Thursday, April 20, 2017

KAMA YESU NI MUNGU, MBONA ALILALA, JE MUNGU ANALALA?






Swali hili la msingi ndilo litakalotufikisha mwisho wa uchambuzi wa mada hii juu ya Maarifa kuhusu Utatu na Uungu wa Bwana Yesu. Na hapa hoja ya msingi inatokana na tukio la Yesu kusafiri na wanafunzi wake naye akiwa amelala katika Shetri hivyo wanafunzi wake baada ya kupata taharuki ya kubwa ya dhoruba wakaanza kumwamsha ili awape msaada katika kadhia hiyo kama tunavyosoma:-
Marko 4:37-38
Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji.
38 Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
Tendo hilo la kulala kwa Bwana Yesu linalosimuliwa hapo ndilo linalozalisha hoja hiyo ambapo waulizaji wa swali hilo hukaza hoja yao kwa kusoma pia andiko la kitabu cha Zaburi hii ifuatayo:-
Zaburi 121:4-5 Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
Andiko hilo la Zaburi linaeleza kuwa Mungu aliye mlinzi wa Israel hatosinzia wala kulala, hivyo wajengaji wa hoja hii hudai kuwa tendo la Yesu kulala kama yeye ni Mungu basi ni hatua ya kukana Uungu wake.
Jibu la msingi la swali hili’
kimsingi hili ni moja kati ya maswali rahisi sana katika hoja hii juu ya Utatu na Uungu wa Bwana Yesu, lakini kile kinachoonekana kuwa ni mapungufu kidogo kwa waulizaji wa swali hili ni kutochukua hatua ya usomaji linganishi wa maandiko na kupitia aya nyingi zaidi ili kutafuta mantiki ya kisa hiki cha Yesu kulala na maelezo ya Zaburi yanayotamka kuwa Mungu halali.
Lakini kwa kujibu swali hili niseme tu kuwa andiko la Zaburi ya Daudi liko sahihi tu kuwa Mungu yeye kimsingi halali usingizi, lakini bado Zaburi hiyo hiyo inaeleza kile anchoweza kufanya Mungu katika dhana hiyo hiyo ya kulala hebu tusome tena andiko jingine la Zaburi ili kuanza hatua hii muhimu ya kupata ufumbuzi juu ya swali hili lenye utata:-
Tusome pamoja katika andiko hilo la Zaburi:-
Zaburi 78:65
Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;
Katika andiko hilo tena nabii Daudi aneleza kuwa kumbe Mungu anaweza kuwa ‘kama aliyelala’ kumbuka andiko la kwanza linasema Mungu halali usingizi ambapo kulala huku kunaonekana kuwa ni halisi, lakini hapa nabii Daudi anatumia neno ‘kama aliyelala usingizi’ neno linaloonyesha kuwa mlalaji hakuwa katika hali halisi ya ulalaji wa kutojitambua na kujiweza.
Hivyo baada ya kupata ufafanuzi huo tunaweza kufanya jumuisho la hoja hii kwa kusema kuwa’ aina ile ya ulalaji wa Yesu inaonekana kulingana na hii ya pili ya kama aliyelala’ maana kwa hali halisi utaona kuwa hapo Yesu alikuwa tu akipima imani ya wanafunzi wake kwa tukio hilo kama ambavyo maandiko ya Isaya yanavyosema juu ya mfumo wa utendaji wa Mungu ambapo wakati Fulani kwa makusudi tu Mungu huweza kuwaacha watu wake kwa muda ili kuwapima:-
Isaya 54:7 Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.
Kwahiyo Mungu anaweza kwa muda fulani kuwageuzia kisogo watu wake ili kuona imani yao itaelekea wapi, na kwa hali halisi utaona kuwa hilo ndilo ambalo Bwana Yesu alilifanya katika tukio hilo akiwa na wanafunzi wake kwakuwa mara baada ya kuona kuwa imani ya wanafunzi wake imejielekeza kwake ndipo maandiko yanasema:-
Marko 4:39-41
Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.40 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
41 Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Hivyo ndivyo Yesu alivyohitimisha tukio hilo kwa kitendo hicho cha kukemea upepo na bahari mara baada ya kuridhika kuwa wanafunzi hao walikuwa na imani iliyoelekezwa kwake katika tukio hilo la dhoruba. Lakini jambo la msingi linalojitokeza hapo ni kuwa tendo hilo lenyewe la kutuliza hali ya Bahari bado pia ni kiashiria tosha cha mamlaka yake ya Uungu na pengine waulizaji wa swali hili wangekichunguza kisa hicho chote wangeona tu jinsi kisa chenyewe kinavyothibitisha zaidi Uungu wa Yesu na si badala yake kukanusha.
Rejea tamko la wanafunzi wake baada ya tukio hilo:-
Marko 4:41
Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Hivyo hata wanafunzi wa Yesu wenyewe walionyesha kushtushwa na tukio hilo na hata kujiuliza swali juu ya nguvu na uwezo huo wa Yesu wakihoji ni nani huyu hata pepo na bahari vinamtii!, hoja ambayo inajibiwa wazi na Zaburi ya Daudi;-
Zaburi 89:8-9
Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. 9 Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.
Nabii Daudi anaweka bayana kuwa ni Mungu pekee awezaye kutawala kiburi cha bahari na yakuwa mawimbi ya bahari yainukapo mwenye uwezo huo wa kuyatuliza ni Mungu pekee na kwahivyo tukio hilo la Yesu kutuliza bahari linaweka bayana kuwa Yesu ni Mungu.
Hitimisho
Matamko ya wazi juu ya Uungu wa Yesu
Nipende kwanza kukushukuru ndugu msomaji wangu kwa kufuatilia kwa makini uchambuzi wa mada hii , na pia nitoe wito kwako kuwa kadri ambavyo umepata bahati ya kujifunza ukweli huu umkubali na kumpokea Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako kwakuwa uweza nguvu na mamlaka juu ya mbingu na dunia viko juu yake pekee.
Baada ya wito huo nipende sasa kumalizia mada hii kwa kukuwekea nukuu chache za Biiblia zinazohitimisha uchambuzi huu kwa kuonyesha wazi juu ya mamlaka hii tukufu ya Bwana Yesu:-
Tito 2:13
Tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;
Mtume Paulo katika andiko hilo la Tito anaweka wazi kabisa juu ya Uungu wa Yesu kama Tomaso na Bwana Yesu mwenyewe katika fungu hili jingine;-
Yohana 20:28-29
Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! 29 Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Mungu akubariki unapotafakari ukweli huu na kuchukua hatua.
Shalom,

No comments:

WHAT DOES IT MEAN "THE WORD OF GOD IS GOD"?

 WHAT DOES IT MEAN "THE WORD OF GOD IS GOD"? Dr. Maxwell Shimba explains: The Word and the Divine Nature – A Comprehensive Exposit...

TRENDING NOW