Huko motoni Jehanum kukoje? Mwanangu, kunatisha, nashindwa hata nikueleze vipi unielewe. Moto wa milele, hatukuwekewa wanadamu bali shetani na malaika zake (MATHAYO 25:41). Kama utakwenda huko baada ya kusoma “note” hii, itakuwa ni kwa sababu ya kiburi chako tu, na kushupaza shingo yako na kukataa kulitendea kazi Neno hili (MITHALI 29:1). Moto wa Jehanum siyo mahali pa mchezo kama walimu wa uongo wanavyofundisha. Walimu hawa huwafariji watu na kusema eti mtu ataunguzwa na moto na kutoweshwa na kupotea na kuangamizwa kabisa na ndiyo mwisho wake. Wanatumia maandiko kama MATHAYO 10:28 (kuangamizwa) na YOHANA 3:16 (Kupotea). Kuangamia katika maandiko hakumaanishi kumalizika kabisa, bali kukabiliwa na mauti (ESTA 4:16). Mauti ya watu walioko motoni, ni mauti ya milele, kama tutakavyoona hivi punde. Kondoo akipotea, haimaanishi hayupo kabisa ila ametengwa na mchungaji (ISAYA 57:1-3).
Biblia inaeleza waziwazi kwamba mtu anapokufa, sekunde ileile ya kufa kwake anakabiliwa na hukumu. Tunasoma katika WAEBRANIA 9:27, ”Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”. Watu wanapofundisha kinyume na kweli ya Neno la Mungu, hufundisha kwamba mtu anapokufa analala tu, na hakuna lolote la hukumu mara moja wakitumia maandiko yafuatayo na kuyatafsiri visivyo – MATHAYO 27:52; 1 WAKORINTHO 15:20; YOHANA 11:11-14 n.k; na pia wanasema wafu hawajui lolote kwa kutumia maandiko kama MHUBIRI 9:5. Ilivyo ni kwamba, kinachobaki kaburini ni mwili tu. Roho ya mtu huondoka na kuingia katika mwili mwingine, unaoitwa mwili wa roho. Miili tuliyo nayo wanadamu kabla ya kufa inaitwa miili ya asili. Tunasoma katika 1 WAKORINTHO 15:40, 44, “Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani,……Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko”.
"Na miale ya moto huwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari njema ya Bwana ya Yesu. Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu" - (2 Wathesalonike 1:8,9).
Moto wa Jehanum ni mkali sana kuliko moto wowote tunaoufahamu duniani. Moto wa gesi wa kuunganishia vyuma, unaotokana na kuwashwa mchanganyiko wa gesi ya “Oxygen”, na “Acetylene”, unaonekana kwa hapa duniani kwamba ni mkali. Moto huu, siyo chochote, ukilinganishwa na moto wa Jehanum. Katika karakana au viwanda vya vifaa vya vyuma, chuma huyeyushwa na kuwa uji katika matanuru ya moto mkali unaofikia nyuzi joto 2,000 hadi 3,000 na zaidi. Moto huu unaoyeyusha vyuma na ukali wake, huo si chochote! (Kumbuka kwamba maji yaliyochemka sana hufikia nyuzi joto 100 tu!) Moto ulio katikati ya jua linalotuangaza, unafikia nyuzi joto milioni kumi (10,000,000°C). Moto wa jua nao, si chochote ukilinganishwa na moto wa Jehanum! Ukali wa moto wa Jehanum, unatisha (WAEBRANIA 10:26-27). Siyo hilo tu, moto wa duniani una rangi mbalimbali, njano,bluu,mwekundu n.k. Moto wa Jehanum ni tofauti kabisa; Ni moto wa rangi nyeusi, unaosababisha giza na kumfanya mtu aliye motoni, awaone wenzake wachache tu wa karibu naye, hivyo hamna faraja ya kusema “tuko wengi!” Moto huu mweusi, ndiyo maana unaitwa “giza la nje” (MATHAYO 8:11-12, MATHAYO 22:13; MATHAYO 25:30; YUDA 1:6). Siyo hilo tu. Moto huu wa Jehanum, una meno! Hivyo una uwezo wa kuwala na kuwatafuna walioko motoni (KUMBUKUMBU 32: 22; WAEBRANIA 10: 26-27). Hata hivyo, pamoja na moto huu kumtafuna mtu, bado una sifa ya kumhifadhi mtu huyo na kumfanya asimalizike, kama jinsi chumvi ilivyo na uwezo wa kuizua nyama kuharibika. Hivyo moto unamtafuna mtu wakati wote, lakini haishi na wala moto wenyewe hauzimiki. Ndiyo maana unaitwa moto wa milele (MARKO 9: 43-49; MATHAYO 25:41).
Watu walioko motoni, hutamani mtu mmoja kati yao atoke motoni aje duniani, awashuhudie ndugu zao, ili waache dhambi, na kukwepa mateso yao, lakini huambiwa kwamba ndugu zao wanapaswa kuyasikia maneno ya manabii walioko duniani, maana hata akitumwa mtu kutoka motoni na kueleza mateso ya huko, watasema ni mwongo, hajaenda motoni. Tunasoma haya katika LUKA 16:27-31, ”Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie,wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, wanao Musa na manabii, wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa (hawatashawishika) hata mtu akifufuka katika wafu”.
Mpendwa msomaji, ikiwa mama yako mzazi alifariki akiwa hajaokoka, ujue yuko motoni, na anakuambia, “Usinifuate huku mwanangu”. Ikiwa baba yako mzazi alifariki akiwa dhambini, anateseka motoni, na hataki umfuate huko aliko! Ndugu, marafiki na jamaa zako walioko huko wanakukumbuka sana, na hawapendi ujiunge nao huko, bali wanataka utubu na kuokoka mateso hayo ya moto. Walioko huko motoni, wakimwona yeyote mwingine kutoka duniani, ambaye alikuwa na nafasi ya kusikia habari kama hizi na akazipuuza, kisha akawafuata huko motoni, humwambia, “Je wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! ” (ISAYA 14: 10).