UTANGULIZI:
Samweli (kwa Kiebrania: שְׁמוּאֵל Šəmuʼel, maana yake labda ni "Anayemsikiliza Mungu" au Mungu Amesikia au Jina la Mungu) ni mtu muhimu wa Historia ya wokovu ya Agano la Kale. https://www.britannica.com/biography/Samuel-Hebrew-prophet
Katika Biblia anatajwa kama mwamuzi na kama nabii, naye ndiye mwanzilishi wa ufalme wa Israeli.
Habari zake zinasimuliwa katika Vitabu vya Samweli.
Vitabu viwili vya Biblia ya Kikristo vinaitwa kwa jina la Samweli, ambaye kwa njia yake Israeli ilianza kuwa na umoja zaidi na hatimaye kuwa ufalme. Badala ya kila kabila kujitegemea, yote 12 yalikubaliana yawe na kiongozi mmoja wa kudumu ambaye cheo chake kirithiwe na mwanae. Kwa umoja huo waliweza kushinda maadui wao wengi.
Vitabu hivyo vimekusanya kumbukumbu zote kuhusu mwanzo wa ufalme (1070-972 hivi K.K.), yaani kuhusu Samweli mwenyewe na wanaume wawili aliowapaka mafuta watawale Israeli kwa niaba ya Mungu: kwanza Sauli, halafu Daudi. Kumbukumbu hizo zilikuwa nyingi na tofauti, hivyo tunakuta humo tata nyingi kuliko katika vitabu vingine vyote vya Biblia. Hasa mna hoja za kukubali mfumo wa ufalme na hoja za kuukataa.
Ukuu wa Samweli ulidokezwa kwanza na uzazi wake wa ajabu, kwa kuwa mama yake, Hàna, alikuwa tasa akampata baada ya kusali na kuweka nadhiri (1Samweli 1). Hivyo baada ya miaka michache alihamia Shilo kwenye sanduku la agano kama mtumishi wa kuhani Eli.
Hapo mwanzo vitabu viwili vya Samweli vilikuwa kitabu kimoja, kikionyesha mfululizo wa historia ya Israeli kuanzia wakati wa Waamuzi mpaka wakati wa utawala wa Mfalme Daudi.
Vitabu hivyo havimtaji mwandishi wake, ingawa kuna fununu kwamba baadhi ya habari zake zilitokana na ripoti zilizokuwa zimeandikwa na Samweli, Nathani, Gadi, Daudi na waandishi wa kitabu cha Yasheri (1 Samweli 10:25; 2 Samweli 1:18; 1 Nyakati 27:24; 29:29).
Habari za vitabu hivyo viwili zinachukua muda wa miaka themanini hadi mia moja.
Mafungu ya kwanza ya 1 Samweli yanaendelea kueleza habari za historia ya Israeli tangu wakati wa kitabu cha Waamuzi.
Wakati wa kuhani Eli, maisha ya Israeli upande wa kisiasa na wa dini yalifuata mfano wa wakati wa Waamuzi, watu walipomwasi Mungu na kuanguka chini ya utawala wa mataifa ya jirani (1 Samweli 2:12, 32; 3:11-13; 4:10-11, 18; taz. Amu 2:13-15).
Lakini Samweli aliyekuwa mkubwa katika Waamuzi wote, alipofaulu kuwahamasisha watu kuondoa miungu yao na kumrudia BWANA, Yeye BWANA katika neema yake aliwaokoa watu wake kutoka kwa maadui zao waliokuwa wamewanyanyasa (1 Samweli 7:3-6, 13, 15-17; taz. Amu 2:18; 3:9, 15).
Lakini Samweli hakuweza kuleta mabadiliko ya kudumu katika taifa, tena wanawe hawakufaa kumrithi, na watu walidai iingizwe serikali ya kifalme, kama ilivyokuwa katika mataifa ya jirani yao (1 Samweli 8:1-5). Baada ya kuimarishwa kwa ufalme sawa sawa, uongozi siku zote ungekabidhiwa au kurithiwa kutoka kwa baba hadi mwanawe (1 Samweli 8:19-22).
Basi, Sauli aliwekwa kuwa mfalme wa kwanza wa Israeli, lakini Samweli aliwaonya watu kwamba jambo hilo lisingeondoa matatizo ya taifa. Chini ya Waamuzi Waisraeli waliadhibiwa kwa ajili ya kuasi na kutokuamini kwao (1 Sam 12:9-11), na chini ya wafalme wangeadhibiwa kwa sababu hizo hizo (1 Sam 12:13-15).
Wakati wa kwanza wa ufalme wa Israeli mambo mengi ya utawala yalifanana na ule wa Waamuzi, hasa kwa jinsi viongozi walivyopewa nguvu maalumu ya Roho wa Mungu, ili waweze kuwaokoa Waisraeli kutoka kwa watawala wa kigeni, na kutimiza kazi nyingine walizopewa (1 Samweli 10:6; 11:6, 11; taz. Amu 3:10; 6:34; 11:29; 14:6, 19).
Sauli alipomwasi Mungu na kukataliwa, Roho wa Mungu alimtoka naye akaja juu ya Daudi (1 Samweli 16:13-14). Kinyume cha Sauli, Daudi alijinyenyekeza mbele ya Mungu, naye alitamani kutimiza mapenzi yake (Zaburi 89:20; Matendo 13:22).
Kwa Daudi wakati mpya kabisa ulianza, na hatimaye Waisraeli waliimarika kitaifa na kufanikiwa, kama walivyokuwa wametamani kwa muda mrefu. Vitabu vya Samweli vinaeleza habari za utawala wa Daudi ambaye, katika nyakati zote zilizofuata, alihesabiwa kuwa mfalme bora wa Israeli, na mzazi mkuu wa Masiya aliyeahidiwa (2 Samweli 7:12-16; Mt 22:42; Lk 1:32-33).
***Muhtasari wa 1 Samweli***
1:1-7:17 Israeli chini ya Eli na Samweli
8:1-12:25 Kuanzishwa kwa ufalme
13:1-15:35 Ushindi wa kwanza wa Sauli
16:1-19:24 Kuinuka kwa Daudi
20:1-31:13 Sauli amwudhi Daudi
***Muhtasari wa 2 Samweli***
1:1-4:12 Vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kifo cha Sauli
5:1-10:19 Daudi aimarisha ufalme wake
11:1-20:26 Matatizo katika nyumba ya Daudi
21:1-24:25 Mambo mengine
Baada ya kusoma UTANGULIZI wa Vitabu viwili vya Samweli, sasa turudi na kujifunza ni kivipi Samweli aliupata UNABII wake. ‘Sema, kwa Maana Mutumishi Wako Anasikiliza’
USIKOSE SEHEMU YA PILI.
Max Shimba Mtumwa wa Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment