Friday, October 21, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA TATU)

Baada ya kusoma Sehemu ya Pili inayozungumzia Bwana Yesu Kuingia kwenye Sinagogi, sasa tuwaangalie Mafarisayo na nini walisema kuhusu Yesu Kristo.
Nitaanza na kuwalezea maana ya Mafarisayo. Je, Mafarisayo ni akina nani hasa? Mafarisayo waliunda madhehebu mojawapo ya Uyahudi ambayo wakati wa Yesu Kristo liliweza kufikia 5% ya Wayahudi wote, lakini lilikuwa na athari kubwa katika jamii yao, kutokana na sifa ya kuwa wanadini hasa. Jina lenyewe lina maana ya waliojitenga (na wakosefu) ili kushika kiaminifu masharti yote ya Torati ya Musa.
Mafarisayo wanajulikana hasa kutokana na Injili ambazo zinawataja kwa kawaida kama wapinzani wa Yesu, ingawa yeye alikuwa anakubaliana nao katika mafundisho mengi ya imani tofauti na yale ya Masadukayo, madhehebu nyingine kubwa iliyokuwa na wafuasi hasa kati ya makuhani.
Mafarisayo walianza mwishoni mwa karne ya 2 K.K. na kuendelea kustawi hadi mwaka 70 B.K. , ambapo Yerusalemu iliteketezwa na Warumi. Maangamizi ya hekalu yalivunja nguvu ya Masadukayo na kuwaachia Mafarisayo uongozi wa dini yao.

Mafarisayo ambao walikuwa WADINI au naweza kusema wenye siasa kali katika dini [utunzaji wa torati ya Musa], walimshitaki Yesu Kristo kwa Makuhani kwa kuwahusu wanafunzi wake wavunje sheria ya Musa ikiwa ni pamoja na kuvunja sabato (Marko 2:23-28). Ikimaanisha kuwa, mbele ya macho ya hawa Mafarisayo, Bwana Yesu na Wanafuzi wake walikuwa wanavunja Torati/Sabato. Je, Bwana Yesu aliwajibuje mashtaka ya hawa Mafarisayo? Hebu angali jinsi Yesu anavyo jibu kwa kutumia hekima! Bwana Yesu anawakumbusha Mafarisayo jinsi Mfalme Daudi alivyo vunja ya sheria.
Moja: Torati ya Musa inasema kuwa ni Makuhani pekee ndio walitakiwa kula mikate lakini tunamsoma Daudi akiingia ndani ya Hema na kuila Mikate, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Musa! Je, kwanini Yesu alifanya na au toa huu mfano wa Daudi kula Mikake? Katika mfano huu, tunajifunza kuwa Yesu anamtetea Daudi alipo kula Mkate ingawa alicho fanya Daudi kilivunja aya katika Hesabu 24: 5 mpaka 9.
Mbele ya Macho ya BWANA, uhai wa Mfalme Daudi alikuwa ni bora Zaidi kuliko kuto kula Mkate, ndio maana Yesu alisema, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, wala si mwanadamu kwa ajili ya sabato.” Kwa maneno hayo Bwana Yesu anaweka wazi kabisa kwamba sabato iliwekwa kwa ajili ya KUMTUMIKIA MWANADAMU na siyo iwe ‘bwana’ juu yake!
Hebu tumsome kwanza Yesu: Yesu alipomponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa muda wa miaka 38, alimwambia ‘jitwike godoro lako, uende.’ (Yohana 58). Hii ilikuwa ni siku ya sabato.
Lakini tunaona kwamba Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwambia, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. (Yohana 5:10). Bila shaka walisema hivi kwa kuwa walifahamu fika jinsi sabato inavyotakiwa kutunzwa.
Hii ni kusema kwamba, kwa kadiri ya kanuni za utekelezaji wa sabato, hili lilikuwa ni kosa. Sasa, swali ni kwamba, kwa nini Yesu alivunja sabato kwa kumruhusu yule mtu abebe godoro?

Wayahudi walipomkasirikia Yesu kwa sababu ya kumruhusu yule mtu kubeba godoro siku ya sabato, Bwana Yesu aliwajibu kwamba: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. (Yohana 5:17). Haya ni maneno ya ajabu sana. Wewe uliye Mungu ulituambia kwamba siku ya sabato tusifanye kazi bali tupumzike; tumemwona mtu anafanya kazi ya kubeba godoro, tumekuja kwako, lakini wewe si tu kwamba hukumkemea, bali unasema tena kwamba na wewe unafanya kazi hata sasa (siku ya sabato)!
Kama sabato hasa ni kuacha kufanya kazi, iweje tena Yesu atamke jambo ambalo ni wazi kabisa linavunja sheria aliyoiweka mwenyewe ya kutofanya kazi; yaani aseme kuwa hata sasa yeye anafanya kazi?
Siku moja Yesu aliingia kwenye sinagogi ambamo mlikuwamo mwanamke mwenye pepo wa udhaifu. Yesu alimponya mama yule.
Hata hivyo, Biblia inasema: Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. (Luka. 13:14).
Maneno haya ya mkuu wa sinagogi yanatuonyesha kwamba, jambo alilofanya Yesu lilikuwa ni kuvunja sabato. Swali ni lilelile, kwa nini Yesu alivunja sabato?
Umeona jinsi ambayo hata Mkuu wa Sinagogi anakasirika alipo mwona Yesu akimponya yule Mwanamke, sembuse Mafarisayo. Unapo msoma Yesu, ndio utapata msingi wa Injili ambayo Bwana wetu Yesu alikuja kutuonyesha au fanya. Hebu msome hapa: “Mwanawa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.” Hiyo sentesi inamaana gani? Hapo Yesu anatuonyesha kuwa mwenye mamlaka ya kuvunja Torati ni yule yule aliye ileta Torati. Mungu aliyetoa sharia kwa Musa kwa kupitia Torati yeye Mungu huyo huyo ndioa anaivunja na au mwenye uwezo wa kuivunja Torati – Yeye ndiye Bwana wa sabato! Na hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyofanya kupitia Yesu Kristo Mwanawe wa pekee. Ningependa uelewe kuwa, wakati wa Torati kulikuwa hakuna wokovu ambao tulio nao leo hii, hii inamaanisha kuwa TORATI HAINA UWEZO AU HAINA MAMLAKA YA KUOKOA. Torati ilitolewa kwa mkono wa Musa bali neema, kweli na wokovu zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.
Sasa basi, tunapo zungumzia Sabato na tunapo ona watu leo hii wanapigania kuitunza Sabato, hawa watu au dini au Imani inafanya kosa lilelile ambalo Mafarisayo walifanya katika karne ya kwanza, yaani, wanafanya sabato kuwa ‘BWANA WAO’ na kwa njia hiyo hawamheshimu wala hawamjali Bwana Yesu ambaye ni ‘Bwana wa wote na Bwana wa Sabato’. Biblia inasema kuwa Yesu ni Bwana wa Mabwana. 1Timotheo 6:15 na Ufunuo 19:16.
Je, wewe unaye itunza Sabato, unaona ni haki kumkana Bwana wa Mabwana na kuisujudu siku na/au Kuifanya SABATO ni Bwana zaidi ya Yesu?

YESU KRISTO NI KUHANI MKUU:
Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa “kidunia.” (Waebrania9:1). Lakini “ile sharia haikukamilisha neno” (Waebrania 7:19). Kwa hiyo Mwana wa Mungu alikuja naye “kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa” (Waebrania 10:14). Basi, Kristo Yesu ni kuhani mkuu wetu sasa, na kwa hiyo, “ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike.” (Waebrania 7:19).

Kumbe basi, ndio maana Mweyezi Mungu alifanya Agano Jipya kwa kupitia Mwane Yesu Kristo, “Kwa kule kusema Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka” (Waebrania 8:13). Agano la Kale lilijionyesha kuwa kuukuu Mungu amefanya Agano Jipya!
Kumbe basi lile agano na Musa ni Kukuu na ndio maana Mafarisayo na Masadukayo na Makuhani walio kuwa Yesu anavunja Torati. Sasa tunafahamu kuwa habari zote ndani ya gano la kale ni “KIVULI, Je, unaweza kula na au tegemea KIVULI? Je, unaweza kunywa kivuli? Je, unaweza kushika kivuli?
KUMBE SADAKA WAKATI WA AGANO LA KALE NI KAMA KIVULI? 
“…wako watoao sadaka kama iagizavyo sheria; watumikiao mfano na KIVULI cha mambo ya Mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema…” (Waebrania 8:4,5)

Umesha ona hapo kuwa, kumbe sadaka zote ambazo za ndani ya hema zilikuwa ni mifano ya kivuli tu cha mambo ya Mbinguni. Sasa unapata faida gani kutoa sadaka kivuli?
Kumbe basi mambo ya kiroho ni mambo ya Yesu Kristo. Kumbe basi mambo ya uzima wa milele ni mambo ya Kristo! Sasa kwanini unashika kivuli “SABATO” na kuachana na Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa Sabato?
KUMBE TORATI ILIKUWA NI KIVULI CHA MEMA YAJAYO?

Hebu tusome Waebrania Mlango wa 10 aya ya 1 mapka ya 10 “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha memo yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao…Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi… Mungu aliondoa agano la kwanza ili alilete au alisimamishe agano la pili kwa kupitia Mwanae Yesu Kristo. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.”

Kumbe basi Sabato wanayo itunza ni jambo la kivuli tu, sasa kwanini utunze kivuli wakati teyari tumesha mpata Bwana wa Sabato “Yesu Kristo”? Yesu alikuja na kutukomboa kutoka maisha ya kivuli ambayo ni pamoja na utunzaji wa Sabato. “Maana katika yeye “Yesu” unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye…” (Wakolosai 2:16-18).
Kumbe basi, mambo yote ya Sheria za Agano la Kale yalikuja ili kututayarisha kumjua Masia ambaye alikuja kukamilisha au rekebisha kosa tulilo lifanya pale kwenye Bustani ya Edeni.
VIPINDI VITATU VYA SABATO
Baada ya kuangalia vipindi vikuu vitatu vya uumbaji kuhusiana na mwanadamu kwa kirefu namna hiyo, hebu tuangalie sasa kama sabato nayo inapita katika vipindi hivyo vitatu.
Kipindi cha mfano
Kama ilivyo kwa mambo mengine, sabato nayo ilianza na kipindi cha mfano. Hiki kilikuwa ni kipindi cha Agano la Kale ambacho kilitekelezwa kwa kupitia watu kupumzika kimwili kabisa.
Hii haikuwa ni hali ambayo Mungu alipanga iendelee hivyo hivyo siku zote, bali alikusudia tulione kusudi lake lililo kuu zaidi kupitia kipindi hicho cha mfano.
Kupitia sabato Mungu alikuwa anasema nasi juu ya kitu kingine bora zaidi. Si makusudi yake mawazo yetu yaishie tu kwenye kupumzika kimwili, kujizuia kazi za kimwili, n.k. Ndiyo maana anasema: Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. (Kol. 2:16-17).
Kipindi cha uhalisia wa kwanza
Hiki ni kipindi ambacho ni cha kiimani zaidi. Kimsingi hiki ni kipindi ambacho kinaendelea hadi sasa. Huu ni wakati wa kupumzika kazi za mwili za uovu, yaani kuacha dhambi na kuishi kwa kumtegemea Kristo. Ni maisha ya imani.
Imeandikwa: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28), yaani, nitawapa ‘sabato’. Pia ndiyo maana ya andiko lisemalo: Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. (Mt. 12:8). Sabato iko kwake, si kwenye siku.


Ni maisha ya kujiachia mikononi mwa Mungu ambaye yeye ndiye anayeshughulikia kila kitu katika maisha yetu. Kazi yetu ni kuamini tu kuwa atafanya; naye hakika anafanya. Hilo ndilo pumziko! Hiyo ndiyo raha! Hiyo ndiyo starehe! Hiyo ndiyo sabato!

Kipindi cha utimilifu wa yote
Hiki ni kipindi cha maisha ya mbinguni. Huo utakuwa ni utimilifu wa yote kwa sababu, mara tutakapoingia humo, tutakuwa tukitekeleza sabato halisi milele na milele.
HOJA KUBWA YA WASABATO “SDA” 
Iko hoja kwamba Sabato ni amri ya muhimu sana kwa sababu ilitoka moja kwa moja kinywani mwa Mungu tofauti na amri zingine ambazo zililetwa kupitia manabii au mitume.

Katika Agano la Kale Mungu alisema, “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase…Kwa siku sita, BWANA aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo BWANA akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.” (Kutoka 20:8,11)
Hoja hii haina uzito kwa sababu kuu mbili:
Biblia kwa ujumla wake ni Neno la Mungu ambalo limetoka kinywani mwake lote. Na maandiko yako wazi kwamba: Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa, apate kutenda kila tendo jema. (2 Tim. 3:16-17).
Na kimsingi maandiko haya, ukisoma kwenye Biblia ya Kiingereza, hayasemi “Kila andiko lenye pumzi ya Mungu”. Badala yake yanasema: All Scripture is God-breathed (NIV); au All scripture is given by inspiration of God (KJV). Hii ina maana kwamba: Maandiko yote yametokana na pumzi ya Mungu.
Kwa hiyo, hakuna mantiki kusema kwamba andiko hili lina maana zaidi kuliko lile kwa kuwa hili alitamka Mungu mwenyewe. Yote yana nguvu ileile; yote yametoka kwa Mungu yuleyule.
HOJA ZINAZOTUMIWA NA WASABATO KUISHIKILIA SABATO YA MWILINI
1. WANASEMA MUNGU SI KIGEUGEU 
Yaani Mungu hawezi kusema alafu akaghairi (Malaki3:6) (Zaburi89:34) (Yakobo1:17)

Ni muhimu kujua Biblia inaposema Mungu hana kigeugeu lazima tujue hana kigeugeu anamaanisha nini?
Mungu hana kigeugeu au habadiliki katika ahadi, yaani Mungu akikuhaidi atakubariki na ukakaa katika njia zake, kubarikiwa ni lazima na hata hivyo akikuhadi kukubariki halafu ukaenda kinyume na mapenzi yake hugeuka na kutokutimiza aliyoyaahidi kwako (1Samweli 2:30).
Tukiyachunguza maandiko yote yanayoelezea kuwa Mungu si kigeugeu utaona chanzo cha maandiko haya ni ahadi (Malaki 3:5-6) Mungu anasema “Nita” maana yake anaahidi mambo kadhaa katika mstari wa 5, na katika mstari wa 6 anaeleza kuwa yeye si kigeugeu katika yale aliyoyaahidi katika mstari wa 5.
2. KILA KAZI AIFANYAYO MUNGU ITADUMU MILELE.
Hii nayo ni hoja nyingine, wanasema eti Sabato ni kazi ya Mungu kwa hiyo inapaswa idumu milele wakinukuu andiko linalotoka katika (Muhubiri 3:14) linalosema “Kazi ya Mungu itadumu milele” kwa hiyo Sabato ni kazi ya Mungu inapaswa idumu milele. Biblia inatuonya kwamba tunapaswa kutumia neno la Mungu kwa halali: Maana yake inawezekana kutumia neno la Mungu isivyo halali (2Timotheo 2:15.).
Andiko la (Muhubiri 3:14) halizungumzii Sabato kabisa, kinachosemwa hapo ni kazi ya Mungu, maana ya neno kazi ni kitu cha kufanya kwa mfano; mtu akiwa anapika hiyo inaitwa kazi, mtu akijenga nyumba hiyo inaitwa kazi, mtu akibeba godoro hiyo ni kazi n.k.
Kazi ni lazima itumike nguvu – Swali lakujiuliza je Sabato ni kazi?
Jibu ni hapana. Sabato sio kazi, Sabato ni kutokufanya kazi. Sasa ni nini kilichozungumziwa katika Muhubiri 3:14?

Kinachozungumziwa hapa ni uumbaji wa Mungu ambao ndio kazi ya Mungu. Mungu alifanya kazi ya kuiumba dunia. Mungu alifanya kazi ya kuwaumba wanyama. Mungu alifanya kazi ya kumuumba mwanadamu na hata leo Mungu akifanya kazi yoyote ya kuinua mtumishi ili akahubiri injili. Mungu anafanya kazi kwanza ya kumtafuta ili aokoke, halafu aanze kumfundisha mambo mengi hatimaye anakuwa kiasi cha kuongoza wengine.
Shughuli yote ya kumtafuta mtu dhambini na kumfundisha hiyo inaitwa kazi. Sasa tazama kwa makini maandiko yanayo zungumzia kazi (Mwanzo 2:1-2) unaona Mungu, kuumba anakuita kazi, lakini alipo pumzika hajaita kupumzika kuwa ni kazi, hivyo tunajua Sabato sio kazi. Kuhubiri injili kunaitwa kazi (Marko 16:19-20) Bwana alikuwa anatenda kazi pamoja nao yaani kazi ya kuokoa, kuponya n.k (Matendo 5:34-39) Kuhubiri injili hapo kunaitwa kazi.
3. MUNGU SI MTU HATA ASEME UONGO 
Wakinukuu andiko la Hesabu 23:19 kwa hiyo wanasema eti kwa kuwa Mungu alisema mtaishika Sabato (Kutoka31:16) basi ni lazima kuishika tu na kamwe Mungu hawezi kusema uongo akiagiza kuishika ni lazima iwe kushika, jibu la hoja hiyo ni hili. Ni kweli Mungu si mtu hata aseme uongo lakini ni lazima tuelewe Mungu ni mwamuzi wa yote,yeye ndiye mfanya sheria na pia ndiye muondoa sharia (Isaya 33:22) Mungu akiweka sheria halafu akaiondoa na kuiweka nyingine haimfanyi Mungu kuonekana muongo au haimaanishi kuwa Mungu kasema uongo.

Mungu aliye iweka sheria ya Sabato ya mwilini na ndiye mwamuzi wa kuiondoa na hakuna wa kumuuliza, vyote ni vyake yeye Mungu baada ya kuweka sheria ya Sabato ya mwilini au ya kupumzika Jumamosi akaahidi kuikomesha au kuisitisha au kuivunja (Hosea 2:11) na anatimiza kwa kuivunja (Yohana 5:2-9) kubeba mzigo siku ya sabato ilikuwa ni kuivunja Sabato (Yeremia 17:21) na huyu Yesu aliyevunja sabato ndiye aliye tuamuru watu wote duniani kumuiga Yesu katika yote ikiwemo na la kuvunja Sabato (Mathayo 11:29).
4. WANASEMA MUNGU ALISEMA HAWEZI KULIVUNJA AGANO LAKE NA HAWEZI KUBADILI NENO LILILOTOKA KINYWANI MWAKE
Kwahiyo wanasema Mungu aliweka agano na mwanadamu na agano hilo ni agano la Sabato na kwa kuwa Mungu alisema watu waishike Sabato basi hawezi kamwe kulibadili neno lake.
Wakinukuu maandiko yafuatayo Zaburi 89:34 na Kutoka 20:8-11. Majibu ni haya, ni muhimu kujua andiko hili la Zaburi 89:34 linazungumzia agano gani, kwa kuwa katika Biblia kuna maagano mengi ambayo Mungu alifanya na wanadamu kwa mfano;
Mungu alifanya agano na Nuhu na kizazi chake (Mwanzo 6:18, 9:9,11-12) Mungu alifanya maagano kadhaa na Ibrahim (kama mawili) na maagano hayo alifanya na Ibrahim na vizazi vyake yaani Isaka, Yakobo na watakaofuata. Agano la kwanza ni la kupewa Nchi ya Kanaani ambayo ndiyo Israeli (Mwanzo 15:18, Kutoka 2:24, Zaburi 105:8-11)
Agano la pili ni la kutahiriwa (Mwanzo 17:9-14). Sasa, Mungu aliposema “sitalihalifu agano langu” na "sitalibadili neno lililotoka kinywani mwangu" alikuwa anazungumzia nini?
Hapa alikuwa anazungumzia agano la Daudi, sio agano la Sabato angalia Zaburi 89:3-4,9-34-35) katika agano hilo na Daudi, Mungu hatalihalifu, na hatalibadili neno lililotoka mdomoni mwake alilosema kuwa amefanya agano na mteule wake Daudi, amemwambia Daudi, kuwa wazao wake atawafanya imara milele, na maneno yote yanayosemwa katika Zaburi 89:3-4,19-35 yanazungumzia agano la Daudi sio agano la Sabato.
5. HATA KWENYE MBINGU MPYA NA NCHI MPYA KUTAKUWA NA SABATO YA JUMAMOSI 
Wakinukuu maandiko yafuatayo Isaya 66:22-23, ni muhimu kwa kila asomaye Biblia kufahamu kuwa wakati mwingine maandiko yanaweza kufuatana lakini yakawa hayaoani kabisa katika maana kwa mfano angalia maandiko yafuatayo (Luka 16:17-18), mstari wa 17 unazungumzia uwezekano wa mbingu na nchi kutoweka na kutokutanguka kwa yodi na torati lakini mstari wa 18 unazungumzia jambo tofauti na mstari wa 18 kwani mstari wa 18 unazungumzia kuwa mtu akiacha na kuoa au kuolewa na mwingine anahesabika kuwa ni mzinzi.

Kwa bababu hiyo andiko la Isaya 66:22 ni tofauti na Isaya 66:23, tunawezaje kujua kuwa mstari wa 22 na 23 ni tofauti?
Mstari wa 22 unazungumzia mbingu mpya na nchi mpya lakini mstari wa 23 hauelezei kwenda mbele za Bwana kila Jumamosi huko mbinguni kwani mbinguni hakuna siku wala juma wala mwaka, maana ili ipatikane siku lazima iwepo dunia na jua na dunia ijizungushe kwenye muhimili wake na ndipo ipatikane siku na hatimaye ipatikane Sabato (Jumamosi) sasa mbinguni hakutakuwa na usiku bali kutakuwa na mchana wakati wote (Ufunuo 21:23-25). 
Andiko la Isaya 66:23 linazungumzia unabii utakaotokea katika taifa la Israeli wa watu kukusanyika katika taifa la Israeli, angalia (Zekaria 14:16-19)

6. WANASEMA KUWA YESU ALIITETEA SABATO KWA KWENDA KWENYE SINAGOGI
Wakinikuu maandiko yafuatayo (Luka 4:16, 31). Wanasema kuwa Yesu aliitetea Sabato kwasababu aliingia katika sinagogi tena ilkuwa ni siku ya Sabato ambayo ni siku ya Jumamosi.

Je ni kweli Yesu aliitetea Sabato kwa kuingia katika sinagogi siku ya Sabato?
Yesu kamwe hajawahi kuitetea Sabato, hebu tuchunguze andiko hilo wanalolitumia la Luka 4:16, kwanza lazima tujiulize Yesu alikwenda katika Sinagogi kufanya nini, Yesu hakwenda katika Sinagogi siku ya Sabato kuabudu, Yesu alikwenda katika Sinagogi siku ya sabato kwa lengo la kuwahubiri wale watu waliokuwa katika sinagogi ili waachane na imani ya kisabato na waambatane na imani aliyokuja kuianzisha Yesu yaani imani ya wokovu, kama alivyo mvuvi pale anapogundua mahali fulani kuwa kuna samaki wengi lazima atawafuata kuwavua iwe mchana au usiku, ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu kama mvuvi wa watu.

Hawezi kuacha kwenda kuvua samaki mahali ambapo samaki wapo wengi kwani Yesu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea (Luka 19:10) kwa sababu hiyo Yesu alijua waliopotea wapo katika Sinagogi na wapo siku ya Jumamosi,hivyo ilimlazimu Yesu kuwaendea wale waliopotea katika siku yao ya kuabudu ili awahubiri waifuate imani ya Yesu, hivyo Yesu hakuitunza Sabato kabisa kama wengine wanavyodai kuwa Yesu aliitunza Sabato kwa kwenda kwenye Sinagogi siku ya Sabato na ukitaka kujua kuwa Yesu hakwenda kusali utaona walimbeba na kutaka kumtupa chini ya kilele cha mlima (Luka 4:28-30) mtu gani ambaye anakuja tu kusali kanisani halafu watu wajae ghadhabu na kumtupa chini ya kilele? Hii inatufundisha pia kuwa Yesu hakwenda kusali siku ya Jumamosi, bali alikwenda kuhubiri ndio maana walikuwa kinyume nae.
Andiko la pili ni (Marko 2:27-28), andiko hili linamaanisha nini? 
Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, maana yake ni kwamba Sabato ilifanywa kwa ajili ya kumfuata mwanadamu bali mwanadamu hakufanywa ili aifuate sabato bali mwanadamu aliumbwa ili amuabudu Mungu na Yesu anaposema mwana wa adamu ndiye Bwana wa sabato maana yake mwana wa adamu Yesu Kristo ndiye mkuu wa sabato maana yake Sabato haifuidafu kwa Yesu. Wanaotetea Sabato pia wanatumia andiko hili (Mathayo 12:10) kwa kusema kuwa Yesu aliruhusu kutenda mema siku ya Sabato lakini mambo mengine aliyakataza, hoja hiyo nayo ni hoja dhaifu, Yesu Kristo anaruhusu kutenda mema siku zote na anakataza kutenda mabaya siku zote.

7. WANASEMA KUWA MITUME WALIITETEA SABATO 
Wakinikuu maandiko kadhaa, ambayo tutayaangalia andiko moja baada ya jingine.

Andiko la kwanza: 
(Matendo 13:14-15). Katika andiko hili Paulo na wenzake hawekwenda kusali siku ya sabato, bali walikuwa wanatafuta nafasi ya kuipenyeza injili ya wokovu na hatimaye wakaipata nafasi hiyo, na baada ya Paulo kuhubiri habari za Yesu watu wengi wakaachana na imani ya Sabato na wakaambatana na imani waliyoileta wakina Paulo na ndipo Paulo na Barnaba wakawatia moyo wale walioifuata imani ya Yesu iliyokuwa inahubiriwa na Paulo (Matendo 13:14-43), kwa hiyo kwa ujumla wake kazi waliyokuwa wanaifanya wakina Paulo ilikuwa ni kuingia kwenye makusanyiko ya watu waliopotea ili wawavue kutoka katika imani hiyo potofu na kuingia katika imani ya wokovu wa Yesu Kristo.

Wakati mwingi walifanyiwa fujo kama ilivyokuwa kwa Yesu alivyotaka kuwavua wale watu kwenye Sinagogi (Luka 4:28-30) (Matendo 13:44-51; 14:1-7).
Andiko la pili: 
(Matendo 16:13) hapa Wasabato wanasema Paulo na Wakristo wa Kwanza walikuwa wanatafuta mahali pa kusali siku ya Sabato, ndio Paulo na wenzake kazi yao ilikuwa kuwahubiri waliopotea na kuwaleta kwenye imani iliyo sahihi ya wakovu.

Hivyo Paulo na Wakristo wa Kwanza walijua waliopotea wengi wanasali siku ya Jumamosi na hivyo iliwalazimu wakina Paulo kutafuta mahali ambapo Wasabato wanasali ili wakawavue, hivyo Paulo na wenzake walitafuta mahali pa kusali Wasabato waliokuwa wanakusanyika siku ya Jumamosi. Walitafuta mahali pa kusali kwa lengo la kuhubiri si vinginevyo ndio maana walipokutana na mtu wa kumuhubiri walisitisha safari ili kumuhubiri mwanamke huyu Lidia kwa kuwa lengo lilikuwa ni kuhubiri sio kusali (Matendo 16:13-15).
Hivyo basi, kwa kuwa lengo lilikuwa ni kuwahubiri watu wengi kwa wakati mmoja, walipomalizana na yule mwanamke Lidia, bado waliendelea na safari ya kutafuta mahali ambapo wanasali umati ili waweze kuwavua wengi (Matendo16:13-16).
Andiko jingine (Matendo 17:1-4) andiko hili nalo linaeleza kuwa Mtume Paulo alikwenda kuwahubiri wanaosali Jumamosi ili waifuate imani ya Yesu Kristo, na Paulo alipowahubiria, waliachana na imani yao na kuambatana na imani aliyokuwa nayo Paulo.
Andiko jingine (Matendo 18:1-4) hapa napo Mtume Paulo alikuwa akitoa hoja akijaribu kuwavuta watu wanaosali Jumamosi waifuate imani ya Yesu aliyokuwanayo Paulo.
8. YESU HAKUJA KUTANGUA TORATI WALA MANABII BALI KUITIMILIZA
Wanasema hayo kwa kunukuu andiko la Mathayo 5:17 kwa hiyo wanasema kuwa tunatakiwa kuendelea kuishika sabato kwani Yesu hakuja kutangua torati wala manabii bali uitimiliza sabato. Andiko hili la Mathayo 5:17 linatafsiriwa vibaya karibu na wasabato wote duniani.Tafsiri hiyo inayotolewa na wasabato sio sahihi kabisa, kwani Yesu katika agano jipya katangua mambo kadha wa kadha. Hebu tuyaangalie aliyoyatangua Yesu katika Torati japo kwa uchache;
(a) Katika Mathayo 5:33-37 Yesu anatangua sheria ya kuapa na anasema watu hawatakiwi kuapa kabisa
(b) Pia katika Mathayo 5:38-42 Yesu anatangua sheria ya jino kwa jino na anatutaka tusishindane kabisa na mtu mwovu. Sasa nini alichomaanisha Yesu katika Mathayo 5:17?
Ni muhumu kujua kuwa Yesu Kristo alinenewa mambo mengi katika agano la kale ambayo Yesu alitakiwa kuyatimiza atakapokuja duniani, na alipokuja aliyatimiza.
Hebu tuyaangalie japo kwa uchache aliyonenewa Yesu na alipokuja aliyatimiza.
AHADI UTIMIZWAJI 
Yesu anaahidiwa kutembea juu ya maji (Ayubu 9:8) Yesu anatimiza ahaadi hiyo (Mathayo 14:22-25)

Ahadi ya Yesu kuinuliwa juu (Hesabu 21:4-9) Utimilifu wa Yesu kuiniliwa (Yohana 3:14-15) (Mathayo 27:32-44)
Ahadi ya Yesu kukanyaga dunia (Mika 1:2-3) Utimilifu wa Yesu kukanyaga dunia (Mathayo 1:21)
Sasa miongoni mwa yale aliyoahidiawa kuyatimiza Yesu ni kutimiza kuivunja Sabato (Hesabu 2:11) na ahadi hii Yesu aliitimiza hapa (Yohana 5:2-9) katika agano la kale kubeba mzigo siku ya sabato ilikuwa ni kuivunja sabato(Yeremia 17:21). Kwa hiyo Yesu aliposema "sikuja kutangua torati wala manabii bali kuitimiliza maana yake sikuja kutangua yale niliyonenewa katika torati bali kuyatimiliza yale niliyoahidiwa kuyatimiliza.
9. SABATO INATAKIWA KUSHIKWA KWA KUWA SABATO NI YA MILELE
Wanazungumza hayo kwa kunukuu (Kutoka 31:15-16), majibu ni haya, neno milele linapotajwa kwenye maandiko linakuwa na maana zaidi ya moja
(a)Maana ya kwanza ni muda mrefu ujao usio na mwisho (Mathayo 25:41)

(b)Maana ya pili ni muda mrefu lakini mwisho unao.
Sasa milele iliyotajwa katika kutoka 31:16 haiizungumzii muda mrefu ujao usio na mwisho, bali inazungumzia muda mrefu lakini una mwisho, angalia maandiko yanayozungumzia muda mrefu ulio na mwisho (Kumbukumbu 15:12-17) mstari wa 17 unasema "naye atakuwa mtumishi wako milele"
Je ni kweli huyu mtu atakuwa mtumwa milele na milele, atakuwa mtumwa hata baada ya kufa? 
Milele inayo maanishwa hapa sio wakati wote ujao, bali ni muda mrefu ujao lakini mwisho unao,pale mtu atakapokufa huo utumishi utakuwa umeishia hapo kwa kuwa hakuna utumishi kaburini wala mbinguni wala motoni.

Angalia andiko jingine (2 Wafalme 5:25-27), hapa tunaona Elisha anamwambia Gehazi kuwa ukoma wa Naamani utamshika Gehazi milele na Gehazi akatoka pale akiwa na ukoma.
Swali la kujiuliza je naamani alikuwa na ukoma mpaka kaburini? 
Je atakapofufuka siku ya mwisho atafufuka na ukoma jibu ni la, sasa kumbe tunajua kuwa milele iliyomaanishwa hapa ni muda mrefu ulio na mwisho.

Katika kutoka 31:16 inatajwa kuwa kushika Sabato katika vizazi vyote, hapa haina maana kuwa ni vizazi vyote visivyo na mwisho kwa mfano (Kutoka 29:38-42) hapa inatajwa kuchinja mwana kondoo na inatajwa kuwa ni sadaka ya milele katika vizazi vyote.
Swali, Je mpaka leo tunatakiwa kuchinja wanyama katika vizazi vyetu vyote?
Hata wasabato wenyewe hawachinji katika vizazi vyao vyote.Kumbe hata vizazi vyote vinaweza kuwana ukomo.

ANDIKO JINGINE WANALOLISIMAMIA. 
Ezekiel 20:12-20. Hapa wanasema kuwa mtu anatakaswa kwa kushika Sabato, hoja hiyo si kweli, andiko hili halisemi hivyo, Mungu hapa anajieleza mwenyewe kuwa yeye ndiye anayetutakasa, sio kwa kushika sabato eti ndio tunatakaswa.

Achana na mambo ya kimwili maana wakati wake ulishapita! Bwana Yesu alisema wazi: Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. (Yoh. 4:23-24).
USIKOSE SEHEMU YA NNE …………… Je wakati wa Mtume Paulo “Kanisa la Kwanza” kulikuwa na WASABATO, watu ambao walikuwa waitetea SIKU YA SABATO? 
Lakini, Biblia inasemaje kuhusu watu hawa?.....................


Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.


© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW