Friday, April 1, 2016

IMAM WA MSIKITI AOKOLEWA NA YESU




Zak Gariba ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia yao. Kwa sababu ya kulitaja jina la Yesu msikitini, Zak Gariba, ambaye alikuwa ni imam alitupwa si tu nje ya msikiti, bali pia nje ya familia yake. Alikataliwa na kujikuta hana tena ndugu; na akapoteza kila kitu. Matokeo yake alifika mahali ambapo aliamua kujiua. Lakini Yesu Kristo mwenyewe alienda kugonga mlango wa nyumba yake na akayabadili kabisa maisha yake kutoka mautini na kumwingiza uzimani.

Kwa maneno yake mwenyewe, Zak anasema:

“Nilizaliwa katika familia ya Kiislamu na kulelewa katika Uislamu na wazazi wangu walinichagua niweze kupata mafunzo ili nije kuwa imam. Nilienda kwenye shule na nikajifunza pia lugha na utamaduni wa Kiarabu.

Nilisomea masomo ya kuwa imam. Baadaye nilienda Nigeria na nikawa imam wa msikiti mmoja. Nilipenda kile nilichokuwa nakifanya.

Kuna wakati nilikutana na Wakristo fulani marafiki zangu ambao walikuja na Biblia zao na tukaanza kubishana, huku nikiwaambia kuwa Quran ina nguvu kuliko Biblia. Tuliendelea kubishana na ikafika mahali nikawapiga. Nikafikia pia wakati ambao nikawa nimewachoka; nikawa nataka waende zao, maana wao walikuwa ni  watu wakimya. Nikawa natafuta namna ya kuwaondoa.

Baadaye waliniomba kama naweza kuwabeba kwa gari hadi mahali fulani ambako kulikuwa na mkutano wa injili. Nikasema, kama hilo ndilo mnalotaka, nitawapeleka – maana niliona hiyo ni njia itakayonisaidia kuachana nao.

Mama mwenye nyumba yangu alikuwa na msichana mdogo ambaye, tangu kuzaliwa,  alikuwa amepooza kuanzia kiunoni kuja chini. Waliniomba nimbebe ili kumpeleka kwenye mkutano. Nilimbeba hadi kwenye huo mkutano uliokuwa unafanyika kwenye uwanja mkubwa.

Niliegesha gari nyuma ya uwanja na kulikuwa na spika kubwa imeelekea kulekule; na kuna mtu akawa anasema Yesu, Yesu!

Baada ya kuegesha gari, watu wengine wenye magari nao walikuja. Nikajikuta nimezingirwa na magari mengine kiasi kwamba haikuwezekana kutoka tena.

Msichana yule akataka kutoka kwenye gari. Ikabidi nimbeba mikononi ili nimpeleke kwenye benchi mojawapo. Na yule mtu wa kwenye spika naye aliendelea tu kusema Yesu, Yesu. Na mimi nikawa ninatamani kufunga masikio yangu ili nisisikie lakini siwezi, maana nimembeba huyu msichana.

Lakini wakati kuo kitu cha ajabu kilitokea. Mguu wa huyu msichana ulisogea kwa namna isiyo ya kawaida. Nikawaza, ‘Ha! Nini hiki tena? Bila shaka hii ni voodoo! Huu utakuwa ni uchawi tu!’

Na kadiri yule msemaji alivyoendelea kusema Yesu, Yesu, miguu ya msichana huyu iliendelea kusogea zaidi na zaidi. Nikawa kama nimechanganyikiwa. Kisha huyu msichana akasema, ‘Nataka kutembea.’

Nikamwambia, ‘Hutaweza.’

Matokeo yake, aliniuma. Ninalo kovu hapa(kwenye mkono). Ikabidi nimwachie hadi chini. Na mbele ya macho yangu, nilimwona msichana huyu akitembea!

Nami nikawa najiuliza, ‘Inawezekanaje mtu mmoja ataje jina la Yesu na mtu mwingine apone kabisa? Nikaanza kuwaza kuwa, ni lazima kuna kitu hapa kwenye kitendo tu cha kutaja jina hili la Yesu.

Baadaye nilirudi nyumbani na jioni ile, kama kawaida, nilienda msikitini. Nilipokuwa msikitini nikiongoza swala, sijui ni kwa vipi, lakini kwa namna nisiyoelewa, ghafla maneno yalinitoka mdomoni ambayo hata sijui yalitoka wapi. Badala ya kusema,  Muhammad-sallal-laahu-alaihi-wasallam, nilijikuta tu nasema kwenye spika za msikitini pale, ‘Yesu Kristo wa Nazareti!’ Katikati ya msikiti! Katikati ya waumini wengi! Nilichanganyikiwa. Matokeo yake waumini wakanitoa nje. Walitaka hata kuniua!

Na huo ukawa ni mwanzo wa matatizo yangu.

Baada ya hapo, kaka yangu mkubwa alinisaidia kuja Kanada kusoma. Nilipokuja huku, niliazimia kuwa nitaishi maisha ya kipagani kabisa. Sikutaka kuwa Mkristo wala kuwa Mwislamu!

Lakini nakumbuka tarehe 3 Januari 1997 nilikuwa chumbani kwangu na nilikuwa nimepanga kujiua. Nilikuwa nimefika mwisho wa maisha yangu kabisa. Wazazi wangu walishanikataa; na hata walishafanya msiba kwa ajili yangu. Kila kitu kilikuwa hovyo kwangu. Nilikuwa nimeshaandaa vidonge na kila kitu.

Ilipofika saa 3:00 asubuhi nilisikia mlango ukigongwa. Nilipandwa na hasira sana. Nikaenda kuangalia, lakini hakukuwa na mtu. Nikawaza, hii ni ajabu! Yaani Kanada? Mbona hapa watu wana simu wanaweza kukupigia kabla ya kuja kwako!

Nikarudi ndani. Lakini nikasikia mtu anagonga tena. Nilipofungua, sikuona mtu tena. Nikafunga mlango na kuwaza, ‘Labda atagonga tena mara ya tatu.’ Kwa hiyo, nikanyagakanyaga sakafu kama vile natembea – ili kwamba huyo mtu afikiri kuwa nimeenda ndani. Lakini nikawa nimesimama palepale karibu na mlango.

Mara kweli nikasikia amegonga tena. Nilipofungua, hakukuwa na mtu; lakini nikasikia sauti ambayo sijawahi kuisikia maishani mwangu. Ilisema, “Mama na baba yako wamekuacha,  lakini mimi nitakuwa pamoja nawe.”

Nikatazama huku na huku na kuwaza, ‘Yaani sasa nimeanza hata kusikia sauti!’

‘Wewe ni nani? Wewe ni nani?’ niliuliza.

Sauti ile ikasema, ‘Mimi ni Yesu. Sasa nakuita kufanya jambo jingine.’

Nikasema, ‘Hebu ngoja kidogo. Nilitaja jina la Yesu wa Nazareti msikitini matokeo yake nikaingia kwenye matatizo makubwa kiasi hiki ...! Sitaki kujihusisha na chochote kinachohusiana na wewe!’

Akasema, “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Niko tayari kukusaidia.’

Na huo ndio ukawa mwanzo wa maisha yangu.

****************

Zak Gariba, kwa neema ya Mungu, pamoja na kukataliwa na ndugu na kila mtu, alimpata Mungu wa kweli. Hivi sasa yeye ni mchungaji. Unaweza kusoma zaidi habari za kanisa lake kwenye www.orilliajubileecc.org.

Yesu yuko tayari kukuokoa na wewe sasa. Usichelewe kumwita na kumkaribisha moyoni mwako. Kanuni ya msingi ya wokovu ni kwa mtu kuamua moyoni mwake na kuchukua hatua ya kusema, ‘Bwana Yesu karibu moyoni mwangu ili unipe uzima wako wa milele.’ Kuna watu wachache tu ambao Bwana Yesu, kwa kuamua mwenyewe, huwaendea uso kwa uso na kuwatoa kwenye upotevu na kuwaingiza uzimani. Kwa hiyo, usije ukasema, nitangoja hadi Yesu atakapokuja kugonga mlango wa nyumba yangu kama alivyofanya kwa Zak Gariba ndipo nitaokoka. Anaweza asije kabisa hadi mwisho kwa namna hiyo; maana hiyo si kanuni ya msingi ya wokovu. Lakini usiku na mchana anagonga kwenye moyo wako kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye husema na dhamiri zetu muda wote.

Uzima wa milele haupatikani kwenye dini yoyote – iwe ya Kikristo au isiyo ya Kikristo. Uzima wa milele unapatikana kwa Yesu Kristo pekee. Yesu hakuja kuokoa Wakristo – maana wakati alipokuja duniani hadi anaondoka, wala hakukuwa na Ukristo. Yesu alikuja kwa ajili ya dhambi za wanadamu wote. Yeye ni Mwokozi wa ulimwengu wote – si Mwokozi wa Wakristo.

Tatizo la dhambi ni tatizo la wanadamu wote. Na hilo ndilo tatizo pekee linalomfanya mwanadamu yeyote aikose mbingu na kuingia jehanamu ya milele. Lakini tumepewa njia rahisi na ya uhakika ya kupona na kuokoka; nayo ni kumwamini Yesu ambaye alikufa ili awe sadaka kwa ajili ya dhambi zetu. Hii ni kwa sababu sisi hatuna kabisa uwezo wa kuishi maisha matakatifu kwa nguvu zetu wenyewe kiasi cha kufikia utakatifu wa Mungu mwenyewe. Maana bila utakatifu, HAKUNA yeyote atakayeingia mbinguni. Na ni mwanadamu gani basi anayeweza kusema kuwa yeye ana maisha matakatifu? Bila shaka hakuna hata mmoja.

Ndiyo maana Yesu aliye Mungu, alikuja kuishi maisha ya kibinadamu, lakini kwa ukamilifu wa kiungu ili kwamba, kwa kule tu kumwamini, sisi si tu tunahesabiwa haki ya kuwa wana wa Mungu, lakini pia tunapewa neema ya kuishi maisha matakatifu.

Amua leo!

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW