Sunday, August 16, 2015

BIBLIA NA SAYANSI

Siku hizi tunaishi katika enzi za sayansi, teknolojia na maendeleo makubwa ya kompyuta. Ni wakati ambao sayansi inaenea kupita kiasi katika pande zote. Katika kipindi tulicho nacho mwanadamu anaweza kuchambua muundo na umbile la ‘molekuli’ na kufanya utafiti kuhusu asili yake. Kupitia njia ya teknolojia ya vinasaba mwanadamu anaweza kuchagua aina ya mnyama au mmea anaotaka kuukuza. Maendeleo haya ya kisayansi yanatufanya tujiulize ikiwa uvumbuzi huu unapingana na ukweli wa Biblia au ikiwa sayansi inakanusha Biblia. Ukweli ni kuwa tunaweza kuiamini sayansi, kuitegemea na kuitumia kuthibitisha kweli zinazopatikana katika Biblia. Mara nyingi watu wasio na elimu ya kutosha na wanaoegemea upande mmoja ndio wanaofikiria kuwa Biblia na sayansi ni vitu viwili vinavyopingana. Misimamo inayofuatwa na baadhi ya watu ya kuwa na imani inayokataa kufikiri na kufikiri kunakokataa imani, ni misimamo hatari isiyotupeleka kwenye ukweli.
Ili tupate jibu kuhusu swali letu lililohoji ikiwa maelezo yaliyoko ndani ya Biblia ni ya kuaminika yakilinganishwa na maelezo ya sayansi, inatubidi kulinganisha maelezo ya pande mbili. Kwa kuwa hatuna muda wa kutosha kujibu swali hili kwa undani, nitazungumzia mifano michache tu inayohusu tafiti na chunguzi za kisayansi zinazohusu elimu ya mambo ya kale, elimu ya sayansi ya mazingira, historia, jiografia, fizikia ya uchunguzi wa miamba, sayansi ya kompyuta na sayansi ya utabibu. Hata maelezo yanayotokana na sayansi ya fizikia na elimu ya uchunguzi wa miamba kuhusu mwenendo na umbile la dunia yanapatana kabisa na maelezo ya Biblia. Mifano ya maelezo haya ni pamoja na yale yanayohusu gharika, utumwa katika nchi ya Misri, kushambuliwa kwa mji wa Yerusalemu, ustaarabu wa miji ya kale kama vile Babeli, Tiro, Sodoma na Gomora. Habari zilizoandikwa katika Biblia kuhusu mifano hii zinaweza kuhakikishwa kwa ushahidi ulioandikwa.
Kwa kuwa matokeo ya tafiti za kisayansi yanathibitisha habari zinazopatikana katika Biblia, inaonyesha wazi kuwa sayansi, inathibitisha kuwa habari zinazopatikana katika Biblia ni za kweli. Ukweli huu unatupa kuamini habari zote tunazokutana nazo katika Biblia. Tunapotafakari upekee wa Biblia, tunaweza kuelewa sababu zinazowafanya watu mashuhuri kuiheshimu na kuipenda, kuliko vitabu vingine vilivyoko chini ya jua. Yafuatayo ni maelezo mafupi ya mtu aliyeipenda Biblia licha umashuhuri aliokuwa nao katika ulimwengu wa sayansi.
“Siku moja mwaka 1890, wanaume wawili walikuwa wakisafiri kwa treni kutoka mji wa Lyon kwenda Paris. Mmoja alikuwa mzee mwenye ndevu nyingi na mvi anayekadriwa kuwa na umri wa miaka 65. Msafiri wa pili alikuwa kijana aliyejulikana kwa jina la Gaston Leroux, mwenye umri wa miaka 25 hivi. Kijana huyu alikuwa anakwenda kuhudhuria semina katika asasi ya Profesa mashuhuri nchini Ufaransa ndugu Louis Pasteur. Katika kusafiri kwao walijikuta katika mazungumzo yaliyokuwa na shabaha ya kufahamiana. Baada ya yule kijana kueleza dhumuni la safari yake, yule mzee alimjibu na kusema. “Ndugu nimefurahi kusikia kuwa unataka kuendeleza kiwango chako cha elimu, sayansi unayotaka kujifunza ni muhimu kutokana na ukweli kuwa itakusaidia kuthibitishia ukuu wa kipekee unaohusu uumbaji. Bila shaka wewe ni mwamini.”
Yule kijana alimwangalia yule mzee kwa macho ya dharau na kusema, “kuamini maana yake ni nini? Ninachojua ni kuwa sayansi inaweza kujitegemea bila huyo Mungu mwenye upendo unayemzungumzia.” Yule mzee kwa heshima na unyenyekevu huku akiwa ameshikwa na butwaa, alimjibu kwa kusema: “Ndugu yangu huo ni mtizamo wako na baadhi ya wasomi wana mtizamo unaofanana huo ila ukweli ni kuwa, sayansi ya kweli ….” Kufikia hapo yule kijana aliingilia kati huku akiwa amekasirika na kusema, “ninafikiri tofauti kabisa na vile unavyofikiri; sayansi unayoizungumzia ni ya zamani na haifanyi kazi katika siku tulizo nazo. Sayansi ya leo ni ya tofauti kabisa na imepiga hatua kiasi cha kutomhitaji Mungu wala usaidizi wowote kutoka kwake.”

Baada ya kuelewa msimamo wa huyu kijana, mzee yule alitambua kuwa kuendelea kuzungumza na yule kijana hakutaweza kuzaa matunda yoyote yaliyo mazuri. Akiwa katika hali ya kuhuzunika, alitoa Biblia ndani ya begi lake, akaomba na kuanza kuisoma. Kabla ya kuachana baada ya kufika mwisho wa safari yao, yule mzee alimpatia yule kijana kikadi chenye jina na anuani yake na kusema, “utakapofika kwenye semina usiache kunitafuta licha ya kutofautiana kwetu kimtizamo, huenda nikakusaidia kwa namna moja au nyingine.” Yule kijana alipoiangalia ile kadi alikutana na majina yafuatayo, Profesa Louis Pasteur!
Katika kuwakumbuka watu mashuhuri waliounufaisha ulimwengu kwa kazi zao, wako wanasayansi na watu wengi waliopita na waliopo walio na msimamo kama wa Profesa Louis Pasteur wa kulipenda Neno la Mungu. Ningekuwa na muda wa kutosha ningetaja majina mengi ya wale wote ambao kwa ujuzi na hekima yao, walisaidia kuelezea kazi kuu za Mungu za ufufuo kuhusu uumbaji kama unavyoelezewa katika Biblia. Kwa unyenyekevu mkubwa watu hawa waliipenda Biblia na kuisoma kila wakati katika maisha yao. Wakati wote watu hawa walimpenda na kumheshimu Mungu kama Muumbaji. Miongoni mwa wanasayansi hawa ni baba wa fizikia ya atomu Albert Einstein, mtaalamu wa elimu ya sayansi maisha ya viumbe hai (physiology) Iwan P. Pawlow, mwanzilishi wa nadharia ya kwanta Max Planck na mtaalamu katika kazi ya uchunguzi wa miali ulimwengu ndugu Robert Millikan.
Watu hawa walimwamini Muumbaji wao wakitambua kuwa, “Sayansi ni juhudi zinazolenga kuuelewa uumbaji. Kila mara sayansi ya kweli hutafuta jibu la swali kuhusu jinsi mifumo ya sayari ilivyotokea wakati ambao imani yenyewe ni kipawa cha Mungu kinachotuwezesha kumfahamu Mungu na sifa yake. Ni muumbaji peke yake ndiye anayeweza kutoa jibu kuhusiana na sayari na mifumo yake”. Wataalamu wa maendeleo wana uhakika kwamba imani na sayansi ni pande mbili zisizotenganishika na zinazohitajika katika maisha ya wanadamu.
Mwisho naomba nimalize maelezo yangu na maneno yaliyozungumzwa na mwanasayansi bingwa wa zamani aliyejulikana kwa jina la Peter Bamm. Mtu huyu alisema kuwa, “Biblia inafundisha kwamba mwanadamu huishi wakati unaoanzia na uumbaji na kumalizikia na hukumu ya mwisho. Kuamini ukweli huu ni faraja kubwa kwa wanadamu na kuzaa matumaini yasiyo na mwisho. Lakini siku hizi wako baadhi ya wanasayansi wanaofikiri kwamba wanadamu wanaishi katika kipindi kilichoanza na nyani na kikomo chao kitasababishwa na vita vya silaha za atomu. Kutokana uzushi huu watu wengi hujikuta katika mashaka makubwa na kukata tamaa. Maneno haya tunaweza kuyaunganisha na maneno ya mtunga mashairi wa Kijerumani Johann Wolfgang von Goethe, aliyesema kuwa uwezo na uchangamfu katika jamii au taifa vinategemea nafasi ya Biblia katika jamii au taifa husika. Hadi kufikia hapa nadhani nimetoa maelezo yanayotosha kujibu swali lililouliza ikiwa maelezo yanayopatikana ndani ya Biblia yanaweza kuaminika au la. Hata hivyo, ziko hoja nyingine nyingi katika Biblia zinazoweza kuondoa mashaka kuhusu yale yaliyoandikwa ndani yake.

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW