Wednesday, September 28, 2016

MBINGUNI, PEPONI, KUZIMU NA JEHANNAM NI WAPI?




Mpendwa mmoja aliniuliza maswali yafuatayo ambayo nimeona ni muhimu niyajibu kama Makala fupi kwa ajili hata ya faida ya watu wengine wenye maswali kama haya:


Swali la 1: Hivi watu wakifa, roho zao zinakuwa wapi hasa?
Swali la 2: Roho hizo zinakuwa katika hali gani hasa?



WATU WAKIFA, ROHO ZAO ZINAKUWA WAPI?


Biblia inasema kuhusu Bwana Yesu kuwa:

Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; (Wafilipi 2:9-10).


Kulingana na mstari huu, tunagundua kuwa kuna sehemu kuu tatu:
                                                 Mbinguni
                                                 Duniani
                                                 Chini ya nchi


Mbinguni ni mahali aliko Mungu; duniani ni mahali tuliko sisi wanadamu tulio hai; na chini ya nchi ni mahali aliko ibilisi.


Tangu nyakati za Adamu kulikuwapo wanadamu wema na waovu. Wanadamu wema walikufa na waovu nao walikufa. Swali ni kuwa, je, walipokufa walienda wapi?


Mwinjilisti Luka anatupatia picha nzuri kutokana na kisa alichosimulia Bwana Yesu juu ya tajiri na Lazaro. Tunasoma katika Luke 16:22-26:


22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.


23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.


24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.


25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.


26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.


Tunachoona hapani kuwa Lazaro alikuwa ni mwenye haki kama Ibrahimu na tajiri alikuwa ni asiye na haki. Hawa walikaa sehemu mbili tofauti, maana zilitenganishwa na bonde. Sehemu hizi zote mbili zilikuwa chini ya nchi.


Kabla ya Yesu kufa, wanadamu wote walipokufa walienda chini ya nchi. Na huko kulikuwa na sehemu mbili – kwa shetani na kifuani mwa Ibrahimu. Katika habari hii ya tajiri na Lazaro – ambayo ilitokea zamani sana hata kabla ya Musa, Bwana Yesu anatuonyesha kuwa tajiri alikuwa kwenye mateso; na Lazaro alikuwa penye raha.


Lakini mtu anaweza kusema hivi, “Huoni kuwa tajiri aliinua macho yake? Je, hii si ishara kuwa Lazaro na Ibrahimu walikuwa mbinguni?


Wakati huo mbingu zilikuwa hazijafunguliwa kwa ajili ya wanadamu. Tuendelee kusoma na hapo mbele tutapata jibu la maswali hayo.


Bwana alipokuja duniani, akateswa na akauawa, tunaambiwa kuwa:


Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri. (1Petro 3:18-19) 


Mbinguni hakuna vifungo; vifungo viko chini ya nchi. Kwa hiyo, Bwana alienda kuwahubiria waliokuwa kifungoni.


Bila shaka hii ndiyo sehemu ambayo Wakatoliki huita toharani. Sehemu hii ilikuwapo zamani kama makao ya muda kwa wale waliokufa kabla ya Kristo. Humo waliwekwa kungojea ukombozi wa mwanadamu ufanye na Kristo. Lakini sasa hivi haipo tena.


Maana ya andiko hili katika Petro ni kuwa, wale waliokuwa kifuani mwa Ibrahimu (au tuseme toharani), Bwana alienda akawahubiria katika zile siku tatu alipokuwa katika tumbo la nchi.


Je, baada ya kuwahubiria, nini kilifuata?


Imeandikwa:
Hivyo husema, alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi? (Efe 4:8) 


Shetani alikuwa amewashikilia wanadamu wote kuzimu, lakini Bwana akaenda akawateka na kuondoka ndao. Na ndiyo maana kabla Bwana hajafa, alisema:


Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. (Mathayo 12:29)


Na ushahidi wa jambo hili uko wazi kwa sababu Biblia inatuambia kwamba baada ya Bwana kufa, watakatifu waliokuwa wamekufa zamani walionekana Yerusalemu.

Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. (Mat 27:50-53) 


Je, alipoteka mateka aliwapeleka wapi?


Imeandikwa kuhusu yule mwizi aliyesulubiwa pamoja na Bwana:

Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja namipeponi. (Luka 23:42-43) 

Ukisoma kwenye Kiingereza, imeandikwa hivi: And Jesus said unto him, Verily I say unto thee, To day shalt thou be with me in paradise. Peponi ndio paradiso.


Paradiso si Yerusalemu Mpya. Paradiso ni makao ya muda kwa ajili ya watakatifu, kusubiria mwisho wa mambo yote ambapo Yerusalemu mpya itafunguliwa na kuwa makao ya milele pamoja na Bwana.


Kama ambavyo watakatifu wako kwenye makao ya muda paradiso, ndivyo ambavyo na wenye dhambi wako kwenye makao ya muda kuzimu aliko shetani sasa – maana shetani hayuko jehanamu bado. Yaani, wako kule alikokuwa yule tajiri aliyezungumza na Ibrahimu kuhusiana na Lazaro kutumwa duniani.


Pia tunasoma kuwa:
Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu. (2Petro 2:4) 

Hawa mashetani wako kifungoni lakini kumbe wala hiyo si hukumu bado. Ndiyo maana anasema wako pale hata ije hukumu. Itakapofika sasa mwisho wa mambo yote, ndipo kila mtu ataenda sasa kwenye makao ya milele.

Biblia inasema kuhusu wakati huo:
Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; (Mat 25:34) 


Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; (Mat 25:41).


Kumbe moto wa milele ndiyo hukumu ya mwisho iliyotajwa hapo juu. 


Hata tukisoma kwenye Ufunuo imeandikwa: Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberitiHii ndiyo mauti ya pili. (Ufu 21:8) 


Kwa nini inaitwa mauti ya pili? Ni kwa sababu japo tajiri yuko kwenye mateso na hayuko duniani tena (yaani alishakufa); japo wale malaika walio kifungoni wako kwenye mateso sasa; lakini iko mauti nyingine tofauti nay a sasa. Kitendo cha kutupwa kwenye ziwa la moto (jehanamu) na kubaki humo milele ndicho kinachoitwa mauti ya pili.


Hata roho hii ya mauti inayotutoa duniani sasa pamoja na kuzimu aliko shetani sasa navyo vitaingia jehanamu kwenye mauti ya pili:


Imeandikwa: Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. (Ufu 20:14) 


JE, ROHO ZILIZOONDOKA DUNIANI ZINAKUWA KATIKA HALI GANI?
Hawa ni watu kamili kama tulivyo sisi. Sisi kama roho tumo ndani ya mwili wa nyama, lakini ukivua mwili huu (yaani, ukifa) unavikwa mwili wa kiroho; na unaendelea kuishi kama kawaida.

Biblia inasema: Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. (1Kor 15:40) 

Tofauti ni majukumu tu. Huku tunafanya kazi, tunasafiri, n.k. Lakini kule wenye dhambi wanateswa na watakatifu wanamfurahia Yesu, kwa mfano kwa kusifu.

HITIMISHO
Kuzimu ni mahali aliko shetani sasa hivi pamoja na wanadamu wote wanaokufa katika dhambi. Haya ndiyo makao makuu ya uovu wote unaoendelea duniani leo. Baada ya mambo yote, yaani mwisho wa nyakati, kuzimu na kila kilichomo ndani yake vitatupwa kwenye ziwa la moto wa milele.

Wanadamu wanaokufa ndani ya Yesu wako paradise sasa hivi. Baada ya mwisho wa mambo yote, wataingia Yerusalemu mpya na kuishi pamoja na Bwana milele na milele.

Usipange kukosa kuingia Yerusalemu Mpya!

1 comment:

Memalo said...

Nimefahamu sasa tofauti kati ya Mbinguni,peponi,kuzimu naJehanam, asante kwa ufafanuzi mzuri.

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW