Tuesday, November 1, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA KUMI NA MOJA)


Baada ya kufahamu kuwa, kushika torati kunaambatana na Torati ya Musa “Sehemu ya Kumi”, sasa tuangalie, Je, Sabato ilikomeshwa?
Je, unafahamu kuwa agizo la kushika siku ya sabato na torati yote kwa ujumla, ilikuwa ni huduma ya mauti au huduma ya adhabu ya kifo?
Siandiki mada hii kuhusu “SABATO” kwa sababu napenda kushindana na watu! La hasha! Kwa upande moja, napenda kuondoa utata juu ya mada hii. Kwa upande mwingine, inanihuzunisha sana na nasikia uchungu kuona watu na au Wakristo wenye nia njema tu ya kufanya mema, lakini wanatumia njia au sheria ambayo haina nguvu na ni kivuli tu, huku tukiwa na Yesu ambaye ndie Bwana wa Sabato.
UTHIBITISHO:
Katika kitabu cha 2 Wakorintho 3:7-8 tunasoma, “Basi, ikiwa huduma ya mauti iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika. Je huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?”
Kwa hiyo torati yote ikiwemo kushika sabato, ilikuwa ni huduma ya mauti. Pia torati haikuwa huduma ya mauti tu, bali ilikuwa ni nguvu za dhambi, kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha 1 Wakorintho 15:56, “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.”
Kwa kadiri unavyozidi kuifuata torati ndivyo nguvu ya dhambi inavyozidi, kwa kuwa torati kazi yake ni kubaini makosa. Haina tofauti na darubini ya kupima vijidudu vya magonjwa. Kwa vile torati ilikwisha tolewa katika agano la kale na imetufanya kujua dhambi nini; hivyo katika agano jipya, haupaswi tena kuifuata torati, bali tunapaswa kuifuata dawa ya dhambi, ambayo ni Bwana wetu Yesu Kristu.
UTHIBITISHO:
Warumi 8:2 Biblia inasema, “Kwa sababu sheria ya Roho ya uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.”
Kwa ujumla ni kwamba, torati ilikuwa ni huduma ya mauti, kwa kuwa sheria walizoshindwa kuzifuata Wana wa Israeli, iliwalazimu kuuawa. Watu wengi walikufa kwa nguvu ya torati; mfano mtu ambaye hakushika sabato aliuawa (Kutoka 31:14-15; Kutoka 35:2-3).
Mtu aliye jaribu kukusanya kuni siku ya sabato kwa kusudi la kujipikia chakula aliuawa (Hesabu 15:32-36).
Watu wagonjwa hawakutakiwa kutibiwa siku ya sabato hivyo kusababisha watu wengi kufa (Luka 13:14), kitu ambacho si mpango wa Mungu.
KUMBE HATA WAISRAELI WALISHINDWA KUISHIKA TORATI
Hata hivyo, pamoja na torati kuwa ni huduma ya mauti, pia Wana wa Israeli wenyewe, hawakuweza kudumu katika lile agano la kwanza walilofanya na Mungu, hivyo kufanya agano hilo, kutofanikiwa;
UTHIBITISHO:
Yohana 7:19 tunasoma, “Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati.”

KWANINI AGANO HUVUNJWA AU VUNJIKA?

Ni vema ifahamike kuwa, kinachofanya agano kudumu, ni kutimizwa kwa masharti au sheria au taratibu za agano husika. Katika agano lolote au mkataba wowote ule, ni lazima kuwepo kwa masharti au sheria zilizowekwa, ili kuulinda mkataba au agano hilo. Kwa hiyo mtu anayevunja sheria katika mkataba au agano fulani, tayari yeye, ndiye anayekuwa amevunja huo mkataba au hilo agano. Wana wa Israeli walifanya agano na Mungu, na agano hilo lililindwa na vifungu vya sheria ambavyo ni torati yote; sasa kwa vile wote walikosa kuitendea kazi torati kama tunavyoona katika Yohana 7:19; Ezekieli 20:21, hivyo, kitendo cha kutoitendea kazi torati, tayari walikwisha vunja agano la kwanza na siyo Mungu. Na ndiyo maana zama za Nabii Isaya, Bwana alimtumia Nabii huyo kuwaambia wana wa Israeli kwamba yeye hataki tena sabato zao na ibada zao; Isaya 1:13 tunasoma, “Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na SABATO, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.”
Vitu hivi vyote, havikuwa na maana tena mbele za Mungu kwa kuwa tayari wana wa Israeli walikwisha liharibu Agano Lake. Na kama agano lilikwisha haribika, kushika sabato na ibada zao zilikuwa na maana gani mbele za Mungu? Hivyo kwa huruma yake, aliamua kufanya mpango mpya wa kuweka agano jipya na sheria zikiwa zimeboreshwa.
Kabla ya kukomeshwa kwa sabato na agano la kwanza kwa ujumla, Mungu kwa hekima yake alianza kuwatumia manabii kutoa matangazo juu ya ujio wa agano jipya na kukomeshwa sabato;
MANABII WALITABIRI KUKOMESHWA KWA TORATI
UTHIBITISHO WA NABII HOZEA:
Nabii Hosea alitoa unabii juu ya kukomeshwa kwa sabato na siku za kusanyiko zilizoamriwa. Hosea 2:11 tunasoma, “Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, NA SABATO ZAKE, na makusanyiko yake yote yalioamriwa.”
UTHIBITISHO WA MUSA:
Baada ya kutofanikiwa kwa torati, Musa alitangaza kabisa ujio wa mdhamini wa agano jipya (Bwana Yesu) na ujio wa sheria ya Kristo. (Kumbukumbu 18:15-19).
UTHIBITISHO WA ISAYA:
Nabii Isaya alianza kupiga debe juu ya ujio wa agano jipya (Isaya 55:3).
UTHIBITISHO WA YEREMIA:
Yeremia naye hakubaki nyuma, naye alianza kupiga mbiu juu ya agano jipya (Yeremia 31:31; 32:40).
SABABU ZA NYONGEZA ZA KUKOMESHWA KWA SABATO NA TORATI YOTE KWA UJUMLA
TORATI ILIKUWA NI KIVULI:
Torati ilikuwa ni kivuli tu cha mema yatakayo kuja na haikuwa kitu halisi.
Waebrania 10:1 tunasoma, “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuja, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao.” Sabato ni sehemu ya torati, hivyo wanaoshika sabato, ni vema waelewe kuwa, sabato si kitu halisi, ilikuwa ni kivuli tu.
KORATI ILIKUA KUTULETEA YESU:
Torati ni kiongozi tu cha kutuleta kwa Yesu.
Wagalatia 3:24-26 tunasoma, “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.” Mfano; Wewe ni mgeni, na umefika maeneo ambayo unataka kukutana na mwenyeji wako, na wakati huo huo, ukakutana na mtu usiyemjua, na kwa baati nzuri huyo mtu, akasema kuwa mwenyeji wako unayemtafuta, ninafahamu alipo, hivyo, akaamua kukupeleka. Baaada ya huyo mtu kukufikisha, je utaamua kumng’ang’ania huyo aliyekupeleka au utabaki na mwenyeji wako, uliyekusudia kufika kwake. Sasa sabato ilikuwa ni kiongozi cha kutupeleka kwa Kristo, sasa kwa sababu tumempata Kristo, hatuhitaji tena sabato.
TORATI ILIKUWA HAINA UWEZO WA KUTOA AU SAMEHE DHAMBI:
Torati ilikuwa haiondoi uhitaji yaani ilikuwa haitibu dhambi bali ilikuwa ikibaini dhambi na kuadhibu.
2 Wakorintho 3:15-16 tunasoma, “Ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.”
KUWA CHINI YA TORATI NI KUWA CHINI YA LAANA:
Kuwa chini ya torati ni kuwa chini ya laana, kwa sababu ilimlazimu mtu kuifuata torati yote bila kuacha hata kitu kimoja. Hii haikuwezekana, hivyo kuwafanya watu wote kuwa chini ya laana (Wagalatia 3:10; 5:3-4).
TORATI HUCHOCHE KUTENDA DHAMBI:
Torati huchochea nguvu ya dhambi (1 Wakorintho 15:56).
ANGALIZO MUHIMU:
1. Torati (ikiwemo na sheria ya kushika sabato) pamoja na manabii, vilikuwapo mpaka Yohana mbatizaji; Luka 16:16 Biblia inasema, “Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu, hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.” Kwa hiyo, kushika sabato ilikuwa mwisho wake nyakati za Yohana Mbatizaji na siyo nyakati hizi za Agano jipya.
2. Watu waliompokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao, hao ni wahudumu wa Agano jipya; 2 Wakorintho 3:6, tunasoma, “Naye ndiye aliyetutosheleza, kuwa wahudumu wa Agano jipya; si wa andiko, bali wa Roho, kwa maana andiko huua, bali Roho huhuisha.”
3. Katika nyakati hizi za Agano jipya, hatuifuati torati bali tunaifuata sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2). Wagalatia 5:14 tunasoma, “Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, umpende jirani yako kama nafsi yako.” Kitabu cha Mathayo 22:37-40 tunasoma, “Akamwambia, mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi, hutegemea torati yote na manabii.” Hizi zote ni miongoni mwa sheria ya Kristo; Wagalatia 6:2 inasema, “Mchukuliane mizigo na kuitimizwa hivyo sheria ya Kristo.”
4. Bwana YESU alifanya kazi siku ya sabato (Yohana 5:16-18; Yohana 9:16), lakini bado Biblia inasema hakufanya dhambi (Waebrania 4:15). Kushika sabato nyakati za leo ni maagizo ya waanzilishi wa dhehebu hilo na siyo maagizo ya Bwana YESU (Waanzilishi hao ni William Miller 1782-1849; Hiram Edson; Joseph Bates na Hellen Gould White).
5. Mpendwa mtoto wa Mungu, kushika sabato katika Agano jipya si maagizo ya Mungu, kamwe usikubali kuifuata, maana utatolewa kutoka katika uanafunzi wa Yesu na kuwa mwanafunzi wa Musa. Na isitoshe neno la Mungu katika Wakolosai 2:16 linasema, “Mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO. Mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” Mtu akikwambia kuhusu kushika sabato au sheria za kutokula vyakula na kunywa vinywaji, mwambie, “Siwezi kushika kivuli, maana Biblia inasema hayo yote yalikuwa ni kivuli cha mambo yajayo, bali ninamshika Kristo.”
6. Anayeitegemea torati (ikiwemo na sabato), huyo ni kiongozi kipofu, mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga. Warumi 2:17-20 tunasoma, “Lakini wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, na kujua hakika ya kuwa wewe mweyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati.”
AGANO JIPYA, LILIKUJA ILI KUKUKOMBOA KUTOKA TORATI
Sasa basi, baada ya kusoma kuwa, hata Manabii wa kwenye agano la kale walitabiri kukomeshwa kwa torati aliyo pewa Musa, kama ukielewa mambo haya, umeshatambua ya kwamba Agano Jipya siyo jambo la kupata Roho Mtakatifu ili wewe uweze ‘kuishi kwa torati’ wala ‘kuwa chini ya torati’ wala ‘kushika torati ya Musa.’

Ndugu msomaji, kupitia Agano Jipya “Yesu Kristo” sisi huzaliwa mara ya pili toka juu, sisi huzaliwa na Mungu, sisi hutokana na Mungu, na tunaishi siyo kwa sheria bali kwa uzima ule ambao Mungu ameweka ndani yetu! Kama ilivyoandikwa, “kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali KIUMBE KIPYA” na tena, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya, Lakini vyote pia vyatokana na Mungu.” (Galatia 6:15; 2 Korintho 5:17,18). Na Petro anatangaza, “Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU…” (2 Petro 1:4).
Ni matumaini yangu na dua yangu kuwa hata mmoja ataguswa moyoni mwake kwa somo hili na Mungu afungue macho yako kuuona wokovu ule ambao uko ndani ya Kristo Yesu!
Tumefika mwisho wa Sehemu ya KUMI NA MOJA, na sasa tutaenda SEHEMU YA KUMI NA MBILI
JE, UNAZIFAHAMU SABABU ZINAZOWAFANYA WAKRISTO KUABUDU JUMAPLI?
********** USIKOSE SEHEMU YA KUMI NA MBILI ***********
Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW