PARADISO/PEPONI NI KWELI NA HAKIKA NI KWA WATAKATIFU TU.
BWANA YESU asifiwe wapendwa, umekuwa ukisikia saana juu ya maneno haya Paradiso au Peponi huenda unaelewa au hauelewi maana yake lkn leo nikuribishe tujifunze juu ya Paradiso au Peponi.
Neno "Peponi" linatokana na neno la kiyunani "Paradeisos"
Neno hilo kwa kiingeleza ni "Paradise" linalotafsiriwa pia kwa kiswahili "Paradiso"
Peponi ndio paradiso.
Neno hilo Paradiso katika asili yake lina maana ya bustani nzuri kubwa iliyojaa matunda mazuri,
Bwana YESU KRISTO katika kuizungumzia Bustani hiyo anasema
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya MUNGU. Ufunuo 2:7"
Na pia neno Paradiso lina maana mahali palipojaa furaha na raha kuu isiyo na kifani.
Biblia inasema juu raha ya paradiso kwamba "Basi, ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Waebrania 4:1"
Mambo ya kujua kuhusu Peponi / Paradiso
•Peponi ndio paradiso, ni mahali ambapo waliokufa tu katika Wokovu wa KRISTO huenda baada ya kufa, Hawa ni waliokufa wakiishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU tu.
•Paradiso ni makao ya muda kwa ajili ya watakatifu, kusubiria mwisho wa mambo yote ambapo Yerusalemu mpya itafunguliwa na kuwa makao ya milele pamoja na Bwana YESU KRISTO yataanza kwa wote waliovumilia hata/mpaka mwisho.
Ufunuo 21:2-7
"Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa MUNGU, umewekwa tayari, kama bibi arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya MUNGU ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye MUNGU mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli. Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure. Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa MUNGU wake, naye atakuwa mwanangu."
Swali :-
Sasa kama Peponi ni mahali walipo watakatifu waliokufa katika KRISTO, Je unajuaje hivyo?
Biblia inajibu katika maandiko
√Luka 23:42-43 "Kisha akasema, Ee YESU, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako, YESU akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi."
YESU akamwambia kwamba siku hiyo hiyo angeingia Peponi baada ya Bwana YESU kumhesabia haki.
Ukiangalia Biblia ya kiingeleza Neno Peponi limetajwa Paradise, ndio maana nikakueleza Mwanzo kwamba Peponi ndio Paradiso
Wanaoingia Peponi ni walio wateule wa YESU KRISTO yaani watu waliompokea kama Bwana na Mwokozi wao na wameishi maisha matakatifu duniani,
Biblia iko wazi sana kwamba baada ya mtu kufa kinachofuata kwake muda huo ni hukumu na moja ya hukumu ni kwenda ama Peponi kama alimcha MUNGU katika KRISTO au mtu huyo kwenda kuzimu kama mtu huyo alikataa kuokolewa na YESU KRISTO.
Ndivyo inavyothibitisha Waebrania 9:27 kwamba "Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;"
Leo katika kila msiba unaotokea utasikia watu wakisema "uende au aende pema Peponi"
Hata watu wa dini wanaomkataa YESU mtu akifa kwao utasikia maneno maarufu zaidi ni kwamba marehemu alale pema Peponi.
Hata kama angefariki mlevi, mchawi, mwizi, mzinzi au mwasherati utasikia watu wakiomba kwamba mhusika aende peponi.
Kusema hivyo ni sawa lakini katika mtindo wa kujifariji tu, ila ukweli ni kwamba hata kabla haujajua kama Fulani amefariki basi anakuwa ameshafika ama peponi au kuzimu.
Ndio maana Biblia iko wazi sana kwamba kama mtu anaitaka hiyo pepo ya mbinguni iliyoandaliwa na MUNGU aliyeumba mbingu na nchi basi dawa ni kumpokea YESU kama Mwokozi kisha kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.
Yohana 3:16-18 "Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."
Ndugu kama kweli unataka siku ukifa watu wasema kweli umeenda Peponi basi unamhitaji sana YESU KRISTO ili awe Mwokozi wako.
Ndugu kama unahitaji kwenda peponi basi inakupasa kuishi maisha matakatifu.
Mtume Paulo siku moja alipelekwa kimaono huko peponi.
2Wakorintho 12:4
"ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene."
Wewe ukiokolewa na YESU KRISTO utaenda Peponi ambako pia ndio Paradiso.
Unachotakiwa ni hiki
"Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. Isaya 55:6-7"
Hivyo Paradiso ni ya muhimu sana kwa kila mtu.
Anayeweza kuiandaa hiyo peponi au Paradiso ni mtu mhusika mwenyewe wakati akiwa hai yaani duniani.
Inawezekana kabisa kuna watu husema Fulani yuko peponi na kumbe Yuko kuzimu kwa sababu mtu hiyo alikataa kuokolewa na YESU KRISTO.
Wako pia waliookoka mwanzo kisha baadae wakamwacha YESU, hao nao hawako peponi Bali wako kuzimu wakiingoja jehanamu.
Ndugu zangu haina mjadala wala maoni ila kama unaitaka pepo ya mbinguni basi mpokee YESU kama Mwokozi wako kisha anza kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Paradiso ni sehemu ya raha, Biblia inakutaka kufanya bidii katika kuishi maisha matakatifu ndipo utafika hapo rahani.
Waebrania 4:11
"Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi."
YESU KRISTO anaokoa Leo hivyo ukimpokea YESU utaokoka na ukifa katika utakatifu utaenda Peponi.
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. Ufunuo 2:11''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu,
Asante kwa kutoa muda wako kukifunza Neno hili la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi ndugu yangu unatambua hilo.
Shalom
No comments:
Post a Comment