Sunday, April 23, 2017

JE, MUNGU ANAZALIWA IKIWA ALIKUJA KAMA BINADAMU?




Kimsingi Mungu yeye kama Mungu hazaliwi na hakuwahi kuzaliwa kamwe, ila kile kinachotajwa kuzaliwa na Mariam ni ubinadamu wa Yesu tu ambao ulizaliwa ili kufunika Uungu ambao kuwepo kwake ni tangu milele. Na kwa hivyo Mariam hakuzaa Uungu bali alizaa ubinadamu uliobeba Uungu, kwakuwa kusema kwamba Mariam alizaa Uungu wenyewe ni sawa na kusema kuwa Mungu ana mwanzo wa kuwepo kwake yaani alianza kuwako mara tu baada ya kuzaliwa na Mariam na kwa hali hiyo Mungu ana umri maalumu na mwanzo wa kuwepo kwake tendo ambalo linapingana na maelekezo tunayoyapata katika maandiko matakatifu:-
Zaburi 102:24-27
Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.25 Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako.26 Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika.27 Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma.

Na ili kukaza uelewa wa hili tunaweza kuona maelezo ya Yesu mwenyewe juu ya hili katika mjadala wake na Wayahudi pindi walipopingana na tamko la Yesu kujihusianisha na Ibrahimu ambapo Wayahudi walimkumbusha umri wake tangu alipozaliwa na Mariam na kutumia kigezo hicho kukosoa madai ya Yesu juu ya mahusiano yake na Ibrahimu hebu tusome majibu ya Yesu:-
Yohana 8:55
Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi.57 Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?
58 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.
Hilo ndilo tamko la Bwana Yesu akibainisha kuwa uwepo wake katika nyanja ya Kiuungu usingepaswa kuwekwa katika vipimo vya miaka ya kibinadamu maana kwa hali halisi yeye alikuwapo hata kabla ya Ibrahimu.
Hivyo kwa muktaza huu haitakuwa sahihi kusema kuwa Mariam ni mama wa Mungu kwakuwa neno lenyewe mama tu humaanisha mzazi (mlezi) hivyo ni kusema kwamba Mariam ni mzazi au mlezi wa Mungu tendo ambalo ni kufuru na ni kosa la wazi la kutotendea haki maandiko matakatifu.
Mifano michache juu ya uwezekano wa Mungu kutwaa ubinadamu.
Ni jambo linalonishangaza sana ninapoona hali ya upinzani juu ya ukweli huu ili hali ziko simulizi mbalimbali ambazo zingeweza kutumika kama vielelezo muhimu vya kurahisisha uelewa wa jambo hili, hebu ona mfano wa kisa hiki kinachosimuliwa na watu wengi majini Dar es salaam:
Kijana mmoja alikuwa akipita njiani na kukutana na binti mzuri aliyetokea kumpenda, na ndipo baada ya maongezi binti huyo alikubali kwenda kupafahamu nyumbani kwa kijana huyo’ baada ya kufika na wakiwa wameketi ukumbini ndipo kijana huyo akamuomba yule binti ampatie rimoti ya TV iliyokuwa mbele kidogo upande wake na kwa namna ya kutisha binti huyo badala ya kuinuka na kwenda kuchukua rimoti hiyo alifyatua tu mkono wake ulioonekana kurefuka kupita kiasi na kuichukua rimoti hiyo. Kwa hali hiyo upendo uliishia hapo na kijana huyo kupiga kichwa mlango na kutoka nje kwa hofu na hatimaye kuzimia mlangoni.
Watu wengi wanaosimulia kisa hicho huonekana kufanya hivyo wakiamini kabisa kuwa huyo alikuwa ni jini aliyebeba taswira ya kibinadamu, na hivyo kile kinachonishangaza ni namna watu wanavyoweza kuamini kuwa shetani anaweza kujibadili ili kutesa watu lakini kwa nguvu zote hupingana na swala la Mungu kuvaa ubinadamu ili kutukomboa’ tafakari upya na badili mtazamo.
Bwana Yesu alichukua ubinadamu ili kumkaribia mwanadamu na hatimaye kusaidia ili aweze kuokolewa, Mtume Yohana alitamka:-
Yohana 1:14
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Hivyo kusudi la Yesu kufanyika mwili na kukaa kwetu ndilo lingepaswa kupokelewa kwa shukrani zaidi maana lilileta utukufu kwa wanadamu tofauti na matukio tunayoshabikia juu ya viumbe vibaya. Tendo hilo la Yesu kukaa kwetu (baada ya kuvaa mwili huo) linatajwa katika lugha ya Kigiriki kama:
Eskenosen’ ambayo maana yake ni kupiga kambi ( English – ‘Tent’/ dwelt among us).
Pamoja na uchambuzi wa Biblia ni jambo lililonifurahisha sana kuona katika vitabu vingine vinavyoaminiwa sana katika ulimwengu wa imani hususani msahafu wa Qur an kuona kielelezo muhimu juu ya dhana nzima ya mabadiliko yanayoweza kufanyika kwa hali moja kuchukua hali nyingine kwa lengo Fulani muhimu, mfano wa hili ni kisa cha Malaika aliyemtokea Mariam kwa nia ya kutotaka kumwogofya Mariam aliamua kubadili maumbile yake alipomtokea. Hebu tusome katika maandiko:-
Qur an 19:17
Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea muhuisha Sharia Yetu (Jibrili) akajimithilisha kwake (kwa sura ya ) binaadamu aliyekamili .
Kama nilivyotangulia kueleza kuwa hicho ni kisa cha Malaika Jibril ambaye alimtokea Mariam kadri inavyoelezwa na kuaminiwa na ndugu zetu wa Kiislam yakuwa Malaika huyo alimtokea kwa umbile la kibinadamu, hivyo swali la kutafakari hapo ni kuwa kama Malaika tu aliweza kubadili umbile na kuja katika hali hiyo je Mungu anawezaje kushindwa?
Hivyo ukweli nikuwa Bwana Yesu alitwaa umbile hilo kwa lengo la kufunika utukufu wake ambao mwanadamu asingeweza kuukabili , andiko la mtume Paulo la Wakoritho linatuhitimishia sehemu hii ya uchambuzi.
2Wakoritho 5:18-19
Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Hivyo ieleweke kuwa umbile la kibinadamu la Yesu ndani yake lilibeba mamlaka kamili ya Uungu, mamlaka ambayo ilikuwepo tangu milele na hata kabla ya kuzaliwa kwa ubinadamu wa Yesu na Mariam.
Kama ni Mungu mbona alisema anaenda kwa Baba yake?
Hii nayo ni miongoni mwa hoja tete katika Ulimwengu wa imani ambapo kile kinachohojiwa hapo ni tendo la Yesu kuonekana mara kadhaa akitaja habari ya Baba katika mazungumzo yake kwa nyakati na matukio tofauti na hivyo kuibua hoja hii kuwa kama Yesu ni Mungu inakuwaje basi aseme anaenda kwa Baba yake na je kuna uhusiano gani baina ya Yesu na Baba?
Jibu la msingi la hoja hiyo”
Kimsingi kama nilivyokwisha fafanua kwa kina juu ya utatu mtakatifu tuliona juu ya uwepo wa nafsi tatu za Mungu mmoja ambapo Baba ni mojawapo ya nafsi hizo, hivyo jambo la msingi katika hoja hii ni kuangalia tu sababu ya Yesu kuitamka nafsi hiyo ya Baba kama mamlaka tofauti wakati Fulani na ndipo tuangalie uhusiano uliyopo baina ya Baba na Neno-Yesu.
Yohana 16:25
Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba.
Katika maelezo yake hayo Bwana Yesu anaeleza kuwa wakati fulani amekuwa akitumia mithali (mafumbo) kueleza juu ya habari ya Baba na sasa anaahidi kuwa hatimaye ipo siku ambapo atatamka wazi wazi juu ya habari ya Baba.

Maelezo hayo yanatoa kanuni ya jumla ya kuzingatia katika kuyajadili matamko ya Bwana Yesu ambapo Yesu mwenyewe anaweka wazi kuwa kauli zake zinaweza wakati Fulani zikawa na uzito kueleweka mpaka pale anapoamua kuziweka bayana yeye mwenyewe, na kikubwa zaidi hapa Yesu anataja wazi kuwa miongoni kwa kauli zake hizo zilizofumbika ni ile inayohusu habari ya Baba na ndipo anaahidi kuwa upo wakati ambapo atafumbua fumbo hilo lihusulo mahusiano yake na Baba.

Hebu sasa tuone namna Yesu alivyoweka wazi mahusiano yake na Baba’
Yohana 10:30-33
Mimi na Baba tu umoja.31 Basi Wayahudi wakaokota mawe tena ili wampige.32 Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?33 Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu 

Hii ni sehemu ya kwanza ya maandiko ambapo Bwana Yesu anaweka bayana juu ya undani wake wa asili na mamlaka moja na Baba kwa kusema wazi kuwa yeye na Baba ni umoja, tamko ambalo Wayahudi walielewa moja kwa moja kuwa lilionyesha kuwa Yesu alikuwa akithibitisha Uungu wake.
Na katika tamko jingine Yesu aliweka wazi kuwa hakuna utofauti wowote baina yake na nafsi ya Baba hebu tusome:-

Yohana 14:7-9
Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. 8 Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.9 Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
Katika andiko hilo Bwana Yesu anaweka wazi zaidi na kufumbua fumbo hilo mbele ya wanafunzi wake ambapo wanafunzi hao wanamhoji na kumtaka awaweke wazi juu ya uhusiano wake na Baba huku wakidai kuwa awaonyeshe huyo Baba, na ndipo kwa namna ya kushangaza Bwana Yesu anawajibu kwa uwazi kuwa tendo la kumfahamu yeye ndiyo kumfahamu Baba mwenyewe na kuwa kwa kumwona yeye tayari wameshamwona huyo Baba hivyo hawakuwa na haja ya kudai kumwaona Baba.

Hapo tendo la kumfahamu yeye ndiyo kumfahamu Baba mwenyewe na kuwa kwa kumwona yeye tayari wameshamwona huyo Baba hivyo hawakuwa na haja ya kudai kumwaona Baba.

Hapo Yesu aliweka wazi kuwa yeye ni Mungu toka katika umoja wa nafsi tatu za Mungu mmoja na kamwe hakuna tofauti za kimamlaka baina ya nafsi hizo kwa kuwa ni Mungu yule yule anayetenda katika katika upana kupitia Nafsi tatu yaani ile ya Baba , Neno na Roho Mtakatifu kama tulivyoona katika uchambuzi mpana wa hoja hiyo hapo mwanzoni 

Hivyo jambo la msingi ni kuweka utulivu tu katika usomaji wa maandiko matakatifu maana kimsingi maandiko hayo yanatoa majibu ya kila swali linalotutatiza katika ulimwengu huu wa imani wenye walimu na farsafa nyingi za kidini.
Kwanini alilia Mungu wangu mbona umeniacha?
Katika mijadala mbalimbali ya imani kumesikika swali hili likihojiwa na walimu mbalimbali na wachambuzi wa dini, kile kinachotatiza hapa ni tamko la Bwana Yesu akiwa msalabani Mathayo 27:46…Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

Hivyo swali linajitokeza hapa kuwa sasa Yesu alikuwa akimwomba Mungu gani ili hali yeye ni Mungu?
Jibu la msingi la swali hili’

Tamko hilo la Yesu msalabani endapo utalichukulia kama lilivyo pasipo kutafuta undani wake linaweza kukuingiza katika jaribu la kufikiri kuwa Bwana Yesu alikuwa ni kiumbe tu kwa hali zote.

Lakini msingi wa maandiko ya Biblia ulihusianisha tukio hilo na upande wa pili wa utendaji wa Bwana Yesu yaani ule wa kutwaa husika ya ubinadamu na kujiweka katika viwango vya ubinadamu ili kuwa kielelezo na hatimaye kutukomboa. Na hivyo hali hiyo ilimpelekea wakati Fulani kutamka na kutenda kama mwanadamu pamoja na kuwa asili yake si ya kibinadamu, na ndipo mtume Paulo anaweka wazi kanuni hiyo:-

Filipi 2:7
Bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

Biblia inafafanua kuwa baada ya Yesu kutwaa mfano wa ubinadamu hali hiyo ilimfanya kujifanya kuwa hana utukufu yaani wakati Fulani alitumia hali ya kawaida tu ya ubinadamu na si Uungu wake (uwezo, mamlaka) hivyo ndiyo maana hata alitamka maneno hayo akibeba husika halisi ya ubinadamu na kwakweli hapo alitamka kwa hali hiyo ya ubinadamu kabisa, ingawa tamko hilo halihafifishi mamlaka yake ya kiasili ya Uungu kwakuwa lilikuwa katika mpango mzima wa hatua zake za kiukombozi na kuvaa kiatu chetu.

Pia Yesu alikuwa akitimiza unabii’

Kwa upande mwingine Biblia inaweka wazi kuwa tamko hilo lililenga pia kutimiza tabiri za kiunabii kama Yesu mwenyewe anavyojenga msingi wa ukweli huu kwa kutamka:-

Luka 24:44
Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.
Katika tamko hilo Bwana Yesu anaeleza kuwa kuna mambo yanayomhusu yaliyoandikwa katika vitabu hivyo vya manabii lazima ayatimize katika kipindi cha huduma yake mambo au unabii ambao uliandikwa tayari katika vitabu hivyo vya manabii lakini anataja kuwa mambo hayo pia yamo katika Zaburi ya nabii Daudi.

Katika Zaburi hiyo ya nabii Daudi unaposoma Zaburi ile ya 22:1’ utagundua kuwa hapo kuna tamko lile lile la Yesu alilotoa pale msalabani kwa kusema “Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha?

Hivyo kwa mtazamo huo utagundua kuwa tamko lile la Bwana Yesu msalabani lililenga pia kutimiza unabii huo wa Zaburi ya Daudi kwakuwa hata Yesu mwenyewe alionyesha wazi kuwa alipaswa kutimiza unabii ulio katika kitabu hicho cha Zaburi hivyo swala hilo halihafifishi asili yake ya mamlaka ya Uungu.
Yesu alitimiza kanuni ya Biblia ya kukabili matatizo kwa kuomba na kuimba.
Pamoja na ufafanuzi huo wa msingi hapo juu bado maandiko ya Biblia yan endelea kupanua wazo katika hoja hii kadri tunavyosoma katika andiko jingine la mtume Yakobo kama ifuatavyo:-

Yakobo 5:13
Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi.
Mtume Yakobo katika mitabu chake hicho anataja kanuni za mbili za kimbingu za kukabili matatizo kuwa jambao la kwanza yule aliyepatwa na matatizo anapaswa kuomba na pia aimbe Zaburi.

Hivyo kwa hali halisi tutakubaliana kuwa katika hali ya kibinadamu Yesu alikuwa akikabiliana na mabaya ya mateso ya msalaba na hivyo kwa tamko lile alikuwa akitimiza masharti hayo kwa njia hiyo ya kuomba lakini pia kuimba maana tamko alilolitoa ni Zaburi (tenzi) ya 22:1 katika kitabu hicho cha mfalme Daudi, na kwa hali hiyo tendo hilo haliathari kwa namna yeyote mamlaka ya asili ya Uungu wa Bwana Yesu.

Hebu nikualike tena tunapokwenda kwenye uchambuzi wa swali jingine muhimu juu ya Uungu wa Yesu.

Shalom.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW