Na maisha ya mwanadamu yamefikia mawazo ya hali ya juu. Wengi wetu wanapenda kuishi katika dunia hii kwa muda mrefu iwezekanavyo. Baadhi yao wanategemeo la kuishi milele katika dunia hii.
Lakini kuna njia moja tu ya kumuingiza mtu katika furaha ya kweli ya milele. Kuna ukweli mmoja tu, umfanyao mtu kuwa huru. Kuna namna moja ya maisha itakayomfikisha mtu katika uzima wa milele. Yesu Kristo Mwana wa Mungu, ndiyo “Njia, na Kweli na Uzima.” Kumbuka Yesu mwenyewe alisema, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya Mimi,” Yoh. 14:6.
Na Yesu Kristo ni “Njia na Kweli na Uzima.” Kwa sababu Yeye alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Wote wametenda dhambi kwa kuiasi Sheria ya Mungu (Rum 3:23; 1 Yoh 3:4). “Na mshahara wa dhambi ni mauti,” Rum 6:23. Hii ndiyo mauti ya pili au Jehanamu (Ufu. 21:8; Mat. 10:28). Kwa sababu ya dhambi zetu tulistahili adhabu ya milele katika Jehanamu, lakini kwa sababu ya upendo mkuu wa Mungu na rehema zake alimtoa mwanawe Yesu Kristo akafa msalabani akalipa deni letu la dhambi zetu (Yoh. 3:16-17; Rum. 5:5-10; 6:17-23).
Yesu ni “Njia na Kweli na Uzima.” Kwa sababu Yeye alifufuka kutoka kaburini. Kabla hajaja Yesu Kristo, kaburi la giza la mauti lilikuwa likitungojea mwisho wa safari yetu pasipo tumaini. Lakini Yesu alishinda kifo akafufuka toka kaburini. Yesu alishinda mauti. Yeye atatupa ushindi juu ya mauti wale tunaompokea na kumtii (1 Kor 15:20-23; Ufu. 1:17-18). Yesu alisema, “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima: yeye aniaminie
mimi, ajapokufa atakuwa anaishi,” Yoh 11:25.
Yesu ni “Njia, Ukweli na Uzima,” kwa sababu Yeye atawahukumu watu wote siku ya mwisho (Mdo. 17:30-31). Kila mtu atasimama mbele ya Yesu Kristo na atatoa hesabu ya matendo yake aliyoyafanya wakati wa maisha ya hapa duniani. Mtume Paulo kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu aliandika hivi: “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda kwamba ni mema au mabaya,” 2 Kor. 5:10.
Yesu ndiye njia pekee ya kwenda mbinguni. Yesu peke yake ndiye kweli. Hakuna atakayepata uzima wa milele isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo. Ili mtu apokee baraka zitolewazo na yesu mwenyewe, ni sharti awe amuamini Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Kumbuka Yesu alisema “....Msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu,” Yoh. 8:24. Pia inampasa kutubia dhambi zake, Yesu alisema
nawaambia; “Sivyo msipotubu ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk. 13:3. Mtu hawezi kupokea baraka zitolewazo na Yesu Kristo iwapo atamuonea haya. Maana Yesu alisema,
“Yeye atakayenikiri mbele za watu nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye Mbinguni, bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye Mbinguni,” Mat. 10:32-33. Pia inampasa mtu abatizwe katika kristo ili apokee msamaha wa dhambi na baraka. Kumbuka Yesu alisema, “Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiye amini atahukumiwa,” Marko 16:16.
Yesu Kristo Mwana wa Mungu hakika ndiye, “Njia na Kweli na Uzima.” Hakuna atakaye okoka isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo. Kama ukimwamini Yesu leo na kumtii ujue ya kuwa furaha na amani na uzima vita kuwa vyako; sio katika ulimwengu huu tu, bali na katika ulimwengu ule ujao.
No comments:
Post a Comment