Friday, September 2, 2016

JE, MUHAMMAD AMETABIRIWA KWENYE BIBLIA? (SEHEMU YA KWANZA)


Waislamu wanashikilia kwamba Muhammad alitabiriwa kwenye Biblia. Andiko lao kuu wanalotumia kutetea hoja hii ni Kumbukumbu la Torati 18:18. Andiko hilo linasema:
Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
Haya ni maneno ambayo aliambiwa Musa na Yehova.
Mmojawapo wa watu ambao walijaribu sana kuonyesha kuwa andiko hili lilimhusu Muhammad, alikuwa ni mwanaharakati wa Kiislamu, marehemu Ahmed Deedat wa Afrika Kusini.
Unaposoma au kusikiliza sababu wanazotoa ili kuthibitisha madai yao hayo, kwa kweli ni sababu zenye nguvu sana (kwa mtu ambaye haelewi Biblia); ingawaje hazina uzito hata chembe ukijua Biblia inasema nini katika ujumla wake na ni nini makusudi na malengo ya Mungu kwa uzao mzima wa Adamu.
Siku moja Ahmed Deedat alimkaba mchungaji mmoja kwa maswali kuhusu mstari huu wa Kumbukumbu 18:18 kiasi kwamba, kwa maneno yake, Deedat anasema kuwa mchungaji yule alikosa cha kusema.
Deedat alimpomsomea mstari huo, alimwuliza, “Unabii huu unamhusu nani?”
“Unamhusu Yesu,” mchungaji alijibu.
“Unajua,” alisema Deedat, “Maneno ya msingi kabisa kwenye unabii huu ni ‘mfano wako’. Sasa, ni kwa vipi Yesu ni mfano wa Musa?”
“Musa alikuwa Myahudi na Yesu alikuwa Myahudi. Pili, Musa alikuwa nabii na Yesu alikuwa nabii,” alijibu mchungaji.
Deedat anaendelea kusema, “Kama hizi ndizo sababu mbili pekee zinazotuwezesha kumtambua mhusika wa unabii huu wa Kumbukumbu 18:18, basi unabii huu unaweza kumhusu yeyote kati ya wafuatao baada ya Musa: Sulemani, Isaya, Ezekieli, Danieli, Hosea, Yoeli, Malaki, Yohana Mbatizaji, n.k. maana hawa wote nao walikuwa Wayahudi na pia manabii. Kwa nini basi useme kuwa unabii huu unamhusu Yesu na si hawa wengine?”
Deedat anasema kuwa mchungaji yule alikosa cha kusema. Kisha Deedat akasema, “Mimi nadhani Yesu ndio hafanani kabisa na Musa.”
Zifuatazo sasa ndizo sababu ambazo Deedat na watoa hoja wa Kiislamu juu ya suala hili wanazozitoa ili kutetea hoja hii:

1. Yesu ni Mungu (kulingana na Biblia), lakini Musa si Mungu. Kwa hiyo, hafanani na Musa.
2. Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu (kulingana na Biblia), lakini Musa hakufa kwa ajili hiyo. Kwa hiyo, hafanani na Musa.
3. Yesu alienda kuzimu siku tatu (kulingana na Biblia), lakini Musa hakwenda huko. Kwa hiyo, hafanani na Musa.
Deedat akaendelea sasa kuonyesha jinsi Musa anavyofanana na Muhammad. Zifuatazo ndizo hoja zake au hoja zao Waislamu:
1. Musa na Muhammad walikuwa na baba na mama, lakini Yesu hakuwa na baba wa kibinadamu. Hivyo, aliye mfano wa Musa ni Muhammad na sio Yesu.
2. Musa na Muhammad walizaliwa kwa njia ya kawaida lakini Yesu aliumbwa kwa njia maalumu ya kimuujiza.
3. Musa na Muhammad walioa na kuzaa wana lakini Yesu hakuoa wala kuzaa kwenye maisha yake yote.
4. Musa na Muhammad walikubaliwa kama mitume na watu wa nyakati zao, lakini Yesu alikataliwa. Na hata leo bado Wayahudi hawamkubali. Na pia Biblia yenyewe nayo inasema: Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. (Yohana 1:11).
5. Musa na Muhammad walikuwa manabii na pia wafalme. Walikuwa manabii kwa vile walipokea ufunuo kutoka kwa Mungu na kuwapatia viumbe wa Mungu. Walikuwa wafalme kwa vile walikuwa na mamlaka ya uzima na mauti juu ya watu wao. Ndiyo maana kwa mfano, Musa alitoa amri auawe mtu aliyekamatwa akiokota kuni siku ya sabato (Hesabu 15:13). Muhammad naye alikuwa na nguvu hizo. Manabii wengine kama vile Yona, Danieli, Ezra, n.k. walikuwa na karama ya unabii lakini hawakuwa na mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu. Yesu naye alikuwa kwenye kundi hili la pili. Hivyo, hafanani na Musa.
6. Musa na Muhammad walileta sheria mpya kwa watu wao. Lakini Yesu hakuleta sheria mpya. Hata Yeye mwenyewe anakiri kwamba: Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. (Mathayo 5:17-18).
7. Musa na Muhammad walikufa kifo cha kawaida, lakini kulingana na Ukristo, Yesu aliuawa kikatili msalabani.
8. Musa na Muhammad walikufa na wamelala mavumbini, lakini kulingana na Ukristo, Yesu yuko mbinguni.
Deedat anasema, “Mchungaji yule alikuwa hana la kujitetea, nilimwambia, Hapa nimekuthibitishia jambo moja tu. Lakini unabii una zaidi ya hapo. Kuna sehemu inayosema kuwa nabii yule atatoka, ‘miongoni mwa ndugu zake’.
Kwa hiyo akaendelea kutoa hoja zake kwamba:
9. Abrahamu alikuwa na watoto wawili. Ishameli kutoka kwa Hajiri, na Isaka kutoka kwa Sara. Hawa walikuwa ndugu. Watoto wa Isaka ni Wayahudi na watoto wa Ishamaeli ni Waarabu. Kwa hiyo, watoto wa Ishmaeli ni ndugu wa watoto wa Isaka. Kama basi nabii huyo alitakiwa kutoka miongoni mwa ndugu zake, basi ni kwa Waarabu na si kwa Wayahudi wenyewe. Muhammad, ambaye ni wa uzao wa Ishmaeli ndiye nabii miongoni mwa ndugu za Wayahudi, yaani Waarabu, anayetajwa kwenye Kumbukumbu 18:18, na si Yesu ambaye ni Myahudi. Je, hata Biblia yenyewe haimsemi Ishmaeli kwamba:Wakakaa toka Havila mpaka Shuri, unaoelekea Misri, kwa njia ya kwenda Ashuru. Akakaa katikati yandugu zake wote (Mwanzo 25:18)?
10. Unabii unasema: nami nitatia maneno yangu kinywani mwake. Huyu ni Muhammad kwa sababu alikuwa ni mtu asiye na kisomo, yaani hakuwa amesoma, lakini malaika Jibrili alipomtokea kwenye pango la Hira (au Jabal-un Noor), alimwambia ‘iqra’ au ‘soma’ au ‘sema’. Matokeo yake Muhammad alianza kusema maneno ambayo Allah alikuwa akiyaweka ndani ya kinywa chake kwa miaka 23 iliyofuata – ambayo ndiyo yamekuja kuzaa kitabu cha Quran.
11. Nabii Isaya anasema: Kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi (Isaya 29:12). Andiko hili linamtaja Muhammad kwa sababu alipokuwa anapokea ujumbe kutoka kwa Allah, alikuwa ni mtu asiye na elimu isipokuwa ile iliyotoka kwa Allah mwenyewe.
12. Unabii huu unaendelea kusema: Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake (Kumbukumbu 18:19). Deedat anasema kuwa Quran katika sura Nas aya 114 inaanza kwa kwa kusema: in the name of God, most gracious, most merciful. Pia anaendelea kusema kuwa kila sura nyuma yake, yaani 112, 111, 110, n.k., zinaanza hivyo hivyo. Kwa hiyo, yale ambayo Muhammad anayasema, anafanya hivyo kwa jina la Allah – sawasawa na unabii wa Kumb. 18:19 unavyosema. “Lakini,” Deedat anasema, “Wakristo huanza ‘Kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.’”
Hoja hizi ukiziangalia ni hoja zenye nguvu sana na ambazo, katika hali ya kawaida, zina mantiki kubwa. Hizi ni hoja ambazo zinaweza kabisa kumtoa mtu kwenye uzima wa milele ndani ya Kristo na kumtumbukiza kwenye upotevu na uangamivu wa milele. Na ninaamini zitakuwa zimeshafanya hivyo kwa baadhi ya watu.
Sijui ndugu msomaji, kama ungekuwa ni wewe ungesemaje? Ni kwa kiasi gani imani yako itabakia imara baada ya kukutana na hoja nzito kama hizi?
Unaweza kuzisoma hoja hizi kwa Kiingereza kwa kubofya HAPAhttp://www.answering-christianity.com/ahmed_deedat_muh_bibl… .
Basi nakuomba ufuatane nami katika sehemu ya pili ya makala haya, ambapo nitaeleza jinsi ambavyo hoja hizi hazina ukweli wowote kimaandiko licha ya kuonekana zenye uzito namna hii.
Yesu Kristo ndiye njia, na kweli, na uzima wa milele. Yesu Kristo ndiye safina ya nyakati hizi. Gharika inakuja, ambapo kila aliye nje ya safina atasombwa na moto wa milele.
Mtume Paulo anasema vizuri sana.
Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu; lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.
Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.
Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.
Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. (1 Wakorintho 2:4-15).
Shika sana ulicho nacho asije mwovu akakichukua; maana siku tulizonazo ni nyakati za uovu mwingi.

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW