ya 96 mpaka kati yake. Kisha mtume akaisoma kama alivyosomewa. Hii ndiyo sura ya kwanza kushuka katika Qur’an, ingawa haijawekwa mwanzo.
Mara, yule mtu (Malaika) akaondoka machoni mwake- asimwone kenda wapi. Na mtume naye akarejea kwake-khofu imemshika. Alipofika nyumbani, Bibi Kadhija alidhani ana homa, akamfunika maguo gubigubi na akakaa mbele yake akimsikiliza anavyoweweseka. Hata homa ilipomwachia alimweleza Bibi Kadhija yote yaliyomtokea; na Bibi Kadhija akamtuliza moyo wake, akamyakinishia ya kuwa hapana lolote baya litakalomzukia. Mara bibi huyu akaondoka akenda kwa jamaa yake – Bwana Waraqa bin Naufal- akampa habari yote iliyompata mumewe. Naye akamwamrisha amwite. Na mtume akenda akamweleza habari yake yote. Bwana Waraqa akamwambia; “ Huyo ndiye Jibril aliyemshukia Nabii Musa na Nabii Isa. Basi jibashirie kuwa wewe ni mtume wa umma huu, nami natamani kuwa hai nikuone unavyosimama kuwatengeneza jamaa zako; Inshaallah nitakuwa mkono wako wa kulia” Wakarejea kwao na khofu yote imemtoka”.
Alipokuwa pangoni alichezewa na Shetani: Katika kitabu kiitwacho “ Wakeze Mtume Wakubwa Na Wanawe” kilichoandikwa na Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy uk.12 tunasoma maneno haya
“Basi Mtume akafanya hofu akarejea kwa mkewe akamhadithia; na pale pale homa kubwa kabisa ikampanda akataka afunikwe maguo. Mara akawa anatetemeka kwa nderema na anaweweseka na kusema “Najikhofia nafsi yangu kuchezewa na shetani na kuniharibu akili yangu na kunizuga”. Bibi Khadija palepale alimdakiza akamwambia; “ Wacha hayo; Siyo yatakayokuwa hayo. Wewe huwezi kuchezewa na mashetani. Shetani hawezi kumchezea mtu mwenye sifa zako. Wewe unatazama vyema jamaa zako, unachukuwa mizigo ya hata watu wasiokuwa wako, unawadhihirishia watu sifa zako nzuri ambazo hakuna mwenye nazo. Unafanya hivi na unafanya hivi. Furahi ndugu yangu. Tua moyo wako, Wallahi! Mimi naona umekwishakuwa mtume”.
Katika tukio hili lililompata Muhammad akiwa pangoni , ndipo Waislamu wote ulimwenguni wanapolieleza kuwa hapo ndipo Muhammad s.a.w alipoletewa wahyi (ufunuo) na kupewa unabii na utume. Lakini unapotafakari juu ya ujumbe huo utaona kuwa hata yeye mwenyewe hajui nini kilichokuwa kimemtokea kule pangoni. Ndiyo maana tunasoma kuwa alipofika nyumbani kwake mkewe Bi. Khadija alimfunika nguo mumewe akidhani ana homa. Muhammad alimweleza mkewe kilichomtokea kuwa ni “Shetani” hakumsema malaika yeyote kama Waislamu wanavyotaka kutuaminisha leo. Kwa sababu kama angekuwa ni malaika kama tunavyosoma ndani ya Biblia ,asingesita kujitambulisha kwa Muhammad kuwa yeye ni nani. Hii ni hoja ya kwanza.
Hoja ya pili tunaona kuna mtu anaitwa Waraqah ibn Naufal, binamu yake na mke wa Muhammad s.a.w Bi Khadija. Yeye Waraqah anamwambia Muhammad huyo aliyekutokea ni malaika Jibril. Basi jibashirie kuwa wewe ni mtume wa umma huu !!!!! Je alikuweko pangoni wakati Muhammad s.a.w akitokewa na kiumbe asichokijua?.
Hoja ya tatu tunaona hata huyo mkewe Muhammad anamwambia mumewe utume huo !!!!!!! Je na yeye alikuweko pangoni? Kama hakuweko ni nani aliyemwambia kuwa yule ni malaika Jibril ikiwa Muhammad mwenyewe aliyetokewa alisema nimetokewa na Shetani? Tafakari
Katika kitabu kiitwacho Tafsir Al-Kashif, cha Muhammad Jawad Mughniyyah, uk74 paragrafu ya 7 inasomeka“ Hakuna njia ya kumjua Iblis, Shetani na Jini, isipokuwa kwa njia ya wahyi (ufunuo) tu”
Qurani Suratul Sad 38:69 Muhammad amenukuliwa akisema “Sikuwa na ilimu ya viumbe watukufu(Malaika)…
Kwa sababu ya Muhammad s.a.w kutowajua malaika kwake yeye anasema unapomwona punda akilia basi kamwona Shetani. Katika Kitabu kiitwacho Mkweli Mwaminifu, Juzuu 3-4 Hadith 789 uk 38 “ Punda akilia kamwona Shatani”
Jambo hilo ni tofauti na jinsi Biblia Takatifu inavyoeleza kuhusu punda. Mungu anaweza kumtumia hata punda kuongea na wanadamu ili kuwajulisha ujumbe wake. Katika kitabu cha Hesabu 22:22-31 tunasoma habari ya Balaamu jinsi Mungu alivyomtumia punda kumwambia Balaamu asiendelee na safari yake , baada ya punda huyo kumwona malaika wa Bwana akiwa ameshika upanga na amesimama mbele yao akiwa amezuia njia aliyotakiwa kupita. Punda alimwambia Balaamu ule msitari wa 30-31 “ Yule punda akamwambia Balaamu, Je mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema La!. Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu, akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa; naye akainama kichwa, akaanguka kifudufudi”
Inaonekana kwa tukio hili lililomtokea Balaamu, Mungu alimfunua macho yake akamwona malaika. Lakini kwa Muhammad yeye anachokiona ni Shetani tu. Na ndiyo maana anasema punda akilia amemwona Shetani
Kwa hiyo kama ufunuo wa Muhammad unaanza na Shetani kama vitabu sahihi vya dini ya Kiislamu vinavyoeleza, kwa mujibu wa ufafanuzi wa kitabu hicho cha Tafsir Al Kashif, inaonesha kwamba ufunuo, unabii na hata utume wa Muhammad una walakini mkubwa ukilinganisha na ujumbe wa manabii na mitume waliotajwa ndani ya Biblia Takatifu.
Katika Biblia shetani ametajwa kuwa anaweza kujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.
2 Wakorintho 11:13-15 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu, maana shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakajigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao”.
Muhammad akiwa Medina aliulizwa na Wayahudi ikiwa ufunuo wake umetoka kwa Mungu wa Kweli kwa kumtaka atoe sifa za manabii. Akijibu swali hilo alisema:
Mkweli Mwaminifu Juzuu 3-4 Uk.63.Hadithi Na. 880. “Kasema Mtume (s.a.w):- (Mambo) mane ya sheria za mitume (Kuwa na) na haya,na kujipaka mafuta mazuri,na kuowa (wake),na kupiga mswaki.
Hizi si sifa za Ki-Mungu kwa nabii na mtume bali ni za kibinadamu tu.
Manabii na watu mbalimbali katika Biblia hawakuona haya. Soma Isaya 50:7 “ Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimeukaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya”. Zaburi 34:5 “ Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya” Zab 119:46 “ Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu” Warumi 1:16 “ Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye kwa Myahudi kwanza , na kwa Myunani pia” 1Petro 4:16 “ Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.
Zaidi ya hayo tunaona Muhammad alirogwa. Kurogwa ni hali ya mtu kuathirika na nguvu za giza yaani uchawi.. Je nabii au mtume wa Mwenyezi Mungu wa Kweli anaweza kurogwa?
Katika Qur’an Suratul Ban-Israel, 17:47 “ Tunajua sana, sababu wanayosikiliza, na wanaponong’ona, wanaposema hao madhalimu. Nyinyi hamfuati isipokuwa mtu aliyerogwa”
Pia katika Suratul Falaq, 113:1-5 “ Ninajikinga kwa mola wa ulimwengu wote na shari ya Alivyoviumba, na shari ya giza la usiku liingiapo, na shari ya wale wanaopulizia (vivia) mafundoni (wakavunja) mashikamano yaliyo baina ya watu yaani shari ya mafatani, Na shari ya hasidi anapohusudu”
Tunasoma tukio hilo katika ufafanuzi wake uliyomo ndani ya Qur’an chapa ya nane uk.977 unaofafanua Sura ya 113-114 “Athari ya uchawi juu ya mtume (s.a.w). Swali la pili lijitokezalo kuhusu sura mbili hizi ni kwamba kwa mujibu wa hadithi uchawi ulifanywa dhidi ya mtume (s.a.w) naye akawa mgonjwa, na ili kuiondoa athari hiyo ya uchawi Jibril (a.s) alikuja na kumpa maelekezo Mtume (s.a.w) ya kusoma sura mbili hizi. Watafiti wengi zamani na wa sasa wamelifanyia upinzani jambo hilo, kwamba ikiwa hadithi zitakubaliwa, basi mfumo wote wa sharia utakuwa ni wa kutiliwa shaka, kwa sababu kama mtume (s.a.w) aliweza kuathirika kwa uchawi, na kwa mujibu wa hadithi hizi kweli uchawi huo ulionesha athari yake, basi hatuwezi kukaidi au kukana hadi kiwango gani maadui waliweza kumfanya Mtume (s.a.w) aseme na atende mambo kwa nguvu ya uchawi, na katika mafundisho yake mambo mangapi yatoka kwa Allah na mangapi yatokana na athari ya uchawi juu yake. Si hiyo tu, bali pia wasema kuwa baada ya kuyatambua hayo kuwa ni kweli katu haitawezekana hata kule kukaidi kuwa (s.a.w) alishawishiwa kudai utume kwa mauzauza ya kinjozi kuwa alimjia malaika. Pia wanasema hadithi hizi zapingana na Qur’an, na kama ilivyo katika Qur’an kuwa tuhuma hiyo batili kwa makafiri ilivyotajwa kuwa mtume s.a.w amerogwa naye ameathirika na uchawi: wanaposema hao madhalimu, ‘Ninyi hamumfuati isipokuwa mtu aliyerogwa’.” (17:47), lakini hadithi hizi zinathibitisha madai ya makafiri kuwa kwa kweli aliathirika na kuongozwa na uchawi……Kadri historia inavyohusika,ukweli kuwa kiasi fulani cha athari ya uchawi juu ya Mtume (s.a.w) ni hakika iliyothibiti; na kama kwa ustadi wa ubishi inawezekana kuthibitisha kuwa kweli.Limesimuliwa jambo hilo na Bukhari, Muslim, Nasai, Ibn Majah, Ahmad, ‘Abdur Razzaq, Humaid, Baihaqi, Tabarani, Ibn Sa’d, Ibn Marduyah, Ibn Abi Shaibah, Hakim, Abd bin Humaid na Muhadithina wengine toka kwa Bi. ‘Aisha (r.a), Zaid bin Arqam, Ibn ‘Abbas kupitia silsila nyingi mno kiasi kwamba jambo lenyewe limefikia hali ya ufululizo kamili, isipokuwa kila Hadithi, yenyewe ni ripoti kamili.
Hii ni uthibitisho mwingine mzito unaoonesha kuwa utume wa Muhammad una utata. Ikiwa na wao Waislamu kwa mujibu wa hadithi hizi hawajui ni mambo mangapi Muhammad aliyoyasema yanatoka kwa Allah na mangapi aliyasema akiwa ameshinikizwa na wachawi , Je ufunuo na utume wake utakuwa umetoka kwa Mungu wa Kweli? Tafakari !!1
Ndani ya Biblia Takatifu hakuma kurogwa kwa mtu wa Mungu. Hesabu 23:23 “ Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israel. Sasa habari za Yakobo na Israel zitasemwa , Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!”
Kwa mujibu wa kitabu cha Biblia Takatifu, manabii na mitume wa kweli wa Bwana Mungu wanatoka katika taifa la Israel.
Kitabu cha Ezekiel 13:9 “ Na mkono wangu utakuwa juu ya manabii wanaoona ubatili, na kutabiri uongo;hawatakuwa katika mashauri ya watu wangu, wala hawataandikwa katika maandiko ya nyumba ya Israel, wala hawataingia katika nchi ya Israel; Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU” .
Pia kwa mujibu wa kitabu cha Qur’an manabii na mitume ni lazima watoke kwa Yakobo ambaye ni mtoto wa Is-haqa ambaye naye ni mtoto wa Ibrahim. Qur’an Suratul Al-Ankabuut, (Buibui), 29:27 “ Na tulimpa (kumzaa nabii) Is-haqa na (kumjukuu nabii) Yakubu na tukauweka katika kizazi chake unabii na (kupata) kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye katika akhera kwa yakini atakuwa miongoni mwa watu wema”.
Aya hii, inaendelea kusisitiza kuwa ni kupitia kizazi cha Yakobo ndiko uliko unabii na kupata kitabu. Kwa bahati mbaya Muhammad ibn Abdullah, hatoki katika kizazi hicho wala kwa Ishmael kama wanavyodai Waislamu . Kwa sababu Ishmael ni Mwebrania kama baba yake mzee Ibrahim alivyo Mwebrania (Mwanzo 14:13) na Muhammad ni mwarabu kutoka kabila la Maqureysh. Kwa kutambua hilo ndipo tunamwoma Muhammad akiwaonya watu wengine wajiepushe na watu wa kabila lake.
Sahih Al-Bukhari Vol.1.Hadithi Na. 801 na Al-Lu’lu Kitabu cha 3. Uk.1089.Hadithi Na.1846 inasomeka“Hadithi ya Abu Huraira (r.a) amesema ,“Mtume wa Allah (s.a.w) amesema,Kabila hili la Makuraish litawateketeza watu.’ Wakauliza, ‘Unatushauri nini?’ Akasema, Nashauri watu wajitenge nalo.”
Kumzamisha nzi kwenye kinywaji
Bukhar vol. 4 Hadith 537 “ Narrated Abu Huraira: The Prophet said: If a house fly falls in the drink of any one of you, he should dip it (in the drink) for one of its wings has a disease and the other has the cure for the disease”
Tafsiri: Ilisimuliwa na Abu Huraira: Nabii alisema kama nzi akiangukia ndani ya kinywaji cha mmoja wenu, anapaswa kumzamisha kabisa (ndani ya kinywaji) kwa kuwa bawa lake moja lina ugonjwa na bawa lake jingine lina dawa
Mitume wa Yesu ndani ya Biblia Takatifu walikwisha kutuonya kuhusu uchafu huo. Katika 2 Kor 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu”
Miongoni mwa mafundisho ya Muhammad ni kwamba kuna mambo kumi yanayokamilisha Uislamu nayo tunayasoma katika kitabu kiitwacho Mkweli Mwaminifu , Kilichoandikwa na Sheikh Said Moosa Al-Kindy wa Muscut, Juzuu 3-4 Uk 63.Hadithi Na.880 “ Kasema Mtume (s.a.w) (Mambo) kumi ya Uislamu (yanayokamilisha Uislamu):Kukata masharubu,na kuziweka ndevu,nakuziweka ndevu (kutozinyoa) ndevu,na kupiga mswaki,kusafisha ndani ya pua kwa maji,na kukata kucha,kuosha mikono baina ya vidole,na kung’oa (au kunyoa) nywele za kwapani,na kunyoa nywele za mbeleni (mavuzi),na upungufu wa maji. La kumi,kasema sahaba aliepokea hadithi hii kuwa nimesahau,lakini kasema bila shaka la kumi ni “kutahiriwa.”
Kwa mujibu wa Biblia manabii na mitume wanathibitishwa kwa njia ya miujiza.
Kutoka 14:21” Musa akanyosha mkono wake juu ya bahari,BWANA akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki,usiku kucha,akaifanya bahari kuwa nchi kavu”.
Matendo 19:11-12 “Mungu alifanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida . Hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka”. Tazama pia Matendo 16:16-18, 20:7-12 na Matendo 13:6-12.
Qur’an nayo inathibitisha kuwa manabii na mitume ni lazima wafanye miujiza.
Qurani 40:78 Suratul Al-Muumini [Waumini] inasomeka “Na kwa yakini tumewatuma mitume kabla yako wengime katika wao tumekusimulia (majina yao na habari zao) na wengine hatukukusimulia na haikuwa kwa mtume yoyote kuleta muujiza wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu”
Muhammad hakupewa kufanya muujiza wowote ili kuthibitisha madai ya unabii na utume wake.
Qur’an 29:50 Suratul Al-Ankabuut (Buibui). “Na walisema “Mbona hakuteremshiwa miujiza kutoka kwa Mola wake? Sema miujiza iko kwa Mwenyezi Mungu tu (akitaka atakuteremshieni na kama hataki basi),nami hakika ni mwonyaji mbainishaji (dhahiri tu).” (Taz. Qur,an 6:35-37 13:7,)
Katika Qur’an iko aya ambayo tunapaswa tuitafakari wote kwa pamoja.Katika Surat An-Nisaa, (wanawake), 4:79 “Wema uliokufikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu na ubaya uliokufikia unatoka nafsini mwako, mwenyewe umefanya mambo hata yakakufika hayo. Nasi tumekupeleka kwa watu kuwa mtume na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kutosha (hapaitajiwi shahidi mwingine)”
Aya hii inaonesha kuwa Muhammad mtume wa Waislamu, alipelekwa kwa watu kuwa mtume, huku Mwenyezi Mungu akiwa shahidi tu. Siku zote shahidi si mtendaji bali ni mwonaji tu wa tendo lililotendeka.Hoja yetu tungependa kuwajua hao watu waliompeleka Muhammad kwa watu ni akina nani?. Kwa sababu tumeona kule nyuma baada ya Muhammad kutoka pangoni, mkewe Bi. Khadija anamwambia Muhammad kuwa “utume huo!!!!!!! Na Bwana Waraqah ibn Naufal akimwambia Muhammad kuwa “ basi jibashirie kuwa wewe ni mtume wa umma huu” kabla ya Qur’an .Je hao si wale “Nasi tumekupeleka” wanaotajwa kwenye aya hiyo hapo juu? Tafakari!! .
Waislamu hudai kuwa Muhammad ametumwa na Mwenyezi Mungu wao, ambaye ni Mfalme wa Wafalme . Lakini tusomapo Biblia Takatifu katika kitabu cha Ufunuo 17:14 “ Hawa watafanya vita na Mwanakondoo, na Mwanakondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme; na hao walio pamoja naye ndiyo walioitwa na wateule, na waaminifu”
Katika Ufunuo 19:11-16 “ Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa Neno la Mungu. Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA “
Yesu Kristo ndiye Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana.Lakini tunaposoma Hadithi sahihi za Kiislamu zinaeleza kuwa adui mkubwa wa Allah (s.w) Mungu wanayemwabudu Waislamu, ni yule anayeitwa Mfalme wa Wafalme.
Sahih Al- Bukhari, Vol.8.Hadithi Na.225, Al-Lu’lu Wal-marjan,Juzuu ya 3,Hadithi Na.1385 “Hadithi ya Abu Huraira (r.a) amesema,Mtume wa Allah (s.a.w) amesema,”Majina yaliyo dhalili mno na mabaya mbele za Allah ni mtu kujiita,Malikil-Amlaak (Mfalme wa Wafalme).”
Hivyo, ufunuo aliopokea Muhammad, ambao anatutaka na sisi Wakristo tuuamini haujatoka kwa Mungu tunayemwamini sisi Wakristo, yaani, Yesu Kristo.Bali kama alivyonukuliwa katika vitabu vya Kiislamu, unatokana na kuchezewa na Shetani, na kwa sababu hiyo kwetu anakuwa nabii na mtume wa uongo’
Biblia Takatifu imetuonya kuwachunguza mitume na manabii. Katika kitabu cha Ufunuo 2:1-2 “ Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao siyo ukawaona kuwa waongo”
Kwa mujibu wa aya hizi Muhammad s.a.w hastahili kuitwa nabii na mtume wa Mungu wa Kweli, bali anaangukia katika kundi la manabii na mitume wa uongo. Hatufai.
.
Wasiliana nasi kwa maswali, maoni au kutaka ushauri:
+255 755 680101,Email: www. Findtruefaith.blogspot.com , d_mwankemwa@yahoo.co.uk
Shalom,
Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo Mungu Mkuu. Tito 2:13
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WHAT DOES IT MEAN "THE WORD OF GOD IS GOD"?
WHAT DOES IT MEAN "THE WORD OF GOD IS GOD"? Dr. Maxwell Shimba explains: The Word and the Divine Nature – A Comprehensive Exposit...
TRENDING NOW
-
Baba umenipa funguo muhimu katika Mathayo 16:19 za kufunga na kufungua. Ninatumia funguo hizo kufunga na kufungua, kuvunja na kubamiza kil...
-
Kuna watu wanapitia mateso mengi sana, wengine wamefungwa katika vifungo bila wao kujijuwa basi chukua muongozo huu utakusaidia au itasaid...
-
Adui anakuja kuiba, kuua na kuharibu kila kitu chetu, ni lazima kuwa tayari kupambana na maadui, tujue silaha zetu, na kutumia neno la Mun...
-
Twakusalimu kwa mara ingine katika jina tukufu na takatifu la Yesu Kristo Bwana wetu. Twazidi pia kukushukuru kwa ajili ...
No comments:
Post a Comment