Friday, July 14, 2017

JE’ BWANA YESU ANAPATAJE KUWA MUNGU?







UKWELI KUHUSU UUNGU WA YESU

JE’ BWANA YESU ANAPATAJE KUWA MUNGU?

Baada ya kujipatia maarifa makini juu ya nafsi tatu Mungu mmoja;
Ni vyema sasa tukapiga hatua nyingine ya ufahamu kwa kuangalia swali hili makini ambalo kwa kiasi kikubwa pia huchanganya hisia za watu wengi katika ulimwengu wa imani, ambapo kile kinachoonekana kuwachanganya watu wengi hapa ni uelewa juu ya ukweli kuhusu chimbuko la Uungu wa Bwana Yesu na hivyo watu wengi kuhoji kuwa Yesu anapataje sasa kuwa Mungu?.
Ni wazi kuwa swali hili hasa hulenga kutafut kujua asili au chimbuko la mamlaka ya Kiuungu ya Yesu anayotajwa kuwa nayo hasa kutokana na kile kinachoonekana kuwa Bwana Yesu alikuwa na mwonekano unaoonyesha kuwa huenda naye alikuwa na asili au chimbuko la dunia hii.
Hivyo ili kupata majibu ya msingi ya hili ni vyema kwanza tuanze na hoja juu ya asili ya Yesu na ndipo tunaweza kufunguka zaidi kiufahamu na kuelewa mengi zaidi juu ukweli kuhusu Uungu wa Yesu.
Ufahamu juu ya asili ya Yesu
Kile kilichoongeza upinzani mkubwa wa Mafarisayo na baadhi ya Wayahudi juu ya Uungu wa Yesu ni uelewa usiyo sahihi juu ya asili ya Yesu.
Ufahamu wa wengi kati ya Wayahudi uligotea katika dhana ya mwonekano wa ubinadamu wa Yesu na historia yake ya uzazi wa kidunia toka katika tumbo la Mariam, ambapo kama matokeo ya hili Wayahudi walisikika wakati fulani wakitamka:-
Yahana 6:42
Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni?
Unaweza sasa kupata pichani juu ya mzizi wa hoja hii, na ni kama tunavyoona katika nukuu hiyo ya kitabu cha Yohana kuwa hoja kuu ya Wayahudi ilikuwa ni kile walichoona kuwa haikuwa sahihi kwa Yesu kusema ameshuka toka mbinguni maana kile wao wanachojua ni kuwa alizaliwa na bi’Mariam na baba yake ni Yusufu kwahivyo asili yake ni duniani tu.
Hivyo kwa hali hiyo iliwapa ugumu kukubali pale Yesu alipojitaja kuwa na asili ya mbinguni na kimsingi ndicho kilichokuwa chanzo kikubwa cha upinzani wao dhidi ya matamko ya Yesu.
Habu ona tena hoja ya Wayahudi pale Yesu alipoeleza uwepo wake wa milele’
Yohana 8: 56-58
Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi.57 Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu? 58 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.
Katika andiko hilo tena Wayahudi walipingana na Yesu kutokana na tamko lake lililoonyesha uhusiano wake na ukaribu na mzee Ibrahimu, kitendo ambacho kilifanya Wayahudi hao kumhoji kwa madai kuwa yeye ni kijana mdogo hasiyepata hata miaka hamsini anawezaje kuwa amemwona Ibrahimu?, na ndipo Yesu anajibu na kuwaambia bayana kuwa uwepo wake ni wa kabla ya Ibrahimu’ 58 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.
Hivyo kwa mtazamo wangu binafsi ninaona kuwa tatizo la Wayahudi au wale wanaopinga Uungu wa Yesu kwasababu ya ubinadamu alokuwa nao au sababu ya kuzaliwa na Mariam tatizo lao kuu si hilo bali zaidi ni kutolewa kabisa msingi mzima wa asili ya Yesu kabla ya kuzaliwa kwake na Mariam.
Je’ Asili ya Yesu ni wapi?
Katika kujibu swali hili Bwana Yesu mwenyewe mara kadhaa aliwaelimisha Wayahudi juu ya ukweli kuhusu asili yake ili kuwasaidia kuondokana na dhana au mtazamo wa kumchukulia kama mtu mwenye asili ya kidunia na badala yake alitaka waone kuwa yeye alikuwako kabla ya kuja duniani kama mwanadamu kwa kusudi la ukombozi wa watu. Soma kwa makini maandiko haya:-
Yohana 8:23
Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu
Yahana 6:62
Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza?
Katika maandiko hayo yote mawili, Bwana Yesu kwa uwazi kabisa anaweka bayana juu ya asili yake ya mbinguni kabla ya kufanyika mwanadamu na kuzaliwa na bi’ Mariam, katika andiko lile la kwanza Bwana Yesu anaweka utaofauti wa wazi baina yake na wanadamu wa kawaida kwa kusema ‘Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
Na katika tamko jingine Yesu anawauliza Wayahudi kuwa Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza?, kwahivyo Yesu anaonyesha kuwa kabla ya ujio wake duniani kuna mahali (mbinguni) alikokuwako kwanza.
Asili ya Yesu na msingi wa mamlaka yake ya Uungu
Uelewa juu ya asili ya Yesu linakuwa ni jambo rahisi tu sasa kadri ya msingi mzuri tuloujenga tangu mwanzo wa uchanbuzi wa mada hii na hususani kupitia matamko mbalimbali hata yale ya Yesu mwenyewe yanayotoa picha ya wazi kuwa Yesu hakuwa kamwe na asili ya dunia hii ya ubinadamu licha ya kwamba alizaliwa na Mariam kwakuwa pale alipozaliwa na Mariam haukua ndiyo mwanzo wa kuwepo kwakwe, bali kupitia kuzaliwa na Mariam alikuwa tu akitengenezewa njia ya kufunika mamlaka yake ya kuu ili aweze kumfikia mwanadamu kama tutakavyoona katika kipengele kinachofuata.
Hatahivyo kanuni za msingi zinazofanya Yesu kuwa mwanadamu wa asili ya kawaida hazikufikiwa katika mchakato wa kuzaliwa kwake, hebu tusome kidogo andiko hili’
Mathayo 1:18
Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Hivyo kuzaliwa kwa Yesu kunatofautiana kabisa na kanuni ya kawaida ya uzazi wa wanadamu wengine ambapo kadri ya andiko hilo Biblia inaweka bayana kuwa Mariam alipata mimba ya kumzaa Yesu kabla hajakaribiana na mwanamume na yakuwa mimba hiyo ni kwa uwezo wa roho mtakatifu.
Kwa hali hiyo katika uzazi wa Yesu hapakuwepo kamwe na mfumo wa kawaida wa kibaolojia unaohusisha hatua mbalimbali za Kisayansi za uzazi kama ambavyo hata maandiko ya Qur an yanavyoainisha katika sura mojawapo ya kitabu cha msaafu wa Qur an kama tunavyosoma hapo chini:-
Qur an 22:5
Enyi watu! Kama mumo katika shaka juu ya ufufuo; (mnaona haimkiniki kufufuliwa), basi (tazameni namna Tulivyokuumbeni); kwa hakika Tulikuumbeni kwa udongo. (Mzee wenu Nabii Adamu),kisha (Tukawa Tunakuumbeni ninyi) kwa manii, (mbegu ya uhai)
Msahafu wa Qur an hapo unaweka bayana hatua hizo za uumbaji na inazitaja kama kanuni zilizo na zinazotumika kuibua mwanadamu na kuendeleza kizazi cha wanadamu huyo, ambapo njia hizo mbili yaani ile awali ya kuumbwa kwa udongo (Nabii Adam na Hawa) na ile ya mbegu ya uzazi (Viumbe wengine).
Hivyo Yesu alizaliwa kipindi ambacho mfumo wa kupatikana kwa mwanadamu au kiumbe cha kawaida unapaswa kuhusisha jinsia mbili za wanadamu ambao hujamiiana na hatimaye mama hutunga mimba na kuzaa binadamu mwingine wa kawaida baada ya miezi tisa ya kubeta ujauzito kama sayansi inavyoeleza kwa upana zaidi:-
‘Sexual reproduction is a process that creates a new organism by combining the genetic material of two organisms; and this is followed by exchange of genetic information (a process called genetic recombination). After the new recombinant chromosome is formed it is passed on to progeny.’
Uzazi wa kujamiiana ni hatua inayoumba kiumbe kipya kwa njia ya kukutanisha viini vya uzazi vya pande mbili za viumbe hai; na hili linafuata baada ya mbadilishano wa taarifa baina ya viini vya uzazi (mchakato huu hutambulika kama muunganiko wa kiuzazi). Baada ya muunganiko mpya nyuzi zenye jeni za urithi wa tabia za maumbile katika kiini cha seli hutengenezwa na kupita katika homoni za kike ambazo huwezesha hali ya uzazi katika uterasi na kukuza kiini tete.(na hatua mbalimbali huendelea hadi kuzaliwa kiumbe).’
Hivyo kwajumla kiumbe kingine hutokea kwa kanuni hiyo tu ya mmunganiko wa seli za uzazi toka pande zote mbili za jinsia yaani toka kwa baba na kwa mama tendo ambalo kamwe halikufanyika katika hatua za kuzaliwa kwa Bwana Yesu na hivyo kuibua tafakari kubwa juu ya asili yake na mamlaka yake hasa.
Na hivyo katika sehemu hii tutakwenda moja kwa moja katika maandiko ya msingi ili kupata ufumbuzi kamili juu ya mamlaka hasa ya asili ya Bwana Yesu na kwa hali hiyo basi nivyema kwanza kujenga msingi wa hili kupitia maelezo ya ya mtume Yohana:-
Yohana 1:1
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu 2’ Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
Ni wazi msomaji wangu kuwa’ sasa unaweza kuanza kupata nuru baada ya kusoma andiko hilo la Injili ya Yohana ambapo kwa uwazi kabisa mtume Yohana kwa msaada wa Roho Mtakatifu anabainisha msingi wa asili ya Yesu na kumtaja dhahiri Bwana Yesu kuwa ndiye ‘Neno’ aliyekuwako mbinguni ,na kimsingi ndiye mhusika wa kazi nzima ya uumbaji.
Na kama utakumbuka vizuri ndugu msomaji wangu hapo nyuma nilishazungumzia kwa upana kabisa juu ya utendaji wa Mungu katika nafsi tatu za milele Mungu mmoja, ambapo Neno (Mwana)’ni miongoni mwa nafsi hizo:-
Hivyo kwa hali hiyo mtume Yohana anaweka bayana na kumtambulisha Neno huyo kwamba alikuwa ni Bwana Yesu mwenyewe kabla hajafanyika mwanadamu. Rejea maelezo ya aya ya 14’ ya Injili ya Yohana sura ya 1’.
14’Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Aya hiyo ya 14’ inataja wazi kuwa Neno huyo ni Yesu ambaye hatimaye alifanyika mwili na kukaa kwetu ndipo kwa kuonekana katika utukufu ikaonekana kuwa ni mwana pekee atokaye kwa Baba. (Tutaliona hilo mbele).
Na kwa msingi huo basi Biblia inaweka bayana kuwa Bwana Yesu yeye alikuwako kabla ya Ulimwengu huu kuwako na kama ni msomaji mzuri wa Biblia utagundua kwamba hata Yesu mwenyewe katika matamko yake mbalimbali ameweka bayana swala hili la kuwepo kwake mbinguni katika umoja wa Mungu naye akiwa ni nafsi ile ya Neno. Hebu tusome wote aya hii:
Yohana 17:5
Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.
Hapo Bwana Yesu mwenyewe anatamka wazi kuwa alikuwako kabla ya ulimwengu kuwako na zaidi ya yote anaonyesha kuwa alikuwa katika umoja wa utendaji na umiliki na nafsi ya Baba na hivyo utagundua kwamba maelezo hayo yanawiyana sawia na yale aliyowahi kuyatoa mbele ya Wayahudi na kupelekea Wayahudi hao kuadhimu kumpiga kwa mawe kwakuwa waligundua kuwa kwa kutamka hivyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye kiasili ana mamlaka ya Kiuungu kiasili. Reje aya hiyo hapo chini:-
Yohana 10:30-33
Mimi na Baba tu umoja.31 Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige.32 Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?33 Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.
Pamoja na hayo kipengele muhimu sana katika aya ile ya Yohana 1:1, ni kile kinachotaja bayana juu ya mamlaka aliyokuwa nayo Bwana Yesu akiwa mbinguni kwa kusema:- (rejea sehemu ya mwisho ya aya ya kwanza’)
Yohana 1:1……naye Neno alikuwa Mungu.
Hapa mtume Yohana anataja wazi kabisa juu ya nafasi hasa ya kimamlaka aliyokuwa nayo Bwana Yesu akiwa mbinguni kwamba alikuwa katika mamlaka kamili ya Uungu.
Kimsingi hiyo ndiyo mamlaka halisi ya Bwana Yesu kama inavyowekwa bayana katika mafungu lukuki ndani ya Biblia kama tulivyoanza kuona katika maandiko hayo ya awali na yale tutakayoendelea kuyapitia katika vipengele mbalimbali vya uchambuzi wa mada hii.
Vinginevyo katika andiko hilo la Yohana 1;1-3 huwa ninasikia hoja fulani ikijengwa ambayo ninatamani kuiweka wazi pamoja na kuipatia majibu mafupi ili kuondoa chachu inayojaribu kuwekwa na baadhi ya walimu wenye lengo la kuhafifisha maana ya msingi ya andiko hilo ili kupingana na ukweli huu.
Hoja inayaojengwa hapo ni ile yenye lengo la kupingana maelezo ya andiko hilo juu ya kuwepo kwa Neno aliyekuwako kwa Mungu naye kuwa Mungu, na katika kupingana na maelezo hayo ya wazi ya andiko wamekuwa wakiweka mfano kwa kudai kuwa kuyakubali maelezo hayo ya andiko la Yohana ni sawa na kusema:- (Yohana 1:1-3)
“Hapo mwanzo kulikuwa na kistuli, nacho kistuli kilikuwa kwa fundi, nacho kistuli kilikuwa fundi’“
Hivyo kwa mfano huo unaowekwa na baadhi ya walimu katika ulimwengu wa imani zetu ndipo wafuasi na baadhi ya waamini wa dini hizo hujikuta wakitiwa moyo na kupinga kwa nguvu zote juu ya ukweli huu wa mamlaka ya Yesu ya Uungu.
Jibu la msingi la hoja hii’
Endapo utachunguza kwa makini juu ya hoja hii utagundua kuwa ni hoja ndogo sana hasa ukiwa na utulivu wa kiakili na kuanza kwanza kwa kuuchunguza mfano wenyewe unaotumiwa ambapo utagundua kuwa mfano huo umechanganya dhana mbili zisizopaswa kuchanganywa, dhana hizo zilizochanganywa ni ile ya kunasibisha Neno na Mungu na kielelezo cha Kistuli na Fundi pasina kujali kuwa kistuli ni mti na fundi ni mtu na hivyo haviwezi kuakisi dhana ya umoja tofauti na uhusiano na umoja wa kiasili uliyopo baina ya Neno na Mungu.
Hivyo ni vyema ikaeleka kuwa uhusiano uliyopo baina ya Neno na Mungu kamwe hauwezi kulinganishwa na fundi na kistuli na badala yake ungeweza kulinganishwa na uhusiano wa Kistuli na Mti’ , na kwa hali hiyo mfano ambao ungeweza kutumika ni ule wa kusema:- (Yohana 1;1-3).
“Hapo mwanzo kulikuwako na Kistuli, nacho Kistuli kilikuwa kwa Mti, nacho Kistuli kilikuwa Mti.”
Mfano huo ndiyo unaoweza kuwiyana na andiko hilo la Yohana kwakuwa kimsingi unahusisha dhana mbili zinazowiyana (Kistuli na Mti) na hivyo kuakisi msingi halisi na mantiki ya maelezo ya andiko lile la Injili ya Yohana.
Hivyo kwajumla mfano unaotumiwa na walimu hao si sahihi na kwa lugha nyingine ni kumaanisha kuwa Neno na Mungu ni mamlaka zisizoweza kutenganishwa kiasili, kama ambavyo huwezi kutenganisha kati ya kistuli na mti maana kimsingi asili ya kistuli ni mti kama ambavyo asili ya Yesu ni Uungu.
Kama Yesu ni Mungu kwanini azaliwe na kuvaa mwili wa kibinadamu?
Baada ya hoja na maswali mengi tuliyokwisha yapitia juu ya uhalali wa Uungu wa Yesu ndipo swali hili hufuatia ambapo hoja ya msingi hapa ni juu ya kile kinachoonekana kama kitu kisichowezekana kwa Yesu kuwa na asili ya Uungu na huku akiwa na umbile la kibinadamu umbile ambalo alilipata kwa njia ya kuzaliwa na Mariam, na kimsingi hapa ndipo mahali maswali mengi zaidi hujitokeza.
Kwanini kama ni Mungu avae ubinadamu?
Tendo la dhambi ya Adamu na Hawa lilimuingiza mwanadamu katika deni kubwa lisiloweza kulipwa na mwanadamu mwenyewe hebu tusome:-
Mwanzo 3:17
Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
Kwa kadri ya Andiko hilo tunasoma kuwa Mungu alipomuweka Adamu na Hawa katika bustani ya edeni aliwapa masharti yahusuyo ulaji ambapo wanadamu hao walikatazwa kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, lakini mbali na kukatazwa huko pia walionyeshwa hasara ambayo wangeipata kama matokeo ya kukaidi agizo hilo la kula matunda hayo ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Kwa uwazi kabisa Mungu aliwaambia juu ya hatari hiyo ambayo wangejiingiza kwayo kuwa ilikuwa ni kifo’ (siku utakapokula utakufa hakika) kwahivyo kimsingi tendo la wazazi hao kujiingiza katika tendo hilo la dhambi ilikuwa ni sawa na kujiingiza katika deni la dhambi ambalo malipo yake ni mauti (kifo).
Na kwa hali hiyo basi mwanadamu huyu alihitaji msaada wa kunasuliwa toka katika deni hilo la dhambi, hivyo ilipasa upande wa pili unaoweza kukabili deni hilo kujitokeza ili kumsaidia mwanadamu kwakuwa kimsingi hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kukabili deni la kifo maana liko nje ya uwezo wa mwanadamu kama Daudi anavyoeleza:-
Zaburi 49:7-8
Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake,8 (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;)
Hilo ni tamko la wazi la Biblia likibainisha kuwa kamwe mwanadamu hawezi kujiokoa au kumwokoa jirani yake kwakuwa nafsi ya mwanadamu inagharama ambayo haiwezi kulipwa na mwanadamu mwenyewe.
Hivyo kwa hali hiyo swali la msingi hapa linaloibuka ni kuwa sasa ni mamlaka gani yenye uwezo huo wa kulipa deni hilo la mauti na hivyo kumnusuru mwanadamu?. Ili kupata urahisi katika kujibu swali hili jambo la msingi hapa ni kuangalia sifa za msingi za mamlaka inayoweza kufanya kazi hiyo ambapo kimsingi sifa hizo ni lazima zihusiane na:-
- Uwezo wa kuasisi uhai (kuumba).
- Mamlaka dhidi ya kifo (mauti).
Kadiri ya sifa hizi ninaamini haitakuwa jambo la kufikiri kwa muda mrefu kuwa jukumu hili la ukombozi linaangukia kwa nani hasa kutokana na ukweli kuwa sifa hizo zote zinaonekana kwa Bwana Yesu na jambo jema ni kuwa vitabu vyote vya dini vinathibitisha ukweli huo hebu tuchunguze.
Uwezo wa kuasisi uhai (kuumba).
kwa upande wa Biblia tulishaona kupitia kitabu cha Mtume Yohana akiweka wazi kuwa Yesu (Neno) ni muumbaji wa vitu vyote…rejea Yohana 1:3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
Katika vitabu vingine vya kidini dhana ya uumbaji wa Yesu au uwezo wa kuasisi uhai huwekwa wazi ingawa kwa upande mwingine huelezwa kuwa Yesu naye aliwezeshwa na mamlaka nyingine kuwa na uwezo huo wa kuumba, hebu tulione hilo kwa upana wake katika Qur an tukufu:-
Qur-an 3:49
na atamfanya mtume kwa wana wa Israel awaambie nimekujieni na hoja kutoka kwa mola wenu ya kuwa “ninakuumbieni”katika udongo kama sura ya ndege kisha “nampulizia” mara anakuwa ndege kwa “Idhini” ya Mwenyezi Mungu …
Andiko hilo la msahafu kwanza linaweka wazi ukweli huo kuwa Bwana Yesu katika maisha yake ya utumishi aliwahi kufanya tendo hilo la kuasisi uhai kwa kuumba ndege kwa udongo na hatimaye kumpulizia pumzi ya uhai na mara ndege huyo akawa hai ambapo Qur an humalizia kwa kuonyesha kuwa alifanya hayo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu tamko ambalo bado haliondoi uzito wa kuhusika kwa Bwana Yesu katika jukumu hilo la kuasisi viumbe linalomhusu Mwenyezi Mungu peke yake.
Tukiacha kujadili hoja hiyo inayojitokeza hapo bado wazo la msingi la Bwana Yesu kuhusika na uumbaji ndilo linalobeba msingi mzima wa aya hiyo ya Qur an kwa kuweka wazi ushiriki wake katika kazi hiyo mahsusi ya uumbaji na kwa hivyo anaingia katika sifa ya kuhusika kuasisi viumbe.
Katika hili kile kinachofanya uzito zaidi ni umaalumu wa tendo lenyewe la uumbaji ambalo kamwe Mungu hawezi kulifanya kwa kuhusisha mamlaka nyingine katika hatua nyeti za uumbaji kama tunavyosoma katika maandiko kadhaa toka vitabu vyote vya dini;-
Isaya 44:24
BWANA, Mkombozi wako, yeye aliye kuumba tumboni asema hivi, mimi ni Bwana, nifanyaye vitu vyote: nizitandazaye mbingu peke yangu: niienezaye nchi ni nani aliye pamoja nami?
Hapo Mungu mwenyewe anaonyesha jinsi tendo hilo la uumbaji lilivyo rasmi sana na yakuwa si tendo tu analoweza kuhusishwa kiumbe tu wa kawaida kushiriki mamlaka hiyo ya uasisi wa viumbe kwa kuwa kimsingi muasisi wa viumbe huwa juu ya viumbe hivyo.
Na katika kuonyesha uzito wa hilo maandiko ya msahafu tena huonyesha kuwa uumbaji ni mojawapo ya sifa muhimu inayompa Mungu vigezo na haki ya kuombwa na wanadamu katika mahitaji yao ya kilasiku, hivyo uumbaji ni ishara ya uwezo na haki ya kimamlaka ya Mungu.
Qur-an surat Al-hajj 22:73
Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni, hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu hawawezi kuumba (hata) nzi …
Hivyo kwa muktaza huu tutakubaliana kuwa tendo hilo la Yesu kutajwa kuhusika na mamlaka ya uumbaji linampa Bwana Yesu haki ya msingi ya kustahili kuhusika na jukumu la ukombozi wa mwanadamu kwakuwa uwezo huo wa Yesu wa uumbaji unatoa picha juu ya uwezo wake hata katika jukumu la kukomboa.
Mamlaka dhidi ya Kifo (mauti).
Jambo jingine la msingi juu ya sifa za yule anayeweza kuvaa jukumu hilo la kumkomboa mwanadamu ni hili la uwezo dhidi ya nguvu ya mauti na kifo, katika hili pia tunaona jinsi Bwana Yesu anavyohusika moja kwa moja kwa kile kinachoonekana katika maandiko ya vitabu vyote yakimtaja Bwana Yesu kuwa na uwezo wa kufufua watu waliokufa ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kushinda mauti na kufufuka:-
Qur-an 3:49
…Na ninawaponyesha vipofu na wenyewe mabalanga, na ninawafufua (baadhi ya) waliokufa, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu…….
Katika andiko hilo la Qur an zinatajwa sifa nyingine za Bwana Yesu kuwa pamoja na mambo sifa nyingine aliki pia alikuwa na uwezo wa kuponya vipofu na wakoma lakini zaidi sana Qur an inaweka wapi pia kuwa Bwana Yesu (Isa) alikuwa na uwezo wa kufufua watu waliokufa.
Sifa hii ya kufufua hubeba dhana nzima ya ushiriki wa Bwana Yesu katika jukumu la kubatilisha matokeo ya dhambi yanayozaa kifo na hivyo kuwa na sauti dhidi ya nguvu ya mauti kwa kuamuru kurejea kwa uhai kwa mtu aliyepoteza uhai huo.
Mkazo zaidi juu ya hili katika maandiko ya Biblia:-
Yahana 11:25
Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;
Hilo ni mojawapo kati ya matamko aliyowahi kuyatoa Bwana Yesu akionyesha mamlaka aliyonayo juu ya mauti na kwajumla Bwana Yesu anaonyesha hapo kuwa yeye ndiye mwenye dhamana na jukumu zima la kuwafufua wanadamu katika siku ya mwisho.
Kumbuka pia maandiko ya Biblia yanaweka bayana kuwa ukombozi dhidi ya hukumu ya mauti hauwezi kutolewa na mamlaka yeyote ile isipokuwa Mungu mwenyewe ndiye mwenye njia za kumnusuru mwanadamu dhidi ya mauti, tunaweza kuyasoma maneno hayo katika maandiko ya Biblia toka katika kitabu cha nabii Daudi:-
Zaburi 68:20
Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.
Hivyo wajibu wa kukomboa wanadamu kwa mujibu wa Biblia unatajwa kuwa ni wa kimbingu na hivyo kuhusika na Mwenyezi Mungu mwenyewe tendo ambalo linakaza wazo la ujio wa Yesu kwaajili ya ukombozi
Yesu alishuka kama mwanadamu toka asili ya Uungu ili kutukomboa’
Ninaamini kwa msingi huo wa maandiko tumepata ushahidi wa kutosha jinsi Bwana Yesu anavyostahili kuhusika na jukumu hili la ukombozi wa mwanadamu kwa kuwa kimsingi jukumu hilo la ukombozi wa mwanadamu lazima lifanywe na mtu mwenye sifa hizo mbili muhimu yaani ile ya uwezo wa kuasisi uhai pamoja na kurejesha uhai uliotoka.
Na kama hatua ya utekelezaji wa jukumu hilo ndipo ilimladhimu Bwana Yesu kufunika utukufu wa mamlaka yake ya kiungu ili kushuka na kutukomboa tendo ambalo ndilo linaibua hoja hii ya kudai kuwa Mungu hawezi kuzaliwa na kuonekana katika umbile la kibinadamu.
Lakini Katika kujibu swali hili ni vyema kwanza tujenge msingi kwa kusoma maandiko kadhaa katika mafunuo ya Biblia na hatimaye tupate maoni ya vitabu vingine ili kukaza uelewa wa mada hii nyeti.
Hebu tupitie maandiko haya yafuatayo:-
Kutoka 33:20
Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.
Katika andiko hilo la kwanza tunapata msingi wa uchambuzi wa mada hii kwa tamko hilo la Mungu akimweleza nabii Musa kuwa kamwe mwanadamu hawezi kumwona Mungu bayana akaishi.
Hivyo andiko hilo linazalisha madai muhimu kwa Mwenyezi Mungu katika jukumu lake la kushuka ili kumkomboa mwanadamu, madai ambayo yanaitaka mbingu kubuni kanuni ya kumfikia mwanadamu huyu kwa namna ambayo haitomwangamiza na badala yake kumwokoa.
Na kwa hali hiyo swali la msingi linalojitokeza hapa ni kuwa sasa’ ni kwa namna gani basi Mungu anaweza kumfikia mwanadamu huyu pasina mwanadamu huyo kuangamia kama matokeo ya kukabili uwepo wa Mungu wa ana kwa ana? Ili kujibu swali hilo nikuombe tusome maandiko haya yafuatayo:-
Ebrania 2:16-17
Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu.17Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.
Biblia hapo inatoa majibu ya swali hilo la msingi kwa kutajwa dhahili kuwa asili au hali ambayo Mungu angeitwaa katika kutekeleza jukumu hilo ni asili ya ubinadamu na pia inaeleza kuwa katika utekelezaji wa jukumu hilo ilikuwa ni lazima Yesu kuchukua hali ya mfanano na wanadamu nadipo hatimaye aweze kufanikisha jukumu hilo la kuleta suluhu ya dhambi kwa watu wake.
Kisa cha mama msamaria’
Kulikuwa na mama mmoja msamaria, mama huyu alikuwa akiishi eneo la baridi kali..siku moja alipokuwa akiota moto ndani katika nyumba yake ya vioo ndipo akaona ndege kwa nje’,ndege huyu alikuwa katika hali ya kuelekea kufa kutokana na baridi ingawa hatimaye ndege huyo alitimiza hatua ya kwanza ya furaha ya mama huyo kwa kutua kwenye mti mkubwa ulioota nje ya dirisha dogo la nyumba yake, na ndipo mama huyu akachukua mti mwingine mrefu anaoutumia kuchochea moto ndani na kuupitisha kwenye dirisha hilo ili ukaungane na ule wa nje na kutengeneza daraja na hatimaye kumwezesha ndege huyo kupita na kuingia ndani ili kujinusuru’…lakini ndege huyo alipoona mti huo ukichomoza toka kwenye dirisha hilo alihofu kwa kufikiri kuwa huenda ni mtu anayetaka kumpiga ili hatimaye kumfanya kitoweo na kwasababu hiyo ndege huyo aliruka na kutokomea kwenye baridi zaidi na hatimaye akafa huko’
Tamko la mama msamaria, alibaki kusema:- Laiti kama ningelikuwa na uwezo wa kujimithilisha’ nikawa mfano wa yule ndege’ ningelimsogelea na kumwambia’ ndege wenzangu eeeeh twende mule ndani tujinusuru na baridi!!!!!!
Kisa hicho kinaweka mkazo na kutoa mwangaza juu umuhimu wa tendo hilo la Bwana Yesu kuvaa umbile la kibinadamu katika harakati za kumfikia na kumwokoa mwanadamu, ambapo tunaona jinsi ambavyo haikuwa rahisi kwa mama msamaria kufanikisha dhamili yake ya kumwokoa yule ndege kwa njia ya kutumia mti ambao kimsingi kwa ndege huyo ulikuwa ni kitisho.
Kumbuka kuwa endapo Bwana Yesu angelikuja katika halihalisi ya utumkufu wake wa Kimungu wanadamu wangelihofu na kuangamia kama ambavyo tunaweza kuliona hilo katika mifano kadhaa ya matukio katika Biblia, soma historia hii ya kipindi cha wana wa Israel kwa utulivu:-
Kutoka 19:11-12
wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. 18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.19 Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.20 Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu. 21 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa Bwana kutazama,kisha wengi miongoni mwao wakaangamia.
Katika andiko hilo tunaona historia hiyo ya kile kilichowapata wana wa Israel ambao kimsingi walitoa madai ya kutaka kuonana na Mungu, na katika tukio hilo la kushuka kwa Mwenyezi Mungu ili kujifunua kwao wa Israel wengi walikufa kutokana na Mungu huyo kuja katika hali ambayo hawakuweza kuikabili.
Swali! Je’ Mungu aje katika hali gani ili mwadamu aweze kuikabili?
- Aje katika hali ya ng’ombe!
- Au aje katika hali ya simba! Au hali gani?
Biblia inataja namna Mungu alivyojidhihirisha kwa Kristo katika hali ambayo mwanadamu aliweza kuikabili.
1Timotheo 3:16
Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.
Hivyo maandiko hayo ya Biblia yantaja njia hiyo ambayo Mungu aliitumia kujidhihirisha kwa wanadamu yaani kwa kutwaa mwili wa kibinadamu ingawa haki yake ilijulikana katika ulimwengu wa roho.
Maelezo ya vitabu vingine, je’ Mungu anaweza kuja katika maumbile tofauti?
Kabla ya kuhitimisha kipengele hiki ni vyema tukapata kwanza maoni toka katika vitabu vingine vya kidini ili kukaza uelewa wa uchambuzi huu na pengine kufungua zaidi ufahamu wa masomaji wangu ikiwa huenda si Mkristo.
Katika hatua ya awali maandiko ya msahafu wa Qur an yanataja sifa za Mwenyezi ambazo zitaanza kutujengea msingi wa uchambuzi katika kipengele hiki:-
Qur an 57:3
Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, Naye ndiye wa Dhahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kilakitu.
Andiko hilo linataja sifa hizo za msingi za Mungu ambapo moja ya sifa hizo ni ile Dhahiri na Siri, kupitia sifa hizi tunapata uthibitisho wa dhana nzima ya utendaji wa Mwenyezi Mungu katika hali mbalimbali yaani kwanza katika hali yake ya kutoonekana (Siri) na ile ya kujifunua Dhahiri na jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa maandiko ya Qur an tukufu yameweka mifano muhimu juu ya aina zote hizi za mifumo ya utendaji wa Mwenyezi Mungu ambapo kwa mfano ile hali ya dhahiri inaonekana katika kisa cha nabii Musa kama tunavyosoma:-
Qur an 20:9-12
Na je imekujia hadithi ya Musa? 10’alipouona moto, akawaambia watu wake (aliokuwa nao) “Ngojeni, hakika nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga katika huo (moto)au nitapata mwongozaji katika moto huo (wakutuonyesha njia).11’ Basi alipofika akaitwa “Ewe Musa! 12’”Bilashaka Mimi ndiye Mola wako.Basi vua viatu vyako.hakika wewe uko katika bonde takatifu la Tuwa.
Hapo tunaona katika kisa hicho cha Nabii Musa kutokewa Mungu anajifunua kwa Musa kupitia kichaka cha moto ambapo Musa kwa kutojua anadhani hicho ni kichaka cha moto wa kawaidia tu na kumbe kichaka hicho kilikuja na uwepo wa Mungu, hivyo Musa kwa kukiona kichaka hicho alipaswa kukubali kuwa hapo alikutana na Mungu bayana. Rejea tamko la Mungu mwenyewe’ “Bilashaka mimi ndiye Mola wako”.
Je Mungu anazaliwa ikiwa alikuja kama mwanadamu?
Kimsingi Mungu yeye kama Mungu hazaliwi na hakuwahi kuzaliwa kamwe, ila kile kinachotajwa kuzaliwa na Mariam ni ubinadamu wa Yesu tu ambao ulizaliwa ili kufunika Uungu ambao kuwepo kwake ni tangu milele. Na kwa hivyo Mariam hakuzaa Uungu bali alizaa ubinadamu uliobeba Uungu, kwakuwa kusema kwamba Mariam alizaa Uungu wenyewe ni sawa na kusema kuwa Mungu ana mwanzo wa kuwepo kwake yaani alianza kuwako mara tu baada ya kuzaliwa na Mariam na kwa hali hiyo Mungu ana umri maalumu na mwanzo wa kuwepo kwake tendo ambalo linapingana na maelekezo tunayoyapata katika maandiko matakatifu:-
Zaburi 102:24-27
Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.25 Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako.26 Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika.27 Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma.
Na ili kukaza uelewa wa hili tunaweza kuona maelezo ya Yesu mwenyewe juu ya hili katika mjadala wake na Wayahudi pindi walipopingana na tamko la Yesu kujihusianisha na Ibrahimu ambapo Wayahudi walimkumbusha umri wake tangu alipozaliwa na Mariam na kutumia kigezo hicho kukosoa madai ya Yesu juu ya mahusiano yake na Ibrahimu hebu tusome majibu ya Yesu:-
Yohana 8:55
Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi.57 Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?
58 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.
Hilo ndilo tamko la Bwana Yesu akibainisha kuwa uwepo wake katika nyanja ya Kiuungu usingepaswa kuwekwa katika vipimo vya miaka ya kibinadamu maana kwa hali halisi yeye alikuwapo hata kabla ya Ibrahimu.
Hivyo kwa muktaza huu haitakuwa sahihi kusema kuwa Mariam ni mama wa Mungu kwakuwa neno lenyewe mama tu humaanisha mzazi (mlezi) hivyo ni kusema kwamba Mariam ni mzazi au mlezi wa Mungu tendo ambalo ni kufuru na ni kosa la wazi la kutotendea haki maandiko matakatifu.
Mifano michache juu ya uwezekano wa Mungu kutwaa ubinadamu.
Ni jambo linalonishangaza sana ninapoona hali ya upinzani juu ya ukweli huu ili hali ziko simulizi mbalimbali ambazo zingeweza kutumika kama vielelezo muhimu vya kurahisisha uelewa wa jambo hili, hebu ona mfano wa kisa hiki kinachosimuliwa na watu wengi majini dare s salaam:
Kijana mmoja alikuwa akipita njiani na kukutana na binti mzuri aliyetokea kumpenda, na ndipo baada ya maongezi binti huyo alikubali kwenda kupafahamu nyumbani kwa kijana huyo’ baada ya kufika na wakiwa wameketi ukumbini ndipo kijana huyo akamuomba yule binti ampatie rimoti ya TV iliyokuwa mbele kidogo upande wake na kwa namna ya kutisha binti huyo badala ya kuinuka na kwenda kuchukua rimoti hiyo alifyatua tu mkono wake ulioonekana kurefuka kupita kiasi na kuichukua rimoti hiyo. Kwa hali hiyo upendo uliishia hapo na kijana huyo kupiga kichwa mlango na kutoka nje kwa hofu na hatimaye kuzimia mlangoni.
Watu wengi wanaosimulia kisa hicho huonekana kufanya hivyo wakiamini kabisa kuwa huyo alikuwa ni jini aliyebeba taswira ya kibinadamu,na hivyo kile kinachonishangaza ni namna watu wanavyoweza kuamini kuwa shetani anaweza kujibadili ili kutesa watu lakini kwa nguvu zote hupingana na swala la Mungu kuvaa ubinadamu ili kutukomboa’ tafakari upya na badili mtazamo.
Bwana Yesu alichukua ubinadamu ili kumkaribia mwanadamu na hatimaye kusaidia ili aweze kuokolewa, Mtume Yohana alitamka:-
Yohana 1:14
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Hivyo kusudi la yesu kufanyika mwili na kukaa kwetu ndilo lingepaswa kupokelewa kwa shukrani zaidi maana lilileta utukufu kwa wanadamu tofauti na matukio tunayoshabikia juu ya viumbe vibaya. Tendo hilo la yesu kukaa kwetu (baada ya kuvaa mwili huo) linatajwa katika lugha ya Kigiriki kama:
Eskenosen’ ambayo maana yake ni kupiga kambi ( English – ‘Tent’/ dwelt among us).
Pamoja na uchambuzi wa Biblia ni jambo lililonifurahisha sana kuona katika vitabu vingine vinavyoaminiwa sana katika ulimwengu wa imani hususani msahafu wa Qur an kuona kielelezo muhimu juu ya dhana nzima ya mabadiliko yanayoweza kufanyika kwa hali moja kuchukua hali nyingine kwa lengo Fulani muhimu, mfano wa hili ni kisa cha Malaika aliyemtokea Mariam kwa nia ya kutotaka kumwogofya Mariam aliamua kubadili maumbile yake alipomtokea. Hebu tusome katika maandiko:-
Qur an 19:17
Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea muhuisha Sharia Yetu (Jibrili) akajimithilisha kwake (kwa sura ya ) binaadamu aliyekamili .
Kama nilivyotangulia kueleza kuwa hicho ni kisa cha Malaika Jibril ambaye alimtokea Mariam kadri inavyoelezwa na kuaminiwa na ndugu zetu wa Kiislam yakuwa Malaika huyo alimtokea kwa umbile la kibinadamu, hivyo swali la kutafakari hapo ni kuwa kama Malaika tu aliweza kubadili umbile na kuja katika hali hiyo je Mungu anawezaje kushindwa?
Hivyo ukweli nikuwa Bwana Yesu alitwaa umbile hilo kwa lengo la kufunika utukufu wake ambao mwanadamu asingeweza kuukabili , andiko la mtume Paulo la Wakoritho linatuhitimishia sehemu hii ya uchambuzi.
2Wakoritho 5:18-19
Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Hivyo ieleweke kuwa umbile la kibinadamu la Yesu ndani yake lilibeba mamlaka kamili ya Uungu, mamlaka ambayo ilikuwepo tangu milele na hata kabla ya kuzaliwa kwa ubinadamu wa Yesu na Mariam.
Kama ni Mungu mbona alisema anaenda kwa Baba yake?
Hii nayo ni miongoni mwa hoja tete katika Ulimwengu wa imani ambapo kile kinachohojiwa hapo ni tendo la Yesu kuonekana mara kadhaa akitaja habari ya Baba katika mazungumzo yake kwa nyakati na matukio tofauti na hivyo kuibua hoja hii kuwa kama Yesu ni Mungu inakuwaje basi aseme anaenda kwa Baba yake na je kuna uhusiano gani baina ya Yesu na Baba?
Jibu la msingi la hoja hiyo”
Kimsingi kama nilivyokwishafafanua kwa kina juu ya utatu mtakatifu tuliona juu ya uwepo wa nafsi tatu za Mungu mmoja ambapo Baba ni mojawapo ya nafsi hizo, hivyo jambo la msingi katika hoja hii ni kuangalia tu sababu ya Yesu kuitamka nafsi hiyo ya Baba kama mamlaka tofauti wakati Fulani na ndipo tuangalie uhusiano uliyopo baina ya Baba na Neno-Yesu.
Yohana 16:25
Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba.
Katika maelezo yake hayo Bwana Yesu anaeleza kuwa wakati fulani amekuwa akitumia mithali (mafumbo) kueleza juu ya habari ya Baba na sasa anaahidi kuwa hatimaye ipo siku ambapo atatamka wazi wazi juu ya habari ya Baba.
Maelezo hayo yanatoa kanuni ya jumla ya kuzingatia katika kuyajadili matamko ya Bwana Yesu ambapo Yesu mwenyewe anaweka wazi kuwa kauli zake zinaweza wakati Fulani zikawa na uzito kueleweka mpaka pale anapoamua kuziweka bayana yeye mwenyewe, na kikubwa zaidi hapa Yesu anataja wazi kuwa miongoni kwa kauli zake hizo zilizofumbika ni ile inayohusu habari ya Baba na ndipo anaahidi kuwa upo wakati ambapo atafumbua fumbo hilo lihusulo mahusiano yake na Baba.
Hebu sasa tuone namna Yesu alivyoweka wazi mahusiano yake na Baba’
Yohana 10:30-33
Mimi na Baba tu umoja.31 Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige.32 Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?33 Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu
Hii ni sehemu ya kwanza ya maandiko ambapo Bwana Yesu anaweka bayana juu ya undani wake wa asili na mamlaka moja na Baba kwa kusema wazi kuwa yeye na Baba ni umoja, tamko ambalo Wayahudi walielewa moja kwa moja kuwa lilionyesha kuwa Yesu alikuwa akithibitisha Uungu wake.
Na katika tamko jingine Yesu aliweka wazi kuwa hakuna utofauti wowote baina yake na nafsi ya Baba hebu tusome:-
Yohana 14:7-9
Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. 8 Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.9 Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
Katika andiko hilo Bwana Yesu anaweka wazi zaidi na kufumbua fumbo hilo mbele ya wanafunzi wake ambapo wanafunzi hao wanamhoji na kumtaka awaweke wazi juu ya uhusiano wake na Baba huku wakidai kuwa awaonyeshe huyo Baba, na ndipo kwa namna ya kushangaza Bwana Yesu anawajibu kwa uwazi kuwa tendo la kumfahamu yeye ndiyo kumfahamu Baba mwenyewe na kuwa kwa kumwona yeye tayari wameshamwona huyo Baba hivyo hawakuwa na haja ya kudai kumwaona Baba.
Hapo tendo la kumfahamu yeye ndiyo kumfahamu Baba mwenyewe na kuwa kwa kumwona yeye tayari wameshamwona huyo Baba hivyo hawakuwa na haja ya kudai kumwaona Baba.
Hapo Yesu aliweka wazi kuwa yeye ni Mungu toka katika umoja wa nafsi tatu za Mungu mmoja na kamwe hakuna tofauti za kimamlaka baina ya nafsi hizo kwa kuwa ni Mungu yule yule anayetenda katika katika upana kupitia Nafsi tatu yaani ile ya Baba , Neno na Roho Mtakatifu kama tulivyoona katika uchambuzi mpana wa hoja hiyo hapo mwanzoni
Hivyo jambo la msingi ni kuweka utulivu tu katika usomaji wa maandiko matakatifu maana kimsingi maandiko hayo yanatoa majibu ya kila swali linalotutatiza katika ulimwengu huu wa imani wenye walimu na farsafa nyingi za kidini.
Kwanini alilia Mungu wangu mbona umeniacha?
Katika mijadala mbalimbali ya imani kumesikika swali hili likihojiwa na walimu mbalimbali na wachambuzi wa dini, kile kinachotatiza hapa ni tamko la Bwana Yesu akiwa msalabani Mathayo 27:46…Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Hivyo swali linajitokeza hapa kuwa sasa Yesu alikuwa akimwomba Mungu gani ili hali yeye ni Mungu?
Jibu la msingi la swali hili’
Tamko hilo la Yesu msalabani endapo utalichukulia kama lilivyo pasipo kutafuta undani wake linaweza kukuingiza katika jaribu la kufikiri kuwa Bwana Yesu alikuwa ni kiumbe tu kwa hali zote.
Lakini msingi wa maandiko ya Biblia ulihusianisha tukio hilo na upande wa pili wa utendaji wa Bwana Yesu yaani ule wa kutwaa husika ya ubinadamu na kujiweka katika viwango vya ubinadamu ili kuwa kielelezo na hatimaye kutukomboa. Na hivyo hali hiyo ilimpelekea wakati Fulani kutamka na kutenda kama mwanadamu pamoja na kuwa asili yake si ya kibinadamu, na ndipo mtume Paulo anaweka wazi kanuni hiyo:-
Filipi 2:7
Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Biblia inafafanua kuwa baada ya Yesu kutwaa mfano wa ubinadamu hali hiyo ilimfanya kujifanya kuwa hana utukufu yaani wakati Fulani alitumia hali ya kawaida tu ya ubinadamu na si Uungu wake (uwezo, mamlaka) hivyo ndiyo maana hata alitamka maneno hayo akibeba husika halisi ya ubinadamu na kwakweli hapo alitamka kwa hali hiyo ya ubinadamu kabisa, ingawa tamko hilo halihafifishi mamlaka yake ya kiasili ya Uungu kwakuwa lilikuwa katika mpango mzima wa hatua zake za kiukombozi na kuvaa kiatu chetu.
Pia Yesu alikuwa akitimiza unabii’
Kwa upande mwingine Biblia inaweka wazi kuwa tamko hilo lililenga pia kutimiza tabiri za kiunabii kama Yesu mwenyewe anavyojenga msingi wa ukweli huu kwa kutamka:-
Luka 24:44
Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.
Katika tamko hilo Bwana Yesu anaeleza kuwa kuna mambo yanayomhusu yaliyoandikwa katika vitabu hivyo vya manabii lazima ayatimize katika kipindi cha huduma yake mambo au unabii ambao uliandikwa tayari katika vitabu hivyo vya manabii lakini anataja kuwa mambo hayo pia yamo katika Zaburi ya nabii Daudi.
Katika Zaburi hiyo ya nabii Daudi unaposoma Zaburi ile ya 22:1’ utagundua kuwa hapo kuna tamko lile lile la Yesu alilotoa pale msalabani kwa kusema “Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?
Hivyo kwa mtazamo huo utagundua kuwa tamko lile la Bwana Yesu msalabani lililenga pia kutimiza unabii huo wa Zaburi ya Daudi kwakuwa hata Yesu mwenyewe alionyesha wazi kuwa alipaswa kutimiza unabii ulio katika kitabu hicho cha Zaburi hivyo swala hilo halihafifishi asili yake ya mamlaka ya Uungu.
Yesu alitimiza kanuni ya Biblia ya kukabili matatizo kwa kuomba na kuimba.
Pamoja na ufafanuzi huo wa msingi hapo juu bado maandiko ya Biblia yan endelea kupanua wazo katika hoja hii kadri tunavyosoma katika andiko jingine la mtume Yakobo kama ifuatavyo:-
Yakobo 5:13
Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi.
Mtume Yakobo katika mitabu chake hicho anataja kanuni za mbili za kimbingu za kukabili matatizo kuwa jambao la kwanza yule aliyepatwa na matatizo anapaswa kuomba na pia aimbe Zaburi.
Hivyo kwa hali halisi tutakubaliana kuwa katika hali ya kibinadamu Yesu alikuwa akikabiliana na mabaya ya mateso ya msalaba na hivyo kwa tamko lile alikuwa akitimiza masharti hayo kwa njia hiyo ya kuomba lakini pia kuimba maana tamko alilolitoa ni Zaburi (tenzi) ya 22:1 katika kitabu hicho cha mfalme Daudi, na kwa hali hiyo tendo hilo haliathari kwa namna yeyote mamlaka ya asili ya Uungu wa Bwana Yesu.
Hebu nikualike tena tunapokwenda kwenye uchambuzi wa swali jingine muhimu juu ya Uungu wa Yesu.
Mbona alilala, je Mungu analala?
Swali hili la msingi ndilo litakalotufikisha mwisho wa uchambuzi wa mada hii juu ya Maarifa kuhusu Utatu na Uungu wa Bwana Yesu. Na hapa hoja ya msingi inatokana na tukio la Yesu kusafiri na wanafunzi wake naye akiwa amelala katika Shetri hivyo wanafunzi wake baada ya kupata taharuki ya kubwa ya dhoruba wakaanza kumwamsha ili awape msaada katika kadhia hiyo kama tunavyosoma:-
Marko 4:37-38
Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji.
38 Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
Tendo hilo la kulala kwa Bwana Yesu linalosimuliwa hapo ndilo linalozalisha hoja hiyo ambapo waulizaji wa swali hilo hukaza hoja yao kwa kusoma pia andiko la kitabu cha Zaburi hii ifuatayo:-
Zaburi 121:4-5 Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
Andiko hilo la Zaburi linaeleza kuwa Mungu aliye mlinzi wa Israel hatosinzia wala kulala, hivyo wajengaji wa hoja hii hudai kuwa tendo la Yesu kulala kama yeye ni Mungu basi ni hatua ya kukana Uungu wake.
Jibu la msingi la swali hili’
kimsingi hili ni moja kati ya maswali rahisi sana katika hoja hii juu ya Utatu na Uungu wa Bwana Yesu, lakini kile kinachoonekana kuwa ni mapungufu kidogo kwa waulizaji wa swali hili ni kutochukua hatua ya usomaji linganishi wa maandiko na kupitia aya nyingi zaidi ili kutafuta mantiki ya kisa hiki cha Yesu kulala na maelezo ya Zaburi yanayotamka kuwa Mungu halali.
Lakini kwa kujibu swali hili niseme tu kuwa andiko la Zaburi ya Daudi liko sahihi tu kuwa Mungu yeye kimsingi halali usingizi, lakini bado Zaburi hiyo hiyo inaeleza kile anchoweza kufanya Mungu katika dhana hiyo hiyo ya kulala hebu tusome tena andiko jingine la Zaburi ili kuanza hatua hii muhimu ya kupata ufumbuzi juu ya swali hili lenye utata:-
Tusome pamoja katika andiko hilo la Zaburi:-
Zaburi 78:65
Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;
Katika andiko hilo tena nabii Daudi aneleza kuwa kumbe Mungu anaweza kuwa ‘kama aliyelala’ kumbuka andiko la kwanza linasema Mungu halali usingizi ambapo kulala huku kunaonekana kuwa ni halisi, lakini hapa nabii Daudi anatumia neno ‘kama aliyelala usingizi’ neno linaloonyesha kuwa mlalaji hakuwa katika hali halisi ya ulalaji wa kutojitambua na kujiweza.
Hivyo baada ya kupata ufafanuzi huo tunaweza kufanya jumuisho la hoja hii kwa kusema kuwa’ aina ile ya ulalaji wa Yesu inaonekana kulingana na hii ya pili ya kama aliyelala’ maana kwa hali halisi utaona kuwa hapo Yesu alikuwa tu akipima imani ya wanafunzi wake kwa tukio hilo kama ambavyo maandiko ya Isaya yanavyosema juu ya mfumo wa utendaji wa Mungu ambapo wakati Fulani kwa makusudi tu Mungu huweza kuwaacha watu wake kwa muda ili kuwapima:-
Isaya 54:7 Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.
Kwahiyo Mungu anaweza kwa muda fulani kuwageuzia kisogo watu wake ili kuona imani yao itaelekea wapi, na kwa hali halisi utaona kuwa hilo ndilo ambalo Bwana Yesu alilifanya katika tukio hilo akiwa na wanafunzi wake kwakuwa mara baada ya kuona kuwa imani ya wanafunzi wake imejielekeza kwake ndipo maandiko yanasema:-
Marko 4:39-41
Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.40 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
41 Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Hivyo ndivyo Yesu alivyohitimisha tukio hilo kwa kitendo hicho cha kukemea upepo na bahari mara baada ya kuridhika kuwa wanafunzi hao walikuwa na imani iliyoelekezwa kwake katika tukio hilo la dhoruba. Lakini jambo la msingi linalojitokeza hapo ni kuwa tendo hilo lenyewe la kutuliza hali ya Bahari bado pia ni kiashiria tosha cha mamlaka yake ya Uungu na pengine waulizaji wa swali hili wangekichunguza kisa hicho chote wangeona tu jinsi kisa chenyewe kinavyothibitisha zaidi Uungu wa Yesu na si badala yake kukanusha.
Rejea tamko la wanafunzi wake baada ya tukio hilo:-
Marko 4:41
Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Hivyo hata wanafunzi wa Yesu wenyewe walionyesha kushtushwa na tukio hilo na hata kujiuliza swali juu ya nguvu na uwezo huo wa Yesu wakihoji ni nani huyu hata pepo na bahari vinamtii!, hoja ambayo inajibiwa wazi na Zaburi ya Daudi;-
Zaburi 89:8-9
Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. 9 Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.
Nabii Daudi anaweka bayana kuwa ni Mungu pekee awezaye kutawala kiburi cha bahari na yakuwa mawimbi ya bahari yainukapo mwenye uwezo huo wa kuyatuliza ni Mungu pekee na kwahivyo tukio hilo la Yesu kutuliza bahari linaweka bayana kuwa Yesu ni Mungu.
Hitimisho
Matamko ya wazi juu ya Uungu wa Yesu
Nipende kwanza kukushukuru ndugu msomaji wangu kwa kufuatilia kwa makini uchambuzi wa mada hii , na pia nitoe wito kwako kuwa kadri ambavyo umepata bahati ya kujifunza ukweli huu umkubali na kumpokea Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako kwakuwa uweza nguvu na mamlaka juu ya mbingu na dunia viko juu yake pekee.
Baada ya wito huo nipende sasa kumalizia mada hii kwa kukuwekea nukuu chache za Biiblia zinazohitimisha uchambuzi huu kwa kuonyesha wazi juu ya mamlaka hii tukufu ya Bwana Yesu:-
Tito 2:13
Tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;
Mtume Paulo katika andiko hilo la Tito anaweka wazi kabisa juu ya Uungu wa Yesu kama Tomaso na Bwana Yesu mwenyewe katika fungu hili jingine;-
Yohana 20:28-29
Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! 29 Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Mungu akubariki unapotafakari ukweli huu na kuchukua hatua.

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW