Monday, April 4, 2016

KWA NINI YESU ALIVUNJA SABATO?


Ndugu msomaji,
Hebu tuangalie mifano kadhaa hapa:
MFANO WA KWANZA
Yesu alipomponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa muda wa miaka 38, alimwambia ‘jitwike godoro lako, uende.’ (Yohana 58). Hii ilikuwa ni siku ya sabato.
Lakini tunaona kwamba Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwambia, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. (Yohana 5:10). Bila shaka walisema hivi kwa kuwa walifahamu fika jinsi sabato inavyotakiwa kutunzwa.
Hii ni kusema kwamba, kwa kadiri ya kanuni za utekelezaji wa sabato, hili lilikuwa ni kosa. Sasa, swali ni kwamba, kwa nini Yesu alivunja sabato kwa kumruhusu yule mtu abebe godoro?
MFANO WA PILI
Wayahudi walipomkasirikia Yesu kwa sababu ya kumruhusu yule mtu kubeba godoro siku ya sabato, Bwana Yesu aliwajibu kwamba: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. (Yohana 5:17). Haya ni maneno ya ajabu sana. Wewe uliye Mungu ulituambia kwamba siku ya sabato tusifanye kazi bali tupumzike; tumemwona mtu anafanya kazi ya kubeba godoro, tumekuja kwako, lakini wewe si tu kwamba hukumkemea, bali unasema tena kwamba na wewe unafanya kazi hata sasa (siku ya sabato)!
Kama sabato hasa ni kuacha kufanya kazi, iweje tena Yesu atamke jambo ambalo ni wazi kabisa linavunja sheria aliyoiweka mwenyewe ya kutofanya kazi; yaani aseme kuwa hata sasa yeye anafanya kazi?
MFANO WA TATU
Siku moja Yesu aliingia kwenye sinagogi ambamo mlikuwamo mwanamke mwenye pepo wa udhaifu. Yesu alimponya mama yule.
Hata hivyo, Biblia inasema: Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. (Luka. 13:14).
Maneno haya ya mkuu wa sinagogi yanatuonyesha kwamba, jambo alilofanya Yesu lilikuwa ni kuvunja sabato. Swali ni lilelile, kwa nini Yesu alivunja sabato?
Tunafahamu kuwa maandiko yanasema kwamba kuvunja sabato ni dhambi, tena ambayo iliadhibiwa vikali sana. Na katika mifano hiyo hapo juu, tunaona kwamba Yesu alivunja sabato kwa kufanya mambo ambayo jamii nzima ilikuwa haiyafanyi siku ya sabato. Kwa harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba, Yesu alitenda dhambi.
Lakini wakati huohuo, maandiko yanasema kwamba, katika kuishi kwake kote hapa duniani, Bwana Yesu hakuwahi kutenda dhambi. (Waebrania 4:15).
Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, iweje uvunje sabato, jambo ambalo ni dhambi, halafu uhesabiwe kuwa hujatenda dhambi? Pili, iweje wewe ambaye ndiye ulisema watu wapumzike siku ya sabato, ndio uwe wa kufanya kinyume na agizo lako mwenyewe? (Maana Yesu ndiye Mungu aliyeagiza sheria ya sabato ifuatwe). Iweje hapa yeye ndiye awe wa kuivunja?
Hapa jibu ni moja tu. Sabato si siku katika juma! Kama sabato ingekuwa ni siku katika juma, Bwana Yesu angekuwa na hatia ya kuvunja sabato, maana ni wazi kuwa alitenda mambo ambayo ni kinyume na sabato kama siku!
Lakini kwa sababu sabato ina maana tofauti na siku, ndiyo maana aliruhusu mtu yule abebe godoro siku sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na uponyaji siku ya sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na wanafunzi kukwanyua masuke mashambani!
MAANA HALISI YA SABATO
Sabato ni kitu gani basi kama si siku katika juma?
Maandiko yanasema: Basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye (yaani mwanadamu) aliyeingia katika raha yake (yaani raha ya Mungu) amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake. (Waebrania 4:10).
Aha! Kumbe sabato si kupumzisha damu na nyama katika siku mojawapo ya wiki; si kujizuia kukoka moto, kubeba mzigo au kusafiri mwendo mrefu kimwili!
Sabato ni kitendo au hali ya mwanadamu kuacha ‘kazi zake’ kama Mungu alivyoacha zake. Mungu ni mtakatifu, kwa hiyo kazi zake ni takatifu na kamilifu. Mwanadamu ni mpungufu, kwa hiyo kazi zake ni uasi, yaani dhambi. Hizo ndizo anazotakiwa kupumzika kwazo, yaani kuziacha na kumgeukia Mungu.
Ili kuweza kuingia rahani mwa Bwana, yaani kwenye sabato yake, Bwana akasema: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Matayo 11.28).
Pumziko au raha au sabato hiyo si kupumzisha damu na nyama katika siku fulani ya wiki, bali Bwana anasema: Nanyi mtapata raha (sabato) nafsini mwenu. (Matendo ya Mitume 11:29) – si kwenye miili yenu!
Na pale unapowezeshwa kuacha dhambi na ukamgeukia Bwana na kumfuata maishani mwako, ndipo raha au sabato hiyo inapokuwa ni kwa faida au kwa ajili yako, yaani sabato inakuwa ni kwa ajili ya mwanadamu. Lakini ukishikilia kutunza siku, hapo wewe ni kwa ajili ya siku (sabato) na wala si sabato kwa ajili yako.
Kwa hiyo, sabato si siku bali ni pumziko, raha na starehe ndani ya Kristo katika Roho Mtakatifu. Imeandikwa: Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. (Warumi 14:17).
HITIMISHO
Tumalizie kwa kujiuliza swali hili. Je, kuabudu siku ya sabato au jumamosi ni vibaya?
Yapo mambo mawili ya kutofautisha hapa. Kuna kushika siku kama siku tu; na kushika siku kama sehemu ya utekelezaji wa sheria.
Ukishika siku kama siku tu, unaweza kumwabudu Mungu katika siku yoyote upendayo maana siku zote ni sawa tu.
Lakini ukishika siku kama sheria, hutaweza kuabudu katika siku yoyote, maana sheria ina siku yake maalumu.
Kuabudu katika siku ya sabato (jumamosi) kama siku tu haina tatizo hata kidogo. Lakini kuabudu katika siku hiyo kama sheria kunaweza kuwa na maswali.
Tumeshaona kwa ushahidi mwingi kwamba, sabato ilikuwa ni kivuli au mfano au taswira ya kitu kingine.
Jambo la msingi ni kuwa, sabato au pumziko halisi ni kuwa ndani ya Yesu, yaani kuokoka. Ukishaingia ndani ya Yesu, haijalishi tena endapo utamwabudu siku ya kwanza, ya pili au ya mwisho ya juma.
Biblia inasema: Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona kuwa siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. (Warumi 14:5-6).
Tena imeandikwa: Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. (Wakorintho 2:16-17).
Vilevile imeandikwa: Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu. (Wagalatia 4:9-11).
Je, umeokoka?
Kama jibu ni ndiyo na unapenda kumwabudu Bwana wa sabato (pumziko) siku ya jumamosi, basi songa mbele katika hilo, maana siku kama siku haikuongezei wala kukupunguzia chochote.
Je, hujaokoka?
Kama jibu ni ndiyo, nasikitika kusema kwamba kushika kwako siku hakutakusaidia, maana hapo hakuna tofauti na kung’ang’ania mfano au kibao na kuacha jambo lenyewe ambalo hasa ndilo lililolengwa na kibao au mfano huo.
Mtu akiwa mwizi, wizi wake hautoki kwa sababu ameabudu katika siku fulani ya juma. Na mtu mtakatifu, utakatifu wake hauji kutokana na kuabudu katika siku fulani. Utakatifu unatoka kwa Bwana wa sabato, Yesu Kristo mwenyewe.
Umeona mwenyewe hapo juu kwamba Mungu anaita ‘kushika siku’ kuwa ni ‘mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge!’
Achana na mambo ya kimwili maana wakati wake ulishapita! Bwana Yesu alisema wazi: Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. (Yohana. 4:23-24).
Si katika mwili!!
Mungu awabariki sana.
By permission: Yesu ni Njia, Injili Timilifu, James John, NKJV, Christ Nations and Max Shimba Ministries Org.
Ni mimi Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo,
For Max Shimba Ministries Org,
MAX SHIMBA MINISTRIES ORG ©2016. ALL RIGHTS RESERVED
Everyone is permitted to copy and distribute verbatim copies of this license document, but changing it is not allowed.
April 4, 2016

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW