UTANGULIZI
Mwandishi mmoja alimwuliza Bwana Yesu: Katika amri zote ni ipi iliyo kuu? (Mk. 12:28).
Bwana alimjibu: Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. (Mk. 12:29-30). Hicho ndicho kipimo cha utimilifu wa utii.
Tunapoamua kumfuata Yesu, hata hivyo, hatukamiliki kwa siku moja. Maisha ya wokovu ni safari; ni mchakato wa kukua kuanzia uchanga, utu uzima, hadi utimilifu wa Kristo. (1 Pt. 2:2; Ebr. 5:12-14).
Mabadiliko ya ukuaji wetu kiroho hayafanyiki kwa juhudi zetu wenyewe – ni Roho Mtakatifu ndiye anayetubadilisha. Wajibu wetu ni kumpa nafasi ili aweze kufanya hivyo. Hiyo ni kusema kwamba, kazi ya Roho Mtakatifu ndani yetu inategemea mwenendo wetu na kiwango kile cha utayari tulio nao wa kutii neno lake; na pia bidii na shauku yetu ya kumtafuta Bwana. Yeye anasema: Nawapenda wale wanipendao na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. (Mith. 8:17).
KABLA YA KUOKOLEWA
Kabla ya kuokolewa tunakuwa ni watu wa duniani. Mawazo, maneno, na matendo yetu yanakuwa ni ya kidunia; maana dunia ina kawaida zake ambazo ni tofauti kabisa na zile za kimbingu.
Maandiko yanasema: Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu. (1 Kor. 6:9-11).
Vilevile imeandikwa: Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo ... (Gal. 5:19-21).
Huko ndiko ambako tunakuwa kabla ya kuamua kumpokea Yesu mioyoni mwetu na kumwachia utawala wa maisha yetu. Wakati tungali kule, maandiko yanasema: Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nao tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. (Efe. 2:1-3).
BAADA YA KUOKOLEWA
Bwana alipowaokoa wana wa Israeli, hakuwaacha wabakie palepale Misri. Aliwaambia wajiandae kuondoka ili awapeleke katika nchi ya Kanaani. Hali kadhalika, Bwana anapotuokoa, anataka tutoke duniani na kuingia kwenye ufalme mpya wa Kristo. Imeandikwa: Kwa hiyo, Tokeni kati yao, mkatengwe nao, asema Bwana, msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi. (1 Kor. 6:17-18).
Japokuwa bado tunaendelea kubaki hapahapa duniani, maandiko yanasema: Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake. (Wakolosai 1:13). Ukiokolewa unakuwa umeingizwa katika ufalme wa Kristo; na jambo hili ni halisi kabisa katika ulimwengu wa roho!
Wana wa ulimwengu wana tabia na mwenendo wao unaowatambulisha. Hali kadhalika wana wa Mungu nao wanatambulishwa na tabia na mwenendo tofauti na ule wa dunia.
Unapoona kwamba mwana wa Mungu ana tabia za kidunia, basi hapo liko tatizo ambalo mhusika anatakiwa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo. Bwana anasema sasa: Kama watoto wenye kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. (1 Petro 1:14-16).
Kuwa watakatifu maana yake nini? Ni kuwa tofauti kabisa na dunia na kuwa sawasawa na Mungu. Imeandikwa: Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. (1Yoh. 2:15- 16).
MAISHA YA AINA MBILI
Hebu tujiulize maswali yafuatayo. Kama Mungu anasema kwamba tutoke kati ya dunia; pia tusiipende dunia na mambo yake; je, tuseme nini juu ya mtu mwenye hali hizi:
Akiwa kanisani ni mtu mnyenyekevu lakini akiwa nje ni mkali na mgomvi.
Jumapili anavaa kwa heshima lakini siku zingine anavaa mavazi ya kidunia (yaani yale ambayo hata yeye mwenyewe anayaonea aibu kuyavaa kanisani).
Jumapili anasikiliza muziki wa injili lakini siku zingine ni muziki wa kidunia.
Simu yake ina nyimbo za injili na taarabu za mipasho.
Anahudhuria matamasha ya Kikristo na matamasha ya muziki wa kidunia; au hata disko na klabu za usiku.
Kanisani anatoa sadaka lakini ofisini anaandika risiti za uongo ili apate malipo zaidi ambayo si haki yake.
Mbele za wapendwa anaongea maneno ya Mungu lakini mbali nao amejaa mizaha na maneno ambayo mbele ya wapendwa hana ujasiri wa kuyatamka.
Kanisani anaonekana mkamilifu lakini akiwa nje anaangalia picha za ngono; na hata kwenye simu yake anazo.
Jumapili anavaa kwa heshima lakini siku zingine anavaa mavazi ya kidunia (yaani yale ambayo hata yeye mwenyewe anayaonea aibu kuyavaa kanisani).
Jumapili anasikiliza muziki wa injili lakini siku zingine ni muziki wa kidunia.
Simu yake ina nyimbo za injili na taarabu za mipasho.
Anahudhuria matamasha ya Kikristo na matamasha ya muziki wa kidunia; au hata disko na klabu za usiku.
Kanisani anatoa sadaka lakini ofisini anaandika risiti za uongo ili apate malipo zaidi ambayo si haki yake.
Mbele za wapendwa anaongea maneno ya Mungu lakini mbali nao amejaa mizaha na maneno ambayo mbele ya wapendwa hana ujasiri wa kuyatamka.
Kanisani anaonekana mkamilifu lakini akiwa nje anaangalia picha za ngono; na hata kwenye simu yake anazo.
Unadhani Mungu anaposema, “Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia”, mambo hayo ni yapi? Je, ni tofauti na hayo tuliyoyaona hapo juu ambayo yanatendeka nje ya kanisa? Ni wazi kwamba ndiyo hayohayo.
Kama Mungu anasema: “Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake”, je, unatambua kwamba mtu kusema tu kwamba “mimi ni Mkristo” lakini bado akawa anayatenda hayo kunabatilisha kabisa ukristo wake?
Kumkataa Mungu si lazima mpaka mtu atamke hivyo waziwazi. Wengi wanajiita Wakristo lakini kwa kitendo cha kuipenda dunia, Mungu anasema, kumpenda Baba hakumo ndani yao.
HASARA YA MAISHA MAWILI
Kwa nini ufanye kazi yenye hasara? Kwa nini uende kanisani maisha yako yote, kisha mwisho wake uje ukataliwe? Bwana anasema: Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani, lakini akisitasita, roho yangu haina furaha naye. (Ebr. 10:38). Kusitasita maana yake ni kuingia kanisani, lakini hutaki kubaki kwa Mungu asilimia mia moja. Badala yake kanisani umo nusu na duniani umo nusu.
Pia imeandikwa: Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala hu moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. (Ufu. 3:16-16). Mtu aliye uvuguvugu hahesabiwi miongoni mwa wana wa Mungu!
Vilevile Bwana anasema: Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyotenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilokosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. (Yer. 18:24).
Wako watu wengi ambao, katika maisha yao yote wanadhani kuwa wako ndani ya Mungu, lakini siku ya mwisho itakuwa ni masikitiko makubwa. Watajikuta wakikataliwa kwa vile walikuwa wakiishi maisha mawili – upande mmoja wanamkubali Mungu; upande wa pili bado wameshikilia kawaida za dunia.
NINI CHA KUFANYA?
Bwana anataka tuwe na msimamo na kuchagua upande mmoja tu. Maandiko yanasema wazi kuwa: ....nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako. (Kumb. 30:19). Kupotea ni ama mtu ameamua kwa makusudi kutomtii Mungu au hakutafuta maarifa ya Mungu. Makwazo unayokutana nayo hayapo hapo kwa bahati mbaya. Bwana anaruhusu yakufike ili uweze kuchagua kati ya kumtii yeye au kufuata mawazo ya adui.
Yafuatayo ni maandiko ambayo yanatupa maarifa au maelekezo ya nini cha kufanya ili tusiwe watu wenye maisha mawili ambayo mwisho wake ni kukataliwa:
Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya mto, ....lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. (Yoshua 24:15). Ni vema kuchagua kumtumikia Bwana. Usianze kutoa visingizio kwamba, “Unajua maisha ni magumu, ndiyo maana ninafanya hivi.” Sababu hizo hazitakusaidia mwisho wa safari. Chagua kusimama na Bwana naye atashughulikia mambo yako.
Usiwe na mawe ya kupimia mbalimbali, kubwa na dogo, katika mfuko wako. Usiwe na vipimo mbalimbali, kikubwa na kidogo, katika nyumba yako. Uwe na jiwe timilifu la haki, uwe na kipimo kitimilifu cha haki; zipate kuwa nyingi siku zako, katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako. Kwa kuwa wote wayatendao mambo kama haya, wote watendao yasiyo haki, ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako. (Kumb. 25:13-16). Hapa hazungumzii tu wafanyabiashara, bali anazungumzia suala la viwango. Usipunguze viwango viwe vya kimwili au vya kiroho. Usipime mambo, upande mmoja kwa mtazamo wa kimungu na upande mwingine wa kidunia. Jiwe timilifu la haki ni Neno la Kristo. Kama neno linasema ‘fanya hivi’, basi hicho ndicho cha kufanya hata kama dunia yote iko kinyume nacho.
Macho yako yatazame mbele, na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, na njia zako zote zithibitike. (Mith. 4:25-26). Chagua upande wa Mungu na uwe thabiti ndani yake badala ya kuyumbayumba – mara duniani, mara kwa Mungu.
Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. (1Yoh. 2:15- 16). Maadamu tungali duniani, tutakabiliana na tamaa na misukumo mbalimbali yenye nguvu kutoka kwa marafiki, ndugu, hali ya uchumi, wafanyakazi wenzetu, nk. Lakini, tunalazimika kukataa kuvutwa na mambo ya dunia yaliyo kinyume na neno la Mungu hata kama yanaonekana ni ya kisasa; na hata kama sisi tutaitwa tumepitwa na wakati. Kuna faida kumpenda Mungu kuliko kuipenda dunia ambayo ni ya muda mfupi tu. Mungu wetu ni wa milele yote!
HITIMISHO
Usipofanya uamuzi, usidhani kwamba Mungu atakulazimisha. Watu wengi hupenda kusema kwamba, “Mungu anisaidie niache hiki au kile ...”. Maandiko yanasema: Asiyetawala roho yake ni mfano wa mji uliobomolewa usio na kuta. (Mith. 25:26). Maana yake ni kuwa, adui shetani anaingia na kutoka apendavyo katika moyo wa aina hiyo; anaingiza takataka zake kama apendavyo na kukuwekea mawazo ya uongo. Mathalani mtu anapofanya mambo mbalimbali anaweza kujitetea kwa kusema: nasikiliza muziki wa kiduania ili kutuliza mawazo na kujiburudisha; nasikiliza muziki wa kidunia ili kujipatia mafunzo mbalimbali; naenda kwenye klabu ili kujumuika na marafiki na kupeana mawazo, n.k. Sababu kama hizo zinaonekana ni nzuri lakini ukweli ni kwamba yote hayo ni uongo wa kuzimu ambao mwisho wake ni upotevu na uangamivu! Kumbuka shetani haji kama shetani, bali huja kama malaika wa nuru. (2 Kor. 11:14).
Kwanza ni lazima uamue kuacha na kisha uanze kuacha; kisha Mungu atakushika mkono kuanzia hapo. Israeli walipofika baharini huku Wamisri wakiwa wanakuja nyuma yao, Bwana alimwambia Musa: Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. (Kut. 14:15-16).
Kugawanyika kwa bahari kulifuatia hatua yao ya imani ya kusonga mbele wakati bahari ingali imejaa. Ilikuwa ni vivyo hivyo pale walipofika kwenye mto Yordani wakiwa na Yoshua. Makuhani walitakiwa kuyakanyaga maji kwanza ndipo maji yalitindika. (Yoshua 3:15-16).
Kwa hiyo, Mungu anasema: Usiandamane na mkutano kutenda uovu. (Kut. 23:2). Yaani, usifanye mambo kwa kisingizio cha kusema kwamba, “Mbona kila mtu anafanya hivyo?” Kama Mungu akizuia jambo, kubali hata kubaki peke yako katika kumtii Mungu. Wacha dunia yote ielekee upande wake lakini wewe amua kusimama na Bwana hadi mwisho!
Bwana anasema: Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. (2 Yoh. 1:8).
Pia anasema: Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. (Ufu. 3:11).
Inawezekana! Unaweza! Amua leo na kusimama na Bwana!
Mwandishi: Injli Ya Kweli Blog.
No comments:
Post a Comment