Thursday, October 20, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA PILI)

Kwanini Bwana Yesu aliingia kwenye Sinagogi siku ya Jumamosi “SABATO”?
Kabla sijaanza kuelezea kwanini Yesu aliingia Sinagogi, ni vyema tukafahamu angalau kiufupi maana ya Sinagogi.
Sinagogi ni nyumba ya dini na ya jamii ya Wayahudi inayotumika hasa kusali. Jina hili Sinagogi linatokana na neno la Kigiriki συναγωγή sinagoge, likimaanisha "mkutano"; ni tafsiri ya neno la Kiebrania בית כנסת beit knesset, yaani "nyumba ya mkutano".
Wayahudi hutumia pia neno la Kiyiddish "shul" (=shule) kutajia sinagogi.

Sasa basi, baada ya kulewa maana ya Sinagogi, huto shangaa kuwa Wayahudi ndio watumiaji wa hayo Masinagogi na waliingia siku ya Saba “Sabato” kusali au kusoma “Shule” kama ambavyo neno hili hutamkwa katika Kiyiddish.
Hivyo, basi, haikuwa jambo la ajabu au kustaabisha tunapo soma kuwa Bwana Yesu aliingia ndani ya Masinagogi ili awafundishe Wayahudi kuhusu Ufalme wa Mbinguni. "Luka 4:16. alipokwenda Hapo Alipozaliwa Nazaret alipozaliwa na Siku ya Sabato(jumamosi) alikwenda katk#Sinagogi kama Ilivyokuwa Desturi Yake. Akasimama ili asome 17. akapewa kitabu cha nabii isaya akafunua mahali palipo andikwa "#Roho_wa_Bwana yuu Juu Yangu. Amenipaka mafuta Kuhubiriia maskini Habari njema "
Basi Wasabato wanapo soma hiyo aya teyari wanasema kuwa Yesu aliitunza Sabato kwasababu aliingia Sinagogi siku ya Saba ya Juma = Jumamosi. Haya madai hayana nguvu yeyote ile bali ni madai dhaifu. Kuingia Sinagogi siku ya Jumamosi hakukufanyi na au hakumfanyi mtu kuwa Msabato.
HILI DAI LA KUINGIA SINAGOGI naweza kulifananisha na dai la Waislam kuwa, eti, Yesu aliingia Sinagogi na hivyo Yesu ni Muislam. Waislam wao wana hoja ya kuwa Sinagogi ni Msikiti, basi ukiingia kwenye Sinagogi basi wewe ni Muislam HUKU WASABATO wana hoja ya kuwa Yesu kaingia SINAGOGI SIKU YA JUMAMOSI, basi Yesu ni Msabato. HOJA ZOTE MBILI ZA WAISLAM NA WASABATO NI DHAIFU.
Wakristo wa mwanzo hawakutumia Sinagogi katika ibada zao ndio maana Bwana wetu Yesu Kristo alisema hivi: Kwa mfano, baada ya kumtakasa mtu yule aliyejaa ukoma, Yesu alimwambia, “Asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao.” (Luka 5:14). Haya maneno yanaashiria kuwa Yesu alipo fanya huu muujiza hakuwa kwenye Sinagogi na ndio maana alimwambia Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao.” (Luka 5:14).
Hiki ni kipindi ambacho ni cha kiimani zaidi. Kimsingi hiki ni kipindi ambacho kinaendelea hadi sasa. Huu ni wakati wa kupumzika kazi za mwili za uovu, yaani kuacha dhambi na kuishi kwa kumtegemea Kristo. Ni maisha ya imani.
Imeandikwa: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Matayo 11.28), yaani, nitawapa ‘sabato’. Pia ndiyo maana ya andiko lisemalo: Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato. (Matayo 12:8). Sabato iko kwake, si kwenye siku.


Ni maisha ya kujiachia mikononi mwa Mungu ambaye yeye ndiye anayeshughulikia kila kitu katika maisha yetu. Kazi yetu ni kuamini tu kuwa atafanya; naye hakika anafanya. Hilo ndilo pumziko! Hiyo ndiyo raha! Hiyo ndiyo starehe! Hiyo ndiyo Sabato!

SABATO SI SIKU

Upo ushahidi wa kutosha katika Biblia unaoonyesha kwamba sabato si siku katika juma. Bwana anapoongelea kuhusu safari ya wana wa Israeli anasema:
Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, nikasema, Siku zote ni watu waliopotoka mioyo hawa ... hawataingia rahani mwangu. (Ebr. 3:10-11).

Pia imeandikwa: Maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu. (Ebr. 4:4-5).
Katika maandiko haya Mungu anasema kwamba, kutokana na kukasirishwa na uasi wa wana wa Israeli kule jangwani, alimua kwambahawataingia kwenye raha aliyokuwa amewaandalia. Neno rahani hapa, au kwa Kiingereza rest, ndilo hilohilo sabato. Ndiyo maana hapo juu katika Waebrania 4:4-5, anahusisha siku ya saba na kuingia rahani.
Lakini hebu tujiulize maswali yafuatayo ili tuweze kupiga hatua zaidi.
• Je, Israeli walipokuwa jangwani kwani hawakuwa wakitunza Sabato kama siku? Jibu ni ndiyo, waliitunza. Biblia inasema:Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu mara dufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA,Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA ... (Kutoka 16:22-23).
• Kama basi waliitunza sabato, iweje tena Mungu aseme, ‘Hawataingia rahani mwangu’? Kama ingekuwa ni kumwuliza Mungu, mtu ungesema, “Bwana, unasemaje hawataingia rahani mwako wakati kila siku ya saba wanapumzika?” Hii ni ishara ya wazi kwamba sabato hasa si kupumzika au kutofanya kazi kimwili katika siku ya saba. Sabato ni jambo jingine tofauti na siku ya saba. Iko sabato halisi ambayo siku ya saba na kupumzika kwake vilikuwa ni kivuli chake tu.
• Jambo jingine la kujiuliza ni kwamba, japo ni kweli kwamba wale ambao Mungu alisema hawataingia rahani mwake walifia wote jangwani, lakini walikuwapo wengine wengi walioingia, yaani watoto wao. Sasa je, hao walioingia waliipata hiyo raha (Sabato)?

Mtu anaweza kujibu, Ndiyo, maana sote tunajua kuwa hata wakati alipokuja Bwana Yesu, alikuwa akifundisha mara nyingi kwenye masinagogi 'siku ya Sabato'. Kwa hiyo, mtu anaweza kusema, ‘Ndiyo, waliingia kwenye raha au kwenye sabato.’
Hebu sasa tumsome Mtume Paulo:
Kwa hiyo mtume Paulo anafundisha kuwa ni jambo la udanganyifu kuwafundisha watu washike siku ya Sabato. Kwa sababu ya wokovu wetu ndani ya Kristo (Wakolosai 2:11-15) Paulo anasema, “Basi, MTU ASIWAHUKUMU ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (mstari wa 16).

Paulo anaanzisha mstari huo na neno hili, “Basi.” Kwa nini? Kwa sababu ya mistari 14 na15, “(Yesu) akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”
Walikuwepo watu wa dini – kama tunavyojua kwa kusoma hasa Matendo na Wagalatia – waliotaka wakristo waishi chini ya sheria, yaani, kushika mambo ya nje ya torati; kwa mfano watahiriwe au washike ‘siku’ ya torati. Paulo anafundisha hapo kama mtu akisema, “Lazima ushike sabato ili kumpendeza Mungu au kuokoka ‘kweli’, usimruhusu akuvute chini ya sheria hiyo na humjali kama anakuhukumu! Tunasoma kwenye Matendo 15 na Wagalaia juu ya watu waliojaribu kupotosha njia ya Ukweli kwa kuwalazimisha waumini wayarejee mambo ya torati ya Musa. Ni vivyo hivyo siku hizi. Wasabato wanawahukumu wakristo kwa sababu hawashiki siku ya sabato! Paulo aliwaonya wakristo juu ya watu wa dini kama hao hao!
Hayo ni mafundisho ya Agano Jipya. Hatuwezi kusema au kufundisha kwamba ni lazima tukusanyike siku ya Sabato (jumamosi). Kama fulani akifundisha hivyo anawadanganya watu, sawasawa na maneno ya Paulo. Au je, tunataka kusema Paulo alifundisha uongo? Au tunataka kutumia mstari mmoja dhidi ya mstari mwingine kana kwamba Biblia siyo neno la Mungu? Mistari yote ina muktadha (mazingira) yake! Nani aliyekupa wewe ruhusa na mamlaka kupendelea mstari mmoja na kuudharau mstari mwingine au kutokujali kabisa? Hakika hiyo haitokani na Mungu.
Ndugu msomaji, ningependa ufahamu kuwa wokovu wetu sisi Wakristo upo ndani ya Yesu Kristo, siyo kwa kushika Torati ya Musa kama ambavyo WASABATO “SDA wanavyo amini, SIKU HAINA UWEZO WOWOTE ULE KATIKA MAISHA YAKO, LAKINI YESU NDIE MUWEZA WA KILA KITU NA YEYE NDIE ALIYEIUMBA HIYO SIKU YA SABA YA JUMA.
Wasabato hutumia hii aya kumhukumu Mtume Paulo kuwa alifundisha uongo Kwa mfano wananukuu, ‘Imeandikwa katika Kutoka 20:8-11 lazima tushiike sabato!’ Sasa, inamaana Mtume Paulo alikuwa anafundisha uongo alipo sema tuna haki ya kumtukuza na kumwabudu Mungu siku yeyote ile?
Mtume Paulo anatueleza kiuwazi kuwa, ni vigumu sana kumfuata Yesu kwa asilimia 100 na wakati huo huo unafuata sheria za Musa. Hebu tusome jinsi Mtume Paulo alivyo ianza baruka yake kwa Wagalatia “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”
Hapa ni wazi kuwa Mtume Paulo alikuwa anaongea juu ya waumini ambao walikuwa wanataka kufuata sheria ya Musa. Ndio maana tunamsoma Mtume Paulo akitumia lugha au maneno makali kwa Wagalatia.
Hii tabia ya watu kupenda kushika sheria za Musa tunaiona kwa kanisa la SDA ambalo wanafuata sheria za Musa na kusahau kuishi kwa Imani kama jinsi ambayo Biblia inatufundisha katika Waebrania 11:6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
Paulo alihuzunishwa sana, kwa sababu anasema wazi hivi “…..sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini KUYAREJEA TENA MAFUNDISHO YA KWANZA yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? MNASHIKA SIKU, na miezi, na nyakati, na miaka.”(Wagalatia 4:9,10).
“Maana yale YASIYOWEZEKANA kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa DHAIFU kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma “YESU KRISTO” Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ILI HAKI YA TORATI YATIMIZWE NDANI YETU sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (Warumi 8:3,4).
Kwa hiyo, mtume Paulo anasisitiza, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO.”
Ningependa ufahamu kuwa kiwango cha haki ya Injili ya Yesu Kristo KIPO JUU ZAIDI ya kiwango cha Torati ya Musa. Imeandikwa, “torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.” Yohana 1:17:
SWALI KWAKO MSOMAJI, wewe unaishi kwa uongozi wa NEEMA YA YESU KRISTO AU UONGOZI WA TORATI YA MUSA?
Kumbuka kuwa sheria ambayo ipo nje yako haiwezi kuishinda neema ya Yesu ambayo inaishi ndani yako.
KWA NINI YESU ‘ALIVUNJA’ SABATO?
Hebu tuangalie mifano kadhaa hapa:
Mfano wa 1
Yesu alipomponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa muda wa miaka 38, alimwambia ‘jitwike godoro lako, uende.’ (Yohana 58). Hii ilikuwa ni siku ya sabato.
Lakini tunaona kwamba Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwambia, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro.(Yohana 5:10). Bila shaka walisema hivi kwa kuwa walifahamu fika jinsi sabato inavyotakiwa kutunzwa.
Hii ni kusema kwamba, kwa kadiri ya kanuni za utekelezaji wa sabato, hili lilikuwa ni kosa. Sasa, swali ni kwamba, kwa nini Yesu alivunja sabato kwa kumruhusu yule mtu abebe godoro?

Mfano wa 2
Wayahudi walipomkasirikia Yesu kwa sababu ya kumruhusu yule mtu kubeba godoro siku ya sabato, Bwana Yesu aliwajibu kwamba: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. (Yohana 5:17). Haya ni maneno ya ajabu sana. Wewe uliye Mungu ulituambia kwamba siku ya sabato tusifanye kazi bali tupumzike; tumemwona mtu anafanya kazi ya kubeba godoro, tumekuja kwako, lakini wewe si tu kwamba hukumkemea, bali unasema tena kwamba na wewe unafanya kazi hata sasa (siku ya sabato)!
Kama sabato hasa ni kuacha kufanya kazi, iweje tena Yesu atamke jambo ambalo ni wazi kabisa linavunja sheria aliyoiweka mwenyewe ya kutofanya kazi; yaani aseme kuwa hata sasa yeye anafanya kazi?
Mfano wa 3
Siku moja Yesu aliingia kwenye sinagogi ambamo mlikuwamo mwanamke mwenye pepo wa udhaifu. Yesu alimponya mama yule.
Hata hivyo, Biblia inasema: Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. (Luka 13:14).
Maneno haya ya mkuu wa sinagogi yanatuonyesha kwamba, jambo alilofanya Yesu lilikuwa ni kuvunja sabato. Swali ni lilelile, kwa nini Yesu alivunja sabato?
Tunafahamu kuwa maandiko yanasema kwamba kuvunja sabato ni dhambi, tena ambayo iliadhibiwa vikali sana. Na katika mifano hiyo hapo juu, tunaona kwamba Yesu alivunja sabato kwa kufanya mambo ambayo jamii nzima ilikuwa haiyafanyi siku ya sabato. Kwa harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba, Yesu alitenda dhambi.
Lakini wakati huohuo, maandiko yanasema kwamba, katika kuishi kwake kote hapa duniani, Bwana Yesu hakuwahi kutenda dhambi. (Waebrania 4:15).
Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, iweje uvunje sabato, jambo ambalo ni dhambi, halafu uhesabiwe kuwa hujatenda dhambi? Pili, iweje wewe ambaye ndiye ulisema watu wapumzike siku ya sabato, ndio uwe wa kufanya kinyume na agizo lako mwenyewe? (Maana Yesu ndiye Mungu aliyeagiza sheria ya sabato ifuatwe). Iweje hapa yeye ndiye awe wa kuivunja?
Hapa jibu ni moja tu. Sabato si siku katika juma! Kama sabato ingekuwa ni siku katika juma, Bwana Yesu angekuwa na hatia ya kuvunja sabato, maana ni wazi kuwa alitenda mambo ambayo ni kinyume na sabato kama siku!
Lakini kwa sababu sabato ina maana tofauti na siku, ndiyo maana aliruhusu mtu yule abebe godoro siku sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na uponyaji siku ya sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na wanafunzi kukwanyua masuke mashambani!
Namalizia sehemu ya pili kwa swali hili: Je, kuabudu siku ya sabato au jumamosi ni vibaya?
USIKOSE SEHEMU YA TATU – Kwanini Mafarisayo walimshitaki Yesu kuwa anawaruhusu wanafunzi wake wavunje sheria ya Musa, kuvunja sabato. Marko 2:23-28. Lakini Bwana Yesu aliwajibuje? ……………………………..

Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW