Thursday, October 27, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA NANE)



JE, UNAZIFAHAMU SABABU ZILIZOMFANYA BWANA YESU KUINGIA HEKALUNI SIKU YA SABATO?
Wasabato wa karne hii, wanadai kuwa, kitendo cha Yesu kuingia Hekaluni/Sinagogi ni ushahidi tosha kuwa Yesu alikuwa Msabato na au alikuwa anatunza Sabato. Lakini wanashindwa kuelewa kuwa, Yesu aliingia Hekaluni siku ya Jumamosi KUHUBIRI HABARI NJEMA [kuvua Samaki] na sio kutunza siku, maana Yesu yeye ndie Bwana wa Sabato.
USHAHIDI KUHUSU SIKU YA SABATO:
Biblia inasema, Matendo 13:13-15 “Kisha Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri kutoka pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Kisha baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, NDUGU, KAMA MKIWA NA NENO LA KUWAFAA WATU HAWA, LISEMENI.”
SABABU YA YESU KUINGIA HEKALUNI:
Katika karne ya kwanza, kwenye Mahekalu/Masinagogi KULIKUWA NA UTARATIBU kwamba, baada ya kusoma torati na chuo cha manabii, wakuu wa Masinagogi, walikuwa wakikaribisha watu, waliokuwa na jambo jema la kuwaambia watu kwenye kusanyiko.
Ndio maana wahubiri kama Bwana Yesu na Paulo, hii kwao ilikuwa ni fursa na au nafasi ya pekee sana ya kuwahubiria Wayahudi habari njema za ufalme wa Mungu, kwani walikuwa wamepotea kwa kuendelea kushika sheria ya sabato na mapokeo mengine. Kwa hiyo, Bwana Yesu na Mhubiri kama Paulo walitumia nafasi hii, kuwafikishia Mafarisayo na Wayahudi wengine habari njema, kwa kuwa siku ya sabato, watu wengi walifika hekaluni.
Hivyo basi, Bwana Yesu na mitume kama Paulo, hawakwenda hekaluni kukusanyika kwa kusudi la kushika au kutunza sabato au kushiriki kusanyiko la Wasabato, bali waliwafuata Wayahudi waliokuwa bado wamefungwa na mzigo wa sabato “sheria” na mapokeo mengine. Na kwa kulithibitisha hilo, Bwana Yesu, alikuwa akienda hekaluni kila siku kufundisha, na siyo siku ya sabato tu.
YESU ANAFUNDISHA HABARI NJEMA KILA SIKU KWENYE HEKALU/SINAGOGI NA SIO JUMAMOSI PEKE YAKE KAMA WANAVYO DAI WASABATO
UTHIBITISHO:
Luka 19:47 tunasoma, “Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza.”
Luka 21:37 tunasoma, “Basi kila mchana, alikuwa akifundisha hekaluni, na usiku huenda kulala katika mlima uitwao wa Mizeituni.”
Zaidi ya hapo, katika Yohana 18:20 tunasoma, “Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu wazi wazi; siku zote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote.”
Kwenye aya za hapo juu, tumemsoma Bwana Yesu na anathibitisha kuwa alikuwa akienda kwenye sinagogi na hekalu kila siku ili kufundisha watu, kwani ilikuwa ni sehemu ambayo angeweza kuwapata Wayahudi, hivyo kumpa nafasi ya kufundisha kweli ya neno la Mungu. Kwa lugha nyingine, Yesu alikuwa anavua Samaki.
WASABATO WANADAI KUWA SABATO NI YA MILELE, JE HAYA MADAI NI KWELI?
Wasabato hudai kwamba, sheria ya kushika sabato haijakomeshwa na inaendelea hata sasa kwani imeamriwa kuwa ni agano la milele kama Biblia inavyosema katika Kutoka 31:16, “Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika sabato, kuiangalia sana hiyo sabato, katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.”
NINI MAANA YA NENO MILELE KAMA LILIVYO TUMIWA KWENYE “KUTOKA 31:16”?
Kabla hatujaingia kwa undani zaidi katika kutafuta ukweli wa hoja hii, ni vizuri, watu wakielewa maana ya neno MILELE kwa msingi wa maisha ya duniani. Neno MILELE, likitumika kwa matumizi ya kidunia haimaanishi isiyo na mwisho, kwa kuwa hakuna umilele kwenye maisha ya hapa duniani, bali humaanisha muda mrefu. Lakini neno MILELE, likitumika nje ya matumizi ya kidunia, mfano maisha baada ya kufa, hapo ndipo milele humaanisha “isiyo na mwisho”. Kwa ujumla, siyo kila palipoandikwa kwenye Biblia MILELE, inamaanisha isiyo na mwisho.
UTHIBITISHO:
Kwa mfano, katika kitabu cha 1 Samweli 27:12 tunasoma, “Hivyo akishi akamsadiki Daudi, akasema, amewachukiza kabisa hao watu wake Israeli; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu hata MILELE”
Daudi anatangazwa kuwa ni mtumishi Akishi hata milele, lakini, ebu tujiulize, kama kila litumikapo neno milele, lina maana isiyo na mwisho, je Daudi aliendelea kuwa mtumishi wa Akishi? Je baadaye hakuwa Mfalme? Akishi hapa, alimaanisha kwamba, Daudi kuwa mtumishi wake kwa muda mrefu.

UTHIBITISHO:

Mfano mwingine ni pale Bath-sheba alisema, “Mfalme Daudi na aishi MILELE.” (1 Wafalme 1:31), Bath-sheba alijua kuwa mwanadamu hawezi kuishi duniani bila kuwa na mwisho, hivyo hapo alimaanisha Mfalme Daudi aishi kwa muda mrefu. Pia Kumbukumbu 15:17 imezungumzia mtumishi wa milele; hapa haimaanishi mtu anakuwa mtumishi kwa muda usiyo na mwisho bali kwa muda mrefu.
JE, MUNGU ALIMAANISHA NINI ALIPO TUMIA NENO LA MILELE KWENYE AGANO LA KUSHIKA SABATO?
Mungu alipotumia neno milele kwenye agano la kushika sabato, hakumaanisha isiyo na mwisho, bali alimaanisha ni agizo la muda mrefu mpaka wakati wa kuikomesha ulipofika. Na kama, alimaanisha milele ikiwa na maana ya isiyokoma, je hiyo sabato itashikwa mpaka mbinguni? Na mbinguni hakuna kuhesabu siku hata tukapata siku ya jumamosi. Pia kama ingekuwa milele ya isiyo koma, basi kulikuwa hakuna haja ya Bwana Yesu kuja duniani na kuleta agano jipya, na wala hakukuwa na haja ya Yeye kuwa kinyume na sabato, kama tulivyo kwisha kuona hapo nyuma.
YESU NDIO MWANZO NA MWISHO WA SABATO:
Bwana Yesu ni Mungu, Yeye ndiye aliyeiweka sabato iwe kama kitu cha kumwakilisha, alipokuwa kabla ya hajakuja duniani. Baada ya kuja alikuwa na mamlaka ya kuiondoa sawasawa na makusudi yake. Ni sawa tu na tunapotoa matangazo ya kuja kwa muhubiri fulani au muimbaji fulani, huwa tunaweka picha yake kwenye vipeperushi na matangazo, lakini muhubiri au muimbaji huyo akishafika, hatuendelei kuangalia picha zilizo kwenye vipeperushi na matangazo, bali tunatupa vyote na kwenda kumwona uso kwa uso.
JE, YESU ALIMAANISHA NINI ALIPO SEMA MSIDHANI KUWA NIMEKUJA KUTENGUWA TORATI AU MANABII; LA, BALI KUTIMIZA?
Hoja nyingine kutoka kwa wasabato hujengwa katika kitabu cha Mathayo 5:17-18 inayosema, “Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, BALI KUTIMILIZA. Kwa maana, amini, nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.”
Hoja inayojengwa na wasabato katika andiko hili, ni kwamba, Bwana Yesu anakiri hajakuja kutangua torati wala manabii bali amekuja kuitimiliza, yaani wakimaanisha kuwa, naye amekuja kuishika sabato. Watoto wa Mungu, hii hoja ni ya undanganyifu. Kuupata ukweli, ni vizuri turudi kwenye Biblia ya Kiingereza ya toleo la King James ili tupate tafsiri nzuri zaidi. Mathayo 5:17, “Do not think that I came to destroy the law or the prophets. I did not come to destroy but to FULFILL…..” Kadhalika na matoleo mengine ya Kiingereza, neno ‘Kutimiliza’ kwa Kiingereza limetumika ‘FULFILL’. Kulingana na kamusi ya Kiingereza, neno ‘fulfill’ lina maana zifuatazo; maana ya kwanza ya ‘fulfill’ ni ‘fill up’ yaani ‘jazia.’ Kwa hiyo inaleta maana ya kwamba, Bwana Yesu, hakuja kuitangua bali amekuja kuijazia (fill up), kwani kulikuwa kuna mapungufu katika lile agano. Na ndiyo maana katika kitabu cha Waebrania 8:7 tunasoma, “Maana kama lile la kwanza, lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili.”
Maana ya pili ya ‘fulfill’ ni ‘an act of doing something to satisfaction’ ikiwa na maana kwamba ni kitendo cha kufanya kitu ili kifike kwenye utoshelevu. Kwa hiyo, Bwana Yesu hakuja kuitangua torati na manabii, bali amekuja kuboresha ili ifikie utoshelevu, maana bado torati na manabii, haikuleta utoshelevu wala kuleta matokeo mazuri kwa watu, kwani kila kukicha watu walikuwa wakiuawa kwa kushindwa kuiishi torati. Maana ya tatu ya ‘fulfill’ ni ‘an act of achieving goal’ kwa Kiswahili inamaanisha ni kitendo cha kufanya kitu kifike kwenye malengo.
Kwa hiyo kwa lugha nyingine tungeweza kusema kwamba, Bwana Yesu amekuja kuifanya torati na manabii iweze kufikia malengo aliyokusudia, kwa sababu bado ilikuwa na shida kulingana na uwezo wa mwanadamu. Sasa kwa lugha fasaha ni kwamba, Bwana Yesu, hakuja kuiondoa torati na manabii, bali alikuja kufanya maboresho, marekebisho, masahihisho; ikiwa na maana kwamba kilichotakiwa kuondoka kiliondoka, na kilichotakiwa kubaki, kilibaki; na hii ilifanya na chekecho la msalaba. Mfano, mambo ya kushika sabato yaliondolewa, kwa sababu sabato ilikuwa ni amri ya ishara, ilikuwa ni kivuli, ikimuashira Yeye Bwana Yesu mwenyewe kama pumziko la kweli la kiroho. Hivyo, kwa vile Yeye pumziko halisi amekuja, sabato haikuwa na kazi tena. Bwana Yesu anasema, “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao, na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”(Mathayo 11:28)
Upungufu wa Agano la lake unaozungumziwa katika Waebrania 8:7, haupo katika torati, kwani torati kwa asili, haina tatizo na ni njema maana ni maagizo ya Mungu mwenyewe. Tatizo lilikuwa kwenye uwezo wa wanadamu wenyewe katika kuifuata torati yote kwa nguvu zao; maana kipindi cha agano la kale, walipewa sheria na hukumu tu, lakini hawakuwa na neema ya kuwafanya washike hiyo sheria. Kwa hiyo, kimsingi wana wa Israeli waliipenda torati (sheria) na hukumu walizopewa na Mungu, na waliikubali hiyo torati (sheria) na hukumu, na ndiyo maana walikubali kufanya agano na Mungu, kwa kuwa kila agano ni lazima kuwepo kwa makubaliano katika pande mbili.
Mioyoni mwao waliikubali na kuipenda torati (sheria) na hukumu zake, lakini mwili uliwazuia kuitekeleza hiyo torati, kwa kuwa walipewa torati (sheria) na hukumu tu bila neema au kiwezesho cha kuiishi sheria. Sasa hapo ndipo tunapopata upungufu wa Agano la kale.
UTHIBITISHO:
Katika kitabu cha Warumi 7:14-16 tunasoma, “Kwa maana twajua kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo; kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda.Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.”
Kama nilivyo kwisha kusema hapo nyuma kwamba, wana wa Israeli waliipenda torati na hukumu. Lakini katika viungo vya mwili yaani utu wa nje, sheria ilikuwa ni kama ni mzigo mzito sana; kwa sababu kwa asili, ndani ya mtu halikai neno jema. Na kwa sababu hiyo, wana wa Israeli hawakuweza kudumu katika Agano la kale kama maandiko yanavyotuambia katika, Waebrania 8:9, “Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. KWA SABABU HAWAKUDUMU KATIKA AGANO LANGU, mimi nami sikuwajali, asema Bwana.”
Pia katika kitabu cha Ezekieli 20:21 Biblia inasema, “Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu; ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.”
Kwa ujumla ukisoma vitabu vyote vya Musa, utagundua kwamba wana wa Israeli hawakukaa vizuri kwenye sheria na hukumu za lile agano. Ndipo Mungu kwa huruma yake akaleta Agano lingine, lililo bora zaidi kuliko lile la kwanza, na mdhamini wa Agano hili ni Mungu mwenyewe, wakati Mdhamini wa agano la kale alikuwa mwanadmu (Musa). Waebrania 7:22 tunasoma, “Basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.”
Hivyo basi, ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika, kuwa mweka sheria katika Agano la kale, amekuja kurekebisha sheria na kufanya Agano upya, hivyo lile la kwanza kutotenda kazi; Waebrania 8:13 tunasoma, “Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.”
BAADHI YA WASABATO HUDAI KUWA HAKUNA KUOKOKA DUNIANI, JE, HAYA MADAI NI KWELI?
Wasabato hudai kwamba hakuna kuokoka duniani na wala hakuna watakatifu, na wanasimamia hoja hiyo katika maandiko yafuatayo; Mhubiri 7:20; Warumi 3: 12, 23; Warumi 5:12; Zaburi 14:3.
NINI MAANA YA KUOKOKA?
Kabla hatujaingia kwa undani zaidi, si vibaya kama tutafahamu maana ya neno kuokoka kama linavyotumiwa na watoto wa Mungu.
Kuokoka maana yake ni kusalimika kutoka katika hatari iliyo dhahiri. Kwa mfano, mtu aliyesalimika kufa kwenye ajali ya gari, mtu huyo tunasema ameokoka na ajali ya gari.
Kuokoka katika dhana ya Kiroho, haina tofauti sana na maana tuliyoizungumzia hapo nyuma, lakini utofauti wake upo kwenye aina ya hatari.
Mtu ambaye hajamwamini na kumkiri Bwana Yesu, ni wazi kabisa yupo katika hatari ya kwenda kwenye hukumu ya mateso ya moto wa milele, kama maandiko yanavyotuambia katika Yohana 3:18; Yohana 5:22. Lakini kwa mtu ambaye amemwamini Mwana wa Mungu, huyo haukumiwi, kwa maana hiyo, mtu huyo anakuwa ameokoka au amesalimika na hatari ya kwenda kwenye mateso ya moto wa milele;
UKIMWAMINI YESU NA KUBATIZWA UTAOKOKA?
Yohana 3:18 tunasoma, “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” Marko 16:16 Maandiko yanasema, “Aaminiye na kubatizwa ATAOKOKA; asiyeamini atahukumiwa.” Waefeso 2:5 Maandiko yanakiri kwamba tumeokolewa kwa neema. Kadhalika maandiko katika Isaya 45:20 tunasoma, “Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa MATAIFA MLIOOKOKA…..”
Jambo la msingi ambalo watu wanapaswa kufahamu ni kwamba, baba yetu Adamu alipofanya dhambi, na sisi wanadamu wote, tukahesabiwa kuwa tuna dhambi kama maandiko yanavyosema katika Warumi 5:12. Kwa hiyo, kama kwa kuasi kwake baba yetu Adamu, na sisi sote tukaingizwa katika hali ya wenye dhambi, basi kwa kutii kwake mmoja ambaye Bwana wetu Yesu Kristo, na sisi tunaomwamini tumeingizwa katika hali ya wenye haki yaani utakatifu (Warumi 5:19).
LOGIC “MAANTIKI”
Adamu alipokosea na sisi tukawa tumekosea, Bwana Yesu alipopatia na sisi tukawa tumepatia.
Kwa hiyo ni dhahiri kabisa kuokoka ni hapa duniani, na wakamilifu wapo duniani, na Zaburi 16:3 maandiko yanasema, “Watakatifu waliopo duniani ndiyo walio bora, hao ndio niliopendezwa nao.” Paulo anawaita wenzake watakatifu, 2 Wakorintho 13:13 tunasoma, “Watakatifu wote wawasalimu.” Paulo pia anathibitisha kuwepo kwa watakatifu duniani katika Wafilipi 4:21-22 tunasoma, “Msalimieni kila MTAKATIFU katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wawasalimu. WATAKATIFU wote wawasalimu, hasa wao walio wa nyumbani mwa Kaisari.”
Mungu mwenyewe anamthibitisha Ayubu kuwa alikuwa mkamilifu (Ayubu 1:8). Maandiko yanatuthibitishia kuwa Nuhu pia alikuwa mtu wa haki na mkamilifu (Mwanzo 6:9). Watoto wa Mungu, ukamilifu tunaupata hapa hapa duniani na siyo mbinguni, na ndiyo maana Bwana Yesu anasema katika Mathayo 5:48, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” (Soma pia Waebrania 12:14, Walawi 19:2).
Tumefika mwisho wa Sehemu ya NANE, na sasa tutaenda SEHEMU YA TISA.
Wasabato hudai kwamba, Wakristo wanaofanya ibada zao siku ya jumapili, ni makosa mbele za Mungu, maana siyo agizo la Mungu bali ni agizo la mwanadamu, Je, haya madai ni kweli?
********** USIKOSE SEHEMU YA TISA ***********
Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW