Saturday, November 28, 2015

JIFUNZE KUMILIKI MAJIBU YA MAOMBI YAKO

Yoshua 13:1-7
Utangulizi,
Katika dunia ya leo watu wengi sana wamekuwa wakitumia muda wao mwingi ikiwa ni pamoja na kufanya maombi ya kufunga na kuomba ili kumuomba Mungu awabariki, awaponye, awalinde kwa kifupi awajibu mahitaji yao waliyonayo mbele zake siku zote. Wapo waliokuwa hawazai wamezaa, vipofu wameona, wasioajiliwa wameajiliwa, biashara za wengi zimefanikiwa, ndoa nyingi Mungu ameziponya, wapo waliotaka kuolewa au kuoa na Mungu amewapa waume na wake wazuri.
Sasa hao hao watu ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi katika kuomba Mungu awatendee miujiza katika maisha yao, imefika mahali wanaona yale ambayo yalikuwa ni majibu ya Moambi yao shetani ameyavamia na kuleta balaa zaidi na limekuwa pigo kubwa sana kwa wana wa Mungu. Na kwa sababu hiyo wamejikuta wakimlalamikia Mungu kama vile wana wa Israeli na imefika mahali pa wengine kuona kama Mungu hawezi na hivyo kumuacha.
Tatizo la haya yote ni kwamba wakristo wengi hawana tabia ya au mazoea ya kumiliki mujibu ya maombi yao toka kwa Mungu. Huenda ulikuwa huna mtoto na Mungu amekupa kuzaa mtoto, sasa huyo mtoto ndiyo jibu lenyewe kutoka kwa Mungu. Sasa ni lazima ujifunze kumiliki huo muujiza wa mtoto, sasa si mtoto tu bali ni pamoja na ajira, ndoa, uponyaji, kanisa, Nchi, Biashara nk.

Kusudi la waraka huu mfupi ni kukufundisha njia zitakazokusaidia kumiliki majibu ya maombi yako na kukupa maarifa yatakayokusaidia kuwa makini na majibu ya Mungu katika maisha yako.Tafsiri ya Kumiliki, Neno kumiliki linapozungumziwa kibiblia lina maana ya kukiweka kitu au jambo fulani chini ya utawala wako, maana yake unakuwa na nguvu au umri juu ya hicho kitu. Una hakikisha hakiwezi kutoka kwako. Kumiliki siku zote kunahusisha mapambano makali Sasa mimi sijui Mungu amekutendea nini? Ila ninachojua kwa namna moja au nyingine lazima kuna mambo ulikuwa unamuomba Mungu akufanyie na mengine tayari ameshakufanyia na mengine ndiyo anayafanya na bado kuna mengi atafanya.sasa katika hayo aliyokwisha kufanya huenda amekupa mke au mme mtarajiwa, huenda ameiponya ndoa yako, nafsi yako, mwili wako, Afya yako, Huenda amekupa mtaji, amekupandisha cheo, amekupa mtoto, amepanua mipaka ya huduma yako nk.
Katika lolote ambalo amekufanyia unatakiwa kulimiliki kwa maombi. Kama shetani alikuwa hataki uzae usidhani atamfurahia mtoto uliyemzaa. Kama alishindwa kumzuia asizaliwe usidhani atakubali aendelee kuishi. Shetani atafanya kila analoweza kuua huyo mtoto au kuharibu chochote kile ambacho Mungu amekutendea kama jibu. Sasa kwa sababu hiyo ni lazima uzijue njia za Kibiblia zitakazokusaidia kumiliki hayo majibu ya maombi yako kutoka kwa Mungu.
Huenda zipo njia nyingi zifuatazo ni sehemu na ni za msingi kati ya hizo nyingi.
Njia ya kwanza, kumiliki kwa kuupigania na kuujenga huo muujiza au jibu lako toka kwa Mungu.
Yoshua 13:1-7, 2 Samwel 2:1-7.Ule mstari wa kwanza wa kitabu cha Yoshua katika kitabu Yoshua 13 unasema “Basi Yoshua alipokuwa mzee na kuendelea sana miaka yake BWANA akamwambia wewe umekuwa mzee na kuendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa” Kumbuka katika ile sura ya kwanza ya kitabu cha Yoshua Mungu anamwambia Yoshua uwe Hodari na moyo wa ushujaa maana ni wewe utakayewarithisha watu wa nchi hii. Na ukisoma vizuri kitabu chote cha Yoshua unaona kabisa Yoshua alitekeleza agizo la kuwarithisha wana wa Israel nchi ya ahadi.
Wakati Mungu anamwambia Yoshua bado inabaki nchi yaani maeneo mengi sana ambayo bado hayajamilikiwa tayari Yoshua alikuwa ameshapiga zaidi ya wafalme 32 na kuiteka miji yao, lakini bado Mungu anamwambia bado nchi nyingi inasalia. Kitu gani Mungu anataka tujifunze hapa? Sikiliza Yoshua alipewa kuwarithisha wana wa Israel nchi hii lakini sio kuwamilikisha. Suala la kumiliki lilikuwa kwa yule aliyekabidhiwa nchi au mji lakini sio kwa Yoshua. Sasa ndiyo maana Mungu akamwambia Yoshua kwa sababu wewe ni mzee igawanye hiyo nchi kwa wana wa Israeli kwa kufuata kabila zao ili waweze kumiliki. Maana yake waingie kwenye mapambano ya kile ambacho Mungu amewapa kupitia Yoshua.
Niseme hivi chochote unachokipata kwa njia ya maombi kinamilikiwa kwa njia ya maombi, jifunze kukipigania na kukijenga yaani kuendelea kukiri uwepo wa hicho kitu siku zote. Mfano kama uliomba mke au mme na Mungu amekupa usipunguze kuomba maana shetani usidhani anafurahia ndoa au uhusiano wenu. Ukiendelea kusoma zile sura zinazofuata za kitabu cha Yoshua ndipo utakapoona makabila yalivyopambana ili kumiliki jibu lao toka kwa Mungu la nchi.
Njia ya Pili; Miliki majibu yako kwa kutafuta maarifa zaidi ya kutunza huo muujiza.
Hosea 4:6a inasema “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa”.Sikiliza muujiza au jibu lolote lile ambalo Mungu amekujibu au amekutendea una maarifa yake ya kuutunza. Maarifa hayo yanaweza kuwa ndani ya Biblia na hata katika vitabu vingine nje ya Biblia. Mfano umemwomba Mungu akupe mtaji uanze biashara na Mungu amekupa, sasa huo mtaji una namna zake za kuuendesha ili uweze kuzaa kwa faida. Kuna namna fulani ambayo ukiwekeza utapata faida nzuri. Sasa maarifa hayo ya kuwekeza yapo mengine kwenye Biblia lakini mengine ni kupitia watu wenye uzoefu katika hilo eneo, vyombo vya habari, kuna semina za kiserikali kuhusu biashara nenda huko ufuatilie ili ujue zaidi, maana apendaye mafundisho hupenda maarifa. Huenda ulikuwa hujaoa au kuolewa na sasa uko kwenye ndoa. Hudhuria semina za ndoa na kusoma vitabu husika ili upate maarifa yatakauokusaidia kuishi katika ndoa vizuri.
Umezaa watoto wengi wanakufa kwa malaria halafu watu wanasema ni shetani tu wakati mwingine si shetani ila ni wewe ulimweka mwanao katika mazingira ya kuumwa na mbu vizuri ndio maana akafa. Soma habari za matumizi ya ngao, chandarua yanayotolewa na serikali hujui kwamba serikali yoyote ile imewekwa na Mungu. Kwa kifupi muujiza wowote amabo Mungu amekutendea una maarifa yake ya kuutunza na chanzo kikubwa cha maarifa ni neno la Mungu. Hivyo lisome likae kwa wingi ndani yako.
Njia ya Tatu; Miliki majibu yako kupitia shukrani, sadaka au utoaji wa aina yoyote ile.
2Wafalme 5:17”Naamani akasema kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili, kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA.
Hizi ni habari za Namani Jemedari wa jeshi la shamu alikuwa na Ukoma. Alipokwenda Istraeli kwa nabii Elisha ili aombewe kuhusu tatizo la ugonjwa wake Elisha alimpa maagizo ya kutekeleza kuwa akajichovye / akajizamishe ndani ya mto Yordani mara saba na ndipo atapona. Baada ya Namani kutii maagizo Biblia inasema alipona na ngozi yake ikatakasika ikawa kama ya mtoto mchanga.Baada ya jibu hilo kwanza Namani alimshukuru Mungu wa Elisha na kisha akasema tangu siku ile hatatoa tena sadaka kwa miungu yao kule shamu isipokuwa kwa Mungu wa Elisha pekee.
Unapomshukuru Mungu kwa lile alilokutendea ni ishara ya kupokea kwa kuonyesha kujua nani aliyekutendea hilo jambo na hivyo kumrudishia yeye utukufu. Pia unaweza kumiliki majibu ya maombi yako kwa njia ya kutoa sadaka kwa yatima, wajane na pia unaweza kumshukuru Mungu kwa kushuhudia kwa wengine nini Mungu kakutendea au kutoa sadaka ya shukrani au utoaji kwa makundi mengine yasiyojiweza katika jamii.
Njia ya nne: Kumiliki muujiza kwa kuwatunza watumishi wa Mungu na kuchangia huduma mbalimbali.
Yoshua 12:1-3 kwenye ule mstari wa pili Biblia inasema “Basi wakamwandalia karamu huko naye Martha akamtumikia na Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja nao.
Hii pia ni habari nyingine inamhusu Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua baada ya kuwa amekufa kwa siku nne. Sasa Lazaro aliumiliki muujiza wake wa kufufuliwa kwa kumtunza Yesu pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. Hii ina maana Lazaro pamoja na dada zake waliingia gharama kwa ajili ya kuwatunza Yesu pamoja na wanafunzi wake, Kwa siku zote ambazo Yesu alikaa kwa Lazaro, Lazaro alihakikisha hawalali njaa, anawapa mahali pa kulala nk.
Sasa unaweza kumiliki muujiza wako kwa kuruhusu watumishi wa Mungu wakae nyumbani kwako. Huenda wamekuja kwenye mkutano au semina kwa wiki moja au mbili itoe nyumba yako itumike, kufanya hivyo ni kumfanya Mungu aendelee kukulinda wewe na yale aliyokupa maana anajua hutamnyima siku moja atakapohitaji kuvitumia. Wapo wengine wanaomiliki kwa kutoa magari yatumike kipindi chote cha mikutano, unaweza pia kumiliki kwa kuchangia gharama za mikutano si lazima pesa lakini hata kufanya kazi mbalimbali katika mkutano huo, huenda ni usafi, kubeba vyombo, kufanya usafi walikofika watumishi, kuombea huo mkutano au semina nk. Nakuambia unaweza ukaona kama ni vitu vidogo lakini ndivyo mujibu ya maombi yanavyomilikiwa bila kujali Mungu amekutendea nini.
Nija ya tano: Kumiliki muujiza kwa kufanya maamuzi ya kuokoka endapo Mungu alikufanyia huo muujiza kabla hujaokoka, na kuwaambia wengine habari ya Yesu aliyekuponya.
Ukisoma ile sura nzima ya 9 ya kitabu cha Yohana utakutana na habari ya kipofu mmoja tangu kuzaliwa kwake ambaye Yesu alikuwa amemponya. Ule mstari wa 39 unasema “akasema,Naamini, Bwana akamsujudia” Ukisoma vizuri habari hii utagundua baada ya mahojiano marefu kati ya mafarisayo na yule kijana kuhusu uponyaji wake ndipo Yesu akamwuuliza je unamwamini mwana wa Mungu? Yule kijana akamwuliza ni nani huyo nipate kumwamini? Kwa kifupi Yesu akamjibu unayezungumza naye. Ndipo yule kijana akasema, naamini Bwana akamsujudia.
Mtu mwingine ni Naamani ambaye tumekwisha ona habari zake, kitendo cha yeye kusema toka leo sitatoa sadaka kwa miungu ya shamu ila kwa Bwana ni dalili ya kuonyesha kumwamini Mungu wa Israel. Hivyo hata leo wapo ambao Mungu anawatendea mambo mengi hata kabla hawajaokoka sasa ili kumiliki hayo ambayo Mungu amekufanyia mwamini Yesu ndio huo muujiza utadumu. Wapo watu leo wanafunguliwa kwenye nguvu za mapepo huo ni uponyaji. Sasa badala ya kuwasaidia watu wamwamini Yesu tunawaacha, nakuambia pepo watarudi kwa huyo mtu wenye nguvu zaidi kuliko yule wa kwanza.
Pia ukisoma vizuri habari hiyo hiyo utagundua kwamba huyu jamaa alimiliki uponyaji wake kwa kuwaambia wengine habari za Yesu na kukiri kwamba mponyaji ni Yesu na si mtu mwingine, nakuambia kufanya hivyo ni kujihakikishia kudumu kwa huo muujiza na Mungu ataendelea kuutunza huo muujiza maana wewe ni chombo chake. Mungu akikuponya au kukubariki usinyamaze kimya waambie wengine habari za Yesu aliyekuponya. Jifunze kutoka kwa mwanamke msamaria. Uponyaji wa nafsi yake ulipelekea watu wengi wa mji wa Samaria kuokoka. Soma kile kitabu cha Yohana sura ya nne mistari 30 ya kwanza utaiona habari hii.
Mpenzi msomaji wangu mpaka hapa naamini utakuwa umepata kitu cha kukusaidia labda nikuambie hivi siri kubwa ya mafanikio ni kuliweka neno la Mungu kwenye matendo, si unajua imani pasipo matendo imekwisha kufa katika nafsi ya huyo mtu mwenye imani hiyo. Nimeamua kuandika ujumbe huu baada ya kuona wana wa Mungu wengi imefika mahali wanakuta yale ambayo Mungu aliwapa kama majibu ya maombi yao yameshaharibiwa na shetani, wapo waliozaa watoto wao wakafa na walimuomba sana Mungu kuhusu hao watoto nk. Sasa ni imani yangu kwamba tangu sasa jambo lolote ambalo Mungu atakupa kama jibu la maombi yako utalimiliki.
Ndimi katika huduma
Patrick Samson Sanga
Tuendelee kuombeana.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW