Sunday, January 29, 2017

FURAHA KATIKA ROHO MTAKATIFU

Image may contain: text
Mara kadhaa nimesikia watu wakisema, “Nikienda kanisani najisikia raha kweli; lakini nikitoka, hali ya uzito wa moyo inanirudia tena.”
Ndugu, Biblia inasema: Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. (Rum. 14:17).
Hebu tujiulize swali hapa. Sehemu nyingine tunaposoma, Bwana anasema kwamba:
Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo. Mimi nimeushinda ulimwengu. (Yohana 16:33)
Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. (Mathayo. 10:22);
Jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu. (1Wakorintho10:13)
Hata mtume Paulo aliye mtume mkuu namna ile wa Bwana hakuweza kuyaepuka majaribu licha ya kuwa mwaminifu sana kwenye huduma aliyokabidhiwa. Lakini licha ya mateso mengi aliyopitia, ni yeye huyohuyo ndiye anayeongelea juu ya kuwa na furaha katika Roho Mtakatifu!
Paulo alipitia mambo magumu sana ambayo si wengi wanaweza kustahimili. Anasema: ...katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang‟anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. (2Wakorintho 11:23-27). Hebu piga picha ya maisha hayo!!
Na hii hali ya kupita kwenye majaribu ndiyo hali halisi ya maisha ya kila mwanadamu! Majaribu si lazima yafanane kwa kila mtu lakini suala la msingi ni kwamba, hakuna mtu ambaye hayamkuti.
Inakuwaje basi Mungu anataka tuwe na furaha huku wakati huohuo anasema kuwa tutapita katika majaribu? Unapataje furaha huku unaumwa; huku huna mtoto; huku umefukuzwa kazi au umefukuzwa nyumbani kwenu?

Mara nyingi wengi wetu tunadhani kuwa furaha ni ile hali ya kuwa na hisia zinazoambatana na vicheko pamoja na kutokuwa na shida yoyote. Ndiyo maana basi mtu mwingine anapoenda kanisani anajisikia burudani na furaha lakini akitoka hapo anarudia tena majonzi na huzuni na tabu zake za mwanzo. Yamkini hiyo ‘furaha’ ya kanisani kwa mtu huyo inatokana tu na kule kusikia mapambio na ujumbe wa kutia moyo kutoka kwa watumishi na ndugu katika Kristo.
Lakini hiyo ni aina ya furaha ambayo mtu anaweza kuipata hata katika kusikiliza muziki wa kidunia, kucheza michezo aipendayo, ushabiki wa mpira, kuangalia sinema za kusisimua, kununua gari, kushinda mitihani, n.k. – ni hisia chanya zinazoletwa na mambo mazuri.
Japokuwa haina maana kwamba hisia hizi ni mbaya, lakini hii siyo maana ya furaha katika Roho Mtakatifu inayotajwa katika maandiko.
Unajua, dunia haikukusudiwa kuwa mahali pa urahisi tu kwa kila kitu. Vinginevyo basi ingekuwa ni mbingu; hakungekuwa na haja ya kuja kwenda tena mbinguni baadaye.
Badala yake, duniani ni mahali pa mapambano kabisa! Biblia iko wazi inaposema kwamba:
Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuzipinga hila za shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka; juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu. (Waefeso 6:12).
Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. (2Wakorintho 10: 3–5).
Haya ndiyo maisha ambayo Mkristo anayo. Maadamu bado tuko duniani, hatutakwepa kamwe mapambano dhidi ya shetani na majeshi yake ya mapepo!
Lakini bado Bwana aliwaambia wanafunzi wake (pamoja na sisi) kwamba: Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu wala msiwe na woga. (Yoh. 14:27). Wakristo hawaambiwi kusubiri amani na furaha baada ya kufa; badala yake wanatakiwa kuipokea hapahapa duniani katikati ya shida na majaribu haya wanayopitia!
Kwa nini Bwana anasema tusifadhaike wala kuwa na woga? Ni kwa sababu kutakuwa na mambo ambayo, katika hali ya kawaida, yanasababisha hizo fadhaa na huo woga mioyoni mwa watu.
Amani na furaha zinaenda pamoja. Kulingana na mitazamo ya kidunia, hizi zinatokana na mtu kuwa na fedha, kazi nzuri, nyumba, umaarufu, n.k. Cha ajabu zaidi, dunia pia inadhani kuwa amani na furaha zinaweza kupatikana kwenye dhambi kama vile matumizi ya dawa za kulevya, uzinzi na uasherati, ulevi, nk!
Sasa, Mkristo mwenye furaha ni yupi? Furaha ya Roho Mtakatifu inatokana na mambo yafuatayo:
Kujua kabisa moyoni mwako kwamba umesamehewa dhambi zako kwa kuwa umetubu kwa kumaanisha kuziacha (Mith. 28:13). Hatia ya dhambi inapokuwa moyoni ni chanzo kikubwa cha kukosa furaha.
Kujua hakika kwamba jina lako limeandikwa mbinguni kwenye kitabu cha Mwanakondoo (Lk. 10:20). Watu wa aina hii, kwao Kristo si dini bali ni Bwana na Mwokozi ambaye anaongoza maisha yao kila dakika ya maisha yao. Hofu ya kutupwa jehanamu inayotokana na maisha ya dhambi ni chanzo kingine cha kukosa furaha maishani.
Kuwa na uhakika kwamba Bwana anajishughulisha na maisha yako kwa kila hali – hata pale ambapo mambo ni magumu kabisa. Biblia inasema: Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema ... (Rom. 8:28). Dhambi hutufanya tumwogope Mungu, hivyo tunakuwa tunajisikia wapweke. Matokeo yake hofu ya mambo mabaya kama vile kifo, ajali, n.k., inatufanya tukose furaha.
Kwa hiyo, furaha ya Roho Mtakatifu ni hali ya utulivu wa ndani; ni uhakika wa kwamba maisha yako yamo mikononi mwa Mungu – uwe unapitia katika kipindi kisicho na matatizo yoyote au katika kipindi chenye matatizo mazito kabisa! Utulivu huu unaweza kuambatana na vicheko na tabasamu au usionyeshe chochote kabisa; bali mhusika anakuwa nao ndani yake tu.
Unaweza kuipata furaha hii sasa kwa wewe kuamua kuyatoa kikamilifu maisha yako kwa ajili ya Kristo Yesu; kuacha kuona shaka juu ya Mungu kuhusika kabisa na kila kitu katika maisha yako – yaani uamini kabisa kwamba kila kitu kiko mikononi mwake kwa usalama wote; hata kama kwa nje mambo yanaonekana kwenda vibaya.
Acha kulia kwa kukata tamaa na kuanza kumwuliza Mungu, “Kwa nini Bwana haya yamenipata?” Badala yake wewe mwamini tu Yeye na kuwa mwaminifu kwake. Kumbuka kwamba Bwana hatasahau kamwe uaminifu na imani yako kwake, na hasa pale unaopita katika hali ngumu!

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW