Friday, February 8, 2019

ASIYE NA DHAMBI AWE WA KWANZA KUTUPA JIWE

Image may contain: 1 person, text


Tuanze na kujifunza maana ya "Dhambi". Dhambi ni nini?

Dhambi ni tendo, hisia, au wazo lolote linalopingana na viwango vya Mungu. Inatia ndani kuvunja sheria za Mungu kwa kutenda mabaya, au ukosefu wa uadilifu, kwa maoni ya Mungu. (1 Yohana 3:4; 5:​17) Biblia pia inaeleza kuhusu dhambi ya kutofanya lililo sawa ingawa mtu anajua alipaswa kulifanya.​—Yakobo 4:​17.

Katika lugha za awali za Biblia, neno dhambi linamaanisha, “kukosa shabaha.” Kwa mfano, askari fulani katika Israeli la kale walikuwa na ustadi wa kutupa mawe kwa kombeo “bila kukosea.” Maneno hayo yanapotafsiriwa kihalisi yanamaanisha “bila kufanya dhambi.” (Waamuzi 20:16) Hivyo, kufanya dhambi ni kukosa shabaha ya viwango vikamilifu vya Mungu.

Kwa kuwa Mungu ndiye Muumba, ana haki ya kuwawekea wanadamu viwango. (Ufunuo 4:​11) Tunawajibika kwake kwa matendo yetu.​—Waroma 14:12.

Sasa tusome aya kutoka Biblia Takatifu Injili kutokana na Yohana Mlaongowa 8 aya ya 2 mpaka 11:

“2 Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. 3 na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”] (Yohana 8:2-11)

KWANINI MAFARISAYO WALIMLETEA HII KESI YESU KRISTO?

Kisa hiki ni maarufu sana katika Biblia. Hii ilikuwa ni mojawapo ya kesi ngumu iliyowasilishwa kwa Yesu ili kumjaribu wamwone atasemaje. Maandiko yanasema waziwazi ya kwamba nia ya washtaki wa mwanamke mzinzi kwenye kesi hii haikuwa nia njema ya kuzuia uvunjwaji wa sheria; bali waliitumia kesi hiyo kama kisingizio cha kumjaribu Yesu huku wakimtafutia “sababu ya kumshtaki Yesu”.

Yesu hali akijua hila zao, alinyamaza kimyaaaa. Tunasoma maandiko yakisema “nao walipozidi kumhoji”, yaani waliendelea kumshinikiza wakitaka atoe majibu kama anakubali sheria ichukue mkondo wake dhidi ya mwanamke mzinzi, au anapingana na sheria halali, ili wapate “sababu ya kumshtaki”. Mwishowe Yesu akatoa tamko lake akisema: “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe” kisha aliinama chini akaanza kuandika chini kwa kidole chake. Sasa hapa ndipo palipo na ujumbe kuhusu mada hii. Kwanini Yesu alisema yeye asiye na dhambi miongoni mwao awe wa kwanza kumtupia jiwe? Pili, alipoinama akaanza kuandika chini aliandika nini?

YESU ANAJUA YALIO NDANI YETU.

Kujibu swali la kwanza ni kwamba, Yesu kusema asiye na dhambi miongoni mwenu hakuwa na maana kwamba alikuwa anatafuta mtu asiye na dhambi kabisa miongoni mwao. Lugha asilia inasema Yesu aliwahoji kama kweli yupo mmoja kati yao ambaye “hajafanya dhambi yoyote iliyostahili hukumu ya kifo kama ya mwanamke mzinzi”. Yaani hakutaka wengi wasio na dhambi iliyostahili hukumu ya kifo, bali alitaka angalau hata mmoja tu kati yao asiyekuwa na dhambi inayostahili hukumu ya kifo!

Haya swali la pili, la alipoinama chini aliandika nini? Hakuna ushahidi wa kimaandiko ya kwamba aliandika nini chini. Lakini baadhi ya wataalamu wa tafsiri za maandiko ya kale wanasema alikuwa akiandika orodha ya dhambi zilizostahili hukumu ya kifo ambapo kila mmoja alisoma dhambi yake na kuamua kuondoka bila kuaga kuanzia mzee mpaka mtu wa mwisho.

ORODHA YA DHAMBI ZILIZOSTAHILI HUKUMU YA KIFO

Kimsingi, ni kweli ya kwamba katika Agano la Kale, ambalo lilikuwa na katiba (torati) iliyozingatia utawala wa sheria, lilidhibiti uhalifu na makosa ya jinai kwa adhabu kali kuanzia kupigwa viboko mpaka hukumu ya kifo cha kupigwa mawe.

Zilikuwepo zaidi ya sheria kumi na nne ambazo makosa yake yalistahili hukumu ya adhabu ya kifo. Baadhi yake ni kama hizi zifuatazo: Dhambi ya kuua kwa kukusudia ( Kutoka 21:12-14; Mambo ya Walawi 24:17,21), dhambi ya kushambulia au kulaani mzazi (Kutoka 21:15,17), Kutokutii wazazi (Kumbukumbu la Torati 21:18-21); biashara ya binadamu(Kutoka 21:16), mifugo ya wanyama ikishambulia na kuua watu na mwenye mifugo asizuie maafa hayo (Kutoka 21:28-29); dhambi ya uchawi (Kutoka 22:18; Mambo ya Walawi 20:27), Kutoa kafara binadamu (Mambo ya Walawi 20:2-5); Kufanya ngono na mnyama (Kutoka 22:19, Mambo ya Walawi 20:16), kufanya kazi siku ya Sabato (Kutoka 31:14; 35:2; Hesabu 15:32-36); Kuzini (Mambo ya Walawi 20:10; Kumbukumbu la Torati 22:22), ushoga na ulawiti (Mambo ya Walawi 20:13), Binti ya kuhani akifanya ukahaba (Law.21:9); Dhambi ya kukufuru (Mambo ya Walawi 24:14,16,23), dhambi ya kumwasi kuhani (Kumbukumbu la Torati 17:12).

WOTE SISI NI WATENDA DHAMBI

Haya tukirejea kwenye hoja ya msingi ya jibu la Yesu kwa waandishi na mafarisayo akiwataka kama yuko hata mmoja asiyekuwa na dhambi iliyostahili hukumu ya kifo sawa na ile waliyokuwa wakimshtakia yule mwanamke mzinzi; na wote wakaondoka bila kuaga, hiyo ikathibitisha waziwazi ya kwamba, hapakuwepo hata mmoja ambaye alistahili kumhukumu yule mwanamke mzinzi.

Kumbe wote walikuwa wamefanya dhambi mbali mbali zilizostahili nao wapigwe mawe kama yule mwanamke mzinzi. Inawezekana kweli hapakuwepo mzinzi kama yule mwanamke, lakini walikuwa na dhambi nyingine zinazostahili hukumu yenye uzito ule ule sawa na mwanamke mzinzi!

Biblia ndicho kitabu pekee chenye kuhukumu kwa haki bila upendeleo wala ubaguzi. Neno la Mungu katika Biblia halina unafiki wala hila ndani yake. Tunapolisoma na lenyewe linnatusoma na kutuhukumu dhamiri zetu hata kama tutajifanya hatuna hatia kwa nje. Biblia imeandika waziwazi ya kwamba: “Kwa sababu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;..” (Rum.3:23); na kisha imeandikwa ya kwamba: “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti;..” (Warumi 6:23)

KUKUBALI KOSA KABLA YA KUSAMEHEWA.

Mwanamke aliyefumaniwa uzinzi,alijikubali kwamba amefanya kosa,ndio maana tunaona hakujibu chochote cha kujitetea mbele za Yesu. Sababu kama asingekubali kosa lake angeliweza kujitetea,lakini alikaa kimya hata akasamehewa.

Mara nyingi sisi tunajihesabia haki penye makosa.

Yeye mwenye kujihesabia haki hali ni mdhambi,hawezi kupokea msamaha wa kweli. Kwa sababu kanuni ya kusamehewa ni lazima mmoja akubali makosa yake ndipo msamaha uachiliwe na msamaha wa namna hii uwa na nguvu sana.

YESU KRISTO ANAYO AMRI DUNIANI YA KUSAMEHE DHAMBI.

Imeandikwa;

“ Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. “Luka 5:24

Hakuna mwanadamu anayepaswa kumuhukumu mwanadamu mwenzake kwa sababu ya dhambi aliyotenda sababu mwenye kuhukumu ni Mungu mwenyewe.

KAMA HAKUNA ALIYEKUHUMU HATA MIMI SIKUHUKUMU

Sasa tumefika kwenye kiini cha ujumbe wa leo. Baada ya washtaki wote kukimbia na mwanamke mzinzi kuachwa peke yake, ndipo Yesu alipomwuliza kama hakuna hata mmoja aliyejitokeza kumhukumu kuwa na hatia, na mwanamke akasema hakuna. Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu”!

Kumbuka ya kwamba, kwa viwango vya kimaadili, ni Yesu peke yake ambaye hakuwa na dhambi hata moja. Kwa hiyo, kibinadamu Yesu ndiye aliyestahili kumhukumu huyu mwanamke mzinzi. Lakini pasipo kutarajia mwanamke mzinzi alishangazwa na kauli ya Yesu pale alipotamkiwa “uhuru wa kuishi” tena. “Wala mimi sikuhukumu”

Swali ni kwanini Yesu hakumhukumu mwanamke mzinzi wakati Yesu alisema alikuja kuitimiliza torati? Hivi kumwachia huru sio kuendeleza uzinzi badala ya kuudhibiti? Majibu ya maswali haya yapo ndani ya tafsiri ya jina la Yesu mwenyewe ambalo ndilo lilibeba utume wa kuja kwake duniani:

“Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” (Yohana 3:17)

Bila shaka hapa unaweza kubaini ya kwamba, Yesu kutokumhukumu mwanamke mzinzi alikuwa akitekeleza utume aliotumwa na Baba yake. Kuokoa na sio kuhukumu! Kuokoa na sio kuhukumu! Hili lilitabiriwa na malaika Gabrieli kuhusu kazi ya jina la Yesu kama tusomavyo:

“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” ( Mathayo 1:21)

ENENDA ZAKO USITENDE DHAMBI TENA

Kwa hiyo, maana ya “kutokuhumu” sio “kubariki maovu” yaendelee kushamiri pasipo udhibiti. “Kutokuhukumu” kwa mujibu wa Yesu maana yake ni kumpa nafasi nyingine (second chance) mwenye dhambi aweze kujirekebisha kitabia baada ya kufutiwa makosa yake bure na Yesu Kristo. Na ndivyo Yesu alivyofanya kwa yule mwanamke mzinzi: “Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”

Kauli ya “usitende dhambi tena” ni kiashiria cha kufutiwa dhambi zilizokwisha kufanywa nyuma, na kwamba inawezekana kuishi pasipo kutenda dhambi tena baada ya kukutana na Yesu ana kwa ana kama mwanamke yule mzinzi!

Mpendwa msomaji wangu. Kabla hutujatoa hukumu dhidi ya wakosaji wengine miongoni mwetu, hebu tujihoji kwanza kama sisi wenyewe pia tuna hatia katika maisha yetu ya faragha. Ukijikuta nawe una hatia katika eneo lolote hata kama watu wengine hawajui ukweli wa dhambi zako za siri, basi uzuie ulimi wako kutoa hukumu dhidi ya dhambi za wengine.

Hii haina maana mtu akikosea asiambiwe ukweli wa makosa yake kwa nia ya kumshawishi ajirekebishe. Kinachokatazwa ni kumtakia hukumu ya adhabu ambayo ikikugeukia wewe hutaifurahia. Jifunze kusamehe bila masharti. Lakini kama dhamiri yako inakuhukumu kwa dhambi zako, ufumbuzi wake ni kumkaribisha Yesu Kristo katika maisha yako na kumwomba akujaze Roho Mtakatifu atakayekusaidia kuishi maisha mapya ya utakaso wa kweli.

Kama ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like post hii, wajulishe marafiki zako kuhusu page hii pia. Mungu akulinde na kukubariki kwa wingi wa fadhili zake katika jina la Yesu, AMINA!!

Shalom

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW