Saturday, February 17, 2018

JE, NI KWELI MUHAMMAD NDIYE MSAIDIZI ALIYETABIRIWA NA YESU?



Je, unazijua sifa kumi za kipekee za huyo Msaidizi aliye tabiriwa na Yesu?

Bwana Yesu katika Yohana 14 aya ya 15 mpaka 17  akizungumza kuhusu Msaidizi na kuweka sifa za Msaidizi alisema haya:

Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ILI AKAE NANYI HATA MILELE, ndiye ROHO wa kweli, ambaye ulimwengu HAUWEZI KUMPOKEA, Kwa kuwa HAUMWONI WALA HAUMTAMBUI, bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, Naye atakuwa NDANI yenu."

Hapo tunapata sifa kumi za huyo Msaidizi, kama ifuatavyo:

1. MSAIDIZI ATAKAA NA SISI MILELE:
Hiyo ndio sifa ya kwanza ya Msaidizi, lazima akae na sisi milele. Je, Muhammad yuko wapi sasa? Kama Muhammad ndiye huyo Msaidizi mbona amekufa ametuacha, kwa nini hakukaa na au hakai na sisi Milele kama ilivyo tabiriwa?

Hapo utagundua kuwa Muhammad sio Msaidizi, maana Msaidizi wetu hafi, Yesu Kristo alisema "Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele ". Yohana 14:16. Sasa mbona Muhammad alishakufa kitambo sana. Hivyo Muhammad hana sifa ya kuwa Msaidizi.


2.  MSAIDIZI NI ROHO,
Wala Sio kiumbe cha kawaida kama mwanadamu. Yesu alisema "ndiye ROHO wa kweli, ambaye ulimwengu HAUWEZI KUMPOKEA, Kwa kuwa HAUMWONI..." Yohana 14:17. Uthibitisho rejea Yohana 15:26 "Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo ROHO wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia" Soma pia Yohana 16:13,"Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake"

Je, Muhammad ni ROHO? Muhammad sio Roho, ila alikuwa mtu na sasa ni marehemu. Hivyo Muhammad hana sifa ya kuitwa Msaidizi.


3.  MSAIDIZI HAONEKANI WALA HATAMBULIKI NA ULIMWENGU:
Hiyo ndio sifa nyingine ya Msaidizi. Haonekani kwa sababu ni Roho. Rejea Yohana 14:17 "ndiye ROHO wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, Kwa kuwa HAUMWONI WALA HAUMTAMBUI, bali ninyi mnamtambua..."

Je, Muhammad alikuwa HAONEKANI? Au Je ulimwengu haukumtambua marehemu Muhammad? Ukweli ni kuwa Muhammad alikuwa ANAONEKANA, maana alikuwa MWANADAMU na alitambulika na Ulimwengu. Kama Muhammad hakuwa anaonekana, Waislam thibitisheni leo, ili tujue ukweli.

Yesu pia aliwaambia wanafunzi, "bali ninyi mnamtambua..." Kumbe Msaidizi wanafunzi walikuwa wanamtambua, sasa ukisema Msaidizi ni Muhammad, je wanafunzi wa Yesu walikuwa wanamtambua mtume Muhammad? Walimuona wapi? Maana mpaka wanakufa, Muhammad hakuwepo. Hivyo Muhammad tena hana sifa ya kuitwa Msaidizi.


4.  MSAIDIZI ANAKAA NDANI YETU:
Hii ndio sifa nyingine ya huyo Msaidizi, kwamba sharti akae ndani ya mioyo ya watu. Rejea Yohana 14:17 "...bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, Naye atakuwa NDANI yenu"

Ili Muhammad awe Msaidizi, lazima uwepo ushahidi kuwa, Muhammad alikuwa anakaa ndani ya watu. Kitu ambacho hakipo kabisa! Maana mtume Muhammad hakuwahi kukaa ndani ya mioyo ya wanafunzi wa Yesu. Kwanza atakaaje ndani yetu wakati alishakufa? Je marehemu aweza kukaa ndani ya mioyo ya wafuasi wa Yesu? Hapa tena mtume Muhammad S.a.w amepoteza sifa ya kuitwa Msaidizi.


5. MSAIDIZI ALITUMWA NA MUNGU KWA JINA LA YESU:
Yohana 14:26 "Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."

Ili Muhammad awe Msaidizi, lazima uwepo ushahidi kuwa Muhammad alitumwa kwa jina la Yesu, cha ajabu ni kuwa hakuna muislam anaeweza kukubali kwamba, mtume Muhammad alitumwa na Allah kwa jina la Yesu. Hii inamfanya mtume Muhammad anapoteze tena sifa ya kuitwa Msaidizi.


6. PIA MSAIDIZI ALITUMWA NA YESU KUTOKA KWA BABA:
Yesu aliwaahidi wanafunzi kuwa atawatumia Msaidizi, rejea Yohana 15:26, "Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia" soma pia Luka 24:49" "Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu, lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.

Hakuna sehemu ambayo Muhammad amedai kuwa alitumwa na Yesu, hata Waislam wenyewe hawakubali kwamba Muhammad alitumwa na Yesu, wanaamini alitumwa na Allah. Kwa hiyo Muhammad siyo Msaidizi, maana hakutumwa na Yesu.


7.  MSAIDIZI LAZIMA AMSHUHUDIE YESU:
Yohana 15:26, Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia.

Cha ajabu ni kuwa Muhammad, anayedaiwa kuwa Msaidizi, hakuwahi kumshuhudia Yesu, Ila alimshuhudia kiumbe mwingine tu aitwaye Allah! Kwa sababu hiyo tena, Muhammad hawezi kamwe akawa Msaidizi, maana hakumshuhudia Yesu.


8. MSAIDIZI SHARTI AMTUKUZE YESU NA ATWAE MAFUNDISHO YA YESU AWAPE WATU:
Yohana 16:13-14  Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. 14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.

Ili mtume Muhammad awe Msaidizi, alitakiwa amtukuze Yesu na atwae katika yaliyo ya Yesu awapashe watu habari. Je Muhammad alifanya hivyo? HAPANA! Badala yake Muhammad alimtukuza kiumbe mwingine anayeitwa Allah, Muhammad hakuwahubiri watu Mafundisho ya Yesu, bali alihubiri mafundisho ya Allah, hivyo Muhammad hana sifa ya kuitwa Msaidizi.


9. MSAIDIZI LAZIMA AWAFUNDISHE NA KUWAKUMBUSHA WANAFUNZI YOTE ALIYOSEMA YESU:

Msaidizi alitakiwa kufanya hivyo kuanzia kwa wanafunzi wa Yesu, rejea Yohana 14:26  Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

Sasa Muhammad yeye alikuja kuzaliwa baadaye sana, wakati ambapo wanafunzi wa Yesu walishakufa zamani sana, hakuwahi hata kukaa nao awafundishe na kuwakumbusha kile alichosema Yesu. Na hata katika mafundisho yake, Muhammad hakuwahi kufundisha wala kukumbushia kile alichosema Yesu, badala yake alikuja kupingana na Yesu, mfano Yesu alisema yeye ni MWANA WA MUNGU, Muhammad akaja kupinga, akasema Mungu hana Mwana. Hivyo basi Muhammad hana sifa ya kuwa Msaidizi.


10.  MSAIDIZI ILITAKIWA AJE ENZI ZA UHAI WA WANAFUNZI WA YESU, TENA WAKIWA BADO HAWAJATAWANYIKA YERUSALEMU:
Yesu Kristo baada ya kufufuka katika wafu, aliwaambia Wanafunzi wake, wasitoke Yerusalem,

Matendo 1:4 "Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu",

Luka 24:49, Yesu anawaambia wanafunzi, "Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu, lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu", Tukio la kuja kwa Msaidizi lilitokea Yerusalem, siku ya Pentekoste, Ndipo Msaidizi alipowashukia wanafunzi, soma Matendo ya Mitume 2:1-5:
1 Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu."

Hivyo ndivyo ahadi ya kuja kwa Msaidizi ilivyotimia. Sasa Muhammad hawezi kuwa Msaidizi, kwa sababu

(Moja):, Muhammad hakuwepo enzi za uhai wa wanafunzi wa Yesu, alikuwa Hajazaliwa bado, Na kwa mujibu wa maelezo ya Yesu, Msaidizi lazima angekuja wakati bado mitume wako hai.

(Mbili): Ujio wa Msaidizi ulitokea Yerusalem, siku ya Pentekoste. Lakini Muhammad hajatokea Yerusalem, na aliyeshuka siku ya Pentekoste hakuwa Muhammad, isitoshe, wakati huo Muhammad hata mimba yake tu haikuwa imetungwa!

Kama Muhammad ndie Msaidizi basi alitakiwa awashukie mitume siku ya Pentekoste kule Yerusalem.

Hivyo basi, Muhammad sio msaidizi ambaye tuliahidiwa na Yesu Kristo Mungu Mkuu, kwasababu ameshindwa na hana sifa zote kumi hapo juu za Msaidizi.


Usikose soma la “Je, Msaidizi aliye tabiriwa na Yesu Kristo Mungu Mkuu ni nani?”

Shalom,


Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo Mungu Mkuu.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW