Thursday, April 7, 2016

JE YESU WA WAKRISTO NDIYE YULE ISA WA WAISLAM?

Ndugu msomaji,
Mara kwa mara, unaweza kuwasikia Waislamu wakisema kuwa Isa a.s. kama anavyotajwa ndani ya Qur’an tukufu, ndiye Yesu Kristo wa Nazareti, kama anavyotajwa ndani ya Biblia Takatifu.
Wanafanya hivyo kwa kulinganisha baadhi ya aya zilizomo ndani ya Biblia Takatifu, na zile zilizomo ndani ya Qur’an. Kwa mfano, wanasema kwa mujibu wa Biblia mama yake Yesu Kristo anaitwa Mariamu. Wanasoma katika Injili ya Marko 6:3-4“Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose na Yuda na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake” .
Wanafananisha aya hiyo na ile iliyomo ndani ya Qur’an katika Suratul Al-Maidah, 5:75 “ Masih bin Maryam si chochote ila ni mtume tu……”,
Hoja nyingine wanayoitumia ni kusema kwamba eti jina Isa ni katika lugha ya Kiarabu. Jambo hilo siyo kweli. Kwa sababu katika lugha ya Kiarabu, Yesu anaitwa Yasu’a siyo Isa. Na ikumbukwe kuwa Biblia ndicho kitabu kilichotangulia kuwepo duniani miaka ipatayo 1500 kabla ya Qur’an.
Hoja yetu kwa Waislamu ni hii nani aliyebadilisha jina Yasu’a kuwa Isa?. Jina Yasu’a linashabihiana zaidi na Jina Yehoshua ambalo hilo ni katika lugha ya Kiebrania, na katika Kiyunani lugha iliyotumika kuandika Agano Jipya anaitwa Iesous (tamka Yesu) tafsiri ya maneno hayo kwa lugha ya Kiswahili ni Mwokozi.
Tunasoma hayo katika Math 1:21-23 “ Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana yeye ndiye atakaye waokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”
Hoja yetu Je Isa a.s naye ni Mwokozi na Imanueli kama alivyo Yesu Kristo?
Jambo jingine tunalopaswa kulizingatia tunapoangalia tofauti zao ni kuhusu mama zao. Mama yake Yesu Kristo ni Mariam anayetoka katika ukoo wa Yuda. Tunasoma hayo katika kitabu cha Mwanzo 49:10 “ Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake,Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki,Ambaye mataifa watamtii”.
Unabii huu umetimia kwa Yesu Kristo.Tunasoma hayo katika Waebrania 7:14 “Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lolote juu yake katika mambo ya ukuhani”
Lakini tusomapo habari za Isa, yeye mama yake anatoka ukoo wa Imrani. Ambaye ni baba yao Haruni, Miriamu na Musa.
Tunayasoma hayo katika Suratul Al-Maryam 19:28 “Ewe dada yake Haruni. Baba yako hakuwa mtu mbaya. Wala mama yako hakuwa hasharati”.
fafanuzi unaoifafanua aya hii ya 19:28 uliyomo ndani ya Qur’an, tafsiri ya King Fahd uk. 405, unasomeka hivi “ This Harun (Aaron) is not the brother of Musa (Moses), but he was another pious man at the time of Maryam (Mary)”
Tafsiri “Huyu Harun siyo ndugu yake Musa, bali alikuwa ni mtu mwingine tu mcha Mungu, aliyeishi wakati wa kipindi cha Maryam”
Kwa mujibu wa Biblia, Haruni ni mtoto wa mzee Amran na mama yao anaitwa Yekobedi na kwao wamezaliwa watoto watatu Haruni, Miriam na mdogo wao Musa. Tunasoma hayo katika kitabu cha Hesabu 26:59 “Na jina la mke wa Amramu aliitwa Yokebedi binti wa Lawi ,ambaye alizaliwa kwake Lawi huko Misri; na huyo Yokebedi akamzalia Amram Haruni,na Musa,na Miriamu umbu lao”
Tofauti nyingine ni kuumbwa kwao: ISSA KAUMBWA. Qur’an Suratul Imran, 3:59 “ Bila shaka hali ya Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama hali ya Adam; alimwumba kwa udongo kisha akamwambia: “Kuwa”; basi akawa”
Lakini tusomapo kumhusu YESU, YEYE HAKUUMBWA BALI NI NENO LA MUNGU.
Yoh 1 : 1,14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu……..Naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu…….”
Mika 5:2 “ Bali wewe, Bethlehem Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israel; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele”
Yoh: 8:58 “ Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahim asijakuwako, mimi niko”.
Zaidi ya hayo Biblia inatujulisha kuwa yeye ndiye Muumbaji mwenyewe
Yoh 1:3 “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika”
Kol 1:16-17 “ Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana ; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake”
2) (A) ISSA A.S : BAADA YA KUONDOKA KWAKE, (KAMA WAISLAMU WANAVYOAMINI), HAJAWAHI KUTOKEA KWA NAMNA YOYOTE ILE.
(B) YESU KRISTO: BAADA YA KUONDOKA KWAKE ALIMTOKEA PAUL (SAUL).
Mdo 9:4 “ Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Saul, Saul, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema , Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe”
3) (A) ISSA A.S: ALITABIRI KUJA KWA MUHAMMAD Quran Suratul As Saff , 61:6
“Na (wakumbushe) aliposema (Nabii) Isa bin Maryamu (kuwaambia mayahudi) enyi wana wa Israili! mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu. Nisadikishaye yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati. Na kutoa habari njema ya mtume atakayewajia nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad(Muhammad). Na maana ya majina mawili yote haya ni moja. Maana yake Mwenye kushukuriwa kwa maneno yake mazuri na vitendo vyake vizuri na kila chake kwani vyake vyote ni vizuri).Lakini alipowajia kwa hoja zilizowazi walisema: “ Huu ni udanganyifu uliyo dhahiri”.
(B)YESU KRISTO ALIMTUMA ROHO MTAKATIFU KATIKA SIKU YA PENTEKOSTE.
Yoh: 14:26 “.Lakini huyo Msaidizi,huyo Roho Mtakatifu,ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,atawafundisha yote,na kuwakumbusha yote niliyowaambia”. Katka Kiyunani anaitwa “Paracletos” yaani msaidizi au mfariji
Yoh 15:26 “ Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia”
Yoh 16:7 “Lakini mimi ninawaambia iliyo kweli; yawafaa nyinyi mimi niondoke,kwa maana mimi nisipoondoka huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu nitampeleka kwenu”.
4) (A) ISSA A.S : JINA LAKE HALINA NGUVU WALA UWEZO WA KUOKOA BALI NI RANGI MBILI
Katika Al-Lu’lu’war-Marjani, Juzuu na1, Hadithi na104 uk. 64 “ Hadithi ya Ibn Abbas (r.a) kutoka kwa Mtume (s.a.w) amesema, “Nilimuona Musa (a.s) katika usiku wa Al-Isra, niliopelekwa,naye ni mtu mrefu, mwenye nywele za hudhurungi zimejikunjakunja kama mtu wa Shanua.Na nilimuona Isa (a.s), naye ni mtu wa wastani wa umbo, unaelekea kwenye wekundu na weupe, ana nywele zilizonyooka……”
(B) YESU KRISTO: JINA LAKE NI WOKOVU. Mdo 4:9-10,12 “ kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu,jinsi alivyoponywa, jueni nyinyi nyote na watu wote wa Israel ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye nyinyi mlimsulubisha, na Mungu alimfufua katika wafu kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu…………………….Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”
Baadhi ya aya ndani ya Qur’an zinaeleza kuwa Isa a.s aliwaponya wenye upofu. Ni akina nani hao tutajiwe angalau mmoja? Yesu alimponya kipofu Batromayo.
Aya zingine zinasema Isa a.s alifufua wafu. Ni akina nani hao?
Yesu alimfufua Lazaro.
Jina tulilopewa ni jina moja tu lenye wokovu la Yesu Kristo. Jina la Isa a.s lisilo na wokovu limehusishwaje na jina la Yesu Kristo wa Nazareth lenye wokovu?

Mdo 16:31 “ Wakamwambia , Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka wewe pamoja na nyumba yako.”
5) (A) ISSA.A.S : YEYE SIYO MWANA WA MUNGU. Qur’ani Suratul Al An-Am,6:101 “Yeye ndiye Mwumba wa mbingu na ardhi. inamkinikanaje awe na mwana, hali hana mke. Naye ndiye aliye umba kila kitu (sio baadhi yake kavizaa). Naye ni mjuzi wa kila kitu”.
Qurani Suratul At-Tawba (Kutubu), 9:30 “Na Mayahudi wanasema “Uzeri ni mwana wa Mwenyezi Mungu” na “Wakristo wanasema “Masihi ni Mwana wa Mwenyezi Mungu” Haya ndiyo wasemayo kwa vinywa vyao (pasi na kuyapima). Wanayaiga maneno ya wale waliokufuru kabla yao, Mwenyezi Mungu awaangamize. Wanageuzwa namna gani hawa!
Fundisho la Uwana wa Mungu kama Biblia inavyofundisha, halimo katika mafundisho na itikadi ya dini ya Kiislamu kwa hiyo Isa a.s siyo mwana wa Mungu.
(B) YESU KRISTO: YEYE NI MWANA WA MUNGU. Luka 1:30-31,35
“Malaika akamwambia usiogope Mariamu,kwa maana umepata neema kwa Mungu.Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Malaika akajibu akamwambia,Roho Mtakatifu atakujilia juu yako,na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli;kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu Mwana wa Mungu.
Hivyo Isa siyo Mwana Mungu lakini Yesu ni mwana wa Mungu. Kwa hivyo Yesu siyo Isa.
6) (A) ISSA A.S: YEYE SIYO MUNGU ALIYEFANYIKA MWILI. Suratul Al- Maidah,(meza), 5:72-73 Bila ya shaka wamekufuru wale waliosema, “ Mwenyezi Mungu ni Masih (issa)bin Maryam”.(Na hali ya kuwa)Masihi alisema “Enyi wana wa Israel! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahali pake (patakuwa) ni Motoni. Na madhalimu hawatakuwa na wasaidizi (wa kuwasaidia siku ya Kiama) “Kwa hakika wamekufuru wale waliosema mwenyenzi Mungu ni mmoja katika (wale waungu) watatu (yeye ndiye watatu wao ) hali hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu mmoja ( tu peke yake) na kama hawataacha hayo wasemayo kwa yakini itawakamata wale wanaoendelea na ukafiri miongoni mwao adhabu iumizayo”.
(B)YESU YEYE NI NENO LA MUNGU LILILOFANYIKA MWILI:
Yoh 1 : 1,14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu……..Naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu…….”
7) (A) ISSA A.S YEYE HAJAWAHI KUSULUBIWA WALA KUUWAWA
Qurani Suratul An-Nisaa (Wanawake) 4:157-158
“Na kwa (ajili ya )kusema kwao sisi tumemuua masihi Isa mwana wa Maryamu, mtume wa Mungu. Hali hawakumuua wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa (mtu mwingine wakamdhani nabii Isa.) Na kwa hakika wale waliokhitalifiana katika (hakika)hiyo (ya kumuua nabii Isa) wamo katika shaka nalo (jambo hilo kusema kauwawa]. Wao (kabisa) hawana yakini juu ya (jambo)hili (la kuwa kweli wamemuua nabii isa) isipokuwa wanafuata dhana tu.Na kwa yakini hawakumuua. Bali mwenyenzi Mungu alimnyanyua kwake. Na mwenyenzi Mungu ni mwenye nguvu (na)mwenye hikima.
(B)YESU KRISTO: YEYE ALISULUBIWA MSALABANI
Yohana 19:18,31,33 “Wakamsulibisha huko,na wengine wawili pamoja,mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati.Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato(maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe,wakaondolewe. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa,hawakumvunja miguu”.
8) (A) ISSA A.S HANA HADHI YA KUABUDIWA NA BINADAMU YEYOTE.
Qur’an, Suratul Al-Maidah, 5:116 “ Na (kumbukeni) Mwnyezi Mungu atakaposema: “Ewe Isa bin Maryam! Je ,wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu’?” Aseme (Nabii Isa): “Wewe umetakasika na kuwa na mshirika, hainijuzii mimi kusema ambayo si haki yangu (kuyasema, kwa kuwa ni ya uongo), kama ningalisema bila shaka ungalijua ; unayajua yaliyomo nafsini mwangu, lakini mimi siyajui yaliyomo nafsini mwako; hakika Wewe ndiye ujuaye mambo ya ghaibu.
B) YESU ANASTAHILI KUABUDIWA NA WANADAMU NA MALAIKA
Math 2: 2 “yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? kwa maana tuliiona nyota yake mashariki nasi tumekuja kumsujudia.”
Yoh 9: 35 “ Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu? Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? Yesu akamwambia Umemwona, naye anayesema nawe ndiye. Akasema, naamini, Bwana, akamsujudia.”
Filipi 2:10-11 “ili kwa Jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Ebr 1:6 “ Hata tena amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu Malaika wote wa Mungu.
9) (A) ISA HASTAHILI KUWA MWOMBEZI WA WATU KWA MUNGU
Sahih Al-Bukhari, vol.6 ,Hadithi no 3, The Noble Qur’an, English Translation uk. 8
“…….Nenda kwa Musa, mtumishi wa Allah ambaye Allah alizungumza naye uso kwa uso na alimpa Torati. Hivyo watakwenda kwake naye atasema ‘ Mimi sistahili kwa jukumu hilo la uombezi, na atataja mauaji aliyoyafanya kwa mtu ambaye si muuaji, na hivyo atajisikia aibu mbele ya Mola wake, naye atasema nendeni kwa Isa, mtumishi wa Allah, Mjumbe wake neno lake na roho iliyotoka kwake. Isa atasema sistahili mimi kubeba jukumu la uombezi…….”
B) YESU ANASTAHILI KUWA MWOMBEZI WA WANADAMU KWA MUNGU
1 Tim 2:5 “ Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;”
Ebr 7:24-25 “ bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka.Naye, kwa sababu hii , aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu Hai siku zote ili awaombee.
10) (a) ISA NI NABII MWINGINE TU ASIYE TOFAUTI NA WENGINE
Qur’an Suratul Baqarah, (ng’ombe)2:136 “ “Semeni nyinyi (Waislamu waambiwe Mayahudi na Manasara; waambieni): “Tumemwamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa, na yale yaliyoteremshwa kwa Ibrahimu na Ismail na Is-haqa na Yaaqubu na kizazi (chake Yaaqubu); na waliyopewa Musa na Isa na pia yale waliyopewa Manabii (wengine) kutoka kwa Mola wao; hatutofautishi baina ya yoyote katika hao. (Wote tunawaamini); na sisi tumenyenyekea Kwake.”
b) YESU YEYE YU JUU KULIKO VITU VYOTE
Efeso 1:20-23 “ aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na malaika, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”
11) (a) ISA ATAKAPORUDI, ATAOA NA KUZAA WATOTO
Mishkat Al- Masabih, vol 2 uk.1159, Sahih Muslim, vol. 1 uk 92 “ Isa atakaporudi ataishi miaka arobaini (40), muda ambao atakuwa ameoa na kuzaa watoto, na atafanya ibada ya hija.”
b) YESU ATAKAPORUDI ATAKUJA KULINYAKUA KANISA, YAANI BIBI ARUSI
Efeso 5:25-26, 32-33 “ Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, Uf 19:7 “ Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana Kondoo imekuja na mkewe amejiweka tayari.akajitoa kwa ajili yake, ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;…..Siri hiyo ni kubwa ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mmewe.”
12)(a) ISA ATAKUFA BAADA YA KUISHI MIAKA AROBAINI (40)
Mishkat Al- Masabih, vol 2 uk. 1159,Sunan Abu Dawud, Hadithi 4310, Sahih Muslim, vol.1, uk.92 , “Isa atakaporudi ataondosha dini zote zisiwepo isipokuwa Uislamu. Atamharibu Masih Dajjal, na ataishi duniani miaka arobaini (40) na kisha atakufa. Na baada ya kufa atazikwa pembeni mwa kaburi la Muhammad.”
B) YESU BAADA YA KUFUFUKA YU HAI SIKU ZOTE HAFI TENA
Rum 6:9 “ tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena.”
Ebr 7:24-25 “ bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka.Naye, kwa sababu hii , aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu Hai siku zote ili awaombee.”
Uf 1:17-18 “ Nami nilipomwona nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, mimi ni wa kwanza na wa mwisho, aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama , ni hai hata milele na milele nami ninazo funguo za mauti na za kuzimu.”
13)(a) ISA ALIPOZALIWA SAUTI YA FARAJA ILITOKA CHINI YA ARDHI
Qur’an Suratul Maryam,19:23-24 “ Kisha uchungu ukampeleka katika shina la mtende, (akawa anazaa na huku) anasema: “ Laiti ningekufa kabla ya haya, na ningekuwa niliyesahaulika kabisa.” Mara ikamfikia sauti kutoka chini yake (inamwambia): usihuzunike. Hakika Mola wako amejaalia (ameweka) kijito cha maji chini yako;”
Mafundisho ya Kiislamu yanaeleza kuwa huko chini ya ardhi kuna mnyama. Na huyo mnyama anazijua aya za Qur’an.
Qur’an katika Suratul Al-Naml, 27:82 “Na kauli (ya kuja kiyama) itakapowathibitikia Tutawatolea mnyama katika ardhi atakayewasemeza kwa sababu watu walikuwa hawaziyakinishi Aya Zetu”
b) ALIPOZALIWA YESU SAUTI ZA MALAIKA ZILITOKA JUU
Luka 2:13-16 “ Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini”
(14)(a) ISA HANA UFAHAMU WA MAMBO MBALIMBALI
katika Al-Lu’lu’ war- Marjan,kitabu cha 3 Hadithi na 1528 uk.883 “Hadithi ya Abu Huraira (r.a) kutoka kwa Mtume (s.a.w) amesema “Issa Ibn Mariam (a,s) alimwona mtu anaiba akamuuliza umeiba? akasema hapana ,Naapa kwa Allah ambaye hakuna mola isipokuwa yeye .Issa (a.s) akasema nimemuamini Allah na limeniongopea jicho langu”.
b) YESU ANAYAJUA YOTE
Yohana 1:47-48 “ Basi Yesu akamwona Nathanael anakuja kwake, akanena habari zake “Tazama Mwizraeli kweli kweli hamna hila ndani yake. Nathaeli akamwambia umepataje kunitambua? Yesu akajibu akamwambia, Kabla Filipo hajakuita ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona”
Yoh 2:24-25 “ Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe aliyajua yaliyomo ndani ya mwanadamu”
15) (a) ISA A.S MAMA YAKE ALIKUTWA PEMBEZONI MWA MSIKITI ALIPOLETEWA HABARI ZA KUZALIWA KWAKE.
Qur’an Suratul Maryam,19:16-17 “ Na mtaje Mariamu kitabuni humu. Alipojitenga na jamaa zake, (akenda) mahali upande wa mashariki (wa msikiti) na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea muhuisha Sharia Yetu (Jibrili)- akajimithilisha kwake (kwa sura ya) binadamu aliye kamili
b) YESU KRISTO, MAMA YAKE ALIKUTWA NYUMBANI KWAO NAZARETI
Luka 1:26-28 “Mwezi wa sita malaika Gabriel alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti. Kwa mwana mwali Bikira aliyekuwa ameposwa na mtu jina lake Yusufu wa mbari ya Daudi. Na jina lake Bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, salamu uliyepewa neema Bwana yu pamoja nawe.”
16)(a) MIMBA YA ISA ILIKUWA NI YA SIKU MOJA
Qur’an Suratul Maryam,19:21-22 “ (Malaika) akasema: “ Nikama hivyo (unavyosema; lakini) Mola wako amesema ‘Haya ni sahali Kwangu, na ili Tumfanye muujiza kwa wanaasamu na rehema itokayo Kwetu (ndiyo Tumefanya hivi);’ Na hili ni jambo lililokwisha kuhukumiwa.” Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka mahali pa mbali”
b) MIMBA YA YESU SIKU ZILITIMIA.
Luka 2:6-7 “ ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni”
NB: Mwezi wa sita uliotajwa katika Luka 1:26 ni mwezi wenye kuelezea umri wa mimba ya Yohana ndani ya tumbo la Elizabethi. Luka 1: 36 “ Tena tazama jamaa yako Elizabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa”
NB: Hori iliyotajwa hapa,ina maana ya chombo cha kulishia wanyama kinachokuwa ndani ya zizi. Kwa Kiyunani (Kigiriki) ambayo ndiyo lugha iliyotumika kuandikia Agano Jipya ,chombo hicho kinaitwa “Fatne” kwa Kiingereza kinaitwa “a manger”
17)ISA (A.S) ATAKAPORUDI ATAKUJA KUVUNJA MISALABA NA KUUA NGURUWE
Mkweli Mwaminifu, Juzuu 3-4, uk.20, Hadithi na. 753 “ Haisimami saa ya (kiyama) mpaka akuteremkieni nabii Isa (a.s) mwana wa Maryamu atahukumu (kwa sheria ya Kiislamu) (na) muadilifu, basi atavunja misalaba (ya Wakristo Makanisani) na ataua nguruwe, na ataondosha fedheha au (aibu), na mali itazidi kuwa nyingi sana mpaka hataikubali (ataikataa) mtu (kwa kuogopa kiyama)” .Soma pia katika Sahihi Bukhar, vol. 3, Hadithi na 425,. Al-Lu’lu’war-Marjan, juzuu ya 1,Hadithi na 95 uk.51. The Noble Qur’an uk.757
b)YESU KRISTO ATAKAPORUDI ATAWATUMA MALAIKA ZAKE KUWAKUSANYA WATAKATIFU
Luka 24:30-31 “ ndipo itakapoonekana ishara ya mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi, naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.”
ONYO LA YESU KRISTO WA NAZARETH
Math 24:24 “ kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini hata walio wateule.” (Angalia pia Marko 13:22)
Yoh 8:24 “ Kwa hiyo naliwambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye mtakufa katika dhambi zenu.”
WEWE MTEULE JE UTADANGANYWA NA KUDANGANYIKA KUWA KWELI ISA A.S NDIYE YESU KRISTO? UKIAMINI HIVYO UTAKUWA UMEDANGANYIKA NA UTAKOSA WOKOVU WA MWENYEZI MUNGU!!!!!!!!!!
YESU KRISTO, YEYE NI IMMANUEL, MSHAURI WA AJABU, MUNGU MWENYE NGUVU, BABA WA MILELE, MFALME WA AMANI!!!! (ISAYA 9:6, MATH 1:23) HIZI SIYO SIFA ZA
Shkhê Êdén Hãzãrd kwa Max Shimba Ministries
Mungu awabariki sana,
Ni mimi Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo,
For Max Shimba Ministries Org,
MAX SHIMBA MINISTRIES ORG ©2016. ALL RIGHTS RESERVED
Everyone is permitted to copy and distribute verbatim copies of this license document, but changing it is not allowed.
April 5, 2016

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW