Sunday, April 22, 2018

Utatu Mtakatifu kwa mujibu wa Biblia na Quran





Sehemu ya Kwanza:
UTATU MTAKATIFU KWA MUJIBU WA BIBLIA
Awali ya yote ningependa ifahamike kwamba, Mwenyezi Mungu ametukuka sana, Sisi kama viumbe wake ni vigumu kumwelewa kwa jinsi tupendavyo. Mwenyezi Mungu ni Muweza wa vyote, hatuwezi kumwekea mipaka kwamba yuaweza jambo hili na hili hawezi. Hatuwezi kumchunguza Mwenyezi Mungu hadi aingie hakilini mwetu, hatuwezi kujua ukomo na mipaka yake. Siku mwanadamu atakapoweza kumwelewa vilivyo Mwenyezi Mungu basi atakoma kuwa Mungu.
Kile tunachoweza kuelewa ni jinisi Yeye alivyojidhihirisha kwetu kupitia maandiko yake Matakatifu tu. Itakuwa ni jambo la ajabu kuanza kupinga jinsi ambavyo Mungu ametaka tumfahamu alivyo kupitia Neno lake. Hivyo ni kusudi langu kuyaleta Maandiko namna ambavyo Mungu amependa tumfahamu alivyo.
Biblia ninafundisha kuwa Mungu ni Mmoja lakini katika Nafsi Tatu (Personalities) za Mililele.
Katika Kitabu cha Mwanzo 1:1-3 tunasoma.
“Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na Nchi, nayo nchi ilikuwa ukiwa tena Utupu, na giza lilikuwa juu ya Uso wa Maji, Roho ya Mungu ikatulia juu ya Uso wa maji.”
Twaweza kusema kuwa Kuna 1. Mungu na 2. Roho yake. Kisha maandiko yanaendelea kusema
“Mungu akasema, Iwe nuru, Ikawa nuru” Aya ya 3
Kwa hiyo twaona kuwa kwa mujibu wa maandiko haya kuna Mungu, Roho yake, na Neno lake.
Hizi ni Nafsi hai zinazojitegemea kabisaa kila moja ikifanya kazi kwa namna Mungu apendavyo.
Kunaushahidi Mwingi katika Maandiko Kuonyeshakuwa Nafsi hizi za Mwenyezi Mungu zimekuwa katika Utendaji wa kazi katika Historia ya Mwanadamu.
Kwa mfano tunaposoma Mwanzo 6:3
“Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na Mwanadamu milele…”. Kumbe Roho ya Mungu inaweza kushindana. “
Isaya 44:3
“…Nitamimina Roho yangu juu ya Wazao wako….”
Roho wa Mungu kama nafsi hai anaweza Kukasirishwa, au kukosewa na mwanadamu
Mathayo 12 :31
“Kwa sababu hiyo nawaambia kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.
Waefeso 4:30
“Wala msimhudhunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwa Yeye mlitiwa mhuri hata siku ya ukombozi”
Roho Mtakatifu ndiye haliyehubiri injili katika Agano la Kale kupitia Manabii.
Manabi walinena Neno la Mungu wakiongozwa na Roho mtakatifu.
1 Petro 1:11
“wakafunuliwa yakuwa si kwa ajili yao wenyewe, baali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi injili kwa Roho Mtakatifu…”
2 Petro 1:21
“Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu”
Tunaposoma katika Warumi 8:26 tunaona kuwa
“…Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa”
Sifa hizi zote za Roho zinatuambia kuwa Roho Mtakatifu wa Mungu ni Nafsi hai ya kuitendaji wa Mungu mwenyewe. Kwa maana nyingine Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe.
Yesu Mwenyewe alisema
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo, yawapasa kumwabudu katika Roho na Kweli” Yohana 4:24
Je Neno la Mungu ni nani ndani ya Biblia?
Maandiko matakatifu (Biblia inatuambia kwamba) Mungu aliumba mbingu na nchi kwa neno lake. Ukisoma mwanzo 1:4-31, utagundua kuwa, Mungu alitamka neno la uumbaji ukafanyika. Zaburi 33:6 inasema.
“Kwa neno la Bwana Mbingu zilifanyika, na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake”
Tunapuchonguza vizuri maandiko tunagungua kuwa Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu. (Soma Waebrania 4:12), linao uwezo wa kuhuisha. Kwa maana hii tunaweza kuhitimisha kwamba, Kama vile ambavyo Roho wa Mungu ni Nafsi hai, Neno la Mungu pia ni Nafsi hai.
Kama tulivyoona Kazi ya uumbaji imefanywa na Neno la Mungu , nafsi ya pili ya Uungu. Pote katika biblia kunaushahidi wa ushirika huu wa Mungu, Neno lake na Roho wake katika uumbaji. Neno mwenyewe anasema katika Methali 8:22-30 kuhusu kushiriki kwake kaatika Kazi ya Uumbaji
“Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele tangu awali kabla haijakuwako dunia…ndipo nilipokuwa pamoja naye kama stadi wa kazi…”
Biblia iko wazi kabisa kwamba Huyu Neno aliyeumba Mbingu na dunia, ni Mungu pia. Hii ni kwa sababu, uwezi kumtenganisha Mungu na neno lake ukasema Mungu ni Mungu na Neno lake ni siyo Mungu bali ni kitu tofauti. Mungu na Neno lake ni UMOJA. Tunasoma katika Yohana 1:1-3 kwamba,
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu…vyote vilifanyika kwa huyu (Neno), wala pasipo Yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika”
Pote katia Biblia twaona Neno akifanya kazi na anapewa sifa ya kuwa nafsi iliyo hai ya Mungu.
Sasa unafika wakati wa kutimiza kazi Nyingine kubwa ya Kumkomboa mwanadamu aliyeanguka dhambini. Kama ilivyo kawaida katika utendaji kazi wa mungu, siku zote mtendaji mkuu ni “Neno lake” . Hivyo Mungu akalituma Neno lake lije kukamilisha kazi ya ukombozi.
Neno alifanyika mwili ili kukamilisha ukombozi wa mwanadamu.
Kanuni ya Mungu kuhusu ukombozi ni Kwamba.
“Pasipo kumwaga damu, hakuna ondoleo la dhambi..” Waebrania 9:22
Hivyo twaona kwamba
“… kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili yeye naye vivyo aishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi” Waebrania 2:14
kwa hiyo ili kumkomboa mwanadamu;
“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na Kweli” Yohana 1:14
Kitendo hiki cha Neno kukubari kufanyika mwili ndiyo kikawa sababu ya Yeye kuitwa “mwana wa Mungu” Kama tulivyoona katika andiko hilo hapo juu, wala siyo kwa jinsi ya kimwili kama wanadamu wanavyozaa. Mungu Mwenyewe alitangaza Baada ya Neno kufanyika mwili kwamba,
“Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa, na tena Mimi nitakuwa kwake baba. Na yeye atakuwa kwangu mwana”Waebarania 1:5
“Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema. Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Mathayo 3:17
Kwa kufanyika Neno kuwa mwili ndiyo hapa tunapata sifa ya Mungu Baba, Mungu Mwana, Mungu Roho Mtakatifu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kitendo hicho cha Neno kufanyika Mwili hakimwondolei sifa ya Uungu. Tunachoweza kuona hapa ni kwamba Neno la Mungu limevaa Mwili na hivyo kukatokea muunganiko wa Neno (Mungu) na Mwili (Mwanadamu). Katika Yesu Kunautimilifu wa Mungu kamili na Kuna ubinadamu Katika Mwili wa wa Mwanadamu. Neno (Yesu) Mwenyewe anasema;
“…Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliniwekea tayari, sadaka za kuteketezwa na na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo…Tazama nimekuja, katika gombo la chuo nimeandikiwa, niyafanye mapenzi yako. Mungu” Waebrania 10:5-7
Twaona kwamba Neno aliandaliwa Mwili, akavaa ubinadamu na ndipo tukamwona na Sifa zote za kibinadamu. Lakini kwa asili yake yeye,
“…mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu, kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa na mfano wa mwanadamu.” Wafiipi 2:6-7
Katika Muunganiko huu, alizaliwa na mwanamke, na Malaika alimwambia Mariamu ambaye angemzaa mwana kwamba.
“Tazama utachukua mima na kuzaa mtoto mwanamme; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa mwana wa Aliye juu (yaani Mungu). … Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli, kwa sababu hiyo, hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”. Luka 1:31-32, 35
Baadaye Malaika Gabriel alimwendea Yufu mchumba wake Mariam na kusema maneno hayo hayo aliyoyasema kwa Mariam.
“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana Yeye ndiye atakaye waokoa watu wake na dhambi zao” Mathayo 1:21
Jambo linalowatatiza wengi ni Pale Neno alipofanyika Mwili na Kuonekana na Umbo la Mwanadamu. Katika umbo hilo Yesu alikuwa na mahiyaji yote ya kibinadamu, aliona njaa na kiuu, alipata usingizi, alitahiriwa kama mwanadamu katika Siku ya nane, alilia machozi, alichoka nk. Kama mwanadamu wa kawaida.
Tunapaswa kufahamukwamba, Yesu alikuja ili kutuonyesha njia ya namna ambavyo tunapoishi kwa kumtegemea Mungu sisi kama wanadamu, tutapata ushindi dhidi ya dhambi kama yeye alivyoishi maisha ya ushindi. Maandiko yanamshuhudia kwama alijaaribiwa kama sisi tunavyojaribiwa bila ya kufanya dhambi. Hakuwa na ila yoyote katika maisha yote. Maandiko matakatifu yanasema,
“… bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote bila kufanya dhambi” Waebrania 4:15
“Yeye hakutenda dhambi wala hila haikuonekana kinywani mwake”           1Petro 2:22
Katika hali ya ubinadamu alimtegemea Mungu kwa kila jambo. Hapaa ndipo utaona kwamba aliomba kwa Mungu Baba, ndipo utaona pia alitamka maneno kama vile ,
“… usinishike, kwamaana sijapaa kwena kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu”Yohana 21:
Katika hali ya Uungu uliokuwa ndani yake (Neno la Mungu) ndiyo maana alisema maneno kama
“Mimi na Baba tu Umoja” Yohana 10:30.
“Aliyeniona mimi, amemwona Baba” Yohana 14:9
Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba. Na Baba yu ndani yangu, la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe” Yohana 14:11
Ni kwa vipi Baba alikuwa ndani ya Yesu? Ni kwa njia ya neno lililovaa mwili wa kibinadamu, Neno la Mungu lilikuwa ndani ya mwili na mwili ulikuwemo ndani ya Neno la Mungu. Na huyo ndiye Yesu.
Katika hali hii haishangazi kumwita Yesu kuwa ni Mungu, na kwa kweli siyo Mungu tu bali ni;
“Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu” Tito 2:13
Hivyo dhana hii ya Utatu mtakatifu (Mungu mmoja katika nafsi tatu) ni dhahiri sana ndaniya maandiko matakatifu wala haihitaji kubishana sana, isipokuwa kukaidi maandiko. Kama nilivyosema hapo awali. Sisi wanadamu hatupaswi kumpangia Mungi jinsi ambavyo anapaswa kuwa, na jinsi gani hapaswi kuwa. Tunaloweza kufanya ni kupokea kwa imani jinsi alivyojidhihirisha kwetu na yale aliyotuonyesha. Maandiko yanasema.
“Mambo ya siri ni ya BWANA Mungu wetu, lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, …”Kumbukumbu 29:29
Mpaka kufikia hapa tumeona katika Biblia kuwa Mungu ni Mmoja lakini amejifunua kwetu katika nafsi tatu za utundaji wake wa Kazi. Katika agano la kale Nafsi hizi ni Mungu, Neno na Roho, na katika agano jipya baada ya Neno kufanyika Mwili, nafsi hizo zinachukua cheo cha Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Sasa tuigeukie Quran Tukufu tuone je Miaka 600 Baadaye Mungu angebadiri mafunuo yake na kufundisha vinginevyo?
Sehemu ya Pili:
UTATU MTAKATIFU KWA MUJIBU WA QURAN TUKUFU
Kwakuwa katika kuchunguza Utatu Mtakatifu katika Biblia tulianzia tokea mwanzo wakati wa uumbaji. Inatubidi tuchukue njia hiyo hiyo kufuatilia mada hii.
Roho Mtakatifu kwa mujibu wa Quran Tukufu.
Kama vile Biblia, Quran Tukufu inawafiki kwamba Mungu aliumba mbingu na ardhi kwa muda wa siku sita
 وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۗ وَلَئِنْ قُلْتَ إِنَّكُمْ مَبْعُوثُونَ مِنْ بَعْدِ الْمَوْتِ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُبِينٌ
“Na yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa siku sita na Arshi yake ilikuwa juu ya maji…” Sura 11:7 (HUD)
Abdalla Farsy, Mfasiri wa Quran kwa Kiswahili, katika kusherehesha ayah ii anatueleza kwamba
“Na kusema kuwa mbingu na ardhi zimeumbwa kwa siku 6, anajua Mwenyewe Mwenyezi Mungu, siku 6 hizo ndiyo muda gani kwa hisabu yake Mwenyewe Mwenyezi Mungu. Na hiyo ARSHI ya mwenyezi Mungu hatujui wala MAJI hayo ambayo ARSHI ilikuwa juu yake”. Abdalla Farsy, Tafsiri ya Quran Tukufu, Sura ya 11:7
Yaonekana kuwa Wafasiri wa Quran wanashindwa kuelewa maneno haya juu ya uumbaji wa Mungu. Lakini hawapaswi kuhangaika, wanachotakiwa kufanya ni Kufuata Ushauri waliopewa ndani ya Quran Tukufu. Katika Sura ya 10:94 Tunasoma,
 فَإِنْ كُنْتَ فِي شَكٍّ مِمَّا أَنْزَلْنَا إِلَيْكَ فَاسْأَلِ الَّذِينَ يَقْرَءُونَ الْكِتَابَ مِنْ قَبْلِكَ ۚ لَقَدْ جَاءَكَ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ
“Na kama unayoshaka juu ya haya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao vitabu kabla yako (Wayahudi na Wakristo)”
Ili kujua juu ya siku hizo za uumbaji, na kwa namna gani Arshi(Enzi yake) ya Mungu ilikuwa juu ya maji wakati huo wa uumbaji, yapaswa kusoma Biblia kama tulivyoona hapo mwanzo. Kwamba, Siku ni ile inayo unda “ikawa asubuhi, ikawa jioni, siku ya…”. (soma mwanzo 1). Haipatikani asubuhi na jioni isipokuwa ni ndani ya masaa 24. Hivyo siku hizo 6 ni siku za masaa 24. Biblia pia inasema,
“Maana kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya sababa; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa. Kutoka 20:11
“Basi mbingu na nchi zikamalizika na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya, akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya.” Mwanzo 2:1-2
Quran inawafiki Biblia pia kwamba Mungu alikuwa juu ya Maji wakati wa uumbaji. Kwa mujibu wa Biblia, ni Roho ya Mungu ndiyo iliyokuwa juu ya Uso wa vilindi vya maji. (Mwanzo 1:2)
Aya nyingi ndani ya Quran zinaonyesha kuwa Roho ya Mungu hutumwa kutoka kwa Mungu ili kuwatia nguvu watumishi (Mitume) wa Mungu, kwa mfano.
 يُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ بِالرُّوحِ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ أَنْ أَنْذِرُوا أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا أَنَا فَاتَّقُونِ
“Huwateremsha Malaika na Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake…” Sura 16 :2 (An Nahl )
 رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ يُلْقِي الرُّوحَ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَنْ يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ لِيُنْذِرَ يَوْمَ التَّلَاقِ
“Yeye ndiye Mwenye vyeo vya juu, Mwenye Arshi. Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuwaonya kwa Siku ya Mkutano” Sura 40:15 (Al Mu’min)
Wafasiri wengi wa Quran Kama Bible Abdalla Farsy wanatafsiri neno hili “roho” lililotumika katika maandiko haya ya Quran, kuwa nlinamana ya Wahyi au Ujumbe, au Utume ambao Mungu huwapatia mitume wake. Aya hii ya sura ya 40:15 kwa Tafsir ya Abdalla Farsy inasomeka kuwa;
“Yeye ndiye mwenye vyeo vya juu kabisa, Mwenye enzi. Hupereka Wahyi wa amri yake kwa amtakaye miongoni mwa watumwa Wake ili kuwaonya viumbe siku ya kukutana naye”
Hapa neno la Kiarabu “ruuh” (yaani roho) limefasiriwa kama “Wahyi” (yaani Ujumbe). Yawezekana ili kukwepa uelewa wa moja kwa moja kwamba Mungu humtuma Roho wake mtakatifu kwa mitume na manabii wake ili watoe ujumbe wa maonyo kwa watu. Hata hivyo bado tafsir hii inawafikiana na dhana tuliyoiona katika Biblia kuwa, manabii walitoa ujumbe wao kwa njia ya uongozi wa Roho Mtakatifu.
“Maana ubnabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya wanadamu, bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu” 2 Petro 1:21
Yesu Mwenyewe baada ya kufanyika Mwili (katika hali ya Ubinadamu) Biblia na Quran zote zinashuhudia kuwa alitiwa nguvu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na kufanya miujiza Mingi.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَقَفَّيْنَا مِنْ بَعْدِهِ بِالرُّسُلِ ۖ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ ۗ أَفَكُلَّمَا جَاءَكُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنْفُسُكُمُ اسْتَكْبَرْتُمْ فَفَرِيقًا كَذَّبْتُمْ وَفَرِيقًا تَقْتُلُونَ
“…na tukampa Isa mwana wa Maryam, hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu…” Sura 2:87 (Al Baqara)
 إِذْ قَالَ اللَّهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ اذْكُرْ نِعْمَتِي عَلَيْكَ وَعَلَىٰ وَالِدَتِكَ إِذْ أَيَّدْتُكَ بِرُوحِ الْقُدُسِ تُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلًا ۖ وَإِذْ عَلَّمْتُكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَالتَّوْرَاةَ وَالْإِنْجِيلَ ۖ وَإِذْ تَخْلُقُ مِنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ بِإِذْنِي فَتَنْفُخُ فِيهَا فَتَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِي ۖ وَتُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ بِإِذْنِي ۖ وَإِذْ تُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِي ۖ وَإِذْ كَفَفْتُ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَنْكَ إِذْ جِئْتَهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ فَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ إِنْ هَٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُبِينٌ
“Na pale Mwenyezi Mungu atakaposema, Ewe Isa bin Maryamu, Kumba neema yangu, juu yako na juu ya mama yako, niipokutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika Utoto na utuuzimani. Na nilivyokufunza kuandika, na hikima na Taurati na Injili, na ulipotengeneza udongo sura ya ndege kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wakoma kwa idhini yagu, na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu…” 5:110 (Al-Maida)
Maneno haya yanapatikana pia ndani ya Biblia, kwamba Yesu alitiwa nguvu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Yesu alisema
“Roho wa Bwana Yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta, kuwahubiri masikini habari njema (Injili), Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kwacha huru waliosetwa…” Luka 4:18
Kukosekana kwa maelezo fasaha juu ya Roho Mtakatifu na utendaji wake wa kazi ndani ya Quran, haina maana kwamba, hakuna Nafsi ya Mungu aitwaye Roho Mtakatifu. Kukasekana huku kunaweza kuwa ni kwasababu mtume Muhammad (S.A.W) mwenyewe alifunuliwa kuwa,
 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُمْ مِنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا
“Na wanakuuliza Khabari za Roho, Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu” 17:85 (Al-Israa)
Kwa mujibu wa aya hii, Allah (S.W) anasema Muhammad alipewa kidogo tu katika mambo yahusuyo Roho Mtakatifu. Hata hivyo kido hayo alichopewa, tunapoyasoma kwatika mwanga wa Biblia Takatifu, tunaweza kuona mnyororo usiokatika wa fundisho la Roho mtakatifu.
Baada ya kuona uwepo wa Roho Mtakatifu atokaye Kwa Mungu ndani ya Quran Tukufu, Sasa tuangalie “Neno la Mungu”na Kazi yake ndani ya Quran.
Neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Quran Tukufu
Katika Biblia tuliona kuwa Neno la Mungu ndilo lililoumba mbingu na Ardhi, Je kuna utofauti katika Quran? Hapana, tunasoma katika Sura ya 2:117
 بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَإِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ
“Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na atakapojambo, basi huliambia tu KUWA! Nalo likawa” Sura 2:117 (Al-Baqara)
Maneno haya yanawafikiana kabisa na Maneno ndani ya Biblia takatifu kwamba,
“Kwa neno la Bwana Mbingu zilifanyika, na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake … maana Yeye alisema, IKAWA, na Yeye aliamuru, Ikasimama” Zaburi 33:6,9
Hivyo twaona kuwa Biblia na Quarn zinawakubaliana kuwa Mbingu na Ardhi ziliumbwa kwa Neno la Mungu. Katika Biblia tumeaona hapo mwanzo kuwa hili Neno lilifanyika Mwili na kukaa kati Yetu, Je katika Quran tunaweza kupata ushahidi kuwa Neno lilifanyika Mwili?
Neno lililofanyika mwili kwa mujibu wa Quran Tukufu.
Katika Quran Sura ya 3:45 tunasoma kwamba,
 إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ
“(Kumbukeni) waliposema Malaika Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria kwa Neno litokalo kwake. Jina lake (huyo Neno) ni Masihi Isa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na Miongoni mwa waliokaribishwa kwa Mwenyezi Mungu”
Katika Aya hii, tunaambiwa kwamba Nabii Isa (Yesu) ni Neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, tena ana heshima duniani na Mbinguni. Kama yeye mwenyewe alivyosema katika Mathayo 28:19 “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani…”
Pote katika Quran Nabii Isa (Yesu) anatajwa kuwa Yeye ni Neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu.
Je ni kwa nini basi Waislam wanaukataa uungu wa Yesu au utatu Mtakatifu, licha ya ushahidi mwingi uliomo ndani ya Quran?
Kusema ukweli hakuna maandiko ndani ya Quran yanayokataa moja kwa moja kuwa Yesu au Nabii isa siyo Mungu, au kupinga dhana ya Utatu Mtakatifu, yaani Mungu mmoja katika nafsi tatu (zingatia kuwa Quran inaposema kuwa Mungu ni Mmoja tu, haimaanishi kukataa Utatu mtakatifu, Ndivyo pia Biblia inafundisha kuwa Mungu ni Mmoja. Lakini umoja huu ni wa nafsi tatu kama tulivyoona katika somo hili)
Maelezo mengi ndani ya Tafsiri za Quran yanayokataa uungu wa Yesu yamekolezwa kwa maelezo au mafundisho ya Wafasiri wa Quran. Ni wazi kabisa kuwa maelezo haya ya wafasiri hupiga Quran Yenyewe.
Hapa nitatoa mfano wa Aya moja ndani ya Quran ambayo hutumika sana kupinga uungu wa Yesu au Utatu mtakatifu. Nitaleta tafsiri Nne (4) za Lugha ya Kiswahili juu ya aya hii ili kuona Wasomi wa Kiislam wanavyohangaika kuficha uungu wa Yesu. Aya yenyewe ni Sura ya 4:1171
 يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ وَلَا تَقُولُوا عَلَى اللَّهِ إِلَّا الْحَقَّ ۚ إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِنْهُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ ۖ وَلَا تَقُولُوا ثَلَاثَةٌ ۚ انْتَهُوا خَيْرًا لَكُمْ ۚ إِنَّمَا اللَّهُ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ ۖ سُبْحَانَهُ أَنْ يَكُونَ لَهُ وَلَدٌ ۘ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ وَكِيلًا
Tafsir ya Aliy Muhsin Barwaaniy (Suni)
“Enyi watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msiseme Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu , ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa Kheri kwenu. Hakika mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na Kuwa na Mwana. Ni vyake yeye vyote vilivyomo katika Mbingu na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha”
Quran Tukufu (Pamoja na Tafsir na maelezo kwa Kiswahili) (Ahmadiyya)
(Hapa imefanywa kuwa aya ya 172)
“Enyi watu wa Kitabu! Mruke mpipaka ya dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli. Masihi Isa mwana wa Maryamu, ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala msiseme watatu. Jizuieni, Itakuwa bora kwenu: bila shaka mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ni mbali na utakatifu Wake ya kwamba Awe na Mwana. Ni vyake vilivyomo katika Mbingu na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi”
Tafsir ya Ali bin Jumaa bin Mayunga (Shia)
“Enyi watu wa Kitabu! Msiruke mpiaka ya dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini mwenyezi Mungu na Mitume yake, wala msiseme: Utatu. Wacheni (Itikadi hiyo) ni bora kwenu. Hakika mwenyezi Mungu ni mmoja tu. Amemeepukana na Kuwa na mtoto. Ni vyake Ni vyake vilivyomo Mbinguni na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi”
Tafsir ya Abdallah Farsy (Suni)
“Enyi watu wa Kitabu! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli. Masihi Isa mwana wa Maryamu , ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na (nikiumbe aliyeumbwa kwa) tamko lake (tu Mwenyezi Mungu) alilompelekea Maryamu. Na ni roho iliyotoka kwake (Mwenyezi Mungu kama roho nyengine). Basi muaminini mwenyezi Mungu na Mitume yake, wala msiseme, “watatu”.. Jizuieni (na itikadi hiyo); itakuwa bora kwenu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ni mbali na utakatifu wake Kuwa ana mwana. Ni vyake (vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa kutosha”
Uchanmbuzi wa Aya hizi;
Nimeileta aya hii katika tafsir tofauti tofauti za Quran ili kuleta uelewa uliokusudiwa na aya hii. Unaporudia taratibu tafsir ya Shekh Balwaniy, utagundua kuwa aya hii inatujulisha sifa tatu za Nabii Isa (Yesu) yaani;
  1. Nabii Isa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (bimaana alitumwa na Mungu)
  1. Nabii Isa ni Neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu alilompelekea Maryamu
  1. Nabii Isa ni roho itokayo kwa Mwenyezi Mungu
  1. Sifa ya kutumwa na na Mungu Baba.
  1. Sifa ya kuwa Yesu ni Neno litokalo kwa Mungu Baba.
  1. Sifa ya kwamba Yesu ni Roho ya Mungu
Imeratibiwa na Philip Joseph wa Loud Cry Ministries
Hivyo twaona kuwa ni makosa makubwa sana kusema kuwa Yesu ni Mtume tu wa mwenyezi Mungu kama walivyo mitume wengine, bali Yeye ni Neno la Mungu na ni itokayo kwa Mungu.
Sifa hizi tatu juu ya Yesu hazipingwi na Biblia takatifu kama ifuatavyo
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kwa Yeye ulimwengu upate kuokolewa” Yohana 3:16-17
“Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi takauona utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.” Yohana 1:12
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo, yawapasa kumwabudu katika Roho na Kweli” Yohana 4:24
Haiwezekani kumtenganisha Mungu na Roho yake na Neno lake. Kama Mungu ni Roho, basi ni sahihi kusema kwamba, Neno naye ni Roho.
Tafsir zote 3 za Quran nilizozileta hapa, yaani, Tafsir ya Balwaniy, Ahmadiyya na ile ya Mayunga, zinakubariana katika ufafanuzi wa aya hii. Wafasiri hawa watatu wamefasiri neno kwa neno kutoka Kiarabu katika sura hii ya 4:171. Sasa tuichunguzi pia Tafsiri ya Shekhe Abdallah Farsy.
“Enyi watu wa Kitabu! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli. Masihi Isa mwana wa Maryamu , ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na (nikiumbe aliyeumbwa kwa) tamko lake (tu Mwenyezi Mungu) alilompelekea Maryamu. Na ni roho iliyotoka kwake (Mwenyezi Mungu kama roho nyengine). Basi muaminini mwenyezi Mungu na Mitume yake, wala msiseme, “watatu”.. Jizuieni (na itikadi hiyo); itakuwa bora kwenu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ni mbali na utakatifu wake Kuwa ana mwana. Ni vyake (vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa kutosha”
Kwa haraka haraka unapochunguza tafsir hii utagundua kwamba, Shekhe Abdallah Farsy anacheza mchezo wa maneno. Maneno yote aliyoweka kwenye mabano ( ) ni nyongeza yake yeye ili kumwongoza msomaji kuelewa anavyotaka yeye iwe. Utagundua kuwa Tafsir hii inafanywa kwa makusudi ili kulinda itikadi ya Waislam kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja, hakuza wala hakuzaliwa.
 قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ اللَّهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ
“Sema: Yeye Mwenyezi Mungu Mmoja tu. Mwenyezi Mungu tu ndiye anayestahiki kuabudiwa na viumbe Vyake. Hakuzaa wala Hakuzaliwa, wala Hana anayefanana Naye hata Mmoja” Sura 112:1-4 (Al-Ikhlas)
Sura hii ndiyo sura Muhimu sana ndani ya Quran kwa Waislam. Yaonekana kwamba, tangu utotoni wanatakiwa kukalili sura hii. Nguzo ya kwanza katika Uislam ni Shahada, Yaani kushuhudia kwamba “hakuna Mwenyezi Mungu mwingine apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na Muhammad ndiyo mtume wake”. Yaonekana kwamaba, mfumo mzima wa Uislam umejikita kupinga dhana hii ya Utatu mtakatifu.
Bahati mbaya ni kwamba Waislam wanafanya upinzani huu bila ya kuwa na uelewa wa dhati kuhusu dhana hii ya utatu mtakatifu. Wakati mwingine hata wametengeneza imani ambayo haipo hata kwa Wakristo wenyewe na kuipandikiza ndani ya waumini wao, ili kuwafanya Wakristo waonekane kuwa wasivyokuwa, yaani, kwamba Wakristo wanaamini miungu watatu.
Kama tulivyoona, katika Somo hili. Imani hii ni Kinyume kabisa na Ukristo, kamwe wakristo hawaamini juu ya miungu watatu, na wala fundisho hili siyo la Biblia, baali Wakristo humwamini Mungu mmoja aliye katika Nafsi Tatu hai, na hili ndiyo tunalolita UTATU MTAKATIFU.
Turudi katika Tafsir ya Abdallah Farsy. Tuangalie hayo maneno aliyoweka kwenye mabano ( ).
“Masihi Isa mwana wa Maryamu , ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na (nikiumbe aliyeumbwa kwa) tamko lake (tu Mwenyezi Mungu) alilompelekea Maryamu.”
Abdllah Farsy hapa anatengeneza Sentensi yake yeye mwnyewe kwa kuchanganya maneno ya Quran Tukufu ili ayaite kuwa ni Maneno ya Mwenyezi Mungu. Maneno yake haya yanamaana tofauti kabisaa na maneno ya Quran kwamba
Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryamu,”
Anaendelea kuweka maneno yake ili kupotoa tafsir kwa kusema
Na ni roho iliyotoka kwake (Mwenyezi Mungu kama roho nyengine).”
Abdallah Farsy anataka tuelewe hapa kuwa, kuna roho nyingine nyinge zimetoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo siyo ajabu kwa Nabii Isa. Kwa maana nyingine Shekhe huyu anataka kutufundisha kwamba, Mungu anayo “store” au ghara la roho za binadamu ambazo huzitoa na kuwapandikiza wanadamu. Maneno haya aliyoweka katika mabano hayamo katika lugha ya kiarabu katika aya hiyo, ndiyo maana utakuta Mashekhe waliofasiri neno kwa neno hawakuweka maneno hayo.
Kama ilivyo katika Biblia, neno lenyewe Utatu Mtakatifu halipatikani katika Quran nzima, lakini kwa kuchunguza vizuri ndani ya Bilbia na Quran, tunaweza kuona kuwa dhana hii ya Utatu Mtakatifu ni fundisho la vitabu vitakatifu. Kwamba vitabu vyote vinakubaliana kwamba Yupo Mungu mmoja wa pekee, asiye na mshirika katika matendo yake yote, naye yu katika Nafsi tatu zilizo hai za utendaji wake wa kazi, yaani Mungu, Neno la Mungu na Roho Mtakatifu wa Mungu. Na ilipofika wakati wa kumkomboa mwanadamu Neno akafanyika Mwili, na hivyo tukapata sifa zinaongezeka kwa Nafsi hizi tatu za Mungu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu.
Shalom
Dr. Max Shimba 

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW