Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake, nao hawakushinda, wala mahala pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na shetani, audanganyaye ulimwengu wote akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye… kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari. Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu (Ufunuo 12:7 – 12).
Shetani hayuko hapa duniani kucheza. Yuko kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kwa hali na mali wewe usiingie mbinguni. Yeye anayo kazi moja tu, ya kupigana na wewe na akushinde. Yeye halali. Akikushindwa leo kesho anatafuta mbinu nyingine. Hivyo yako mashambulizi makali ya shetani, roho waovu mapepo na majini.
Mtu wa Mungu huwezi kuyashinda mashambulizi ya shetani bila kujifunza mbinu zake anazozitumia na huwezi kumshinda bila ya wewe kujifunza upiganaji. Wakristo wengi wameshindwa vita hii japokuwa bado wanaenda kanisani.
Baada ya mtu kuokoka, hupata passport ya kwenda mbinguni. Sambamba na passport hiyo Mungu humpa nguvu, uweza na mamlaka ya kumwezesha kupigana na shetani na kumshinda. Hivyo mkristo anatakiwa ajipiganie yeye mwenyewe na ashinde. Yesu ameshakupa passport ya kwenda mbinguni, hivyo ipiganie hiyo nafasi ili shetani asikumyang’anye, usipojipigania utaikosa mbingu.
Lakini pamoja na hayo, kuwa na nguvu, uweza na mamlaka, bila ya kuwa na ujuzi wa hali ya juu wa kuvitumia ni kazi bure kuwa navyo. Hili ndilo tatizo la wakristo, wanazo nguvu, uweza na mamlaka lakini hawajui mbinu ya kuvitumia. Ni sawa na raia asiyepitia mafunzo ya kijeshi, umpe mzinga, ndege ya kivita, n.k akapigane vita.
Shetani hushambulia kupitia njia kuu mbili. Njia ya kwanza ni kupitia roho waovu walioko ndani ya wazazi, na mababu zetu. Baada tu ya mtu kuzaliwa roho waovu walioko ndani ya wazazi na mababu huingia ndani ya mtu. Hii ni njia ya mapokeo, tunapokezana kutoka kwa wazazi. Wazazi walipokea kutoka kwa mababu. Hawa roho waovu tumeishi nao muda mrefu, hivyo wametutumikisha sana, sasa tumezoea kutumikishwa nao, maana wamekuwa nasi tangu kuzaliwa. Roho waovu hawa hata mtu baada ya kuokoka huendelea kumfuatafuata tu. Ni lazima wakufuate maana wamekuwa ni rafiki wa ukoo na familia yenu. Kama hutajua jinsi ya kupigana na hawa roho waovu wa mapokeo ni razima wakushinde tu. Hawa roho waovu wa mapokeo unaweza kuwashinda kwa kujifunza laana na kuivunja. Bila kuijifunza laana na kuivunja ni lazima wakushinde. (soma kitabu changu kiitwacho, ULIIVUNJA LAANA ULIPO AMINI?
Njia kuu ya pili ya shetani kushambulia ni kwa majeshi yake ya pepo yaliyoko katika ulimwengu wa roho yanayofanya mashambulizi ya kila siku mchana na usiku. Haya mashambulizi ni ya kawaida mashambulizi haya unayashinda kwa maombi ya kawaida lakini yawe yenye nguvu. Nikisema maombi ya kawaida nina maana ya kuwa, maombi ambayo siyo kuvunja laana.
Katika kitabu hiki tunaenda kujifunza mbinu anazozitumia shetani kutushambulia kupitia njia hii ya pili yaani mashambulizi ya kawaida. Sambamba na kujifunza mbinu za ushambuliaji anazotumia shetani, huwezi ukamshinda, bila ya wewe kuwa na mbinu madhubuti. Hivyo tutajifunza pia mbinu madhubuti za kumshinda. Nimetangulia kusema kuwa, utamshinda kwa maombi. Katika kitabu hiki sitazungumzia kuhusu maombi hayo bali tunaenda kujifunza mbinu za kumshinda shetani. Baada ya kuzijua mbinu hizo ndipo utaomba na kumshinda. Ukiomba bila kujua mbinu huwezi ukamshinda, ni sawa na kipofu kupigana na mtu mwenye macho, kipofu hataweza kushinda. (kama unataka kujifunza uombaji wenye nguvu, soma vitabu vyangu, MSINGI WA MAOMBI, KUNENA KWA LUGHA, NGUVU YA UFUNGAJI, UNAYO MAMLAKA.
• Mapigano ya mwili na roho
Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na roho na roho kushindana na mwili, kwa maana hizi zinapigana, hata hamwezi kufanya mnayotaka (Wagalatia 5:17).
Mtu ana mwili, nafsi na roho, mwili ni udongo. Mungu alifinyanga udongo akaupulizia pumzi ya uhai. Baada ya mtu kufa mwili hurudia hali yake ya udongo. Pumzi ya uhai ndiyo roho. Roho hii imetoka kwa Mungu, inayo tabia ya uMungu. Hii roho ndiyo mwanadamu mwenyewe atakayeishi milele, aidha mbinguni au Jehanamu kutegemeana na mtu mwenyewe alivyo hapa duniani.
Roho inayo tabia ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, kwa vile inajua kuwa isipompendeza Mungu itatupwa Jehanamu hivyo inajitahidi kumpendeza Mungu. Matendo ya roho yanaitwa tunda la roho.
Lakini tunda la roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, juu ya mambo kama hayo hakuna sheria
(Wagalatia 5:22 – 23)
(Wagalatia 5:22 – 23)
Mwili unataka kuifaidi dunia, maana unajua kuwa uko hapa duniani kwa muda tu na utarudi katika udongo. Roho hata kama itaenda mbinguni au jehanamu mwisho wa mwili hautabadilika. Hivyo mwili unataka kufanya matendo ya dunia hii ambayo hayampendezi Mungu, mwili hauna juhudi yoyote katika kuifanikisha roho iende mbinguni. Hivyo mwili unataka kufanya mambo yake, na roho nayo inataka ifanye mambo yake, hivyo mwili na roho vinapigana ili kila mmoja anayotaka ndiyo yafanyike.
Basi matendo ya mwili ni dhahiri ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu (Wagalatia 5:19 – 20).
Hivyo mwili unataka matendo ya mwili ndiyo yafanyike, roho inataka ifanye matendo ya roho. Katika kupigana huko anayeshinda ndiye mambo yake yanatendeka.
Baada ya Adamu na Hawa kutenda dhambi roho ya mwanadamu ilikufa japo kuwa tunatembea. Hivyo mtu akabaki mwili na nafsi. Watu wakaendelea kuzaliwa wakiwa mwili na nafsi huku roho zao zimekufa. Baada ya mtu kumpokea Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yake, hapo hapo hutokea badiliko la kiungu katika ulimwengu wa roho. Roho huhuishwa na kuwa hai, wakati huo huo mwili hufa japo kuwa tunatembea. Badiliko hili au tukio hili ndiyo huitwa kuokoka. Huku ndiko kuzaliwa mara ya pili, mara ya kwanza ulizaliwa mwili na mama yako na mara ya pili umezaliwa roho na Yesu. Hapo ndipo jina la mhusika huandikwa kwenye kitabu cha Uzima wa milele.
Na hao walio katika Kristo wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake (Wagalatia 5:24).
Roho na mwili vinapopigana katika mtu ambaye hajaokoka, roho lazima ishindwe maana imekufa. Hivyo mtu ambaye hajaokoka ni lazima atende matendo ya mwili, atake asitake. Roho na mwili vinapopigana katika mtu ambaye ameokoka mwili lazima ushindwe maana utakuwa umekufa. Hivyo mtu aliyeokoka atatenda matendo ya roho, ambayo ni tunda la roho.
Uwanja wa mapambano
(Msitari wa mbele katika vita)
(Msitari wa mbele katika vita)
Nafsi ndiyo sehemu ya ufahamu wa mwanadamu; sehemu ya uwezo wa kujitambua, ndiyo akili (mind). Baada ya udongo kupuliziwa pumzi ya uhai ndipo nafsi ilitokea, kikawa kiumbe hai kinachojitambua. Mwanadamu ataingia mbinguni na ufahamu wake akijitambua. Ni hivyo hivyo hata watu watakaotupwa Jehanamu watatupwa na ufahamu wao, watakuwa wanajitambua.
Kazi ya nafsi katika mtu ni nini? Ili niweze kulijibu swali hili vizuri, hebu nimfananishe mtu na gari. Gari lina kiungo kimoja kiitwacho usukani. Usukani katika gari ni chombo ambacho kinageuza gari mwelekeo, gari liende kushoto, kulia, mbele, n.k.
Nafsi nayo katika mtu inafanya kazi hiyo hiyo. Mtu anafanya mambo mengi sana; anasema mengi, anafikiri mengi; n.k yote haya yanawezeshwa kufanyika na nafsi. Hii ndiyo kazi ya nafsi kuwezesha mambo yote yatendeke anayoyatenda mtu.
Usukani kwenye gari, japo kuwa unaliwezesha gari liende kushoto, kulia, hauwezi kuamua gari liende kushoto, kulia, mbele au vinginevyo. Usukani hauamui gari kukata kona. Anayeamua gari likate kona ni dereva anayeliendesha hilo gari, yeye anakotaka kwenda ndiko gari litakwenda. Na hivyo hivyo hata nafsi. Nafsi haiwezi kuamua kitu gani mtu atende. Tumeona habari ya roho na mwili kupigana. Hawa hupigania nini hasa? Hawa hupigania usukani, nani aushike usukani ili amwongoze mtu kutenda matakwa ya aliyeushika usukani. Hivyo usukani ukishikwa na mwili mtu atalazimika kutenda matendo ya mwili na kama usukani ukishikwa na roho basi mtu atalazimika kutenda tunda la roho.
Mtu ambaye hajaokoka roho yake imekufa hivyo watakapopigana roho na mwili, roho atashindwa. Roho atashindwa kwa sababu amekufa. Mwili atashika usukani, hivyo mtu huyu ataishi maisha ya dhambi. Hata akijiunga kwenye dini na kufuata taratibu zote za dini, hata akipata elimu ya juu ya neno la Mungu na hata akipata wadhifa mkubwa kwenye dini hiyo, yote hayo hayatamsaidia kuishinda dhambi.
Mtu ambaye ameokoka roho na mwili wakipigana, mapigano hayo roho atashinda. Roho ataushika usukani hivyo mhusika atalazimika kutokutenda dhambi.
Uwanja wa vita wa mapambano, ndiyo mstari wa mbele wa mapambano, kwenye vita vyenyewe, kwenye mapigano makali kati ya Mungu na Shetani, wakati wakipigania nani amchukue mtu. Uwanja wa mapambano hayo huwa ni kwenye nafsi. Vita yote ya mtu aende Jehanamu au aende Mbinguni, hupiganiwa ndani ya mtu mwenyewe kwenye nafsi. Wakristo wengi hawalijui hili ndiyo maana wamekuwa wakristo wakushindwa na shetani. Hapa inakuwa ni tofauti na yule mfalme wa uajemi aliyezuia majibu ya maombi ya Danieli. Haya majibu yalikuwa yanatoka mbinguni, shetani akamzuia malaika njiani, Mikaeli alikuja akapigana naye. Hawa walikuwa nje ya Danieli. Kutokana na hili wakristo wengi hata wanapopigana na shetani, maombi yao mapigo wanayaelekeza angani kuelekea mbinguni. Kupigana kwa namna hiyo ni kwa wapiganaji wasio na ujuzi wa kazi ya kuomba, hawana elimu ya kupigana na shetani. Adui yuko mstari wa mbele, hayuko angani, mstari wa mbele ni kwenye nafsi. Mapambano yote yanayohusu maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu, hufanyika kwenye nafsi.
Nchi ya Marekani ilipotaka kuipiga nchi ya Afghanistan ilitafuta rafiki aliyekaribu na Afghanistan ili kiwe kituo cha kuongozea mapambano. Hivyo hivyo Mungu na Shetani wanapopigania kumchukua mtu, huweka vituo vyao karibu na uwanja wa mapambano mwili na roho tayari wako uadui, hivyo shetani huja kushirikiana na mwili kwa sababu nia yao inafanana. Mungu naye huweka kituo chake kwenye roho kwa vile wote nia yao inafanana.
Hii vita hugeuka badala ya mwili na roho kupigana, sasa wanaopigana huwa ni Mungu na Shetani sasa kwenye habari ya matendo ya mwili yaliyo andikwa kwenye Wagalatia 5;19 – 21, badala ya kusomeka matendo ya mwili sasa husomeka, Basi mapepo ya shetani ni uasherati, uchafu, n.k. hivyo hata upande wa Mungu badala ya kusomeka tunda la roho, badala yake inasomeka, Malaika wa Mungu. Nimeweka isomeke hivyo kwa sababu sasa siyo vita ya mwili na roho tena, bali sasa ni vita ya Mungu na Shetani. Hivyo badala ya matendo ya mwili sasa ni mapepo ya shetani, na badala ya tunda la roho sasa ni malaika wa Mungu.
Mungu na Shetani hupigania mtu, anayeshinda anaushika usukani. Kama ni shetani basi mapepo wa shetani huingia kwenye nafsi na kuushika usukani. Na kama aliyeshinda ni Mungu basi malaika wa Mungu huingia kwenye nafsi na kuushika usukani.
Usukani wa gari uko kwenye chumba chenye kiti kipana wanaweza kukaa hata watu watatu japo kuwa dereva aliyeushika usukani atakuwa mmoja tu. Ni hivyo hivyo hata kwenye nafsi ni sehemu ambayo wanaweza kukaa mapepo wengi au malaika wengi, japo kuwa anayeushika usukani anakuwa ni mmoja. Lakini kwa vile wanaokuwemo kwa wakati mmoja ni malaika wengi au mapepo wengi, hivyo hupokezana kuushika usukani leo huyu kesho yule au asubuhi yule, jioni huyu na usiku mwingine anaushika, n.k.
Kama mshindi ni shetani siyo lazima shetani aweke mapepo wake wote ndani ya mtu mmoja. Shetani humwangalia mtu mwenyewe alivyo na kuweka mapepo kadhaa. Mtu akiwekewa mapepo mengi hataziweza kazi zote za mapepo hayo, maana kazi za shetani ni ngumu. Mtu mmoja yeye awe jambazi, mchawi, mgomvi mganga wa kienyeji, shoga, n.k haitakuwa rahisi kwa huyo mtu kuziweza kazi hizo.
Kama mshindi ni Mungu, Mungu huweka malaika zake wote ndani ya mtu mmoja kazi za Mungu ni nyepesi mtu mmoja anaweza kuzimudu zote bila matatizo. Huyo mmoja atakuwa na upendo, furaha amani, utu wema, n.k. na akaziweza.
Mtu ambaye hajaokoka amejaa mapepo kwenye nafsi yake, hivyo mapepo humtumikisha. Mtu anapoamua kuokoka Yesu huingia ndani yake na kuyafukuza mapepo yote. Baada ya kuwafukuza mapepo au roho waovu wote, Yesu huweka malaika wake. Hivyo huyo mtu aliyeokoka kuanzia hapo huanza kuishi maisha matakatifu. Hawezi tena kunywa pombe maana roho iliyokuwa inamwongoza kunywa pombe sasa haiko; hawezi tena kufanya uzinzi, uchoyo, kiburi, ulafi, n.k.
Huyu ndiye mtu wa Mungu anayekwenda mbinguni. Wakristo wa leo wameokoka, wamejazwa Roho Mtakatifu na wananena kwa lugha, lakini bado wana roho waovu wakijidhihirisha. Ni Ukristo gani huu? Ni wokovu gani huu? Mkristo huku ni mzinzi, jambazi, mchoyo, chuki, wivu, mgomvi, hasira, kujikweza, umimi, ubinafsi, kiburi, ubaguzi wa rangi na kabila, n.k kama kweli Yesu aliwafukuza hawa roho waovu ulipookoka na wakatoka ndani yako na malaika wakaingia na kukaa na kuanza kukuongoza, je, imekuwaje tena wewe bado roho waovu wako ndani yako? Wewe unajidanganya kuwa hiyo ni tabia yako! Hiyo siyo tabia bali ni roho waovu. Usifikiri kwenda mbinguni ni kujiunga katika dini na kuwa na bidii ya kwenda kanisani. Kwenda mbinguni ni vita. Vita hiyo haiko kanisani bali iko ndani yako, unatembea nayo, unalala nayo, kila mahali unakokwenda vita unayo ndani yako, unatakiwa uishinde.
Kanisani ni mahali pa kwenda kuongeza ujuzi wa kupigana. Mtu wa Mungu hebu jiulize mara mbili tatu, kuhusiana na wokovu wako, je, kwa nini roho waovu bado wako ndani yako wanakuongoza kutenda mambo yaliyo kinyume na Mungu? Kumbuka watu watendao mambo ya jinsi hiyo roho waovu uliowaruhusu waingie ndani yako, unawapenda wanakutumikisha, hivyo unawatumikia. Umeokoka na kujazwa Roho Mtakatifu lakini bado unatenda dhambi za uzinzi, wizi, rushwa, n.k. kwa nini mkristo aliyeokoka anatenda dhambi?
Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao (Mathayo 18:20).
Neno la Mungu linasema kuwa, watu wawili watatu wakikutana kwa ajili ya Mungu. Mungu naye atakuwa mahali pale ili kulithibitisha jina lake kuwahudumia wote walioko pale, hivyo Mungu, Yesu na Roho Mtakatifu, malaika wanakuwepo pale. Nguvu, uweza na mamlaka ya Mungu vinakuwa pale.
Watu wanapokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Mungu, Mungu anakuwa pale ili kuhakikisha kuwa kila mtu aliyefika pale amehudumiwa, bila ya hata mmoja aliyehudhuria kubaki bila ya kupata huduma. Ingawaje kila mtu hupokea sawasawa na kujitoa kwake. Wengine hupokea kikubwa wengine hupokea kidogo.
Ninamkumbuka mtu mmoja alikuwa mlevi sana wa pombe, mkristo, alikuwa anasali kanisa la Roman Catholic. Alikuwa anapenda kuhudhuria mikutano ya Injili ya hadhara inayohubiriwa na mhubiri Moses Kulola. Mtu huyu alikuwa anayasifu sana mahubiri ya Mhubiri huyu, Mhubiri Moses ana nguvu za Mungu kweli kweli, mimi sitaki kuokoka, lakini nikihudhuria kusikiliza mahubiri yake baada ya mkutano kuisha huwa siwezi kunywa pombe kabisa kwa muda wa miezi miwili, mitatu, ndipo huanza kuwa na hamu ya kunywa pombe tena.
Huyu mtu hakutaka kuokoka, lakini alikuwa anapenda kuhudhuria kwenye kusanyiko la mkutano wa Injili. Mahali hapo Mungu alikuwapo ili awahudumie watu wote waliokuwepo. Hivyo utake usitake ili mradi uko pale lazima utahudumiwa na Mungu, hata kama wewe huzitaki hizo baraka lakini madamu upo pale lazima utaambukizwa hizo baraka. Huyu alikuwa anaambukizwa baraka ambazo alikuwa anakaa nazo mwendo wa miezi mitatu.
Shetani katika utendaji wake naye huiga utendaji kama wa Mungu. Hivyo naye, mahali wawili watatu wamekusanyika kwa ajili ya shetani, shetani naye yuko pale kwa ajili ya kuwahudumia. Hapa ina maana kuwa, shetani, mapepo na roho waovu wanakuwa pale kwa ajili ya kuwahudumia wote watakaokuwa pale.
Roho huhama na kuingia ndani ya watu wakitokea ndani ya watu wengine ambao tayari wanao, aidha roho huhama na kuzagaazagaa wakitafuta watu wawaingie. Utendaji huu wa roho waovu kuhama kutoka mahali na kwenda mahali huitwa uhamisho wa roho (Transference of spirits) kiswahili kizuri ni Uambukizaji wa roho.
Hii ndiyo njia kuu ya pili ambayo shetani huitumia kuwashambulia watu. Hii njia ndiyo hutumika kwa mashambulizi ya kawaida ya kila siku ya shetani. Njia kuu ya kwanza nimesema ni ile ya mapokeo kutoka kwa mababu, ambapo nilisema kuwa roho waovu waliokushambulia kupitia njia hii utawashinda kwa kujifunza kuhusu laana na kuzivunja. Mapepo au roho waovu waliomshambulia mtu kwa njia ya kuambukizwa utawashinda kwa maombi ya kawaida yasiyokuwa ya kuvuja laana. Maombi ya kawaida, lakini yawe ni yenye nguvu.
Kutokana na hili mtu anaweza kuwa na pepo aina moja wengi, lakini wameingia kupitia njia zote mbili, njia ya mapokeo na ile ya kuambukizwa. Utakapopigana nao kwa maombi ya kawaida, wale waliokuja kwa njia ya kuambukizwa watasikia hayo maombi wataondoka, lakini wale waliokuja kwa njia ya mapokeo hawatasikia hayo maombi hivyo hawataondoka. Hawa huondoka kwa kujifunza laana na kuivunja.
Kwa nini hawawezi kuondoka? Hili swali linajibu refu sana, kwa vile somo letu halihusu roho walioingia kwa mtu kwa njia ya mapokeo bali linahusu roho waovu waliomshambulia mtu kwa njia ya mashambulizi ya kawaida, hivyo sitalijibu swali hili bali ukitaka kuelewa soma kitabu changu kinachoitwa, uliivunja laana ulipoamini?
Mungu huhudumia watu wake kwa kupitia watumishi wake mbalimbali, makanisa, mikutano, n.k. ni hivyo hivyo na shetani naye anasambaza mapepo yake ili yawashambulie watu kupitia watumishi wake mbalimbali, wengine wanajijua kuwa ni watumishi wa shetani, wengine wanatumika bila kujijua. Shetani pia anavyo vituo mbalimbali vya kusambazia mapepo yake. Kama vile, vilabu vya pombe, kumbi za starehe, sinema za ngono na za mauaji, magazeti, vitabu, nyumba za kulala wageni, n.k.
Neno la Mungu linasema,
Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki, wala hakusimama katika njia ya wakosaji wala hakuketi barazani pa wenye mizaha (Zaburi 1:1)
Shauri la wasio haki ni kusanyiko lililokusanyika kwa ajili ya shetani. Njia ya wakosaji na baraza la wenye mzaha pia ni mikusanyiko iliyokusanyika kwa ajili ya shetani. Mungu anajua kabisa kusanyiko lolote la watu waliokusanyika kwa ajili ya shetani, shetani, mapepo na roho waovu watakuwa pale, ili kuwahudumia watu wote watakao kuwa pale. Hivyo ndiyo maana Mungu amekukataza usiende katika kusanyiko lililojikusanya kwa ajili ya matendo ya shetani.
Mahali wazinzi wawili watatu wamekusanyika kwa ajili ya uzinzi, pepo la uzinzi liko pale kwa ajili ya kuwahudumia watu wote watakaokuwa pale; mahali wawili watatu wamekusanyika kwa ajili ya ulevi, pepo la ulevi liko pale kwa ajili ya kuwahudumia watu wote watakaokuwa pale. Ni hivyo hivyo hata katika mikusanyiko mingine yote.
Watu baada ya kuokoka Yesu aliingia ndani yao, aliwafukuza mapepo na roho waovu wote. Wakristo kwa uzembe na kutokufahamu neno la Mungu wamekuwa wakiendelea kukaa kwenye mikusanyiko ya kishetani, wameendelea kukaa kwenye mabaraza ya wenye mizaha, wameendelea kusimama kwenye njia za wakosaji, wameendelea kwenda kwenye mashauri ya wasiyo haki. Huko kuna mapepo na roho waovu wanakungoja kukuhudumia. Huko utaambukizwa mapepo.
Mtu mmoja ameokoka, kabla ya kuokoka alikuwa mlevi sana, sasa anasema kuwa, yeye ataendelea kwenda kwenye ile bar aliyokuwa ananywea pombe, anasema anakwenda pale ili akutane na rafiki zake wa zamani ambao bado walevi ili awashuhudie neno la Mungu pale bar. Yeye anasema hatakunywa pombe atakuwa anakunywa soda.
Mimi nakwambia kuwa mkristo wa namna hii ataishia kurudi kunywa pombe tena. Kwenye bar ni kwenye kituo cha shetani cha kusambaza mapepo ya ulevi. Pepo la ulevi liko pale kwa ajili ya kuwahudumia wote watakaokuwepo pale.
Msichana mmoja alikuwa na rafiki yake. Huyu msichana akaokoka. Rafiki yake alikuwa kahaba. Msichana aliyeokoka alikuwa bado anaendelea kuambatana na msichana kahaba katika safari zake za ukahaba, kwa misingi ya kwamba anamsindikiza rafiki yake lakini yeye ameacha ukahaba. Wanapofika kwa hawala wa kahaba yule, msichana mlokole anakaa pembeni kidogo. Kahaba na hawala yake wanaanza kuongea mambo yao ya uzinzi. Wanaongea wanafurahi na kucheka. Huyu mlokole kwa aibu ya kuogopa lawama kwa rafiki yake ili asionekane vibaya, kuwa amedharau maongezi yao, yeye ameamua kuwa asiongee wala asichangie kitu chochote, bali wanapocheka yeye ameaamua kuwa awe anakenua meno pekee. Hivyo wakati mazungumzo yanaendelea yeye yuko kimya, lakini wanapocheka yeye naye mlokole anakenua meno.
Mimi ninasema kuwa huyu msichana hatafika popote baada ya muda ataanza uzinzi, hata kama atakuwa ameshajazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha. Lakini kwa nini ajikute amerudi kwenye uzinzi tena?
Wewe mkristo uliyeokoka na unanena kwa lugha, umejikuta unatenda dhambi tena, umejikuta ni mlevi, umejikuta ni mzinzi, mwizi, jambazi, mseng’enyaji, una wivu, mchoyo, mwasherati, ubinafsi, mshirikina, chuki, n.k umeshambuliwa na shetani na amekushinda, hivyo sasa unamtumikia. Mbinguni huendi maana watendao mambo ya jinsi hii hawataurithi ufalme wa Mungu.
Yesu alifukuza hao pepo uliokuwa nao ulipookoka na walitoka wote. Hapo haikuwa mwisho wa safari. Hapo ndiyo ilikuwa mwanzo wa safari. Biblia inasema, yeye ashindaye. Wewe ulitakiwa undelee kupigana na hawa roho waovu ili wasirudi tena na uendelee kuwashinda. Lakini sasa wamekupiga na wamekushinda. Sasa unawatumikia.
• Mashambulizi kupitia milango ya fahamu
Shetani anapomshambulia mtu, hutupa mishale yake ndani ya mtu huyo kupitia katika milango mitano ya fahamu, yaani kuona, kusikia, kugusa, kuonja na kunusa.
Mishale ya shetani ndiyo hao mapepo huingia ndani ya mtu kupitia hiyo milango ya fahamu.
Mishale ya shetani ndiyo hao mapepo huingia ndani ya mtu kupitia hiyo milango ya fahamu.
Kuona
Siku moja nilikuwa na safari asubuhi mapema sana wakati kulikuwa bado giza giza. Niliondoka kwenda kituo cha magari ya abiria. Kutoka nyumbani nilipita njia za mkato. Nilipita kichochoro fulani katikati ya nyumba na nyumba, ghafla niliona mwanamke na mwanamume wakifanya zinaa pale niliudhika sana, nikageuka na kuamua kupita njia nyingine.
Nilikuwa ninakwenda kuhubiri Injili mji wa mbali. Nilifika safari yangu. Usiku wa manane, nilikuwa ninatafakari mambo mbalimbali. Wakati nikitafakari nilistukia ile picha ya tukio la zinaa nililoliona, ikanijia katika fahamu zangu. Niliudhika sana. Ile picha iliendelea kuja mara kadhaa, na iliendelea muda wa siku kadhaa kuja kwenye fahamu zangu.
Mimi siyo kamera ya sinema, niwe nimelichukua hilo tukio. Kwenye tukio hilo la uzinzi kulikuwepo shetani na mapepo yake tayari kuwahudumia wote watakaokuwepo mahali hapo. Hivyo mimi nilipoona tu tukio hilo, wale roho waovu waliingia ndani yangu kupitia macho yangu. Na pale usiku wa manane nilipoiona tena ile picha, hapo ilikuwa ni yule pepo aliyeingia ndani yangu alitafuta jinsi ya kuingia ndani ya nafsi. Nilipoendelea kuiona ile picha kwa muda wa siku kadhaa, ndivyo hivyo hivyo huyo pepo alivyokuwa akiendelea kujitahidi kuingia kwenye nafsi, ili aushike usukani.
Kusikia
Siku moja nilikuwa nasafiri katika nchi ya Uganda nilikuwa kwenye basi. Ndani ya basi kulikuwa zikiimbwa nyimbo kwenye radio. Nyimbo zile sikuzijua tafsiri zake, zilikuwa katika lugha ya makabila ya huko Uganda. Mimi ni msukuma wa Mwanza, Tanzania kabila za Uganda sikuzielewa. Wakati muziki ukiendelea ulikuja wimbo mmoja ambao kwenye kibwagizo chake uliimba kwa lugha ya kiswahili ambayo niliuelewa tafsiri yake. Wimbo ule ulisema habari za baba mmoja mzee mnene sana, anafanya tendo la ngono na msichana binti mdogo umri wa mjukuu wake. Wimbo huu haukunipendezea kuusikiliza. Baadaye wimbo huu uliisha zikafuata nyimbo zingine ambazo zilikuwa zote za kiganda, hivyo sikuelewa tafsiri za nyimbo hizo. Nilifika safari yangu. Baada ya siku chache niliusikia wimbo huo, hicho kibwagizo tena kikiimbwa ndani yangu. Mimi siyo kinasa sauti bali ile roho ya huo wimbo ndiyo ilikuwa imeingia ndani yangu.
Musa alipotuma wajumbe kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, wajumbe kumi na mbili kila kabila la Israeli mjumbe mmoja mmoja. Kati yao kulikuwa na Yoshua na Kalebu.
Kisha BWANA akanena na Musa. Akamwambia, tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya kanaani, niwapayo wana wa Israeli (Hesabu 13:1 – 2)
Baada ya Musa kuwatuma, walienda wakaipeleleza hiyo nchi wakarudi. Waliporudi walileta habari ya kuwavunja moyo watu, habari ya kuwaogopesha watu. Wana wa Israeli walivunjika moyo na kuogopa kuingia nchi ya Kanaani.
Wakarejea baada ya kupeleleza nchi wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa Wana na Israeli… wakawaletea habari wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakawaambia wakasema. Tulifika ile nchi uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa ile nchi ni hodari, na miji yao ina maboma nayo ni makubwa sana, na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Kalebu akawauliza watu mbele ya Musa akasema, natupande mara, tukaitamalaki, maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea Wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, ile nchi tuliyoipita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi (Hesabu 13:25 – 33).
Wana wa Israeli wakasikia habari ambazo ziliwapa hofu. Hofu ni sumu ya imani, hivyo wana wa Israeli wakaingiwa hofu kuu.
Wana wa Israeli wakaingiwa na roho ovu ya hofu iliyokuwa tayari imeingia ndani ya wapelelezi. Baada ya kusikia hayo ilitokea nini?
Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; wakatoka machozi usiku ule kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni, Mkutano wote wakamwambia, ingekuwa heri kama tungelikufa katika Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake wetu na watoto watakuwa mateka. Je, afadhali turudi Misri. Wakaambiana, tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la Wana wa Israeli (Hesabu 14:1 – 5).
Hapa tayari pepo la hofu lilikuwa limekwisha kuwashambulia Wana wa Israeli kupitia kusikia. Wale wapelelezi walikuwa wameingiwa na hilo pepo la hofu, liliwaingia kupitia kuiona ile nchi, hivyo pepo lilihama na kuwaambukiza mkutano wote wa Wana wa Israeli kupitia kusikia. Tunaona kuwa Yoshua na Kalebu wao lile pepo la hofu halikuwa limewaingia wao walikuwa mashujaa, wao walimwamini Mungu. Walijaribu kuwatoa hofu na kuwatia moyo wa kishujaa, lakini Yoshua na Kalebu walikuwa wamechelewa, maana kwenye nafsi za Waisraeli tayari roho wa hofu alikuwa ameshaingia na kushika usukani na alikuwa ameshaanza kuwaendesha tayari.
Maneno ya Yoshua na Kalebu hayangeweza kuwatoa pepo wa hofu ambao tayari walikuwa wameingia.
Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, walikuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa Wana wa Israeli wakasema, nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wenyeji wa ile nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaongope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe (Hesabu 14: – 10).
Wana wa Israeli roho ya hofu ilikuwa imeushika usukani tayari ikiwaendesha. Huyo alikuwa ni shetani mwenyewe ameshawawahi Wana wa Israeli, ameshawashinda. Yoshua na Kalebu juhudi zao za kuwashawishi Wana wa Israeli, ilikuwa ni sawa na kutwanga maji katika kinu. Kwa vile shetani mwenyewe ndiye aliyekuwa ameshika usukani tayari, hivyo shetani aliamrisha Yoshua na Kalebu wapondwe mawe. Yoshua na Kalebu walifikiri kuwa bado wanaongea na watu wa Mungu, kumbe tayari walikuwa wameshakuwa watumishi wa shetani.
Wakristo wako kanisani wanafikiri bado ni watu wa Mungu kumbe tayari wao ni watumishi wa shetani, ndani yao kuna roho waovu ambao ndiyo wanawaongoza. Haiwezekani kabisa mtu wa Mungu anayekwenda mbinguni, hapo hapo bado anaongozwa na roho waovu wa uzinzi, ujambazi, kujikweza, ubinafsi, ulafi, wivu, hasira, kutokutii neno la Mungu, fitina, n.k. wakristo wanaoleta vurugu kanisani hivi ni roho gani inayowaongoza kuleta vurugu hizo? Hao walishashindwa vita vya kiroho mapepo yaliyomo ndani yao ndiyo yameushika usukani, ndiyo tabia zinazojidhihirisha kwa nje, wanasema, hasira ni tabia yangu, Mungu ataitoa polepole. Unajidanganya wewe mwenyewe, hilo ni pepo la hasira unatakiwa ulishinde. Wengine wanasema, ubinafsi, uchoyo, chuki, n.k. hizi ni tabia tu na wala haziwezi kuwazuia kwenda mbinguni. Sasa nakwambia kuwa, watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurirthi Ufalme wa mbinguni kabisa.
Mungu alikasirishwa na Wana wa Israeli akawaua jangwani wote wale wazee wa miaka ishirini kwenda juu kwa sababu walishindwa kumwamini Mungu, isipokuwa Yoshua na Kalebu ambao walikuwa hawakuingiwa yule roho wa hofu. Mungu akasema Yoshua na Kalebu pamoja na watoto walio na umri wa chini ya miaka ishirini, ndiyo watakaoingia. Hawa watoto wao walikuwa hawapo katika mkutano huo, walikuwa bado hawajafikia umri wa kupigana vita, wao hawakuwa wameingiwa na huyo roho wa hofu. Hivyo Yoshua na Kalebu walichofanya, walikwenda kuwakusanya wale watoto na kuwapandikizia roho ya ushujaa iliyokuwemo ndani yao. Watoto wakawa na roho ya ushujaa na waliingia Kanaani bila woga wala hofu na walishinda.
Njia hii ya kusikia, shetani amewashambulia wakristo wengi na akawaweza. Shetani amewashinda wakristo wengi katika maeneo mbalimbali ya maisha yao. Wengi wameingiwa na roho waovu na wakaanza kutumikishwa katika tabia mbovu za kishetani. Wengine Mungu aliwapa maono fulani mazuri ili wafanye shughuli fulani ya maendeleo yao ya maisha. Kabla ya kutekeleza waliamua kuomba ushauri kwa watu, watu waliwavunja moyo, watu waliwapa hofu kuwa hawataweza. Roho ya hofu ilitoka ndani ya washauri na iliwaingia na waliogopa kuifanya shughuli hiyo ambayo Mungu alikuwa amewaonyesha..
Mungu amekuwa akiwapa watu wake mbalimbali maono mengi kwa ajili ya kazi yake na kwa ajili ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya maisha yao. Walishirikisha watu ili wapate ushauri, ushauri umekuwa ukitolewa wa kuwavunja moyo, hivyo wameshindwa kuyatekeleza maono hayo. Maono hayo umepewa na Mungu kwa nini unatafuta ushauri? Je, humwamini Mungu?
Mtu wa Mungu, shetani huwashambulia watu kupitia roho waovu ambao wako ndani ya watu wengine kwa kupitia kusikia. Wale Wana wa Israeli waliwaangalia wale wapelelezi kwa mtazamo wa wengi wape. Hivyo waliangalia idadi wakaona wale wapelelezi kumi ndiyo wawasikilize, wakaona wale wapelelezi wawili ni waongo, Mungu hatendi kwa mitazamo ya watu, ya kwamba, wengi wape. Mungu haongei na wengi bali Mungu hutumia mtu mmoja au watu wachache. Kuna wasichana ambao walipata wachumba, lakini wakatafuta ushauri wa watu, washauri kumi wakasema mchumba hafai, washauri wawili walisema mchumba anafaa. Wao walifuata ushauri wa wengi wape, kumbe kwa wengi wape ndiko Mungu hakuwepo.
Mtu wa Mungu unapokuwa unaongea na mtu yeyote yule hakikisha unapambanua yale anayoyaongea, maana roho waovu wakati wowote wanatafuta kuingia ndani ya watu wengine kutoka kwa watu wengine. Hili ni pamoja na unapokuwa unasikiliza mahubiri kutoka mhubiri yeyote yule. Wakati mhubiri anahubiri Mungu humtumia mhubiri ili awahudumie watu wanaomsikiliza mhubiri na wakati huo huo shetani naye hutaka kumtumia mhubiri huyo huyo ili naye awahudumie wale wanaomsikiliza huyo mhubiri. Hivyo unaposikiliza neno la Mungu usimeze kila kitu, chambua na kupambanua mifupa tupa, minofu kula.
Mhubiri anaweza kuhubiri vizuri sana neno la Mungu lakini akatumia muda mwingi katika mahubiri yake kujisifu jinsi yeye alivyo mhubiri mzuri au akasifu kanisa lake lilivyo zuri. Waumini wakiondoka pale wataondoka na shida zao walizozileta kanisani ili Mungu akutane nazo, zitakuwa bado zipo. Mungu atakuwa hakukutana nazo, kwa sababu mhubiri hakumwinua Yesu bali alijiinua yeye na dini yake, na kwa vile mhubiri au dini yake havikufa msalabani, hivyo vimeshindwa kukutana na shida za watu. Watumishi wa Mungu haipo sababu ya kujisifu sisi wakati tunahubiri, hebu tumhubiri Yesu peke yake. Tumwinue Yesu peke yake.
Mashambulizi kupitia kusikia ndiyo njia inayotumiwa zaidi na shetani. Hata Mungu ndiyo njia kubwa zaidi anayoitumia. Imani huja kwa kusikia.
Kugusa.
Kuombea au kubariki kupitia kugusa, roho huhama kutoka kwa anayeomba kwenda kwa anayeombewa. Je, wewe unazo roho gani ndani yako? Hivyo roho njema na roho waovu wote waliomo ndani ya mwombaji huhamia kwa anayeombewa. Unapomwombea mtu baraka fulani wakati wewe huna hiyo baraka, ujue hakuna kitu kinachoenda kufanyika. Huna upako unaombea mtu upako!
Watumishi wa Mungu ni muhimu kuishi maisha matakatifu ili usiingiwe na roho waovu na ukaanza kuwaambukiza watu wa Mungu wasio na hatia. Unapoweka mkono juu ya mtu ili kumwombea au kumbariki, katika ulimwengu wa roho hutokea kitu halisi. Tendo hilo siyo maagizo tu. Isaka alipozeeka sana alipokuwa karibu na kufa alitaka kumrithisha Esau baraka zote zilizokuwa ndani yake. Yakobo kwa kutumia ujanja akawa amebarikiwa yeye badala ya Esau. Esau alipokuja aliambiwa kuwa baraka zimeisha. Kwa nini zimeisha? Isaka alikuwa anakufa hivyo alikuwa anahamisha baraka zote kabisa, hivyo alikuwa amezihamishia zote kwa Yakobo. Hata kama Isaka angeamua kumwekea mikono Esau halafu akaomba kwa kutumia maneno yale yale aliyoyasema alipokuwa akimwombea Yakobo, hakungefanyika mbaraka wowote ule, lingekuwa igizo lisilo na maana. Roho wa mbaraka alikuwa ameishahamia kwa Yakobo.
Tofauti na Isaka unapomwombea mtu baraka kwa sasa ambapo wewe huhamishi baraka zote kwa sababu bado unaendelea kuishi na bado unahitaji kuwaombea watu wengine, bado hata wewe unazihitaji, kwa jinsi hii zinaondoka badhi na wewe unaendelea kubaki nazo, akija mwingine naye unamwombea, bado unaendelea kubaki nazo zingine. Isaka alikuwa anahamisha zote ndiyo maana ziliisha.
Watu wa Mungu sasa hivi tuko kwenye kipindi ambacho shetani amejifanya malaika wa nuru. Hivyo anao watumishi wake ambao amewaingiza kwenye kazi ya Mungu. Pia anayo makanisa ya Kikristo yanayomtumikia shetani. Ni kipindi cha kujihadhari sana na mambo ya kuwekewa mikono kila unapoona mhubiri amehubiri na kukusisimua. Wakristo wengi kwa kutokufahamu wamejikuta wamebeba roho za kigeni. Sasa hivi siyo kipindi cha kutegemea uombewe na kuwekewa mikono. Ni kipindi unachotakiwa ujifunze neno la Mungu. Neno la Mungu likijaa kwa wingi ndani yako omba lolote nawe utapewa.
Maelezo hayo kuhusu shetani anavyoshambulia kupitia milango ya fahamu yanatosha kukupa mwanga. Sitazungumzia milango ya fahamu kuonja na kunusa.
Mtu wa Mungu roho waovu wanapoingia ndani ya nafsi yako unawaona kabisa. Kama mimi nilivyosikia wimbo kwa siku kadhaa huo wimbo uliendelea kusikika tena ukiimba ndani yangu. Unaona hapa niliusikia. Pia kama nilivyoona tendo la ngono siku kadhaa niliendelea kuiona hiyo picha tena ndani yangu. Huko ndiyo jinsi roho waovu unavyoweza kuwaona. Unapokumbuka kwenye fahamu zako kitu ulichokiona zamani, huko kukumbuka ujue ni ile roho ya kile kitu ulichokiona huko nyuma. Hivyo ndivyo jinsi ya kuwaona hao roho waovu wanavyokushambulia. Mbali na hivyo kule kuwaza kwenye fahamu jambo fulani ikiwa jambo hilo liko kinyume na neno la Mungu, basi fahamu ya kuwa hao ni roho waovu wanakushambulia.
Roho waovu wanapomshambulia mtu, mtu mhusika huwaona na kuwahisi. Hakuna roho ovu yeyote anayeweza kuingia ndani au anayeweza kumshambulia mtu bila ya mhusika kumwona. Baada ya roho waovu kuingia ndani yako, ndipo huanza mashambulizi. Kama ni roho wa dhambi wanaanza kukushawishi au kukutamanisha kutenda dhambi. Ukiona hivyo ujue kuwa umeshaingiliwa na roho ya kigeni ambayo sasa imeanza kupigana na wewe ili ikushinde utende dhambi. Hapo sasa ndipo kipindi cha vita ya kiroho kilipo. Vita vya kiroho unavyo visikia ndicho kipindi hicho sasa. Hapo usingoje hadi uitende hiyo dhambi. Ukishatenda dhambi ina maana umeshashindwa vita, hata ukija kuitubu hiyo dhambi haisaidii kitu. Sawa utakuwa umesamehewa dhambi hiyo, lakini tatizo utakuwa hujalimaliza, maana roho waovu watakuwa bado wako kwenye nafsi na pamoja na kwamba umetubu. Roho waovu hawataondoka kwenye nafsi kwa sababu ya kutubu, roho ovu huyo ataendelea kukupeleka kutenda dhambi, hivyo utakuwa mkristo wa kuendelea kutumikishwa katika hiyo dhambi. Dawa yake ni kupigana naye huyo roho ovu kwa maombi, mara tu unapoanza kumwona roho ovu ameingia ndani yake. Usimlee wala usimdekeze. Ukitamani dhambi fulani, ujue hapo siyo wewe, bali ujue kuwa umeingiliwa na roho wa kigeni, ujue kuwa roho ovu anakushambulia. Hivyo ndivyo jinsi ya kuwaona hawa roho waovu walioingia ndani yako. Hivyo unao muda wa kutosha kabisa wakupigana na roho waovu kabla hawajakushinda na kuanza kuletea madhara kwako. Maombi ya kawaida yakishindwa, funga na kuomba.
• Mashambulizi ya roho waovu kupitia vitabu, picha, gazeti, sinema, n.k
Wakati fulani nilikuwa ninajifunza kuhusu dini za Kikristo mbalimbali za aina ya cults (ukengeufu) kama vile dini ya Kisabato, Mashahidi wa Jehova, Yesu tu (William Marriot Branham), n.k. wakati nilipokuwa najifunza kuhusu dini ya Sabato, nilisoma vitabu vingi sana. Vinavyohusu misingi mbalimbali ya imani hiyo. Baadaye nilianza kusikia sauti ndani yangu, kuwa, iwapo ningefuata torati ya Musa, nikaongezea katika wokovu nilionao ningekuwa mtakatifu wa hali ya juu sana, kuliko kuokoka pekee au msabato pekee. Nikasikia kuwa waliookoka wamekosea kuutupa Usabato na wasabato wamekosea kuutupa wokovu. Hivyo iwapo nitaacha kula samaki wasio na magamba, nguruwe na niiheshimu siku ya Jumamosi, ningempendeza sana Mungu.
Niligundua kuwa hayo tayari yalikuwa ni mashambulizi kutoka kwa shetani. Vita hiyo niliendelea nayo muda wa siku nyingi kidogo, nilikuwa karibu kushindwa, maana nilifikia hatua ya kujiandaa kuanza kutekeleza. Lakini Roho Mtakatifu akaniambia,
Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato (Wakolosai 2:16).
Niliifukuza hiyo roho hadi nikaishinda ikatoka nikawa siisikii tena.
Wakristo wengi wanasoma vitabu bila kuchagua au kupambanua kuwa kitabu hicho kina madhara kwake kiroho. Biblia ni kitabu kimeandikwa na watu waliokuwa wamejaa Roho Mtakatifu ambaye aliwaongoza kukiandika. Hivyo biblia ni kitabu kilicho na uvuvio wa Roho Mtakatifu.
Ukisoma kitabu kinachohusu mambo ya zinaa kinakuwa kimeandikwa na mtu aliyekuwa ana pepo au roho waovu wa zinaa. Hivyo kitabu hicho kinao uvuvio wa pepo la zinaa. Ukiangalia sinema inayohusu zinaa, walioitengeneza walikuwa na roho waovu wa zinaa ndiyo aliowaongoza kutengeneza hiyo sinema. Hao ni watumishi wa roho ya zinaa, hivyo roho ya zinaa anawatumikisha. Sinema hiyo, hivyo inao uvuvio wa roho waovu wa zinaa. Ni hivyo hivyo hata katika kusikiliza nyimbo mbalimbali.
Wakristo wengi shetani amewashambulia kwa njia hii na kuwashinda kabisa, hivyo sasa wanaendelea kumtumikia shetani, huku wakijidanganya kuwa wanabidii ya kwenda kanisani, wanajidanganya kuwa kwa vile bado wananena kwa lugha, wataingia mbinguni. Mbinguni anaingia mkristo aliyeokoka na kushinda vita. Wewe umeokoka sawa, umejazwa Roho Mtakatifu sawa, unanena kwa lugha sawa, lakini umeshindwa vita.
Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa, kula matunda ya mti na uzima, ulio katika bustani ya Mungu
(Ufunuo 2:17).
(Ufunuo 2:17).
Nimefanya utafiti kuhusiana na magazeti. Magazeti yameanzishwa na watu wanayoyamiliki. Lakini ndani ya wanaoyamiliki magazeti hayo, kuna roho fulani ambayo imewatuma waanzishe hayo magazeti. Japo kuwa gazeti linaweza kuwa na habari nyingi mbalimbali, lakini unaweza kugundua hasa mhimili wa habari zinazotolewa au mwelekeo wa gazeti lenyewe. Kama ni gazeti la siasa utalikuta linakumbatia chama fulani au linaonyesha dalili ya chuki kwa baadhi ya vyama fulani.
Nimeona hapa Tanzania kuna magazeti yanayoongozwa na roho waovu wa mauti. Gazeti ambalo kila toleo au katika matoleo mengi, matukio ya vifo vya kikatili ndiyo hupewa kipauwa mbele, tena habari hizo huandikwa kwa vichwa vya habari vikubwa na kuwekwa ukurasa wa mbele. Habari ya tukio la kifo cha kikatili ni habari, siyo vibaya ikiandikwa kwenye gazeti. Lakini ikiandikwa kwenye gazeti ambalo linaongozwa na roho ya siasa, hiyo habari haitapewa kipauwa mbele, wala haitaandikwa kwa kichwa cha habari kikubwa tena itawekwa katika kurasa za ndani siyo ukurasa wa mbele. Kutokana na hili, shetani naye anayo magazeti yake ya kusambazia roho waovu. Habari moja ya uporaji ulioendeshwa kiufundi sana na kufanikiwa, huyo roho ovu wa uporaji huo anasambazwa na gazeti hilo kwa madhumuni ya kwamba, kupitia watu kuisoma habari hiyo huyo pepo au roho ovu aingie ndani ya watu wengine wengi zaidi, ambao nao watakuwa wakiendesha uporaji kwa ufundi wa hali ya juu.
Habari za kuanguka dhambini mtumishi wa Mungu, mhubiri mkubwa, siyo habari nzuri hata kidogo, siyo habari njema katika kambi ya Yesu. Ni habari njema ya furaha, katika kambi ya shetani, ni habari ya ushindi kwa shetani. Mimi ningeisikia habari hiyo wa kwanza, ningefurahi sana, maana ingeishia kwangu na nisingemwambia mtu yeyote zaidi ya mimi kwa kufanya hivyo ningeizuia habari hiyo isimfikie adui, hivyo ningeitetea kambi ya Yesu. Adui akisikia habari hiyo ataitumia kuwa silaha ya kuwashambulia watu wa Mungu. Wengine watakaposikia wataanguka dhambini na wengine watavunjika moyo, watasema kuwa, kama Mhubiri huyu ameanguka dhambini basi hakuna wokovu. Kuna magazeti yenye kupenda kusambaza habari mbaya zinazotukia katika kambi ya Yesu. Yanasambaza habari hizi si kwa faida ya Yesu bali ni kwa faida ya shetani. Haijalishi gazeti hilo linajiita ni la kikristo au vinginevyo, lakini linaweza kuwepo kwa ajili ya kumtumikia shetani, hivyo badala ya kuujenga ufalme wa Mungu, yanajenga ufalme wa shetani, yanaubomoa ufalme wa Mungu.
No comments:
Post a Comment