Saturday, January 26, 2019

JINSI YA KUMPENDA NA KUMTHAMINI MKEO KWA KUTUMIA BIBLIA

Image may contain: 2 people, people smiling, text and outdoor

Je, unajua mambo yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke?

Waefeso 5:25, 28-29 
“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa”

Mume kumpenda mke ni agizo. Agizo hili halibadiliki mke akiwa mkorofi, sio mtii au vyovyote vile. Biblia inamuagiza mume ampende mke kama Kristo alivyolipenda Kanisa. Huu ni upendo mkubwa sana, japokuwa kanisa lilikengeuka mbali naye bado upendo wa Kristo haukubadilika. Kumpenda mwanamke kama mwili wako mwenyewe, kumjali na kumtunza.

Akiwaandikia waume Wakristo kuhusu jinsi wanavyopaswa kuwatendea wake zao, Petro, mwandikaji aliyeongozwa na roho, aliwahimiza waige mtazamo wa Mungu na Yesu Kristo. ‘Enyi waume, endeleeni kuwapa heshima,’ akaandika. (1 Petro 3:7) Kumpa mtu heshima hutoa wazo la kwamba unamthamini na kumheshimu sana. Hivyo, mtu anayemheshimu mke wake hamwaibishi, hamshushii heshima, au kumtendea kwa jeuri. Badala yake, yeye huonyesha kwa maneno na matendo, hadharani na faraghani, kwamba anamthamini na kumpenda.

Tunaweza kupataje picha kamili ya jinsi ambavyo Mungu Mungu huwaona wanawake?

Njia moja ni kwa kuchunguza mtazamo na mwenendo wa Yesu Kristo, kwani yeye ndiye “mfano wa Mungu asiyeonekana,” naye huonyesha kikamili maoni ya Mungu kuhusu mambo mbalimbali. (Wakolosai 1:15) Jinsi ambavyo Yesu aliwatendea wanawake katika siku zake huonyesha kwamba Mungu anawaheshimu wanawake na hawaungi mkono kamwe ukatili dhidi ya wanawake ambao umeenea sana katika nchi nyingi leo.

Wanaume wengi wanaamini wanawake, kwa kawaida, ‘wanapenda hela.’ Kwamba ukiweza kumhakikishia mwanamke 'uhakika wa kiuchumi' unakuwa umemaliza. Ingawa hatuwezi kupuuza ukweli kuwa uhakika wa 'kiuchumi' ni moja wapo ya mahitaji ya mwanamke, lakini si sahihi kuamini kuwa moyo wa mwanamke unaweza kuthamanishwa kwa fedha.

Fikra hizi walizonazo wanaume [kuwa anachokihitaji mwanamke ni fedha] zimeleta matatizo mengi katika mahusiano na ndoa. Kwa mfano, wapo wanaume ambao baada ya kuhakikisha wenzi wao wamepata mahitaji ya msingi, basi wanawatelekeza kihisia. Hali hii husababisha upweke mkubwa kwa wanawake hawa wanaojikuta hawana mtu wa karibu kuwasikiliza isipokuwa vitu.

Upweke, kwa hakika, huzaa migogoro isiyokwisha inayowafanya wanaume [ambao kimsingi ndio wasababishi wa upweke huo] washindwe kuwaelewa wanawake. Kwa mtazamo wao, ni vigumu kumridhisha mwanamke. Wengine wanaenda mbali na kufikiri , 'mwanamke ni kiumbe mgumu kueleweka' kwa sababu, ‘hata ufanye nini...hata umpe nini hawezi kuridhika’.
Lakini wanachosahau wanaume wenye mawazo haya ni kuwa mwanamke kwa asili yake anayo mahitaji ya msingi ambayo yanapopuuzwa, chochote kinachofanyika kama mbadala wa mahitaji hayo hakiwezi kuwa na maana yoyote. Usipoweza kujua mahitaji yake halisi, unaweza kumpa chochote kile unachodhani anakihitaji na bado mambo yasiende kama unavyotamani iwe.

Kusema hivyo, haimaanishi sielewi kuwa wapo wanawake wengi wanaopenda kujipatia fedha kwa wanaume. Hawa ni wanawake wanaofanya biashara ya mahusiano. Kwao, hakuna sababu yoyote ya kuwa na uhusiano imara na wenzi wao isipokuwa mpangilio wa kujipatia vitu na fedha.
Hatuzungumzii uhusiano huo wa kibiashara kati ya mwanamume na mwanamke bali uhusiano wa dhati unaojengwa katika misingi ya upendo, uaminifu, kuelewana na ahadi ya kuwa pamoja katika dhiki na raha.
Hebu na tutazame mahitaji makubwa ya kihisia aliyonayo mwanamke mwenye upendo wa dhati kwa mwenzi wake.

JINSI MUNGU ANAVYO WAPENDA WANAWAKE

Masimulizi mbalimbali yanayoonyesha jinsi Mungu alivyotenda kwa niaba ya wanawake yanathibitisha kwamba anawajali waabudu wake wanawake. Mara mbili aliingilia kati ili kumlinda Sara asilalwe kinguvu. (Mwanzo 12:14-20; 20:1-7) Mungu alimpendelea Lea, mke wa Yakobo ambaye hakupendwa sana, kwa ‘kufungua tumbo lake la uzazi,’ naye akazaa mwana. (Mwanzo 29:31, 32) Wazalishaji wawili Waisraeli ambao walimwogopa Mungu walipohatarisha uhai wao ili kuwalinda watoto wa kiume Waebrania wasiuawe huko Misri, Mungu alionyesha uthamini wake kwa ‘kuwapa familia.’ (Kutoka 1:17, 20, 21) Pia alijibu sala ya Hana ambayo alitoa kwa bidii. (1 Samweli 1:10, 20) Na mjane wa nabii fulani alipokabiliwa na mkopeshaji ambaye alitaka kuchukua watoto wake kuwa watumwa ili kulipia deni lake, Mungu hakumwacha. Kwa upendo, Mungu alimwezesha nabii Elisha aongeze mafuta yake ili alipe deni, na bado abaki na mafuta ya kutosha kwa ajili ya familia yake. Hivyo akahifadhi familia yake na heshima yake.—Kutoka 22:22, 23; 2 Wafalme 4:1-7.

Mara nyingi manabii walishutumu zoea la kuwatumia vibaya wanawake au kuwatendea jeuri. Nabii Yeremia aliwaambia hivi Waisraeli katika jina la Mungu: “Toeni haki na uadilifu, nanyi mumkomboe yeye anayenyang’anywa kutoka mkononi mwa mpunjaji; wala msimtendee vibaya mkaaji mgeni yeyote, mvulana asiye na baba au mjane. Msiwatendee jeuri yoyote. Wala msimwage damu yoyote isiyo na hatia mahali hapa.” (Yeremia 22:2, 3) Baadaye, matajiri na wenye mamlaka katika Israeli walishutumiwa kwa sababu ya kuwafukuza wanawake kutoka nyumbani mwao na kuwatendea watoto wao kwa ukatili. (Mika 2:9) Mungu wa haki huona na kushutumu uovu huo ambao wanawake na watoto wao hutendewa.

MPENDE MKEO KWA VITENDO

Kumpenda mke wako zaidi ya kitu chochote iwe ni wazazi, kazi, biashara, watoto n.k. Mume mwema siku zote huthamini nafasi ya mke katika maisha yake na mara zote mke wake ni namba moja kwake.

Mwanzo 2:24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

Waefeso 5: 25,28 Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake,..vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

Ni rahisi sana kwa mwanamke kuonyesha utii pale anapoonyeshwa upendo. Wanaume wengi huonyesha upendo wakiwa wanachumbia ila wakishaoa tu wanajisahau na kusahau kama mke anahitaji upendo ili aweze kutimiliza majukumu yake kama mke vizuri kwa furaha. Upendo unaanzia kumjali hisia zake, kumtunza kimahitaji na kumtia moyo, kumsifia na kumuonyesha unamthamini.

Tulishaona kuwa hadhi ya mwanaume inategemea kwa kiasi kikubwa namna anavyoheshimiwa. Kwa mwanamke hali ni tofauti. Hadhi yake inategemea namna anavyopendwa na mwenzi wake.

Upendo kwa mwanamke unaeleweka anapoambiwa bila kuchoka na kuthibitishiwa kwa kutendewa vitendo kuwa anapendwa. Katika lugha ya kiingereza, hapa tungetumia neno affection, yaani matendo yanayoonesha mapenzi kwake.

Hata hivyo, lugha ya mapenzi hutegemea mambo mengi. Kuna athari za utamaduni, desturi na imani zilizopo katika jamii aliyokulia mwanamke. Hata hivyo, yapo matendo yaliyothibitika kuvuka mipaka ya kiutamaduni.

Mfano, kumwambia mwanamke unampenda mara nyingi iwezekanavyo, ni hitaji la msingi. Kwa mwanamume, kuambiwa anapendwa inaweza isiwe jambo la maana, lakini si kwa mwanamke. Mwanamke anatamani kusikia mara nyingi kadri inavyowezekana kuwa anapendwa.

Pia kuna vitu kama kupewa zawadi asizotarajia, kutumia muda wa mapumziko pamoja nae, kutoka naye kwenda mbali na nyumbani na mambo kama hayo yanayoonesha kuwa kweli unampenda.

Ndio kusema, ikiwa unataka kuugusa moyo wa mwanamke, akupe heshima unayoihitaji kama mwanaume, unawajibika kujua vitu gani mahususi ukimfanyia vinatuma ujumbe wa wazi kuwa unampenda. Usipoweza kumfanya mwanamke ajisikie kupendwa, anapoteza hamu ya uhusiano. Huchoka kihisia na anaweza kufanya mambo yasiyotarajiwa ili tu kuhujumu mahusiano.

Huruma nyororo ya Yesu kwa watu ilionyeshwa kwa namna alivyoshughulikia wanawake. Katika pindi moja mwanamke fulani aliyekuwa ameteseka kutokana na mtiririko wa damu kwa miaka 12 alijitahidi kumtafuta Yesu kati ya umati. Hali yake ilimfanya asiwe safi kidesturi, kwa hiyo yeye hakupaswa awe huko. (Mambo ya Walawi 15:25-27) Lakini alikuwa amehitaji msaada sana hivi kwamba akaenda nyuma ya Yesu kimya-kimya.

JINSI YESU ALIVYO WATENDEA WEMA WANAWAKE

Mwanamke huyo alipogusa vazi la Yesu, yeye aliponywa mara moja! Hata ingawa Yesu alikuwa njiani kwenda katika nyumba ya Yairo, ambaye binti yake alikuwa mgonjwa mahututi, Yesu alitua. Akiwa amehisi nguvu ikimtoka, yeye alitazama huku na huku ili amwone yule aliyekuwa amemgusa. Hatimaye, yule mwanamke akaja na kuanguka mbele yake akitetemeka. Je, Yesu angemkemea kwa ajili ya kuwa kati ya huo umati au kwa ajili ya kugusa vazi lake bila ruhusa yake? Kinyume cha hilo, mwanamke huyo alimwona Yesu kuwa mchangamfu na mwenye fadhili sana. “Binti,” yeye akasema, “imani yako imekuponya.” Huo ulikuwa wakati pekee ambao Yesu alimwita mwanamke “binti” moja kwa moja. Ni lazima neno hilo liwe lilistarehesha moyo wa mwanamke huyo kama nini!—Mathayo 9:18-22; Marko 5:21-34.

Yesu aliona zaidi kupita yale ambayo Sheria ilisema. Yeye aliona maana yayo hasa na uhitaji wa rehema na huruma. (Linganisha Mathayo 23:23.) Yesu aliona hali ya kuhitaji msaada sana ya mwanamke huyo mgonjwa akafahamu kwamba yeye alikuwa amechochewa na imani. Kwa njia hiyo yeye aliwawekea kielelezo kizuri wanaume Wakristo, hasa waangalizi. Ikiwa dada Mkristo anakabili matatizo ya kibinafsi au hali ngumu au yenye kujaribu sana, wazee wa kutaniko wapaswa kujaribu kuona zaidi ya maneno na matendo ya sasa hivi na kufahamu hali na madhumuni. Ufahamu huo wenye kina huenda ukaonyesha kwamba subira, uelewevu, na huruma vinahitajiwa badala ya shauri na usahihisho.—Mithali 10:19; 16:23; 19:11.

Yesu alipinga mapokeo ya kirabi naye alistahi heshima ya wanawake si kwa matendo yake pekee bali pia kwa mafundisho yake. Kwa kielelezo, fikiria yale aliyofundisha juu ya talaka na uzinzi.

Kuhusu talaka, Yesu aliulizwa swali hili: “Je! ni halali mtu kumwacha [“kutaliki,”] mkewe kwa kila sababu?” Kulingana na simulizi la Marko, Yesu alisema hivi: “Yeyote yule atalikiye mke wake [isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati] na kuoa mwingine afanya uzinzi dhidi ya mke, na ikitukia wakati wowote mwanamke, baada ya kutaliki mume wake, aolewa na mwingine, yeye afanya uzinzi.” (Marko 10:10-12, NW; Mathayo 19:3, 9) Maneno hayo yenye kusemwa kwa usahili yalionyesha staha kwa heshima ya wanawake. Jinsi gani?

MKE WAKO NI KIPAUMBELE CHAKO

Wajibu wa kuonyesha heshima si kwa waume peke yao. Ingawa mume apaswa kumheshimu mke wake kwa kumtendea kwa upendo na kwa heshima, mke apaswa kumheshimu mume wake kwa kuwa mwenye kujitiisha na kuonyesha staha nyingi. (1 Petro 3:1-6) Zaidi ya hayo, Paulo aliwaonya Wakristo kwa upole, ‘waonyeshane heshima.’ (Warumi 12:10) Huo ni wito kwa wanaume na wanawake kutanikoni kutumikia pamoja kwa kustahiana.

Mwanamke hapendi kujikuta katika mazingira ya kushindania nafasi ya kwanza na kitu kingine chochote iwe ni kazi, mtu au chochote kile unachokipenda wewe mwanamume.

Tulishaona kuwa kwa mwanaume, hadhi yake hutegemea zaidi namna uwezo wake unavyotambuliwa. Hali hiyo humfanya mwanamume atumie muda mwingi kufanya mambo yanaweza kumpa heshima katika jamii. Inaweza kuwa kazi, biashara, mamlaka na namna zozote zile zinazomwongezea uwezo.

Lakini wakati anapotumia muda mwingi katika mambo hayo, ni rahisi kuonekana ameyafanya mambo mengine kuwa ya muhimu kuliko uhusiano wake na mwenzi wake. Wanawake wengi hawapendi kujikuta katika hali hii. Hapa ndiko iliko tofauti.

Mwanamke hatamani kuwa kwenye nafasi ya ‘mengineyo’, ‘ziada’, ‘baadae’ ‘nikipata muda’. Unapomweka 'akiba' mwanamke hawezi kufurahia kwa sababu anatamani awe kipaumbele chako.

Waefeso 5:23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe; kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.

Mambo mengi huthibitisha kuwa umempa nafasi ya kwanza. Mfano kuwa na muda wa kuwa naye mara nyingi kadri inavyowezekana, kuahirisha mambo mengine ya muhimu kwa ajili yake, kuwahi miadi unapoahidi kukutana nae, kuwasiliana naye kwa karibu na mambo kama hayo. Unaposhindwa kufanya hivyo, mwanamke hupata ujumbe kuwa yeye ni mtu wa ziada baada ya mambo ya muhimu.
Kadhalika, ili kumwambia yeye ni kipaumbele, mwanamke anatamani kila unapoongea nae akili yako yote iko pamoja naye. Kuwa pamoja naye maana yake ni kuachana na vyote vinavyokuondolea uzingativu na kumsikiliza kwa makini.

Mwanamke anatamani unapozungumza naye ufuatilie anachokisema, umpe mrejesho kuwa unamwelewa na uonesha kuwa mwili, akili, hisia ziko pamoja naye kumsikiliza. Vinginevyo, mwanamke anakuoana kama hujaweza kumpa nafasi yake anayoistahili.

Tangu wanadamu wafanye dhambi na kupoteza ukamilifu, wanawake katika utamaduni mbalimbali wamevunjiwa heshima. Wametendewa vibaya kimwili, kiakili, na kingono. Lakini Mungu hakukusudia watendewe kwa njia hiyo. Biblia inaonyesha wazi kwamba haidhuru maoni ya kidesturi ambayo yanashikiliwa na watu wengi, wanawake wote wanapaswa kutendewa kwa staha na heshima. Ni haki yao kutoka kwa Mungu.

Mume anapoonyesha kumsikikiza na kujali ushauri wa mkewe na kushauriana naye kabla hajafanya jambo lolote mke anaona anapendwa sana na yeye atazidisha upendo na heshima kwa mumewe. Mpende mkeo ili aweze kukuheshimu kwa furaha na sio kwa kujilazimisha. Kumpenda mke ni kujipenda mwenyewe. Mara moja moja mtoe out bila watoto na umueleze unavyompenda, zawadi sio lazima siku ya sherehe au kitu kikubwa, hata chocolate(unanunua kwa ajili yake na sio watoto), mke atahisi kupendwa sana.

1Petro 3:7 Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.

Shalom,

Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo Mungu Mkuu. Tito 2:13

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW