Wednesday, November 16, 2016

YESU ALIMAANISHA NINI ALIPO SEMA MSIDHANI NALIKUJA KUTANGUA TORATI?


Baadhi ya watu wameshindwa kuelewa kuwa torati imeondolewa kwa sababu ya maneno ya Yesu aliposema “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amini, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie” (Mathayo 5:17-18). Watu hawa hutumia andiko hili kujenga hoja kuwa Torati haikuondolewa.
Maana ya neno tangua:
Kulingana na kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno “tangua” maana yake ni vunja kanuni au maafikiano; batilisha.
Maana ya neno “hata”:
Neno “hata” maana yake ni “mpaka”
Kwanza kabisa naomba nitoe mifano kadhaa ya mambo yaliyokuwa ni lazima muumini wa Agano la Kale afuate ili ahesabiwe haki ambayo leo hii ukiyafuata hauwezi kuhesabiwa haki mbele za Mungu:
1. Kutahiriwa; Katika Agano la Kale muumini asiyetahiriwa hangeweza kuhesabiwa haki hata kidogo. Katika Agano Jipya kutahiriwa siyo lazima ili uhesabiwe haki na Mungu (Mwanzo 17:9-10, Galatia 6:15).
2. Katika Agano Jipya tunaweza kula vyakula vyote isipokuwa vilivyotolewa sadaka kwa sanamu au vilivyonyongwa bila kuchinjwa, lakini wakati wa Agano la Kale kulikuwa na kuzuiliwa kula baadhi ya vyakula hasa baadhi ya wanyama kama vile sungura, nguruwe, samaki wasio na magamba, nk. (Matendo 26:12-18).
3. Katika Agano la Kale kulikuwa na utaratibu wa kutoa sadaka za wanyama ili mtu aweze kuhesabiwa haki. Hii ilikuwa sheria. Katika Agano Jipya Yesu amelitangua kabisa hilo halipo tena. Damu yake iliyomwagika inatosha kuondoa dhambi ya kila amwaminiye Yesu.
4. Katika Agano Jipya Kuhani alipaswa kuwa mtu mmoja tu amabaye alipaswa kuendesha ibada yote na kutoa sadaka za kuteketezwa. Hilo nalo Yesu alilitangua baada ya Kifo chake Msalabani kila amwaminiye anakuwa kuhani wa Mungu na anaweza kufanya ibada ya kuongea na Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa mtu mwingine.

5. Wakati wa Torati ya Musa siyo watu wote waliokuwa wanaweza kumwagiwa Roho Mtakatifu ilikuwa ni kwa makuhani au manabii tu. Lakini hilo naalo Yesu alilitangua na watu wote wenye mwili wanamwagiwa Roho Mtakatifu.
Ni vema kama tutayachunguza maandiko kwa undani kama wale watu wa Beroya ili tujue je madai hayo ni ya kweli? kama neno la Mungu lisemavyo kuwa, “Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo” (Matendo 17:11)
Labda niyanukuu tena maandiko haya, halafu nitakuonesha ambacho watu hawa wanachokosea. Tatizo kubwa hapa ni kwamba mara nyingi wasomaji wa andiko hili wamekuwa wakiishia njiani hawafiki mwisho wa sentensi. Ni wazi kabisa kama utasoma na kuishia njiani, hutaweza kuwa na tafsiri moja na mwingine ambaye alisoma mpaka mwisho wa sentensi.
AYA YA MADA:
“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amini, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, HATA YOTE YATIMIE” (Mathayo 5:17-18).
NENO “HATA” MAANA YAKE NINI?
Katika andiko hilo wanalolinukuu kama uthibitisho, neno “hata” maana yake ni “mpaka”, kama ilivyo katika maandiko yafuatayo “Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu HATA tumwue Paulo” (Matendo 23:12). Watu hawa hawakumaanisha kuwa hawatakula tena katika maisha yao yaliyo salia hapa duniani walichokuwa wakimaanisha ni kuwa kifungo chao cha kutokula kitakoma ikiwa tu watamwua Paulo. Kwa hiyo neno “hata” lilikuwa linaashiria ukomo. “Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe HATA alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU “Mathayo 1:25. Maandiko haya hayamaanishi kwamba Yusufu hakumjua mkewe katika maisha yao yote, la hasha maana Biblia inatushuhudia kuwa Bwana Yesu alikuwa na ndugu zake wa tumbo moja, waliozaliwa baada yake. Maandiko haya yanatuambia kuwa Yusufu alipopata habari za mpango wa Mungu kupitia kwa Mariamu mkewe, Yusufu hakumjua mkewe, lakini baada ya kumzaa mwanawe aliiyemwita Yesu sawasawa na maagizo ya malaika wa Bwana, Yusufu akamjua mkewe. “Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, HATA watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu” (MARK. 9:1)
Kwa mfano, nikikuomba ukae nyumbani kwangu HATA nitakaporudi, neno “hata” “lina-indicating an ending point”. Hebu tafakari kama nikikwambia sentensi hii utaelewaje? Bila shaka sijamaanisha ukae nyumbani kwangu moja kwa moja, bali ninamaanisha ukae nyumbani kwangu “mpaka” nitakaporudi. Kwa hiyo hutaweza kuondoka nyumbani kwangu ikiwa sitarudi, hata kama nitachelewa utalazimika kuendelea kukaa nyumbani kwangu. Ila nitakaporejea utakuwa huru kuondoka.
UTHIBITISHO WA WA AYA WA NENO “HATA”
“Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali,ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara HATA nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake”.Luka 19:12-15
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, HATA hayo yote yatakapotimia. Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.Mathayo 24:34, Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita HATA hayo yote yatimie.Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. Luka 21:32.
“Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye, Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya, Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninaye pendezwa naye; msikieniyeye…Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, HATA (mpaka) Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.” (MATH. 17:3-5, 8, 9).
Baada ya Yesu kufufuka, Petro anasimulia, “Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu”.(2 PET 1:17-18).
Basi, Yesu hakusema kwamba Torati haitapita kamwe. La! bali alisema kwamba Torati haitapita kabla haijatimiIizwa na kwamba alikuja kwa kusudi hilo la kuitimiliza Torati. Baada ya kufufuka, Yesu aliwakumbusha wanafunzi maneno yake akisema: “… Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi… Akawaambia, Ndivyo iliyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu”(Luka. 24:44, 46)
“Maana yale YASIYOWEZEKANA kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa DHAIFU kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ILI HAKI YA TORATI YATIMIZWE NDANI YETU sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (Warumi 8:3,4).
Tazama! huko juu Yesu alisema “yodi moja wala nukta moja ya Torati haitaondoka, hata (au mpaka) yote yatimie.” Kisha, baada ya kufa kwake, Yesu alisema Torati yote ilikwisha kutimilizwa hapo alipokufa na kufufuka! Basi, Yesu hakuitangua Torati, maana alishika kila sheria bila kosa lo lote! Isitoshe, alitimiliza yote yaliyomhusu yaliyotabiriwa ndani ya Torati Twasoma: “Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho si katika hali ya zamani, ya andiko” (Rumi 7:6).
Tangu mwanzo haukuwa mpango wa Mungu kwamba Wakristo waishike Torati. La! bali Torati ilikuwa kiongozi kwa watu kabla Yesu hajaja. Imeandikwa: “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake”. Chunguza hasemi, Kwa wazao wake, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako: yaani, Kristo. “….Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, HATA aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi…Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi” (Galatia 3:16,19, 23-25) Maneno hayo yanatuthibitishia ya kuwa Torati imeondolewa.
Kwa hiyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, kutokana na ukweli kwamba Bwana Yesu alitimiza sheria yote, ndio maana sisi leo tunapokea wokovu kwa njia ya imani na si kwa kujaribu kutekeleza masharti ya torati.
Ilikuwa ni lazima madai au masharti YOTE ya torati yatimizwe. Na hapo ndipo anapoingia Bwana Yesu na haya maneno yake: Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. (Mathayo 5:17-18).
Mafarisayo walimshitaki Yesu kuwa anawaruhusu wanafunzi wake wavunje sheria ya Musa, kuvunja sabato (Marko 2:23-28). Lakini Bwana Yesu aliwajibuje? Kwanza! Aliwakumbusha mafarisayo kuwa Daudi alifanya jambo lisilo la halali kadiri ya sheria.
Hata hivyo, kama tulivyoona hapo juu, tatizo likawa kwamba, hakuna hata mwanadamu mmoja anayeweza kutimiza matakwa YOTE ya torati. Maana: Wote wamepotoka, wameoza wote pia; hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. (Rumi 3:12). Mungu si kigeugeu hata siku moja. Akisema jambo, amesema. Alishasema kwamba matokeo ya dhambi ni mauti basi! Mbele zake hakukuwa na uwezekano hata kidogo wa kuja tena kusema kinyume, labda: “Kwa kuwa mwanadamu ameshindwa kitimiza torati, basi nitamsamehe tu.” Hapana!
Neno la Mungu linaeleza msimamo wa Mungu juu ya dhambi yoyote ile. Imeandikwa: … wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe. (Nah. 1:3). Ilikuwa ni lazima madai au masharti YOTE ya torati yatimizwe. Na hapo ndipo anapoingia Bwana Yesu na haya maneno yake: Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. (Mathayo 5:17-18).
Kulingana na kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno “tangua” maana yake ni vunja kanuni au maafikiano; batilisha. Anachomaanisha Bwana Yesu hapa ni kwamba: Sikuja kubatilisha hata nukta moja ya torati; yote ni lazima itimizwe kama inavyotakiwa, maana uasi ulishafanyika kwa hiyo hukumu inayotolewa na torati ni lazima itimizwe kikamilifu! Kwa sababu dhambi imeshaingia ulimwenguni, na torati inasema kwamba mshahara wa dhambi ni mauti, basi ni LAZIMA hilo litimizwe. Si hivyo tu, lakini pia na madai mengine yote mahsusi kwa dhambi mahsusi nayo ni lazima yatimizwe.
Tumalizie kwa kusoma Warumi 7 aya 1 mpaka ya 5.
“Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.” (Warumi 7:1-5).
Sasa tuangalie maana ya hiyo Warumi 7:1-5:
Inamaanisha kuwa Mtu ukitaka kumfuata Yesu na wakati huohuo unaishi chini ya torati wewe ni kama ‘mzinzi’.
Ukishika torati basi unakuwa kama mtu aliye olewa na torati. Na ukishika neema ya Yesu Kristo, basi unakuwa ni kama mtu aliye olewa na Injili. Sasa, kushika yote mawili kwa wakati mmoja, ni sawa na mwanamke aliye kuwa na waume wawili na humfanya huyo mwanamke kuwa mzinzi.
Kama tukiishi kwa sheria ya Musa tunazalia mauti mazao, lakini tukiishi kwa imani katika Kristo, tutamzalia Mungu matunda!
Ndugu msomaji, uchaguzi ni wako, nini unataka kufuata. Yesu ambaye ni Bwana wa Sabato au Sabato, kumbuka kuwa huwezi kufanya yote mawili kwa wakati mmoja; aidha utakuwa mzinzi kuhusu Injili kwa kufuata torati wakati huohuo unafuata injili!
Ni mimi Dr. Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo,
For Max Shimba Ministries Org,
MAX SHIMBA MINISTRIES ORG ©2016. ALL RIGHTS RESERVED
Everyone is permitted to copy and distribute verbatim copies of this license document, but changing it is not allowed.

2 comments:

Paccowilly said...

Amen, na shukrani Kwa neno hili

Unknown said...

Kama hatupaswi kushika torati, nini maana ya lile fungu aliposema "mkinipenda mtazishika amri zangu?" Na hizo amri alizokua anazungumzia ni zipi kama sio torati?!

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW