“Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa Na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango WA hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu.” (matendo ya mitume 3:1-8)
Ukifuatilia historia ya kilema huyu aliyeponywa utaona ya kuwa alikuwa hivyo tangu kuzaliwa, na alipopona alikuwa na umri uliopita miaka arobaini (matendo ya mitume 4:22)
Siri ya muujiza huu ilikuwa ni nini? Je! Kilema huyo alipona kwa uwezo wa petro na yohana au kwa uweza wa Jina la Yesu Kristo! Nauliza maswali haya kwa kuwa watu wengi wakiona mtu anatumiwa na Mungu katika uponyaji wanaweka imani zao kwa huyo mtumishi badala ya kuweka imani zao katika Jina la Yesu Kristo!
Na ndivyo ilivyokuwa wakati kilema huyu alipopona, watu waliokuwa hekaluni waliwashangaa akina petro na yohana kama vile kilema alipona kwa uwezo wao. Petro alipoona hali hiyo aliamua kuwaeleza watu haoukweli ulivyo, akasema; “Basi alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi?” (Matendo ya mitume 3:11-12).
Petro alikuwa anafanya jambo muhimu hapakwa kusaidia kubadilisha mawazo ya watu ya kufikiria kuwa uwezo uliomponya yule kilema ulikuwa ni wa petro na yohana ambayo haikuwa kweli. Kama uwezo huu haukuwa wao, muujiza huu siri yake ni nini? Petro aliendelea kusema hivi, “Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote.” (Matendo 3:13-16)
Hebu tafakari maneno haya ya petro, “Na kwa IMANI KATIKA JINA LAKE, JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU…” wakina petro na yohana waliweka imani zao katika Jina la Yesu Kristo. Walikuwa na uhakika mioyoni mwao kuwa siri ya muujiza imo katika jina la yesu kristo – ndiyo maana walopomkuta huyo kilema walimwamuru asimame kwa jina hilo!
Weka imani yako katika Jina la Yesu Kristo ukitaka kuona ishara na miujiza ya Yesu Kristo maishani mwako na kwa wale unaowahudumia. Wakijua hili wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo walipokatazwa kuwa wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu Kristo na kuhani mkuu Anasi, waliomba wakisema, “….Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa JINA LA MTUMISHI WAKO MTAKATIFU YESU.” (matendo 4:18,29-31)
Ni muhimu kuwaeleza watu umuhimu wa kuweka imani zao katika Jina la yesu Kristo wakitaka kuona mkono wa Bwana ukiponya na kuokoa, ukifanya ishara na miujiza.
Nakumbuka kuna mama mmoja alifika nyumbani kwangu akiwa anaumwa sana toka nje ya mkoa huu wa Arusha ninaokaa. Baada ya mahojiano naye nilifahamu ya kuwa ameugua bila kupona kwa muda wa miaka miwili. Na katika hiyo miaka miwili amezunguka kwa watu mbalimbali kuombewa bila mafanikio. Alipoona haponi akaenda kwa waganga wa kienyeji ambako nako hakupona. Alipoona kwa waganga wa kienyeji haponi, akaanza kutafuta watumishi tena ili wamwombee.
Katika mazungumzo hayo nilitambua kuwa anapokwenda kuombewa anaweka imani yake katika watu wanaomwombea na wala haweki imani yake katika jina la Jina Yesu Kristo.
Nilifungua biblia yangu na nikaanza kuzungumza naye juu ya uweza wa jina la Yesu Kristo, na umuhimu way eye kuweka imani yake katika jina la , na umuhimu wa yeye kuweka imani yake katika jina la Yesu Kristo na siyo kwangu. Mwishoni nikamwuliza kama ameelewa na ikiwa yuko tayari kwa maombi kwa kulitumia jina la Yesu Kristo. Yule mama akajibu akasema; “ndiyo nipo tayari kwa kuombewa, naamini kwa jina la Yesu Kristo nitapokea uponyaji”
Mara nilipoanza kuomba, aliangushwa chini na mapepo yaliyojidhihirisha toka ndani mwake. Nikayaamuru mapepo hayo yamtoke yule mama kwa Jina la Yesu Kristo- na mara hiyo yakamtoka yule mama na akawa mzima.
Ugonjwa uliomsumbua kwa muda wa miaka miwili ulitoweka, yule mama pamoja na mume wake aliyemsindikiza waliondoka kwa furaha huku wakimsifu Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea. Kumbuka petro alisema, “kwa IMANI KATIKA JINA LAKE (YESU), JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU…”
No comments:
Post a Comment