JE, UNAMJUA NABII WA KIKE DEBORA WA KWENYE BIBLIA?
SEHEMU YA PILI
- DUNIA ILITIKISIKA, MBINGU PIA ZIKATIRIRIKA MAJI -
Baraka alikusanya jeshi lake. Alikusanya wanaume 10,000 jasiri ili kupambana na jeshi la Sisera lenye kutisha. Baraka alipokuwa akiongoza watu wake kuelekea Mlima Tabori alithamini sana kwamba alikuwa na uwezo wa kuchochea ujasiri wao. Tunasoma hivi: “Nabii Debora akapanda pamoja naye.” (Waamuzi 4:10) Wazia jinsi wanajeshi hao walivyotiwa moyo walipomwona mwanamke huyo jasiri akiambatana nao kuelekea Mlima Tabori, akiwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuwa pamoja nao kwa sababu ya imani yake kwa Mungu!
Sisera alichukua hatua mara moja alipojua kwamba jeshi la Israeli limejikusanya ili kupigana naye. Wafalme kadhaa wa Kanaani walimuunga mkono Mfalme Yabini ambaye huenda alikuwa na nguvu zaidi kati yao. Kisha, magari ya kivita ya Sisera yalitikisa ardhi yalipoenda pamoja katika eneo tambarare. Wakanaani walikuwa na uhakika kabisa kwamba wangelishinda jeshi la Israeli.—Waamuzi 4:12, 13; 5:19.
Baraka na Nabii Debora wangefanya nini adui anapokaribia? Ikiwa wangebaki katika miteremko ya Mlima Tabori, huenda ingekuwa rahisi kwao kushinda majeshi ya Kanaani kwa kuwa magari yao ya vita yalihitaji eneo tambarare ili kushambulia vizuri. Hata hivyo, Baraka alitaka kupigana kulingana na maagizo ya Mungu, hivyo alisubiri mwelekezo kutoka kwa Nabii Debora. Hatimaye, mwelekezo ukatolewa. Nabii Debora alisema hivi: “Simama, kwa maana hii ndiyo siku ambayo Mungu hakika atamtia Sisera mkononi mwako. Je, Mungu siye ambaye ameenda mbele yako?” Kisha tunasoma hivi: “Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori akiwa na wanaume elfu kumi nyuma yake.”—Waamuzi 4:14. *
Jeshi la Israeli lilisonga kwa kasi na kushuka mlimani mpaka eneo la wazi, tambarare, kuelekea magari hayo ya kivita yenye kutisha.
Je, Mungu alienda mbele yao kama Debora alivyoahidi?
Jibu lilipatikana baada ya muda mfupi. Tunasoma hivi: “Dunia ilitikisika, mbingu pia zikatiririka maji.” Jeshi la Sisera lenye kiburi halikujua la kufanya. Mvua ikaanza kunyesha. Inaonekana kwamba mvua hiyo ilikuwa kubwa sana hivi kwamba ikasababisha mafuriko makubwa katika bonde hilo. Hivyo, magari hayo ya kivita yaliyotengenezwa kwa chuma hayakufaa kitu. Yalizama kwenye matope kwa sababu ya mvua hiyo.—Waamuzi 4:14, 15; 5:4.
Baraka na wapiganaji wake hawakuathiriwa na dhoruba hiyo. Walijua chanzo chake. Waliyafuatilia majeshi ya Wakanaani. Wakitekeleza hukumu ya Mungu, Waisraeli waliua wanajeshi wote wa Sisera. Mto Kishoni ulifurika na kufagilia mbali maiti zote mpaka Bahari Kuu.—Waamuzi 4:16; 5:21.
Leo, Mungu hatumii watumishi wake kupigana vita halisi. Hata hivyo, anahimiza watu wake kupigana vita vya kiroho. (Mathayo 26:52; 2 Wakorintho 10:4) Tukijitahidi kumtii Mungu katika ulimwengu wa leo, tunaonyesha kwamba tunapigana vita hivyo. Tunahitaji ujasiri kwa kuwa wale wanaomtii Mungu leo wanaweza kukabili upinzani mkali. Hata hivyo, Yehova hajabadilika. Bado anawalinda wale wenye imani na wanaomtegemea kama Debora, Baraka, na wanajeshi jasiri wa taifa la Israeli walivyofanya.
“ATABARIKIWA ZAIDI KATI YA WANAWAKE”
Adui mkubwa zaidi Mkanaani alitoroka! Sisera, mkandamizaji mkuu wa watu wa Mungu, alikimbia kwa miguu kutoka katika uwanja wa vita. Akiwaacha watu wake wakifa kwenye matope, Sisera alifanikiwa kupita katikati ya wanajeshi Waisraeli na kukimbilia eneo kavu, akiwa na lengo la kukimbilia eneo lenye wafalme waliomuunga mkono. Aliteremka katika nyanda tambarare, huku akiwa na hofu kubwa kwamba huenda wanajeshi wa Israeli wangemkamata, alielekea katika mahema ya Heberi, Mkeni aliyetengana na watu wake wahamaji upande wa kusini na kufanya mkataba wa amani na Mfalme Yabini.—Waamuzi 4:11, 17.
Sisera alifika katika kambi ya Heberi akiwa amechoka. Hakumkuta Heberi nyumbani kwake. Hata hivyo, mke wake, Yaeli alikuwapo. Yawezekana kwamba Sisera alifikiri Yaeli angetenda kulingana na mkataba wa amani aliofanya mume wake na Mfalme Yabini. Huenda hakufikiri kwamba mwanamke huyo angetenda tofauti na mume wake. Ni wazi kwamba Sisera hakumjua Yaeli! Hata hivyo, Yaeli aliona wazi uovu aliofanya mkandamizaji huyo Mkanaani kuelekea Israeli; na yawezekana hilo lilifanya aone kwamba alipaswa kuchukua hatua. Alihitaji kuamua ama kumsaidia mwanamume huyo mwovu au kumtegemea Mungu na kumuua adui huyo wa Watu wake. Angefanya nini? Mwanamke atawezaje kumuua mpiganaji mwenye nguvu na uzoefu?
Yaeli alihitaji kufikiria haraka jambo la kufanya. Alimwonyesha Sisera mahali pa kupumzika. Sisera akamwamuru amfiche ili mwanamume yeyote atakayekuja kumtafuta asimpate. Yaeli akamfunika, na alipomwomba maji, akampa maziwa. Baada ya muda mfupi, Sisera alilala usingizi mzito. Kisha Yaeli akachukua kigingi cha hema, chombo ambacho wanawake wanaoishi katika mahema mara nyingi walitumia kwa ustadi. Akiwa amechuchumaa karibu na kichwa cha Sisera, Yaeli alikabili kazi ngumu ya kutenda akiwa mtekelezaji wa hukumu kwa niaba ya Mungu. Kusita au kutokuwa na uhakika wa jambo la kufanya kungesababisha madhara makubwa. Je, Yaeli alikumbuka watu wa Mungu na jinsi mwanamume huyo alivyowatesa kwa miaka mingi? Au je, alifikiria pendeleo alilokuwa nalo la kuchukua msimamo upande wa Yehova? Masimulizi hayatoi majibu. Tunajua tu kwamba Yaeli alichukua hatua. Sisera alikufa!—Waamuzi 4:18-21; 5:24-27.
Baadaye, Baraka alifika ili kumtafuta adui yake. Yaeli alipomwonyesha maiti ikiwa imepigiliwa kigingi katika kipaji cha uso, Baraka akajua kwamba unabii wa Debora umetimia. Mwanamke alimuua Sisera, shujaa mwenye nguvu! Wachambuzi wa mambo wa siku hizi wamemwita Yaeli majina mengi yasiyofaa, lakini Baraka na Debora walijua vizuri alichofanya Yaeli. Katika wimbo wao ulioongozwa na roho takatifu, walimsifu Yaeli kwa kusema kwamba “atabarikiwa zaidi kati ya wanawake” kwa sababu ya tendo lake la ujasiri. (Waamuzi 4:22; 5:24) Ni wazi kwamba Debora alikuwa mkarimu. Hakumsifu Yaeli huku akiwa na wivu; badala yake alikazia zaidi kutimizwa kwa neno la Yehova.
Nguvu za Mfalme Yabini mtawala aliyekuwa tishio kwa taifa la Israeli zilikoma Sisera alipouawa. Ukandamizaji wa Wakanaani ulikoma. Kukawa na amani kwa miaka 40. (Waamuzi 4:24; 5:31) Debora, Baraka na Yaeli walibarikiwa sana kwa sababu ya kudhihirisha imani katika Yehova Mungu. Tukiiga imani ya Debora, tukichukua kwa ujasiri msimamo thabiti upande wa Mungu, na kuwachochea wengine wafanye vivyo hivyo, Mungu atatubariki na kutusaidia kushinda na kutupatia amani ya kudumu.
Shalom,
Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment