R. I. P. MANENO MATAMU SANA NA MAZURI SANA YA FARAJA TUNAPOONDOKEWA NA MPENDWA WETU LAKINI JE MBELE ZA MUNGU YANA NGUVU?
R. I. P. ni maneno ambayo tunayatumia sana tunapoondokewa na mtu wa karibu sana nasi na ambaye tumeguswa sana na kuondoka kwake. Ni kifupi cha maneno ya Kiingereza, Rest In Peace ambayo yana maanisha kwa kiswahili Pumzika kwa Amani. Na kwa kweli hata mimi ningemtakia kila mtu aondokaye hapa ulimwenguni akapumzike kwa amani huko aendako. Ila je kwa mujibu wa maandiko matakatifu kila mmoja afaye atapumzika kwa amani kweli?
Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. (UFU. 14:13 SUV).
Hili andiko linaonyesha wazi kuwa wale wafao katika Bwana ndo wenye uhakika wa kupumzika kwa amani na maandiko yanatuambia wazo kuwa matendo yao yanafuatana nao. Matendo yako, maisha yako uliyoishi hapa duniani je yanakuatahilisha kweli ukapumzike kwa amani huko uendako!
Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. (LK. 16:25 SUV).
Katika mfano wa tajiri na Lazaro ambao nimechomoa andiko hili, tajiri kwa sababu ya mafanikio aliyokuwa nayo alimsahau kabisa Mungu na akasahau kujiandaa kwa ajili ya maisha yajayo. Ila maskini pamoja na kuishi maisha machungu na ya taabu alikumbuka kujiandaa kwa safari ya kwenda kwenye maisha yajayo. Matokeo ya walipofikia wote wawili yalitegea sana maandalizi ya kila mmoja wao.
Wapendwa wangu kila mmoja wetu atakufa siku moja na hakuna ajuaye siku yake yeye ni lini na ataondokaje.
Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuruhusiwa katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea. (MHU. 8:8 SUV).
Hakuna mwenye mamlaka hata kidogo juu ya siku yake ya kufa kuizuia au kuisogeza mbele au kuiwaisha. Itakuja tu siku moja. Siku moja mimi na wewe kila mmoja kwa zamu na wakati wake ataitwa na umauti na huo umauti utaenda kutusimamisha mbele za Mungu na Mungu atakuhukumu na atanihukumu kwa kuliangalia neno Lake na lile alilotuagiza katika maisha haya.
Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; (EBR. 9:27 SUV).
Kila mmoja wetu amewekewa kufa na baada ya kifo ni hukumu na kwa mujibu wa maandiko tutahukumiwa kwa sababu moja tu:
Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; (YN. 16:8, 9 SUV).
Dhambi kubwa kuliko zote mbele ya Mungu kwa mujibu wa neno la Mungu ni kutokumwamini Yesu kama Mwana wa Mungu.
Kwa kuwa kufa ni hakika basi Mungu atusaidie tujiandane maana kufa huko kutatuleta mbele ya Muumba wetu na haitajalisha tena wewe ni mbishi kiasi gani.
Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli. (AMO. 4:12 SUV).
Ni nini hicho ambacho atatutenda na ikatulazimu kujiandaa kuonana na Mungu wetu? Kila mmoja wetu atakufa siku moja. Iandae safari kabla haijafika isije ikafika na haupo tayari ukajuta.
Hujachelewa bado maana hata yule mwizi pale msalabani alitengeneza maisha yake dakika za majeruhi akaahidiwa raha pamoja na Kristo paradiso.
Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. (LK. 23:42, 43 SUV).
Ukitaka kuwa na Yesu peponi kama ambavyo huyu mwizi pale msalabani alipata hiyo fursa jiandane kabla ya kufa kwako na usitegemee kwamba utasaliwa au kuswaliwa ukiwa umeshakufa maana wakati wasaliwa au kuswaliwa tayari siku nyingi unakuwa umeshahukumiwa na hukumu za Mungu hazina kukata rufaa.
Mungu akubariki sana unavyochukua hatua ya kujiandaa.
Sholom
Kwa ruhusa ya Mwalimu Conrad
No comments:
Post a Comment