Saturday, November 28, 2015

NAMNA YA KUMWITA,KWENDA NA KUMUOMBA MUNGU ILI AKUSIKILIZE.

Yeremia 29:12 “Nanyi mtaniita,mtakwenda na kuniomba,nami nitawasikiliza”.

Utangulizi 

Watu wengi wamekuwa wakitamani maombi wanayoyapeleka mbele za Mungukusikilizwa.Watu wanaomba kila aina ya maombi inayowezakana maadam Mungu asikie na kuwaokoa kutoka kwenye shida waliyonayo au kuwapa haja za mioyo sawasawa na uhitaji wao.

Wapo wanaoomba na wanaona majibu yao yanajibiwa lakini pia lipo kundi jingine kubwa ambalo wanaona kama vile Mungu amenyamaza, amewaacha, hawasikii, au wanajiona kama vile Mungu amewakataa na kuziona ahadi za Mungu kwamba si za kweli na mbaya zaidi wengine wamefika mahali pa kumwacha Mungu kwa sababu ya kushindwa kuvumilia majibu kutoka kwa Mungu na hivyo kutafuta njia mbadala za kutatua matatizo yao. 

Wapo walioomba kuhusu watoto, ndoa zao, afya zao,ajira,biashara,Elimu zao nk. Walipoona katika fahamu zao Mungu hajibu basi wakaamua kwenda kwa waganga wa kienyeji,wachawi na kwa miungu mingine kutafuta msaada huko.

Sasa ili Mungu aweze kusikiliza au kujibu maombi yako huenda kuna mambo mengi ya msingi ambayo mwombaji anapaswa kuyajua na kuyatendeakazi. Sasa baada ya kuona maombi mengi ninayoomba na pia ambayo wana wa Mungu pia wanaomba hayajibiwi ili nilazimu nimuombe Mungu anifundishe vizuri kuhusu hili neno.

Hivyo hayo ninayoenda kukushirikisha ni sehemu ya yale ambayo Mungu amekua akifundisha naamini na wewe yatakusaidia maana nimeona yakinisaidia binafsi pamoja na wale ambao Mungu amenipa kuwafundisha kwa njia nyingine.

Lengo la ujumbe huu ni kukupa maarifa yatakayokusaidia kuomba maombi ambayo wewe mwenyewe.Pindi unapoomba utakua na uhakika Mungu anakusikiliza kwa wakati  huo.Zaidi ujumbe huu umekusudia kukufundisha namna unavyoweza ukapeleka maombi mbele za Mungu.

Siku moja nikiwa chuoni mwaka wa kwanza majira ya tisa jioni,nilikua nikipandisha ngazi kuelekea chumbani kwangu ambacho kilikua ghorofa ya tatu juu kabisa.Wakati naanza kupandisha zile ngazi nikasikia mtu ananiuliza ndani yangu 

Je hivi Mungu huwa anaitwaje?Anaendwaje?Anatafutajwe?Anakaribiwaje? Nilipofika chumbani nikaanza kutafakari haya maswali na baadae ndipo nikapata hii mistari katika Yeremia 29:12-13 inayosema “Nanyi mtaniita,mtakwenda na kuniomba,nami nitawasikiliza 13 nanyi mtanifuata na kuniona,mtakaponifuata kwa moyo wenu wote.”Baada ya kuisoma vizuri ndio nikagundua karibu maswali yale yote yalitoka hapa.

Mungu anasema nanyi mtaniita, sasa na mimi nikuulize swali, hivi umeshawahi kujiuliza Mungu tunamwitajemwitaje? Tunamwendeaje? Na tunamtafutaje. Usiishie kusema Mungu ameseam nikaribieni nami nitawakaribia, umneshawahi kujiuliza anaposema tumkaribie yeye yuko wapi? Na pia tunamkaribia kwa namna gani? Sasa hayo ndio maswali yaliokuwa yakinijia.

Picha ambayo Mungu alitaka niipate kwenye zile ngazi ni hii, nifikirie kwamba kile chumba kule juu ndiko aliko yeye yaani mbinguni. Sasa baada ya kufikiria hivyo ndio niwaze na nijiulize amesema nimuite nimwendee nimtafute n.k Sasa hivi ndio ninamwitaje, ninamwendeaje na ninamtafutaje? Nilipozidi kutafakari hiyo mistari roho mtakatifu akanifundisha yafuatayo:
kwanza alinionyesha makosa matatu ambayo watoto wake mara nyingi tumekuwa tukiyafanya wakati wa maombi. Na ningependa na wewe uyajue kwa maana itakusaidia ili bado unayafanya basi usiyafanye tena.


Kosa la kwanza, 
Kuomba kinyume au nje ya mapenzi ya Mungu.
1 Yohana 5:14 inasema Na huu ndio ujasiri tulionao kwake ,ya kuwa,tukiomba kitu sawa na mapenzi yake atusikia” Moja ya tafsiri za kiingereza inasema “We are certain that God will hear our prayers when we ask for what pleases him” Kosa kubwa ambalo tumekuwa tukilifanya mara nyingi ni kuomba vitu au mambo ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

Anaposema sawasawa na mapenzi ya Mungu maana yake ni lazima ujue kwanza nini ni mtazamo au mawazo ya Mungu juu ya hilo unalotaka kuliombea. Maombi ni kuzungumza au kusemezana na Mungu kwa Kumwambia yale ambayo amesema kwenye neno lake kuhusu haja zako wewe.

Kwa lugha nyingine usiombe kitu ambacho hujui nini Mawazo ya Mungu juu ya hicho kitu. Mawazo ya Mungu juu ya kila haja ujyonayo yako ndani ya Neno lake .Hivyo ni lazima Neno la Mungu likae kwa wingi ndani yako ili unapoomba uombe kulingana na ahadi zake na pia sawa na kile alichokisema.

Zaidi pia wengi wanapotaka kuomba huenda kuhusu ndoa,kanisa,Ajira,watoto ,biashara nk huwa wanomba kimazaoea. Maana yake ni hii wengi wamezoea ninpoombea ndoa nitaombea amani,upendo ,furaha nk Sasa sina maana hayo maombi hayafai ila ninachotaka ukipate ni hiki hoja unazozipeleka mbinguni hakikisha umefunuliwa na Mungumwenyewe.Maana yake Mungu ndiye akupe mambo ya kuombea kuhusu nchi ,ndoa,biashara yako nk.


Kosa la pili, 
Kukosa utulivu na uskivu wa rohoni wakati wa maombi na baada ya maombi.
Sikiliza Mungu anayo mambo mengi ya kukuambia wewe kuliko yaje wewe uliyonayo wewe kumweleza yeye. Chungu hakiwezi kumwambia mfinyanzi kwamba ulinumba kwa kazi hii tu, bali mfmyazi ndiye mwenye mengi kuhusu kile chungu. 

Ndio maana Yesu anasema si ninyi mlionichagua mimi bali ni mimi niliyewachagua njnyi (Yohana 15:16),Sasa watu wengi sana wana bidii nzuri ya maombi wanaweza wakakaa hata masaa matatu mfululizo na hata zaidi wanamuomba Mungu tu.

Katika mda huu wote wao ndio wanaojieleza na mara wanapomaliza ni kusema Ameni na kuondoka.Hii ni picha ya mtoto anayekuja kwako kama mzazi anasema baba/mama naomba hela ya daftari, nauli na ya kula shuleni, pia naomba uninunulie suruali nk. Sasa kabla wewe hujamjibu yeye ameshafungua mlango na kuondoka.sasa kibiblia ndiko kunaitwa kukosa utulivu na usikivu wa rohoni mbele za Mungu.


Mara zote unapoomba jifunze kuwa na wakati wa kutulia kusikiliza Mungu naye anasema nini.Kwenye utulivu ndiko Mungu anakosema sio kwenye kelele maana anjua hamwezi kusikilizana.Soma Isamwel 3:1-10 utaelewa ninachokisema hapa.Mungu alisema na Samweli alipotulia.


Kosa la tatu, 
Kumuomba Mungu wakati tayari umeshajitafutiajibu la shida uliyo nayo.

Hili ni kosa jingine kubwa ambalo wana wa Mungu wamekuwa wakilifanya. Wengi wana mahitaji mbalimbali.Wapo watu wengi ambao kweli wanaomba kwa kumaanisha mbele za Mungu na wengine hata kufunga kwa masaa mengi lakini tatizo lao katika fahamu zao wameshafanya uamuzi wa nini watafanya baada ya maombi yao.sasa hata Mungu akikushirikisha mawazo yake si rahisi ukamwelewa kwa sababu tayari kwenye nafsi na ufahamu wako kuna jibu na Biblia inasema Aonavyo mtu katika nafsi yake ndivyo alivyo.

Sambamba na hilo, kosa linalofanana na hili ni wale watu wanaomwomba Mungu afanye kama vile wao waonavyo kataka nafsi zao. Yaani wanamtaka Mungu akubaliane na Mawazo yao na njia zao juu ya shida au haja walizo nazo wao wenyewe.

Na jambo hili tunalielewa vizuri tunaposoma katika Kitabu cha Luka 9:12 -17 .Habari za wanafunzi wa Yesu pindi njaa ilipokuwa ikiwauma watu wakati Yesu anaendelea na mkutano. Wao walimwambia Bwana waage watu wakajijinunulie chakula vijijini na mashambani, wao walidhani hili ndilo jibu la njaa ya watu. Hawakufikiri kwamba sio wote wenye pesa za kununua chakula, Kuwaaga watu kungemaanisha Yesu aache kufundisha nk. Sasa jibu la njaa ya wale watu halikuwa kama wanafunzi walivyowaza na walivyotaka bali jibu lilikuwa kwa Yesu kufanya muujiza wa kubariki mikate mitano na samaki wawili vitosheleze watu wote 5000.

Sasa baada ya kuwa tumeona hayo makosa makubwa matatu tuangalie Mungu anaposema nanyi mtaniita,mtakwenda na kuniomba,nami nitawasikiliza ana maana gani?.

Katika mstari huu kuna mambo makubwa matatu yamezungumziwa.


Moja ni MTANIITA,mbiIi MTAKWENDA NA KUNIOMBA, tatu ni NAMI NITAWA

SIKILIZA.
Jambo la kwanza ni ,
Mtaniita.
Ukisoma kitabu cha Yeremia 33:3 anasema “Niite,nami nitakuitikia ,nami nitakuonyesha mambo makubwa,magumu usiyoyajua. Mungu ansema utakapomwita yeye atafanya mambo mawili.Moja atakuitikia na mbili atakuoyesha mambo makubwa,magumu usiyoyajua.

Maana yake ni hii, kukuonyesha mambo makubwa,magumu usiyoyajua ni kukufunulia mambo ambayo ulikuwa huyajui katika lile ulilomuita.Hivyo basi kumuita Mungu ni kumuomba au Kumtaka Mungu akufunulie mambo makubwa na magumu usiyoyajua kuhusu shida au hitaji au haja uliyonayo mbele zake. Mfano unamuita Mungu akufunulie ndoa yako jinsi ilivyo, nini kinaendelea usichokijua, nini ukiombee, nini hakijakaa sawasawa kwenye hiyo ndoa k.
 Hivyo basi unapotaka kuomba juu ya jambo lolote lile ni vizuri kwanza ukamuita Mungu juu ya hilo jambo.Maana yake muombe Mungu akupe picha kamili ya hilo unalotaka kuliombea,akufunulie jinsi lilivyo ili ujue uanzie wapi kuomba.,kama ni ndoa,nchi,mke au mme mtarajiwa,Huduma yako nk.


Jambo la pili 
Mtakwenda na kuniomba.
Sasa baada ya kuwa umemuita Mungu kinachofuata ni kwenda na kumuomba Mungu. Anaposema mtakweda na kuniomba ana maana mtaanza kuomba sawasawa na vile nilivyowaonyesha au nilivyowafunulia wakati mliponiita katika haja zenu.Hivi ulishawahi kujiuliza ni mambo gani makubwa na magumu ambayo Mungu atakuonyesha_pindi utakapomuita?. Kumbuka tulikotoka tumeona Kumuita Mungu ni kumfanya Mungu akufunulie mambo usiyoyajua kuhusu hitaji lako ili ujipange vizuri kuyaombea.

Sasa kwenda na kuomba maana yake ni kuomba sawasawa na vile Mungu alivyojifunua kwako kuhusu hitaji ulilonalo.Utakapoomba namna hii ndiko kunaitwa kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu maana yake unaombea mambo ambayo Mungu anataka uyaombee kwa wakati huo. Kwa lugha nyepesi jifunze kuomba mambo ambayo Mungu anakuongoza kuyaombea. Labda nitoe mifano michache ndio somo litaeleweka vema.

Mfano wa kanza huenda mnaombea mgonjwa au mtu aliyefungwa na mapepo. Ni kweli Biblia imesema mtaweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata afya. Sasa si kila mgonjwa ni wa kuweka mikono na kuanza kukemea ugonjwa au mapepo, kuna magonjwa mengine yanasababishwa na mawazo yaani tatizo ni mtu mwenyewe, Mwingine huenda ni kwa sababu ya kujeruhiwa nafsi yake na mwingine huenda ni kwa sababu ya dhambi, na mwingine huenda mikataba aliyoingia mwenyewe na mapepo na huenda mengine ni Mungu mwenyewe ameruhusu Shetani aguse afya ya huyo mtu kama alivyomruhusu shetani kwa Ayubu nk..

Saa nafikiri mpaka hapa umeshaona si wagonjwa wote utakawawekea mikono watapona. Hivyo ni vema umuite Mungu akufunulie nini cha kufanya, mwingine atakuambia huyu anahitaji ushauri tu wala si maombi,mwingine anaweza kukuambia huyu ametenda dhambi hii na hii akizitubia nitamponya, na mwingine atakuambia huyu hicho ni kipimo chake mpe tu neno la uvumilivu na Ushindi,Mwingine atakuambia huyu ndugu mwenyewe au wazazi wake waliingia mkataba na mapepo hivyo vunja kwanza mktaba huo nk.

Mfano wa pili,huenda mnaombea kanisa lenu. Ni rahisi kusema tumuombe Mchungaji ndani ya kanisa,mara tuombee kamati ya ujenzi tuombe Mungu kuhusu ujenzi nk.Kweli ni maombi mazuri lakini una uhakika Mungu kwa wakati huo anataka muombee hayo mambo.Huenda kuna roho ya mpinga Kristo ina vamia washirika au kuna maajenti wanajiingiza kwa siri makanisani na kuwapofusha macho ninyi mnakazana kuombea ujenzi. Maana yangu ni hii ikiwa wewe ni mchungaji au kiongozi wa maombi katika kundi lolote lile ni vema kila wakati kumuita Mungu akupe mambo ya kuombea kwa wakati huo. Mungu atakufunulia nini unachotakiwa kuombea kwa wakati huo.

Nina ujasiri na ninachokisema kwa sababu siku moja tukiwa katika kambi la vijana.Nilikuwa kwenye timu ya maombi ya hilo kambi.Ndani ya hiyo timu tulikuwa na wajumbe wa shetani kutoka kuzimu yaani maajenti (vibaraka wa shetani).Hawa jamaa walikuwa wakiomba na kufimga kuzidi masaa yale tuliyokuwa tukifunga sisi.Na wakati wa kuomba walikuwa wanapendekeza tuombee na kukemea roho ambazo hazifanyi kazi katika lile eneotulilokuwepo. Na walikuwa wanajita watumishi wa Mungu.Nina uhakika wa habari hii kwani Mungu alinifungua macho tukaomba na nguvu za Mungu ziliposhuka mmoja wo akasema “sisi ni wajumbe wa shetani kutoka kuzimu,tulitumwa kuleta uharibifu lakini katika yale tuliyotumwa tumeshindwa kuyatekeleza”.

Nakuambia tangia siku hiyo ndipo nilipofunguka macho yangu ya ndani na kuanza kuhitaji uongozi wa Mungu katika yale tunayoomba kila siku.Hujawahi kuona Kiongozi wa maombi anasema jamani hee tutaombea hili na hili na hili,lakini mnapoanza kuomba unakuta Mungu anakuongza kuombea vitu vingine kabisa ?

Kumbuka siku zote katika kila unaloliomba ,mwambie Mungu nifunulie zaidi kuhusu mambo ya kuomba kuhusu hili jambo.lwe ndoa,kanisa,mkutano au semina,Watoto,elimu nk Sasa nimalizie kwa kusema kuomba kwa namna hii ndiko Kibiblia kunaitwa kumtafuta Bwana.Sikiliza huwezi kumtafuta mtu mahali asikopatikana.Unapomtafuta Bwana ni lazima umtafute kwenye maeneo yake yaani kule anakopatikana.Sasa kunaitwa kumtafuta Bwana kwa sababu umeomba kulingana na ufunuo wake

Ni imani yangu kuwa baada ya kuwa umesoma ujumbe huu basi naamini umeshapata maarifa ya kukusaidia katika kumtafuta Bwana na hivyo kwa jambo lolote utakalotaka kuomba siku zote utaomba kwanza ufunuo wa Mungu juu ya hili jambo.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nawe.
Na: Patrick Samson Sanga

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW