Uaminifu katika ndoa ni jambo la kila mmoja, sio la mke peke yake. Inashangaza sana kuona watu wakisema kuwa mwanaume hawezi kukaa bila kutoka nje sababu ndivyo walivyo. Kweli?? Hivi biblia kuna mahali inasema kuwa mwanaume ni kiumbe dhaifu? Nini tofauti kati ya mwanadamu na mnyama kama mwanadamu unasema ulishindwa kujizuia eti ni shetani. Yaani unakuta mwanaume katembea nje ya ndoa tena mara nyingine hadi kupata mtoto akiulizwa anajitetea mara ni shetani, mara nilipitiwa mara mke wangu ndio kasababisha sababu ya hili na lile.
Halafu utakuta analazimisha mkewe amsamehe na haoni kwa nini ashindwe kumsamehe na kila mtu anamshangaa mkewe kwanini amsamehi wakati wanaume ndivyo walivyo na hata kumlaumu mke kuwa ndio sababu. Wakati mke akitoka nje ya ndoa hakuna anayetaka kusikia sababu yoyote tena hao wanawake wanaomlaumu mume akitoka nje ya ndoa ndio wanakuwa wa kwanza kumlaumu na kila mtu anamwambia mume muache huyu mwanamke hakufai. Hivi watu wanapoapa kuwa waaminifu mume huapa kuwa nitakuwa muaminifu kama mke akifanya hili na lile? Hivi wanaume hamuoni kuwa mnajidhalilisha kusema kuwa ulishidwa kujizuia? Ina maana hauna tofauti na jogoo anayemkimbiza kuku na kumaliza haja zake pale anaposikia hamu? Mtu utafute namba ya simu, muwasiliane, mkubaliane, utoke ulipo hadi gest upange foleni reception, upande ghorofani chumbani, uvue nguo bado tu unajitetea hukudhamiria, kweli? Huyo shetani alikufunga kamba?
Usidhani mkeo hapati vishawishi, tena inawezekana vikubwa kukushinda lakini aliahidi uaminifu kutoka moyoni sababu anakupenda na kumheshimu Mungu. Hakuna sababu yoyote inayoweza ku justify mwanandoa kwenda nje ya ndoa. Kila mmoja aheshimu viapo vya ndoa na kumuogopa Mungu. Hii ndiyo silaha pekee ya ndoa.
Shalom,
Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment