Wednesday, August 10, 2016

TUMIA MAMLAKA ULIYOPEWA NA MUNGU


Mungu ametupa mamlaka ya kipekee sisi wanadamu katika ulimwengu huu sema tu ni kwamba tunashindwa kutumia hiyo mamlaka. Ukisoma katika Mwanzo 1:27-30 Biblia inasema Mungu akamuumba mwanadamu kwa mfano wake na pia akampa mamlaka ya kutawala samaki wa baharini na ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu nchi, vyote hivi mwanadamu alipewa kuvitawala na Mungu. Swali la kujiuuliza ni kwamba je inakuwaje mwanadamu wa leo anakuwa hana uwezo wa kuvitawala vitu hivyo?
Tunaweza kuona kuwa baada ya anguko la Adam mwanadamu amekuwa akishindwa kuvitwala viumbe vyote na vyote vilivyomo duniani na hii imekuwa ni kifungo kikubwa kwa wanadamu hadi leo hii kwa maana toka Adamu afukuzwe katika bustani ya Eden watu wamekuwa wakihangaika huku na kule bila kujua nini cha kufanya sababu shetani amekamata fahamu zetu ili tusiweze kukumbuka na kutumia mamlaka hii tuliyopewa na Bwana. Lakini Mungu kwa upendo wake na huruma zake na kwa Neema yake ya pekee alimtoa mwana wake Yesu Kristo ili kutupatanisha naye kutuwezesha kutumia ile mamlaka ya kutawala dunia kama ilivyokuwa kusudi lake hapo awali la kumuumba mwanadamu.
Jambo la msingi na la kipekee ni kupokewa Neema hii tuliyopewa bure ya kumkubali Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi ndani ya maisha yatu ili tuweze kutumia tena yale mamlaka. Ukisoma ktk kitabu cha TITO 2:11-12 utaona kuwa Biblia inatuambia kuwa Neema ya Mungu imefunuliwa kwetu nayo inatufundisha kuukataa ubaya .... hii Neema iliyofunuliwa ndio wokovu wenyewe ambao unatuwezesha sisi wanadamu kukiri kuwa Yesu ni Bwana, kwani yeye alifanyika chombo cha kuweza kutubebea ile laana aliyoipata Adam baada ya anguko. Soma Isaya 53:4-5 .... kwa kupigwa kwake sisi tumpona. Hivyo basi Bwana wetu Yesu ameturejeshea ujasiri na nguvu na uweza wa kutumia ile mamlaka ambayo tunatakiwa kuwa nayo kwani kwa kuliita jina lake tu magonjwa, pepo, na nguvu zote za giza zinakimbia. Hakutakuwa tena na maonevu yaletwayo na yule mwovu shetani katika maisha yetu hofu, kuyumba katika kipato, biashara, ndoa, watoto hata katika ulimwengu wa kiroho kwani utakuwa tayari unajua ni jinsi gani unaweza kupigana vita na ukaweza kuvishinda hakuna kitakachoweza kukudhuru kwani uweza unao mikononi mwako tayari ni jinsi gani tu unaweza kutumia na ni silaha zipi utumie ili uweze kushinda.

Ukisoma tena katika Zaburi ya 91:13 utaona pia Mungu amekupa uweza na mamlaka ya kumwangamiza adui. Anasema hivi : Utawakanya simba na nyoka, mwana simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa hiyo kilichobaki ni wewe kujitambua na kujikubali kuwa uweza na mamlaka unayo kwamba kusudi la Bwana Mungu kukuumba ni ili utawale dunia. Jione kama vile mtoto mchanga anavyomwamini mama yake kuwa akimbeba hatamwangusha na wewe pia mpendwa unatakiwa kumwamini Mungu kuwa hakika hatakuacha mamlaka aliyokupa ni sahihi na hawezi kukuangusha kwani anajua kuwa ukitumia na kufuata kanuni zake lazima utakuwa imara na mshindi siku zote za maisha yako vyote vilivyo katika ulimwengu huu vitatiishwa chini ya miguu yako.
Ukiwa kama mwana wa Mungu umeokoka na unampenda Yesu jua kwamba wewe pia unauwezo na mamlaka ya kuumba na kubomoa pia. Ukisoma katika Zaburi 8:5-6 Biblia inasema kuwa sisi wanadamu tumefanywa kidogo chini ya Mungu kwa maana ya kuwa baada ya Mungu ni sisi wanadamu tunafuata na vile vile bado Biblia inasisitiza jinsi gani tumepewa mamlaka ya kuweza kutawala viumbe vyote. Bwana Mungu ametupa kibali mbele zake kwani katika ufalme wa Mungu wewe na mimi ni Waziri Mkuu vyooote viko mikononi mwako na mwangu unachotakiwa kuitumia tu mamlaka hiyo. Ukiangalia hata katika hali ya kibinadamu mfano wa nchi yetu Waziri Mkuu ni mtu mkubwa sana katika serikali na anayo mamlaka juu ya vyombo vya dola vyote na anasauti katika serikali na katika nchi na pia anao mawaziri chini yake wa kuweza kumsaidia sasa basi kama jinsi alivyo Waziri Mkuu na Mawaziri wake ndivyo na wewe pia ulivyo katika ufalme wa Mungu ni Waziri mkuu unayo mamlaka unayo sauti unao Mawaziri chini yako ambao ni Malaika kwa ajili ya kukusaidia. Je unawatumiaje hao Malaika (mawaziri wako) katika ulimwengu wa kiroho kukusaidia? ni juu yako sasa ewe Waziri Mkuu, Mungu amekupa mamlaka tayari yeye ni Mfalme anasubiri umpe ripoti tu kuwa umefanya nini na unatazamia kufanya nini katika maisha yako kwa familia yako, kwa watoto wako, kwa jamaa zako, kwa majirani zako, kwenye biashara, kwenye kazi nk. Hivyo basi tumia mamlaka hiyo sasa bila hofu fungua moyo wako chukua mamlaka uliyopewa kama Waziri Mkuu fanya maamuzi sahihi vaa ujasiri hakika utauona mkono wa Bwana katika maisha yako.
Bwana wetu Yesu Kristo anakwambia pia katika Mathayo 16:19 Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalofunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalofungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni; sasa rafiki, ndugu yangu unataka upewe nini tena Yesu mwenyewe anasema amekupa ufunguo kwa maana nyingine amekupa mamlaka ya kufungua na kufunga yale uyatakayo; mfano kama mtu ana chumba chenye dhahabu tele na fedha anakuambia chukua funguo hii chochote ukitakacho humo ndani ya chumba uchukue kama ni fedha kama na dhahabu na yeyote anayetaka wewe ndio unayo mamlaka ya kumfungulia mlango kuingia kuchukua au la; mfano mwingine ni kuwa umepewa ufunguo ambao unauwezo wa kuwafungulia wafungwa walioko gerezani au au kuendelea kuwafungia humu. Hiyo ndio mamlaka uliyopewa na bwana. Itumie mpendwa kamata hizo funguo kwa kujiamini kuwa ni zako fungua mlango uingie fungua mlango upate baraka za Bwana alizokusudia uwe nazo.
Usikate tamaa usivunjike moyo Yesu ni yeye yule jana leo na hata milele hatokuacha kamwe ameahidi kutenda atatenda amekupa mamlaka sasa itumie, itumie, itumie.
Kama bado haujaokoka basi rafiki mkubali Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi katika maisha yako leo mpokee Yesu kwa kumaanisha ili mamlaka hii iwe dhahiri kwako uweze kuvishinda vyote na kutawala kama Bwana Mungu alivyokusudia kwa kukuumba kwako ewe mwanadamu. Tafuta uso wake kwa bidii kwa kusoma Neno kwani Neno ndiye Mungu mwenyewe ukisoma Yohana 1:1 Bibilia inasema kuwa...... Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu.
Hivyo Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe kwa hivyo unaposoma hili Neno la Mungu unakuwa umemwingiza Mungu ndani ya maisha yako na yeye basi kwa upendo wake na kwa Neema yake anaanza kutenda kazi ndani ya maisha yako yale yote yaliyokuwa magumu hapo awali kwako yanakuwa mepesi kwa vile unaye Mungu ndani yako na kama nilivyosema hapo juu ni kuwa kwa kuwa Mungu alikuumba punde kidogo chini yake na amekupa mamlaka ya kutawala viumbe vyote na vyote vilivyomo humu duniani basi ni dhahiri vile vyote uvitakavyo utavipata bila wasiwasi. Ukisoma Zaburi 1:2-3 utakuwa na mafanikio katika kila ulitendalo kwa kusoma Neno lake tu na kutumia mamlaka aliyokupa.
Mimi nimejikubali, nimemkubali Yesu kuwa ni Bwana na mwokozi ndani ya maisha yangu na mamlaka naitumia na nimeona jinsi anavyotenda mambo makuu na ya ajabu katika familia yangu. Karibu nawe uweze kutumia mamlaka hiyo.
Ubarikiwe na Bwana.

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW