Sunday, April 10, 2016

KAZI YA MIKATABA YA DAMU NA KAFARA


Ndugu msomaji,
Ningependa tujikumbushe kuhusu "mikataba ya damu na kafara' ambayo watu wengi wanafanya bila ya kuelewa madhara yake katika maisha yetu/yako/yao.
KWANINI WATU WANATOA KAFARA:
Ukiangalia habari ya Nuhu baada ya kutoka kwenye safina Nuhu alimtolea Mungu sadaka na ile harufu ilipofika kwa Mungu; akasema hatailaani nchi tena kumbe ile harufu ina maana sana kwenye ulimwengu wa roho; vivyo hivyo wanapo mtolea shetani kafara wanalenga kumpa ile harufu na ile harufu inamfanya shetani awa tekelezee wanayohitaji. Mtu anamtoa mwanawe ili kuwapa kafara mashetani, wamtekelezee anacho hitaji kama utajiri n.k.
Mambo ya Walawi 2:12 “Vitu hivyo mtavisongeza kwa Bwana kuwa ni malimbuko; lakini visifike juu ya madhabahu kuwa ni harufu ya kupendeza.” Utajiuliza hii harufu na sadaka; hapa ni kafara inayotolewa kwa mashetani.Mambo ya Walawi 3:15, 16, Hesabu 5:17, Sadaka ya vinywaji hii ni baadhi ya mila hapa kwetu ni pale mtu anakunywa pombe alafu anawapulizia watu, hii ndio inaitwa sadaka ya vinywaji inayotolewa. Sasa hii inapotolewa kwa mashetani kwenye ulimwengu wa roho wanakuja mahali pale. Hesabu 15:10; 17:24; 18:7
KUWA MAKINI NA KAFARA ZILIZOTOLEWA KWA MASHETANI:
Kumbe shetani anaweza kutolewa kafaraza aina mbalimbali inaweza kuwa ya vinywaji, uji, nafaka, harufu, watoto au watu wazima; na ni muhimu kuwa makini sana na kuhudhuria sherehe ambazo si za ki Mungu kwasababu waweza kujikuta unashiriki kwenye sadaka hiyo. Kuna watu ambao matatizo yao yamewaanza baada ya kushiriki chakula cha kafara jambo hili biblia imekataza kwasababu ya madhara yake.
Ufunuo 5:8; 8:3 hapa biblia inataja sadaka ya harufu, na ndio maana ukienda kwenye maduka mengi utakuta wameweka vitu vinaitwa ubani; Hii ni sadaka au kafala ya kuteketezwa kwa majini, Isaya 43:23; Yeremia 6:20; 17:26, Ubani na Udi ni sadaka ya kuteketezwa, kimsingi; ile harufu ndiyo inayoifanya iitwe sadaka ya kuteketezwa, kwahiyo mtu unayemuona anachoma ubani ni anakuwa anatoa kafara ya ubani. Nehemia 13:9.. sadaka za unga na sadaka za ubani. Kimsingi watu tuliookolewa hatutoi sadaka za ubani kwasababu biblia inasema maombi ya watakatifu ndio sadaka ya harufu kwa Mungu. (Yohana 19:39)
Kumbe unapoona mahali au duka ukakuta wanachoma udi kimsingi ni kwamba wanaita Mashetani ambayo yanawasaidia kuleta wateja. Na ndio maana maduka mengi yana kuwa na vitu hivi ambavyo ni kafara au sadaka ya harufu; ili majini yaite wateja. Na ndio maana watu wengi wenye majini wanapenda ubani kwasababu kile ndio chakula chao.
NGUVU YA KAFARA:
Unaweza ukajiuliza kafara inafanyaje kazi; kimsingi; sadaka au kafara ya vinywaji, damu au vyote tulivyoona ni chakula cha mashetani. Na kimsingi mashetani yapo katika ngazi mbalimbali kuanzia majoka mpaka kwenye majini majini madogo; kwahiyo wachawi au washirikina huita mashetani kulingana na ukubwa wa kafara kama ikitolewa kafara ya kuku anakuja shetani wa ngazi ndogo. Na ikitolewa kafara kubwa kama ya mtu inaliita shetani la ngazi ya juu sana. Hivyo kama mtu hajaokoka ni rahisi kutolewa kafara kwasababu anakuwa hana ulinzi wa Mungu.
TABIA ZA DAMU KATIKA BIBLIA:
Mwanzo 4:10; Adamu alikuwa na watoto wawili mmoja aliitwa Kaini na mwingine Habili; Kaini alipomuua Habili; Mungu akamwambia Kaini, Damu ya ndugu yako inanililia. Kumbe damu yaweza kulia na inaweza kuongea pia.
Kumbukumbu 12:23 Mungu anasema kuwa “…damu ni uhai”. Kumbe damu ina uhai; kwa namna hiyo kuna tabia kadhaa za damu:
i) Damu ina sauti
ii) Damu yaweza kulia
iii) Damu inaleta laana
Na ndio maana Mungu amekataza kula au kunywa damu, hii ni kwasababu hizi tatu Kumbukumbu7:27; Walawi 17:10,12
DAMU INA SAUTI (INANENA):
Damu iliyomwagika chini inaweza kunena mema au yaweza kunena mabaya,damu inenayo mema ni ya Yesu peke yake, Waebrania 12:24 inasema, “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.” Kumbe kuna damu inayonena mema (damu ya Yesu Kristo) na pia kuna damu inayonena mabaya (damu ya wanyama,ndege hata watu)
Damu yaweza kuongea mabaya juu ya mtu; damu ikimwagwa hunena na ndio maana hata nchi yaweza kuingia kwenye matatizo kwasababu ya damu inenayo iliyomwagika.
Mambo ya Walawi 19:26 “Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.” Mungu amekataza kula nyama pamoja na damu kwasababu damu ni uhai, na ina sauti. Na ukiangalia katika biblia kila mahali ambapo damu imekatazwa na uchawi pia umetajwa. Kwa maana hiyo tunajifunza kuwa uchawi upo na unaushirikiano wa karibu na matumizi ya damu.
MAFUNDO YA KICHAWI:
Ukisoma Ayubu 15:26 “Humshambulia na shingo ngumu, Kwa mafundo makubwa ya ngao zake;” mafundo yapo na wachawi ndio wanayo yafunga. Wachawi wanaweza kuloga katika kufunga mafundo, hivi ni vifungo vya kichawi ambavyo hutumia kudumisha maisha ya watu. Kumbukumbu 18:11 “wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.” Kuna mafundo ya aina mbalimbali mojawapo ni mafundo ya maamuzi; yaani mtu anashindwa kuwa na maamuzi, na ndio maana watu wengi wanashindwa kupiga hatua kwenye maisha kwasababu wamefungwa katika maamuzi.
Wachawi pia hutumia mafundo haya kufunga matumbo ya kina mama ili wasipate watoto; na ndio maana ya maandiko yale yanayosema “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.” Mathayo 18:18. Kwenye ulimwengu wa mwili mtu anaweza akaonekana anaumwa au ana matatizo lakini katika ulimwengu wa roho anakuwa amefungwa. Luka 13:16 huyu mwanamke alionekana amepooza kumbe shetani alikuwa amemfunga.
DAMU INAVYOTENDA KAZI:
Sasa kwa kujua kuwa kila damu iliyomwagwa inauwezo wa kusema, wachawi hutumia tabia hiyo ya damu kufunga maisha ya watu. kwahiyo wanachofanya wachawi au waganga ni kuchukua mnyama na kumchinja yule mnyama na kuinuizia inene tatizo lako. Kimsingi; hii damu iliyomwagwa ndiyo inayoitwa madhabahu ya tatizo lako. Na ndio maana waganga wa kienyeji huagiza kuku, mbuzi au ng’ombe ile ni kwa ajili ya kumwaga damu ili inene mabaya juu ya mtu.
Damu inapomwagwa inatoa sauti; yaani katika ulimwengu wa roho ni sauti kubwa ili mtu akae katika tatizo; kinachotokea pale damu inaponena mashetani husikia rohoni na kwa njia hiyo mashetani yanapata mlango wa kuingia kwenye maisha ya mtu. Hivyo mashetani huja ili kutekeleza sauti ya ile damu inayonena. Kwa njia hiyo shetani amefunga maisha ya watu na kifungo kinakuwa kikubwa kulingana na wingi wa damu iliyomwagwa
DAMU INAYOTOKANA NA KUCHANJWA CHALE:
Biblia iko wazi sana kuhusu kuchanja chale kwenye miili ya watu. Mambo ya Walawi 19:28 “Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana.” Mambo ya Walawi 21:25; Yeremia 48:37 Yaani; mtu huyu sio kwamba imemwagwa damu ya mnyama kwa ajili yake bali anakuwa amechanjwa mwenyewe kwenye mwili na ameitoa damu yake mwenyewe. Kimsingi; mganga anapokuwa anachanja chale huwa ananena maneno ambayo huwezi kuyaelewa. Yale maneno ndio sauti ya ile damu iliyo mwagwa.
Utajiuliza kwanini Mungu anakataza watu kupigwa chale; kimsingi damu inayomwagika ni uhai wako, kwa lugha rahisi ni kwamba unapochanjwa chale unakuwa umeacha uhai wako kwa mganga wa kienyeji. Hivyo mganga anaweza kukuona na kukufuatilia kirahisi, hivyo akiamua kukufanya urudi kwake anaweza kukurudisha kirahisi kwasababu uhai wako umeuacha kwake.
DAMU YA YESU KRISTO:
Unaweza ukajifunza kwanini Yesu alipokuja duniani asingekufa kwa kuumwa au njia nyingine ambayo haimwagi damu, Siri kuu ya kuja Yesu duniani ni kwa ajili yetu sisi tufunguliwe na kutoka kwenye vifungo kwa damu ya Yesu ambayo yenyewe hunena mema daima.
Yaani Mungu alipoaamua kumkomboa mwanadamu ikamlazimu kuvaa mwili ili aje kuukomboa ulimwengu. Na ndio maana aliitwa Immanuel yaani Mungu pamoja nasi, naye alipokuja duniani akaenda msalabani ili atengeneze madhabahu yake kwa njia ya kumwaga damu. Na nguvu ya damu ya Yesu ni kuwa hakutenda dhambi hivyo damu yake ina nguvu dhidi ya madhabahu zote za giza.
Wakati wao wanaitia damu za mafahari na mbuzi sisi tunanena damu ya Yesu, inayonena mema. Kwa kutumia damu ya Yesu twaweza kunyamazisha damu nyingine za giza.
BOMOA MADHABAHU:
Katika jina lenye Nguvu la Yesu Kristo ninaharibu kila madhabahu za kishetani kwa Jina La Yesu. Ninabomoa madhabahu zinazoleta vifungo kwenye maisha yangu katika Jina La Yesu. Madhabahu za magonjwa, mikosi na laana ninazibomoa na kuzisambaratisha katika Jina la Yesu. Ninateketeza madhabahu zote katika Jina La Yesu.
Nyamazisha damu yoyote iliyomwagwa inayonena mabaya kwa ajiliya maisha yako:
Nanyamazisha damu zote zinazonena mabaya juu yangu katika Jina la Yesu, Nanyamazisha damu ya mbuzi na damu zote za wanyama kwa Damu ya Mwanakondoo. Ninaamuru damu yoyote inayonena mabaya juu yangu inyameze Kwa Damu ya Yesu Kristo. Imeandikwa Damu ya Yesu inanena mema nami kwa Damu hiyo ninanyamazisha kila damu za mashetani na damu ya Yesu inene mema kuanzia sasa.
Sasa baada ya kusoma hili jarida, ni uamuzi wako kutumia damu ya Yesu au ya Kafara za Wachawi na waganga wa kienyeji. Nakushauri uchague Damu ya Yesu ambaye inazungumza.nena mambo mema kwa ajili yako.
Katika huduma Yake,
Mungu awabariki sana.
Ni mimi Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo,
For Max Shimba Ministries Org,
MAX SHIMBA MINISTRIES ORG ©2016. ALL RIGHTS RESERVED
Everyone is permitted to copy and distribute verbatim copies of this license document, but changing it is not allowed.
April 10, 2016

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW