Wednesday, April 26, 2017

Je, Muhammad Ametabiriwa Kwenye Biblia? – Sehemu ya II


Katika makala yaliyopita tuliona hoja za ndugu wa Kiislamu wanavyojaribu kwa juhudi nyingi kuonyesha kwamba Muhammad ametabiriwa kwenye Biblia. Katika makala hayo niliahidi kuwa nitaeleza jinsi ambavyo hoja zao hazina ukweli wowote. Licha ya kwamba Mungu wanayemwamini amewahakikishia kwamba Muhammad ametajwa kwenye Biblia, ukweli ni kwamba hajatajwa hata kidogo!


 Katika sehemu ya kwanza ya mfululizo huu, nilimalizia kwa kunukuu kile ambacho Yehova, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, anasema juu ya Neno lake. Hebu tuangalie tena baadhi ya maneno hayo. Imeandikwa: 

Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho,tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. (1 Wakorintho 2:12-15). 

Tatizo mojawapo kubwa ninaloliona mara nyingi kwenye Uislamu na Waislamu ni kutazama mambo kwa jinsi ya mwili. Hapo ndipo penye shida kubwa yanapokuja masuala ya rohoni. Kama uko kwenye safari ya kimaisha katika ulimwengu wa kimwili na unalenga kuishia kwenye ulimwengu wa kiroho (jambo ambalo ndilo linaloendelea kwa wanadamu wote), basi ni lazima utafute maana ya mambo ya ulimwengu wa mwilini kulingana na ulimwengu wa rohoni. Ukiishia tu kutazama mambo katika mwili, una hasara kubwa!! Ni lazima kutambua kuwa Mungu hatupi ujumbe wake ili tuweze kuwa matajiri, maarufu na wenye vyeo wa hapa duniani. Kama hayo ndiyo malengo yako makuu katika maisha haya, basi wewe una hasara kuliko watu wote. Hayo si mambo ya msingi. Mungu ametuweka duniani kwa makusudi makubwa zaidi ya hayo.

Yeye analenga mambo yadumuyo; si mambo ya kupita. Hivyo, kiini hasa cha ujumbe wa Mungu wa kweli ni maisha ya milele yajayo kwenye ulimwengu wa roho.
 Sasa, kwa kuwa ndugu zangu hawa, wao wako zaidi katika mambo ya hapa duniani, ya kimwili, haishangazi basi kumwona Ahmed Deedat na wenzake wakiishia kuangalia tabia za kimwili za Musa na kuzilinganisha na tabia za kimwili za Muhammad na kusema kwamba eti, huo ndio uthibitisho kwamba maandiko ya Biblia wanayonukuu yanamzungumzia Muhammad. Inasikitisha sana kuwa na juhudi kubwa hivyo ambayo mwisho wake ni uangamivu. Na inasikitisha zaidi kwa sababu uko msururu mrefu nyuma yao wa watu wanaowaamini akina Deedat. Hata hivyo, nina uhakika kabisa kwamba nia yao ya ndani kabisa ni nzuri sana. Ni watu waliojitoa kwa moyo mkuu sana kwa Mungu wao na kwa dini yao. Suala tu linabaki kwamba, Je, wako sahihi? 

Lakini mara zote unapowaangalia ndugu hawa wanavyojitahidi katika kuhalalisha Uislamu, tena kupitia Biblia, kwa kweli unawahurumia. Wanahangaika kwa kweli. Kisaikolojia, ni dalili za mtu ambaye nafsi inamsuta usiku na mchana juu ya jambo ambalo nafsi hiyo hailikubali, lakini anajaribu kila njia kuituliza kwa kufunika hali halisi, ili angalau apate amani fulani ya ndani. Naamini umeshaona mtu ambaye amepatwa na jambo zito, kwa mfano kufiwa na mtu wake wa karibu. Kwa sababu nafsi inakataa kukubali ukweli huo, basi ataanza kuongea mambo mengi.

Kwa mfano, anaweza kusema, “Haiwezekani! Musa, tulikuwa naye jana tu. Musa mbona alikuwa mtu mzuri tu? Kwa nini afe? Hii si sawa. Hapana. Musa yupo. Hizi ni njama tu za watu!” n.k, n.k.
 Mtu huyu atahangaika huku nafsi yake ikitamani sana kwamba lile lililotokea lisiwe kweli, bali liwe kama asemavyo yeye. Lakini mwisho wake ni nini? Itambidi akubali tu. Hicho ndicho ninachokitafsiri kwa hawa ndugu ambao wanajaribu kwa juhudi kubwa kutafuta kumhalalisha Mtume wao kupitia Biblia.

Lakini haitawezekana! Ukiikataa kweli, jitihada zozote za kujaribu kuhalalisha uongo, haziwezi kuzaa matunda unayotarajia; hata kama nia yako ni nzuri. Nia nzuri haigeuzi uongo kuwa kweli hata siku moja!
 Na ni jambo la kushangaza sana kwamba Mungu wao amewaambia kuwa Mtume huyo ametajwa kwenye Biblia, jambo ambalo si kweli kabisa! Hili peke yake linatosha kumfanya kila Mwislamu aliye na nia ya kuwa na uzima wa milele kujiuliza mara mbilimbili. Shida tu ni kwamba, wamefundishwa kuogopa kuliko kuuliza na kuhoji mambo. 

Quran inasema kuwa Allah atawarehemu watu mbalimbali, lakini wakiwamo: ...those that shall follow the Apostle – the Unlettered Prophet – whom they shall find mentioned in the Torat and the Gospel. (Sura 7:157). Kwa tafsiri ya jumla ni kuwa anasema, atawarehemu pia wale (Wakristo) wanaomfuata Mtume (Muhammad) ambaye ametajwa kwenye Torati na Injili (Biblia). Ndiyo! Hivyo ndivyo anavyosema. Labda kama watasema kuwa andiko hilo limeongezwa na watu – jambo ambalo hawawezi  kulisema maana ni wepesi sana kung’ang’ania kwamba Biblia imebadilishwa na kupotoshwa, lakini si Quran. 

Kutokana na andiko hili, Waislamu wamejitahidi kwelikweli kutafuta ni wapi humo kwenye Torati na Injili ambako Muhammad ametajwa kama Allah alivyowaambia. Ndio sasa juhudi na bidii yao ikaangukia kwenye maandiko kadhaa yakiwamo Kumbukumbu 18:18 na Isaya 29:12. Kwa hiyo wametoa hoja nyingi (ambazo kama nilivyosema, ni za kimwili tu) ili kujaribu kutimiza hamu yao ya kuona kwamba kile ambacho Mungu wao amewaambia, ni kweli kipo kwenye Biblia. [Waislamu amkeni; tafakarini; mhoji yale mnayoamini]. Kama hujasoma hoja zao hizo, tafadhali tazama kwenye sehemu yakwanza ya makala haya. Nini kinazifanya hoja hizi za Waislamu zikose mantiki? Hata Waswahili husema: Siri ya mtungi aijuaye kata.

Yehova, ambaye ndiye mwenye Biblia, tumeona kuwa anasema katika Wakorintho ya kwamba twayanena maneno: yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.
 Yule mwenye Neno kaweka msimamo juu ya Neno lake mwenyewe – kwamba ukitaka kumwelewa anachomaanisha, ni lazima ufasiri Neno lake kwa namna ya rohoni. Itakuwa ni ajabu kama wewe usiye mhusika uje na sheria zako kwa ajili ya kuendesha mambo ya nyumbani kwa mwingine ambazo mwenye nyumba hakuzipanga. Kisha unataka watu wengine wasimwamini mwenye nyumba, bali wakuamini wewe! 

Dunia hii inapita. Siku zijazo dunia hii pamoja na vitu yote tunavyoviona kwenye anga havitakuwapo kabisa. Kutakuwapo, badala yake, ulimwengu mpya utakaodumu milele. Mungu katika kujishughulisha kwake na mwanadamu, analenga kwenye mambo ya MILELE. Haya mambo ya ugali na nguo na wake na waume, n.k. ni mambo tu ya hapa duniani ambayo yanatuwezesha kuishi tu hapa ili tufikie ile hatima kuu – yaani kuishi MILELE! 

Mambo yote anayoongea Mungu kwenye Biblia yanalenga maisha hayo yajayo ya milele. Hii ni kusema kuwa, yanalenga kwenye ulimwengu ujao wa roho; si ulimwengu huu wa mwili. Mungu anatumia maisha yetu ya kimwili ili kutengeneza au kuandaa maisha yetu ya kiroho yajayo. Pia, ametumia maisha ya kimwili ya taifa na watu wa Israeli kuelezea ujumbe wa mambo ya rohoni. Bibliasi kitabu cha historia juu ya taifa la Israeli. Biblia ni kitabu chenye ujumbe wa rohoni wa sasa na baadaye ambao unawasilishwa kupitia maisha ya kimwili ya taifa la Israeli. Kwa hiyo, kama utasoma Biblia na ukaishia kuona tu kwamba: 
  • Kulikuwa na mwanadamu anaitwa farao.
  • Kulikuwa na watu wanaitwa Waisraeli. Hawa walikuwa utumwani Misri baadaye wakatoka kwenda Israeli.
  • Wayahudi walipita jangwani na baadhi wakafia humo.
  • Musa alikuwa na mke.
  • Aliishi Nuhu akajenga safina. Watu wengi walikufa kwa gharika.
  • Yesu alivua viatu kila alipoingia kwenye sinagogi.
  • Wayahudi waliwatahiri watoto wao.
  • Mtu akikamatwa kwenye uzinzi alipigwa mawe hadi kufa.
  • Wayahudi walinawa mikono kabla ya kula.
  • Wayahudi walifuga ndevu.
  • Musa alikufa kama wanadamu wengine, n.k., n.k.
 Kama haya ndiyo tu unayoyaona, wewe hauna tofauti na mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari anayesoma somo la Historia ya mambo yaliyotokea zamani. Hapo hujajua kamwe kwamba Mungu si mwalimu au mwandishi wa historia. Kufunza Historia si jambo ambalo Mungu anajishughulisha nalo hata kidogo. Hata kidogo!! Ndugu zangu Waislamu, Mungu yuko kwenye kazi inayoamua UZIMA na MAUTI kwa wanadamu. Ujumbe wa Mungu unahusiana na wapi kila mwanadamu atakuwa MILELE! Je, ni mbinguni milele; au ni jehanamu milele? Ni lazima uvuke ngazi ya kimwili ya kutazama mambo, uingie kwenye ngazi ya rohoni. Hapo TU ndipo utaanza kuzungumza mambo ya Mungu ambaye ni Roho; na si damu na nyama kama sisi wanadamu. Ni muhimu sana kutafuta ujumbe wa milele ndani ya ujumbe wa kupita. Hebu tusome tena andiko hilo la Biblia wanalotumia Waislamu kumhalalisha mtume wao: Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. (Kumbukumbu 18:18). Tutaangalia andiko hili hatua kwa hatua na jinsi ambavyo kamwe halimhusu Muhammad. 
  1. Maneno ‘miongoni mwa ndugu zao’
Yehova alimwambia Musa kuwa atawaletea Israeli nabii ambaye angetokea miongoni mwa ndugu zao. Ni wazi kabisa kwamba katika andiko hili, Mungu wa Israeli anamlenga nabii mmoja tu, licha ya kwamba Israeli kumekuwako na manabii wengi. Kwa hiyo, ili lisimhusu kila nabii basi nabii huyo ni lazima awe tofauti na manabii wengine kwa jinsi atakavyokuwa anafanana na Musa. Na Ahmed Deedat na Waislamu wenzake wanasema kuwa nabii huyo ni Muhammad kulingana na sababu ambazo tuliziona kwenye sehemu yakwanza ya makala haya. Hebu tuanze kwa kuweka msingi. Mungu aliweka amri inayohusu watawala wa Israeli. Amri hiyo inasema kwamba:Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kando-kando yangu; usiache kumweka yule atakayechaguliwa na Bwana, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katikandugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako. (Kumbukumbu 17:14-15). Ahmed Deedat anadai kwamba maneno ndugu zao kwenye Kumbukumbu 18:18 yanamaanisha uzao wa Ishmaeli (yaani Waarabu). Katika karne na karne za watawala wa Israeli,  je, ni lini alishawahi kuwako mfalme wa Israeli aliye Mwishmaeli (Mwarabu)? Jibu ni HAIJAWAHI KUTOKEA! Andiko hili tu peke yake linatosha kabisa kumwondolea mbali Muhammad katika uhusiano na Kumb. 18:18. Lakini hata hivyo, ngoja tuendelee. Hebu tazama maandiko yafuatayo: 
  • Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zaowana wa Israeli. (Waamuzi 20:13)
  • Kisha itakuwa, hapo baba zao au ndugu zao, watakapokuja kushitaki, sisi tutawaambia, Kwa ihisani yenu tupeni sisi; kwa kuwa hatukumtwalia kila mtu mkewe katika vita; wala ninyi hamkuwapa wao, au kama sivyo ninyi sasa mngekuwa na hatia. (Waamuzi 21:22)
  • Basi itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao? (2 Samweli 2:26)
  • Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao, juu yandugu zao Wayahudi. (Nehemia 5:1)
  • lakini watatumika pamoja na ndugu zao katika hema ya kukutania, kushika ulinzi, lakini wasitumike katika huo utumishi tena. (Hesabu 8:26).
  • Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. (Mwanzo 48:6).
  • lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng'ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. (Yoshua 22:7).
 Maandiko haya yanataja maneno ‘ndugu zao.’ Lakini yoteyanamaanisha Waisraeli na si Waarabu. Ninachotaka kuonyesha hapa ni kwamba, maneno ‘ndugu zao’ yametumika mara nyingi sana katika Biblia. Pamoja na kwamba kuna sehemu chache ambako yametumika kumaanisha wana wa Ishmaeli, lakini kwa ujumla yanamaanisha Waisraeli wenyewe. Na uzuri ni kwamba, katika Kumbukumbu 18 hiyohiyo ambayo Waislamu wanainukuu, maneno hayo yametumika. Mungu anaeleza kuhusu kabila la Walawi kwamba watakuwa ni makuhani. Anasema: Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama alivyowaambia. (Kumb. 18:2). Je, hapa nako akina Ahmed Deedat wanataka kutuambia kuwa hawakutakiwa kuwa na urithi kati ya Waarabu? Kwa kifupi ni kuwa nabii yule alitabiriwa kuwa angetoka kwenye mojawapo ya makabila ya Israeli na si nje ya hapo. Yesu Kristo alitoka kwenye kabila la Yuda. 
  1. Maneno ‘mfano wako wewe’
Ni kwa vipi Yesu Kristo ni mfano wa Musa? Kama nilivyosema, Mungu analeta ujumbe wa kiroho na wala si wa kimwili katika Biblia. Ufuatao ni baadhi tu ya ulinganisho kati ya Musa na Yesu: 
  • Musa aliacha maisha ya kitajiri na kifalme nyumbani kwa farao na kwenda kuishi pamoja na ndugu zake Waisraeli waliokuwa maskini na watumwa. Imeandikwa:
 Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. (Waebrania 11:24-26). Yesu naye aliacha utukufu mkuu mbinguni. Imeandikwa: Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. (Wafilipi 2:5-8). 
  • Musa alitumwa na Mungu kwenda kuwatoa Israeli kwenye nchi ya utumwa wa farao na watesi wake ili kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi. Yesu alitumwa na Mungu kuja kuwatoa wanadamu kwenye utumwa wa ibilisi (farao wa kiroho) ili kuwaingiza kwenye mbingu.

  • Musa alikuwa ni mpatanishi kati ya wana wa Israeli na Mungu pale walipotenda dhambi. Maombi yake ndiyo yaliyoepusha mapigo kutoka kwa Mungu. Yesu ndiye mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu. Yeye huwaombea wale wanaomwamini ili hatimaye wasije kuingia jehanamu ya moto.

  • Musa aliwakomboa wana wa Israeli kutoka kwenye utumwa wa Misri kupitia sadaka ya damu. Waisraeli waliambiwa wachinje mwanakondoo wa Pasaka na kupaka damu yake kwenye miimo ya milango ya nyumba zao. Kisha Biblia inasema:

Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. (Kutoka 12:13, 23)
 Bwana Yesu naye aliwakomboa wanadamu wote kutoka kwenye utumwa wa shetani kupitia sadaka ya damu. Biblia inasema:

 Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele.(Waebrania 9:11-12).  
  • Musa aliwaagiza Waisraeli waokote mana iliyodondoka jangwani kila siku ili wapate kula na kuishi jangwani. Imeandikwa:
Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa … (Kutoka 16:21). Kwa kuwa hayo yalikuwa ni ishara ya mambo yajayo, alipokuja Bwana wa uzima mwenyewe, Yesu Kristo, akawa ameleta kile halisi ambacho kilikuwa kinasubiriwa. Imeandikwa: Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. (Yohana 6:31-33). 
  • Watu waliumwa na nyoka jangwani. Mungu akamwambia Musa atengeneze nyoka wa shaba. Amwinue juu ili mtu aliyeumwa na nyoka akitaka kupona, ainue macho yake na kumtazama yule nyoka wa shaba. Waliofanya hivyo walipona. Walioshindwa kufanya hivyo walikufa. Imeandikwa:
 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi. (Hesabu 21:9). Yesu alipokuja naye kafanya yaleyale. Nyoka ni ishara ya ibilisi na mashetani wote. Kuumwa na nyoka ni ishara ya kuwa na dhambi. Kila mwenye dhambi anatakiwa kumtazama Yesu kwa imani, naye atapona mauti – yaani kutupwa jehanamu ya moto. Anayekataa kumtazama Yesu anakuwa amechagua kufa! Imeandikwa:

Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.(Yohana 3:14-15)
  
  • Musa alikataliwa na watu wake. Walimwambia: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. (Kutoka 2:14).
  •  
 Kisha aliondoka na kwenda nchi ya Midiani. Huko alioa mke ambaye hakuwa Mwisraeli. (Tazama: Kut. 2:16-21). Lakini baada ya hapo alirudi tena Misri na kuwatoa Israeli utumwani. Yesu naye alikataliwa na watu wake. Imeandikwa: Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. (Yohana 1:11). Ni jambo lililo wazi kuwa hadi sasa Wayahudi hawamtambui Yesu kama Masihi wao. Lakini kama ilivyokuwa kwa Musa, Bwana Yesu akatoka kwa hao walio wake akaja kwa Mataifa, yaani watu wengine wote wasio Wayahudi. Huko amejipatia na anaendelea kujipatia ‘bibi harusi’ – maana Kanisa la Yesu, kwa ujumla wake, linaitwa ni bibi harusi wa Bwana Yesu (Tazama 2 Wakorintho 11:2). Na tena imeandikwa: Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu.(Warumi 9:25). Lakini kabla ya kuingia Kanaani (yaani dunia kufika mwisho), Bwana Yesu, kama Musa, atamrudia Israeli. Imeandikwa: Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. (Warumi 11:25-26).  
  • Musa aliteua watu kumi na mbili akawatuma Kanaani. Imeandikwa: Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila. (Kumbukumbu 1:23). Bwana Yesu naye aliteua mitume kumi na mbili akawatuma. Imeandikwa: Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri.(Marko 3:14).

  • Musa aliteua watu sabini kwa ajili ya kusimama mbele za Bwana. Imeandikwa:  Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. (Hesabu 11:16). Bwana Yesu naye alifanya vivyo hivyo. Imeandikwa: Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. (Luka 10:1).

  • Musa alikuwa kuhani. Imeandikwa:  Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia (Zaburi 99:6). Bwana Yesu naye ni kuhani. Imeandikwa kumhusu Yeye kwamba: bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. (Waebrania 7:24).

  • Musa aliwapa watu wake maji katikati ya jangwa. Imeandikwa: Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. (Hesabu 20:11). Yesu naye anafanya jambo lilelile. Imeandikwa:  Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.(Yohana 7:37).

  • Musa alibeba dhambi ya watu wake, hivyo akaadhibiwa yeye kwa niaba yao. Imeandikwa: Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao (Zaburi 106:32). Kila mtu anafahamu kuwa Bwana wetu Yesu naye alibeba dhambi ya ulimwengu wote. Aliadhibiwa kwa niaba yetu. Imeandikwa: Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. (Isaya 53:5-6).
  •  
 Tungeweza kuendelea zaidi na zaidi, lakini mifano hii michache inatosha kuonyesha kwamba kweli Musa alikuwa ni mfano wa nabii aliyekuwa anasubiriwa. Alikuwa ni mfano kwa sababu yeye alikuwa akitenda wajibu wake kimwili, ilhali Yule aliyekuwa anasubiriwa angeyatenda kiroho, ambalo hasa ndilo kusudi la Mungu. 
  1. Maneno ‘nitatia maneno yangu kinywani mwake’
  2.  
Nabii Yeremia anasema: Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako (Yeremia 1:9). Kwa hiyo, kama Kumbukumbu 18:18 inahusu nabii ambaye Mungu aliweka neno kinywani mwake, kwa nini tudhani kuwa ni Muhammad, ambaye ni mgeni wa mbali, na si Yeremia ambaye ni Mwisraeli? Vipi kuhusu Isaya?

Imeandikwa: Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu. (Isaya 51:16).
 Kila nabii wa kweli wa Mungu alisema maneno ambayo Mungu aliyatia ndani yake. Hayakuwa ni maneno yao waliyotunga; wala hayakuwa ni maneno waliyoenda kuyasomea kwenye shule au vyuo fulani. Yalikuwa ni maneno ambayo Roho wa Mungu alikuwa anasema kutokea ndani yao. Kwa kifupi ni kuwa, maneno haya hayamtambulishi Muhammad kamwe. Kwa nini asiwe Yeremia? Kwa nini asiwe Isaya? Lakini Bwana Yesu naye anasemaje?  Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. (Yohana 17:8). Kwa hiyo, kama ambavyo Deedat alimpa changamoto yule mchungaji kwamba Uyahudi na unabii unaweza kumhusu nabii yeyote, si lazima awe Yesu, kanuni ileile inamfunga yeye. Kuwekewa maneno kinywani kunaweza kumhusu nabii yeyote na wala huo si ushahidi kwamba anayesemwa ni Muhammad. Na haiingii akilini kwamba Mungu ambaye ametumia maelfu ya miaka kuandaa hili taifa teule aje aishie kumweka mgeni juu yao!! 
  1. Maneno ‘sina maarifa’
  2.  
Nabii Isaya ameandika kwamba: Kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi (Isaya 29:12). Waislamu walipoona andiko hili wakadhani kuwa tayari wameshapata ushahidi kuwa Muhammad ametabiriwa kwenye Biblia kwa kuwa Muhammad alikuwa ni mtu ambaye hakuwa amesoma. Ukifuatilia sura nzima ya 29 na mantiki iliyozaa mstari huu wa 12, unaweza kuishia kucheka tu, ingawaje hili si jambo la kucheka. Wanachofanya Waislamu ni upotovu mkubwa ambao unaangamiza mamilioni ya watu wa Mungu milele katika jehanamu ya moto. Watu wanaaminishwa uongo na wao wanaukumbatia kana kwamba ni ukweli. Kwa ujumla, ukisoma sura ya 29 ni sura ambayo inatamka hukumu juu ya Ariel (Yerusalemu) kutokana na uasi wao juu ya sheria na maagizo ya Mungu, Yehova.

Hebu tusome sura hiyo kwa karibu:
 1  Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake, 2  ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli. 3  Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke. 4  Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini; na sauti yako itakuwa kama sauti ya mtu mwenye pepo, ikitoka katika nchi, na matamko yako yatanong'ona toka mavumbini. 5  Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi membamba, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafula. 6  Naye atajiliwa na Bwana wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sautikuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao. 7  Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, nao wamwudhio, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku. 8  Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni. 9  Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewaya-waya wala si kwa sababu ya kileo. 10  Kwa maana Bwana amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji. Maneno yaliyo katika wino mwekundu ndizo hukumu zenyewe. Mbali na hukumu hizo hapo juu, Mungu bado akaendelea kusema kuwa, kutokana na uasi wao, hata neno lake hawatalielewa. Yaani hawataweza kusikia au kujua Mungu anasema nini hata kama watasoma au kusikia neno lake. Hii ni pamoja na wale ambao ndio wanatarajiwa kuwa wenye kuelewa neno hili – yaani manabii na waonaji – ukiachilia mbali wale wasio na maarifa juu ya neno la Mungu, yaani watu wa kawaida. Kwa hiyo, anaendelea kusema: 11  Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri; 12  kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi. Sasa basi, kama kweli Muhammad ndiye anayetajwa kwenye Isaya 29:12, kimantiki ina maana kuwa yeye ni kati ya wasioelewa lolote kwa kuwa wako chini ya hukumu ya Mungu; maana kama tulivyoona, sura hii ni tamko la hukumu ya Mungu kutokana na uasi. Si vibaya hata hivyo! Ndiyo maana nikasema kwamba unaposoma hoja hii ya Waislamu unaweza kuishia kucheka tu.

Hata hivyo, kwa kuwa sasa Muhammad ni nabii asiyeelewa chochote kutokana na kuwa chini ya hukumu ya Mungu kulingana na mantiki ya andiko hili, maana yake ni kuwa ujumbe alioleta kwa wanadamu hautoki kwa Mungu aliyeumba mbingu na nchi. Ndiyo! Labda kama, kwa makusudi tu, hutaki mantiki iliyopo. Kwa nini basi umfuate mtu wa namna hiyo?
 
*******************
 Enyi Waislamu, swali langu hapa ni moja. Kwa mtu yeyote anayependa kweli atatambua kwamba Kumbukumbu la Torati 18:18 au Isaya 29:12 hazimhusu Muhammad hata kidogo licha ya kwamba Wanazuoni wa Kiislamu kwa makundi wanajaribu kuwaambia hivyo. 

Shida moja kubwa kuhusiana na maarifa ya aina yoyote ni pale unapokuwa mtu wa kumeza tu kila unachoambiwa bila kuchunguza ukweli wa mambo. Hata haya ambayo mimi nimekuambia katika makala haya, itakuwa ni vema usiyameze tu. Fanya uchunguzi wako mwenyewe juu ya ukweli na uongo wa hoja za pande zote mbili. Kama wanazuoni wanasema kweli, basi shika kweli. Kama makala haya yanasema kweli, basi shindana na hofu yako na ukatae uongo. 

Sasa, swali langu ni kwamba, kama kweli Allah amesema kuwa Muhammad ametajwa katika Torati na Injili wakati sio kweli, hiyo maana yake nini? Kazi kwako! 

Yesu anakupenda. Njoo kwa Yesu kungali mapema. Hakuna wokovu nje ya Yesu. Jitihada zako zote unazofanya kujaribu kumpendeza Mungu wakati huna Yesu nina uhakika asilimia mia moja kuwa hujafanikiwa. Na kila unapojitahidi, unajikuta unatafunwa na hatia na hofu moyoni mwako. Hauko tayari kukiri hilo wazi, lakini huwezi kuudanganya moyo wako. Moyo wako unajua wazi kwamba umeshindwa vibaya sana! 

Na kadiri unavyozidi kumkataa Yesu, kushindwa kwako huko kuishi maisha matakatifu ndilo litakuwa fungu lako hadi mwisho. Yesu anakupenda MNO! Alikufa kwa ajili yako.

Njoo kwa Yesu sasa.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW