Na Mwandishi Wetu, Moshi
IMEDAIWA kwamba jengo la Waislamu lililopo katika shule ya Msingi Mwenge limeuzwa bila ya ridhaa wala kutolewa taarifa kwa kamati husika za Bakwata Mkoa.
Habari zilizotolewa na kiongozi mmoja wa Bakwata wilaya zimedai kwamba jengo hilo limeuzwa kwa jumla ya shilingi milioni nane.
Aidha, kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amedai kwamba mauzo hayo yamefanywa na Katibu wa Mkoa Bw. Rashid Malya bila ya kuishirikisha ofisi.
Jengo hilo ambalo lilirithiwa na Waislamu toka kwa EAMWS lilikuwa likitumika kwa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikutano pamoja na ofisi za Bakwata Wilaya.
Kwa sasa jengo hilo limekuwa likitumiwa na Walokole kama Kanisa ambapo huendesha kwaya zao.
Ijumaa iliyopita aliyewahi kuwa Katibu wa Bakwata Mkoani Kilimanjaro Alhaj Omar Sinare alilaani vikali kuuzwa kwa jengo hilo kinyemela na kugeuzwa Kanisa lisilo rasmi.
Alhaj Sinare akiungwa mkono na mamia ya waumini walioswali katika Msikiti wa Riadha alimtaka Sheikh wa Mkoa na Katibu wake kuwapa Waislamu maelezo ya kutosha kuhusu amana zao.
Habari zaidi zimeeleza kwamba imeteuliwa Kamati ambayo itafuatilia suala hilo na Bw. Malya ametakiwa atoe taarifa ya kueleweka kwa kipindi cha wiki moja.
Baadhi ya waumini walioongea na mwandishi wa habari hizi, wamedai kwamba wanachofanya hivi sasa ni kuandaa bakora zao huku wakisubiri taarifa ya Kamati.
Wamesema kwamba hawatavumilia kuona Walokole wakiimba ndani ya jengo lao au kuuzwa kwa yoyote wala hawatamvumilia Bw. Malya kama wakati ule alivyouza gari la ofisi.
Taarifa kamili itakayoamua matumizi ya bakora hizo imedaiwa kwamba itatolewa (leo) Ijumaa baada ya swala katika Msikiti wa Riadha.
No comments:
Post a Comment