Saturday, April 21, 2018

Roho Mtakatifu kwa Mujibu wa Biblia na Quran





JE ROHO MTAKATIFU NI NANI NDANI YA BIBLIA NA QURAN?
Vitabu vitakatifu vinatutaka kumpwekesha Mwenyezi Mungu, ya kwamba Yeye hana mshirika wala anayefanana naye. Tunasoma katika Quran;
“Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni mmoja tu, Mwenyezi Mungu tu ndiye anayestahiki kukusudiwa na viumbe Vyake (vyote kwa kumwabudu na kumwomba na kumtegemea), Hakuzaa wala hakuzaliwa, wala hana anayefanana naye hata mmoja” (Sura ya 112:1-3)
Mwenyezi Mungu naye anasema maneno hayo hayo ndani ya Biblia, kwamba.
“Sikia, Ee Israel; BWANA Mungu wetu, Bwana ndiye Mmoja” Torati 6:4
Dhana ya kuwa kuna Waungu watatu imepingwa kabisa kwa nguvu na vitabu vitakatifu, kama tunavyosoma katika Quran;
“Kwa hakika wamekufuru wale waliosema: Mwenyezi Mungu ni mmoja katika wale waungu watatu (yeye ndiye wa tatu wao), hali hakuna Mungu ila mwenyezi Mungu mmoja (tu peke yake). Na kama hawataacha yale wayasemayo, kwa yakini itawakamata—wale wanaoendelea na ukafiri miongoni mwao—adhabu iumizayo” (Sura ya 5:73)
“Enyi watu wa Kitabu! Msiruke mpiaka ya dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila kwa lililo kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Na neno lake tu alilompelekea Maryamu, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini mwenyezi Mungu na Mitume yake, wala msiseme: Utatu. Wacheni (Itikadi hiyo) ni bora kwenu. Hakika mwenyezi Mungu ni mmoja tu. Amemeepukana na Kuwa na mtoto. Ni vyake Ni vyake vilivyomo Mbinguni na katika ardhi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi” (Sura ya 4:171)
Kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na wapekee na kwamba hafananishwi na kitu chochote haina shaka kabisa ndani ya vitabu vitakatifu. Hoja ya msingi hapa itakuwa ni kuweza kuelewa huo upekee ni wa namna gani. Vitabu vyote vitakatIfu vinamaelezo mazuri kuhusu hali ya Mwenyezi Mungu. Kwa mfano tunaposoma katika 1Yohana 5:8 tunaona kuwa
“Kwa maana wako watuatu washuhudiao mbinguni, Baba na Neno, na Roho Mtakatifu na Watatu hawa ni Umoja”
Hapa tunaona kwamba kumbe Umoja katika habari ya Uungu hupatikana katika Watatu, yaani kwa maana nyingine, haupatikati umoja kwa Mungu mpaka paweta watatu.
Tunapochunguza vizuri maandiko matakatifu, tunaweza kugundua kwamba, dhana hii ya umoja katika utatu (wingi) inapatikana kwa wazi kabiza, kwa mfano. Wakati alipoumba mbingu na ardhi, tunaambiwa kwamba;
“Mungu (mmoja) akasema ‘Na tufanye (wingi) mtu kwa mfano wetu (wingi)” (Mwanzo 1:26)
Twaona kwa mujibu wa Aya hii kwamba Mungu anaongea katika hali ya umoja lakini kuna kiashiria kwamba yeye siyo mmoja kwa maana tunayojua sisi wanadamu, lakini ni mmoja katika hali yake yeye mwenyewe, yaani hali ya wingi. Na kwa mujibu ya 1Yohana 5:8, wingi huo ni wa Nafsi tatu.
Dhana hii iko wazi pia ndani ya Quran kuwa Mungu anaposema ni Mmoja, hana maana ya Umoja wa nafsi moja lakini ni zaidi ya nafsi moja, kwa mfano.
“Na hakika tulimuumba mtu, kutokana na udongo mkavu, kwa matope meusi yenye kufinyangwa” (Sura 15:26)
“Hatukuziumba mbingu na ardhi, na vilivyomo baina yake, ila kwa haki na kwa Muda uliowekwa…” (Sura ya 46:3)
Tamko hili ndani ya Quran linaonyesha wazi kwamba Mungu anazungumza katika hali ya wingi, nafsi zaidi ya moja. Wanazuoni wa Kiislamu wanatueleza kwamba, kauli hii ya Mwenyezi Mungu haina maana ya nafsi zaidi ya moja isipokuwa ni pale Mwenyezi Mungu anapozungumza kwa hali ya kujitukuza. Lakini uchunguzi zaidi ndani ya vitabu vitakatifu unaonyesha kuwa dhana hii haina msingi wowote, isipokuwa ni mafikara tu ya wanadamu.
Katiba Biblia takatifu tunaona kwamba, Wakati wa Uumbaji, neno linasema;
“Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa Maji…” Mwanzo 1:1
Kumbe kwa Mujibu wa Aya hii, Wakati wa Uumbaji, Mungu alikuwa pamoja na Roho yake. Je, huyu Roho wa Mungu ni nani?.
Tunaambiwa wakati wa Kuzaliwa kwa Nabii Isa (a.s) wakati Malaika Gabrieli (Jibril) alipokuwa kwa Maryamu, alisema.
“Roho Mtakatiafu atakujilia juu yako, na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli…” (Luka 1:35)
Nabii Isa (Yesu) Mwenyewe alipoanza kazi yake alisema kuwa
“Roho wa Bwana yu Juu yangu…” (Luka 4:7)
Kwa Maandiko haya tunaona kwamba Kumbe, Mwenyezi Mungu, anaye Roho Mtakatifu wake, na Roho huyo, Mwenyezi Mungu humtuma kwa Manabii wake kama tunavyosoma;
“Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, akapaza sauti kwa nguvu akasema…”
(Luka 1:41-42)
“Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii akisema:..” (Luka1:67)
“Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho Muda wa siku arobaini nyikani”(Luka 4:1)
“Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara akapanda kutoka majini, na tazama, mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake” (Mathayo 3:16)
Roho Mtakatifu ni nafsi hai,  kwasababu, Mtu anaweza kufanya Ujeuri na Kushindana naye. Roho anatuombea, Roho mtakatifu anazungumza
“Bwana akasema Roho yangu haitashindana na Mwanadamu milele…” (Mwanzo 6:3)
“Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho wake Mtakatifu…” (Isaya 63:10)
“Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye Mlitiwa Mhuri hata siku ya Mwisho” (Waefeso 4:30)
“Naye mtu yeyote atakayesema neno juu ya Mwana wa Adamu, atasamehewa, bali yeye atakaye neno neno juu ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa katika Ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao” (Mathayo 12:32)
Roho Mtakatifu wa Mungu anawaombea watu wa Mungu. Sifa ya kuomba siyo ya kitu kisichokuwa na uhai. Hii inamaana kwamba Roho Mtakatifu ni nafsi hai.
“Kadharika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamukwa” (Warumi 8:26)
Roho Mtakatifu huzungumza. Sifa hii ya kuzungumza ni sifa ya Nafsi hai, siyo kitu kisichokuea na uhai, au kama wengine wasemavyo kwamba ni nguvu tu.
“Roho akamwambia Filipo, sogea karibu na gari hili ukashikamane nalo” (Matendo 8:29)
“Basi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo” (Luka 2:25
“Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati uo huo mnachopaswa kusema” (Luka 12:12) (Msisitizo ni wangu katika aya hizi)
Wanazuoni wa Kiislamu wanapokutana na hoja ya Roho wa Mungu wanamnasibisha Roho wa Mungu na Mtume Muhammad, kwamfano wanaposoma katika Yohana 16:13
“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa Kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote, kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na maneno yajayo atawapasha habari zake”
Aya hii Waislamu wanapoisoma, wanaona kuwa hapa katabiriwa Mtume Muhammad (s.a.w). Lakini, Tumekwisha kuona kuwa Roho Mtakatifu wa Mungu sifa zake ni kwamba.
Alikuwepo wakati wa Uumbaji (Mwanzo 1:1)
Alikuwepo toka wakati wa Nuhu (Mwanzo 6:3)
Alikuwepo wakati wa Musa Isaya (63:10)
Kazi yake ni Pamoja na kuwatia nguvu mitume na pia ni Mwombezi wetu.
Sifa hizi zinamtoa kabisa Muhammad kuwa Roho Mtakatifu, au Roho wa Mungu. Kamwe Muhammad hajaletwa ili awe mwombezi wetu, badalayake. Waumini ndio wanaamulishwa kumwombea Muhammad. Na kwa kweli Mwenyezi Mungu ndiye hasa mwombezi wa Muhammad.
“Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika Wake humsalia Mtume; enyi mlioamini, msalieni (Mtume) na mwombeeni amani” (Sura 33:56)
Mwenyezi Mungu anamsalia mtume, na hivyo waumini nao wanaamrishwa wamsalie mtume. Siyo yeye awalalie au kuwaombea. Na ndiyo maana Mwislamu anapolitaja jina la Mtume lazima aishie na kuseama “Swala llhau aleyhi wa salaam”. Yaani Swala za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake pamoja na amani (Msisitizo ni wangu). Je Mwenyezi Mungu angewezaje kusali kwa Mtume, je asali kwa Mungu gani ikiwa yeye ni wa Pekee? Hivyo twaona kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja lakini siyo umoja huu tujuavyo sisi. Ni umoja wa Nafsi tatu, na ndiyo maana kwa habari ya kuwaombea watakatifu wa Mungu, nafsi moja yaweza kuomba kwa nafsi nyingine. (Tutaangalia kwa upana zaidi hoja hii ya kumnasibisha Muhammad na Roho mtakatifu mwishoni mwa somo hili)

Je Roho Mtakatifu ni nani ndani ya Quran?
Kama tulivyoona katika Biblia, Mwenyezi Mungu alimtia nguvu Nabii Isa kwa Roho Mtakatifu na alifanya miujiza mingi.
“Na hakika tulimpa Musa Kitabu, na tukawafuatisha mitume baada yake; na tukampa Isa mwana wa Maryam, hoja zilizo wazi wazi, na Tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Kila alipowafikia mtume kwa yale yasiyopenda nafsi zenu, mlitakabari, kundi moja mkalikadhibisha, na kundi jingine mkaliua” (Sura ya 2:87)
“Atakaposema Mwenyezi Mungu: Ewe Isa Mwana wa Maryam! Kumbuka neema yangu juu yako na juu ya mama yako. Nilipokutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu utotoni na katika utu uzima, na nilivyokufundisha kitabu na hekima, na Taurati na Injil, na ulipotengeneza kwa udongo kama umbo la ndege kwa idhini yangu, kisha ukapulizia likawa ndege kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha vipofu na wenye mbalanga kwa idhini yangu, na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu, na nilipokukinga na wana wa Israeli ulipowafikia na hoja zilizo wazi…” (Sura ya 5:110)
Waislamu kwa kuepuka somo la utatu Mtakatifu katika Quran wanasema eti Roho Mtakatifu aliyekusudiwa katika aya hizi ni Malaika Jibril. Lakini wakiulizwa fundisho la kusema Roho Mtakatifu ni Jibril wanapata wapi ndani ya Quran, hawawezi kuwa na jibu. Ni dhana tu ya kumnasibisha Jibril na Roho Mtakatifu. Kuna aya mbili ndani ya Quran zinazotumiwa na Waalimu wa Kiislamu kudai kuwa Jibril ndiye Roho Mtakatifu. Na hapa tuzichunguze aya hizi.
“Sema: Anayemfanyia ushinde Jibril (kwa kuwa ndiye aliyemteremshia utume Nabii Muhammad asiwapelekee Mayahudi) (ni bure, hana kosa Jibril); hakika yeye ameiteremsha Quran Moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (siyo kafanya kwa kupendelea kwake); (Quran inayosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake, na ni uwongozi na khabari njema kwa wanao amini” (Sura ya 2:97)
“Sema: Roho takatifu (yaani Jibril) ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki, ili kuwathibitisha wale walioamini, na kuwa uwongozi na khabari njema kwa walioamini” (Sura ya 16:102)
Hivyo Mwislamu kwa aya hizi mbili anajenga hoja kwamba, “kwakuwa 2.97 inasema Quran iliteremshwa na Jibril, na 16:102 inasema Qurani iliteremshwa na Roho Mtakatifu basi tunahitimisha kuwa Jibril ndiye Roho Mtakatifu”. Kwa kwei hii ni hoja dhaifu sana na isiyozingatia maana na Mantiki ya maandiko yote kwa ujumla. Hakuna mahali popote katika Quran, Jibril amtamkie Mtume kwamba, “mimi Jibril ndiye Roho Mtakatifu”, wala hakuna katika hadithi Mtume alipofunulliwa ya kwamba Jibril ni Roho Mtakatifu. Tuchunguze hoja hii kwa kina zaidi.
Je ufunuo (Wahyi) kwa mtume ulikuja katika njia (daraja) ngapi?.
Tunaambiwa katika kitabu kiitwacho Ar Raheeq al Makhtum ukrasa wa 109 juu ya mafungu ya Wahyi yalikuwa kama ifuatavyo;
1. Kudhihiri kwa ndoto za kweli, ilikuwa mwanzo wa Wahyi kwa mtume (s.a.w)
2. Kwa yale ambayo Malaika alikuwa akiyapenyeza kwenye fikra na Moyo wake
3. Kwa Malaika kujidhihirisha kwake katika Sura ya Mwanadamu
4. Mtume kujiwa na Wahyi kwa mfano wamlio wa Kengele uliokuwa na kishindo
4. Mtume alikuwa akimwona Malaika katika sura yake halisi
5. Maneno ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja.
Hivyo kwa hili tu tunaona kwamba, haifai kabisa kuchukua aya moja ya namna alivyoshushiwa Wahyi Mtume (s.a.w) na kufananisha na aya nyingine inayoongelea kushushwa kwa Wahyi kwa mtume. Kufanya hivyo ni kuonyesha kwamba Mtume alishushiwa Wahyi kwa njia moja peke yake na hivyo kukana Historia ya Maisha yake na namna yeye mwenyewe alivyoeleza namna alivyokuwa akifunuliwa Wahyi.
Roho Mtakatatifu na Kuhusika kwake kuleta Wahyi kwa Mtume.
Unaporudia kusoma vizuri Sura ya 16:102 bila kuweka maneno ya Fikra za Wafasiri na Wasomi wa Kiislamu, udagunua inasema kwamba
“Sema: Ameiteremsha Roho takatifu kutoka kwa Mola wako, ili awathibitishe wale waliamini na kuwa ni uwongofu na bishara kwa Waislamu” (Sura 16:102)
Katika aya hakuna neno Jibril, lakini mtafsiri anatia mikono yake ili kuleta maana kwamba huyo Roho mtakatifu ni Jibril.
Tumekwisha kuona kuwa Mtume alipata ufunuo kwa nyanja au njia mbalimbali, ni wazi kuwa moja wapo ni kushukiwa na Roho Mtakatifu kama ambavyo tunaona kuwa, Mitume hupata ufunuo ama kwa Malaika kutumwa na kuwaletea ujumbe. Na wakati mwingine Roho Mtakatifu huwapatia uvuvio. Ni wazi kuwa Roho Mtakatifu ametofautishwa kabisha na Malaika kuonyesha yeye ni nafsi tofauti na Malaika pale tunaposoma katika Quran
“Hushuka Malaika na Roho, katika usiku huo, kwa idhini ya Mola wako kwa kila Jambo” (Sura ya 97:4)
Hapa tunaona Malaika hushuka na Wahyi na Roho Mtakatifu naye hushuka na Wahyi. Jibril ni Malaika ndiye aliyekusudiwa na kisha Roho Mtakatifu. Wote wawili wametajwa kwa pamoja wakihusika katika kuleta Wahyi.
Kwa Mujibu wa Quran, Roho Mtakatifu ndiye aliyemwezesha Maryam, Mama wa Isa kuwa na mtoto.
Kama ilivyo katika Biblia, kwamba Malaika Gabrieli alikuja kwa Mariamu na kumpasha habari njema za kuzaa mtoto kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Soma Luka 1:35 na Mathayo 1:20) ndivyo ilivyo katika Quran pia, tunasoma kwamba;
“Na Mariamu mtotto wa Imrani aliyejihifadhi nafsi yake, na tukampurizia humo roho yetu (inayotokana na sisi), na akayasadikisha maneno ya Mola wake, na vitabu vyake; na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu.” (Sura ya 66:12)
“Na (Mtaje yule mwanamke) aliyejilinda (aliyejihifadhi), nafsi yake, na tukampulizia roho yetu na tukamfanye yeye na mwanae kuwa miujiza ya kudra ( ya mwenyezi Mungu) kwa walimwengu” (Sura ya 21:91)
Katika aya hizi haiwezekani kusema kwamba Jibril ndiye roho iliyopulizwa kwa Mariamu. Neno linasema “ttukampurizia humo roho yetu”. Yaani Roho ya Mwenyezi Mungu. Na ndivyo kukawa kuzaliwa kwa Nabii Isa (a.s)
Malaika Gabriel katika Biblia alisema “mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu” (Mathayo 1:21)
Haiwezekani wala haiingi akilini kwamba Malaika Jibril ndiye awe Roho Mtakatifu tena. Kwani aya za Quran zinasema, Mwenyezi Mungu alipuliza Roho yake ndani ya tumbo la Mariamu, na Roho huyo akafanyika Mwili.
Kwa Mujibu wa Quran, Roho Mtakatifu huwatia nguvu waumini ili wafanye vitendo vyema.
Tunafahamu kwamba, kwa mujibu wa Mafundisho ya Uislamu, Jibril hutumwa kwa mitume, na kazi yake ni kuletu ufunuo (Wahyi). Aya hii ifuatayo ndani ya Quran, inaondoa dhana ya kumdhania Jibril kuwa ni Roho Mtakatifu
“Huwapati (huwaoni) watu wanaomwamini mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, kuwa wanawapenda wale wanompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake; hata wakiwa ni baba zao au watoto wao au ndugu zao au jamaa zao. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu ameandika, ( amethibitisha kweli kweli) nyoyoni mwao imani na akawatia nguvu kwa Roho itokayo kwake, na atawaingiza katika mabustani yapitayo mito ndani yake, humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu amekuwa radhi nao, na wao wamekuwa radhi naye. Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu. Sikilizeni! Hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo linalofaulu.” (Sura ya 58:22)
Tunaambiwa kwamba Mwenyezi Mungu huwatia nguvu waumini “kwa Roho itokayo kwake”, hii kwa hakika siyo kazi ya Jibril. Ni wazi kwamba, waumini kwa mujibu wa aya hii, hufanya vitendo vyema kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Uelewa huu wa kwamba waumini hupewa uwezo kwa njia ya Roho Mtakatifu ndiyo fundisho kuu la Biblia. Yesu aliahidi kuwapatia Roho wake Mtakatifu wafuasi wake, ambaye angewasaidia katika kufanya kazi aliyo waachia;
“Lakini mtapokea nguvu, akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu…” Matendo 1:8
“Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao”
(Luka 12:13)
Je Roho wa Kweli ni nani kwa mujibu wa vitabu vitakatifu?
Waislamu hudai kwamba Mtume Muhammad ametabiriwa ndani ya Biblia kuwa yeye ndiye Roho wa kweli. Wanasema kuna Roho Mtakatifu, na pia kuna Roho wa kweli. Wao kwao neno Roho Mtakatifu na Roho wa kweli ni vitu viwili tofauti. Chakushangaza katika dhana hii ni kwamba, Roho wa kweli siyo mtakatifu. Sasa jambo la kujiuliza je yeye Roho wa kweli ni Roho Mchafu? Maana kinyume cha utakatifu ni uchafu.
Kwa mujibu wa Vitabu vya Mungu, Roho atokaye kwa Mungu ni Roho Mtakatifu naye ni Roho wa kweli. Ameitwa Roho wa Kweli ili kumtofautisha na roho za mashetani ambazo Biblia inazielezea soma maandiko haya;
“Basi Roho anena wazi wazi ya kwamba, nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani” (1Timotheo 4:1)
“Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizi ndizo roho za mashetani…” (Ufunuo 16:13-14)
Hivyo Yesu alimtaja Roho Mtakatifu kuwa Roho wa kweli ili kumtofautisha na hizi roho za uongo zinazodanganya ulimwengu wa imani katika zama zetu. Hata hivyo tuichunguzi aya hii ambayo Waislamu huitumia wakidai kuwa inamkusudia Muhammad.
“Lakini amin nawaambia, yafaa Mimi niondoke kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu. Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini Mimi, kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa. Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa. Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili Yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. Atanitukuza Mimi, kwa maana atayachukua yaliyo Yangu na kuwajulisha ninyi. Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo Yangu na kuwajulisha ninyi.” (Yohana 16:7-15)
Kwa mujibu wa aya hii Waislamu wanasema, aliyekusudiwa hapo ni Muhammad kwa sababu
Roho wa kweli angeuthibitishia Ulimwengu kwa habari ya dhambi—Muhammad alianzisha dini ya Uislamu akionya watu juu ya maovu na dhambi
Roho wa kweli atauthibitishia Ulimwengu kwa sababu ya haki—Muhammad alifundisha dini ya haki
Roho wa kweli atauthibitishia Ulimwengu kwa sababu ya hukumu—Muhammad alifundisha Uislamu ambamo ndani yake zimu sharia na hukumu.
Hoja ya msingi tutaangalia iwapo sifa za huyo Roho wa kweli zinamfaa Muhammad, na kisha tuone habari ya dhambi, haki, na hukumu
Sifa za Roho wa kweli kwa mujibu wa maneno ya Yesu.
Yesu Mwenyewe amesema juu ya huyo Roho wa kweli kwamba
“Kama mnanipenda, mtazishika amri Zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu
hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu” (Yohana 14:15)
Kwa Mujibu wa aya hii tunagundua mambo yafuatayo
Roho wa kweli anaitwa Msaidizi na analetwa kwa waumini pale wanapompenda Yesu na kushika amri zake. Swali la kujiuliza je Waislamu wanampenda Yesu na kuzishika amri zake
Roho wa kweli anakaa nasi milele. Swali la kujiuliza, je Muhammad anakaa na Waislamu milele? Hapana. Muhammad alikufa jumatatu mchana tarehe 8 mwezi wa 6 mwaka 632. Miaka zaidi ya 1400 iliyopita. (Abdala Farsy, Maisha ya Nabii Muhammad, uk. 81)
Roho wa kweli ulimwengu haumwoni anajulikana kwa waumini tu. Swali la kujiuliza, je Muhammad hakuonekana na makafiri? Hapana, Muhammad alionekana na wapinzani wa Uislamu, naye akapigana nao vita.
“Walipomwona haondoki, wale ‘Mashekhe’ waliamrisha watu wa mji wampige mawe kila wamwonapo, mpaka aende zake. Basi haikuwahi kutangaa habari hii ila kila mtu alitoka na akiba ya mawe mkononi mwake ili mpige mtume atakapomwona. Alipotokeza nje tu, mara walimtopoa kwa mawe, husemi watoto wanapopoa embe zilizoiva! Hakujamsaidia chochote hata kusema anakwenda zake; lakini waliendelea kumfuata njiani na kumpiga mawe, na huku wakimpigia sokole, muda wa maili 2. Aliloa damu tangu kichwani mpaka miguuni, hawajamwacha kupumzika hata chembe muda wa maili 2 zote hizo!” (Abdala Farsy, Maisha ya Nabii Muhammad, uk. 30)
Kisa hiki kinaonyesha ni wazi Muhammad alionekana na watu wa ulimwengu huu waliokuwa wapinzani. Roho wa kweli haonekani wala kufahamika na wale wasiomjua Mungu. Sana sana watapinga uwepo wake wakidai “Mungu hana mshirika”
Roho wa kweli hukaa ndani ya watu wa Mungu
“Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu ye yote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo. Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki. Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, Yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho Wake akaaye ndani yenu.” (Warumi 8:9-11)
Muhammad hawezi kumwingia mtu akakaa ndani yake, kamwe ni jambo lisilowezekana. Ni dhahili kwamba Roho wa kweli siyo Muhammad.
Kwa mujibu wa Yohana 16:7 Roho Mtakatifu anatumwa ana Yesu. “lakini nikienda nitamtuma kwenu”. Swali la msingi, ikiwa Muhammad ni Nabii, na tunatambua kwamba Manabii hutumwa na Mwenyezi Mungu, Yesu anasema yeye ndiye atakayemtuma huyo Roho wa kweli, kwa kuwa Waislamu wanadai aliyekusudiwa hapa ni Muhammad, Je Yesu atakuwa nani kwa Muhammad? Bila shaka kwa kuwa ametumwa na Yesu, Basi Yesu ndiye Mungu wa Muhammad. Jambo ambalo kamwe Mwislamu hawezi kukubaliana nalo. Na kama hakubali hili, basi aachane na aya hii kabisha haimhusu Muhammad.
Je Roho Mtakatifu anauhakikishiaje Ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu?
Tumekwisha kuona kuwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hunena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu
“Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu” 2 Petro 1:21
“wakafunuliwa yakuwa si kwa ajili yao wenyewe, baali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi injili kwa Roho Mtakatifu…” 1 Petro 1:11
Hivyo watumishi wa Mungu wanapohubiri wakikemea dhambi na kuwaonya watu juu ya hukumu ijayo, kazi hiyo hufanywa na Roho Mtakatifu aliye ndani yao.
“Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. 8Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya. Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbali mbali za lugha, kwa mwingine tafsiri za lugha. Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo mwenyewe.” (1Wakorintho 12:7-11)
Mungu ni Mmoja, lakini umoja huo wa Mwenyezi Mungu hauna maana ya umoja kama ambavyo akili ya mwanadamu inatambua. Mungu ni mmoja katika nafsi tatu zilizo hai. Na katika utatu huo ndio anasema hafanani na yeyote, kwa sababu hakuna mungu au miungu inayoweza kuwa na sifa ya Mungu mmoja na hapo hapo akawa na nafsi tatu zilizo hai. Quran inapokata utatu ni kwasababu Makuraishi wa maka walikuwa na waungu watatu walioabudiwa kwa mfano wa Masanamu. Muhammad akaipiga marufuku dini hiyo ya kipagani, na akawakataza watu wasimwabudu Mwenyezi Mungu kwa mifano ya waungu hao. Tunasoma katika Quran
“Je mmewaona Lata, na Uza na Manat mungu wenu mwingine wa tatu (kuwa ndio waungu hao badala ya Mwenyezi Mungu?). Je kwenu muwe na watoto wa kiume na Kwake waweko watoto wa kike? Huo ni mgawanyo wa dhuruma! (Mnamdhurumu basi Mungu!) (Sura ya 53:19-22)
Muhammad analalamika kwamba miungu hiyo inawatoto wa kike tuu! Na kwamba wale wanaoiabudu wanawatoto wa kiume. Kufanya hivyo—yaani kusema miungu yao makafiri ina watoto wa kike peke yake ni kufanya dhuruma kwa miungu hiyo, yaani hawaitendei haki.
Kisha anaendelea kusema
“Hayakuwa haya (majina ya Lata, mungu mwanamke na Al uzza, mungu mwanamke mwenye enzi na Manata, mungu mwanamke anayeneemesha) ila ni majina tu mliyowapa nyinyi na baba zenu (masanamu hayo; wala hawana lao jambo). Mwenyezi Mungu hakuteremsha dalili juu yao. Hawafuati ila dhana na zinayopenda nafsi (zao). Na kwa yakini uwongozi umewafikia kutoka kwa Mola wao…” (Sura ya 53:23
Hawa ndiyo waungu watatu ambayo Quran nzima inapinga itikadi ya makafiri wa Makka. Wayahudi na Wakristo hawakuwa wakiabudu miungu watatu wakati wa Muhammad, wala katika Biblia halipofundisho la waungu watatu, isipokuwa MUNGU NI MMOJA MWENYE NAFSI TATU ZILIZO HAI
Shalom,
Dr. Max Shimba

No comments:

Muhammad’s Fear Of Judgment Day

  Muslims beware! The next  eclipse  could be the  Day of Judgment .  This warning comes from none other than Muhammad himself. During the l...

TRENDING NOW