Katika sehemu ya kwanza ya ushuhuda huu wa Nabeel, aliyekuwa Mwislamu kisha akakutana na Bwana Yesu na kupokea wokovu, tuliona jinsi ambavyo alimwomba Mungu ampe maono yatakayomwonyesha imani ya kweli. Alionyeshwa misalaba kwenye maono lakini yeye akasema labda ni macho yake tu yamemchezea mchezo. Kwa hiyo, alimwomba tena Mungu kwamba, kama yale maono yalitoka kwake, basi ayathibitishe kwa ndoto. Je, Mungu alifanya nini? Tafadhali endelea kusoma sehemu hii ya pili.
…………………………………
Mungu alinipatia ndoto ile kwa uwazi sana kiasi kwamba sikuwa na ulazima wa kuitafsiri. Lakini ilikuwa wazi hata zaidi kuliko nilivyotarajia. Saa chache baadaye niliwasiliana na David na kumwambia kuwa nimeota hivi na hivi.
David aliniambia, “Sina ulazima wa kutoa maoni yangu juu ya hilo. Kila kitu kiko kwenye Biblia.”
Nikasema, “Unasemaje?”
Akasema, “Nenda kwenye Luka 13.”
Nilienda kwenye Luka 13 mstari wa 22 hadi 29. Niliposoma nikakuta kumeandikwa kuhusu kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, na Kristo akasema kwamba, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. Jitahidini kuingia kupitia mlango mwembamba. Na watu watakuwa wamesimama kwenye mlango huo wakibisha hodi.
Na hicho hasa ndicho kilichotokea kwenye ndoto yangu. Nilikuwa kwenye huo mlango ambao ulikuwa haujafungwa bado. Fursa ya mimi kuingia humo kwenye kushiriki sherehe ile ilikuwa bado ipo. Nilichotakiwa tu kufanya ni kukubali mwito.
Papo hapo nilitambua kile ninachotakiwa kufanya. Nilibaini kwamba Uislamu haukuwa ile kweli. Mungu alikuwa ananivuta nitoke humo. Japokuwa mimi nilikuwa siko tayari, lakini aliendelea kunivuta.
Ikawa ni kama naingia kwenye majonzi na msiba. Nilikuwa nalia ninapoelekea shuleni. Siku moja nikamwambia Mungu, “Mungu, nipe tu siku chache ili niomboleze. Nahitahi kuomboleza, maana nina watu wengi ambao nitawapoteza.”
Niliporudi kwenye chumba changu, nilifungua Quran na hakukuwa na kitu cha kunisaidia humo. Nilifungua Biblia kwenye kitabu cha Mathayo, na kabla hata sijamaliza sura ya 5, nikakutana na maneno: Heri wenye huzuni; maana maana hao watafarijika. Na nikasoma Ayubu, na uchungu wote niliokuwa nao ukaisha. Lakini kwenye Quran sikuwa na msaada wowote! Quran ilikuwa ikinipa tu maelezo ya mambo ya zamani, lakini hakuna kitu cha kunisaida sasa. Hakuna kabisa! Lakini kila mara nilipofungua Biblia, msaada ulikuwa pale.
Ninamwomba Mungu kitu halafu namwuliza, “Nitajuaje kuwa nitapata hiki?” Kisha ninafungua 1 Yohana 5:14-15 na inasema: Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba – maana tunaamini mioyoni mwetu kwamba Yesu ni Bwana. Niliamini moyoni mwangu kwamba Kristo ni Bwana lakini sikuwa nimekiri.
Warumi 10 nayo inasema kitu hichohicho. Inasema: Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Na mimi nilikuwa sijafanya hivyo.
Kisha akili yangu ilifunguka nilipokuwa nasoma kwenye Mathayo, inaposema: Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Na pia inasema: Bali, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Ilikuwa ni hapo ndipo sikuweza kumkana Kristo tena! Sikuweza kumkana Mungu tena! Sikuendelea kushikilia tena maisha yangu na mitazamo yangu ambayo nilikuwa nayo, si kwa sababu niliamini, bali kwa vile tu nilizaliwa na kukua katika hiyo. Nilianza kutambua kwamba ile haikuwa kweli na nikaanza kumkubali Kristo maishani mwangu.
Nilimwomba Roho Mtakatifu anibadilishe maisha yangu. Na baada ya kuomba sala ile, ulimwengu wote ukawa tofauti. Niliposema maneno yale, nilishtushwa kana kwamba nimepigwa shoti ya umeme. Yalikuwa ni maneno tu, lakini yalikuwa ni maombi ambayo Mungu aliyatimiza.
Na Roho Mtakatifu alipoingia ndani yangu wakati huo, nikawa nimeshikwa kwa dakika zipatazo kumi kama mtu aliyenaswa na umeme. Kwa dakika kumi nilikuwa siwezi hata kusogea! Na pale nilipoweza kusogea, niliutazama ulimwengu ulionizunguka na ulikuwa mzuri sana! Kulikuwa kumejaa matumaini; kulikuwa kumejaa maana! Nilitambua nini maana ya maisha.
Si suala tu la kuishi kama mtu mwema - ni kweli unatakiwa kufanya hivyo. Lakini lengo la msingi kabisa la maisha yetu ni kumsifu na kumwabudu Mungu mmoja wa kweli, aliyekuja kwenye ulimwengu huu, na kufa kwa ajili ya dhambi zetu ili tuweze kuona jinsi anavyotujali; ili tuweze kumwabudu Yeye kikamilifu, kwa furaha – kama ambavyo Paulo anasema kwenye Wafilipi: Furahini wakati wote – maana Mungu yuko karibu.
Maisha yangu yalikuwa na maana sasa, maana nilikuwa sasa naweza kwenda nje na kuhubiri. Haikuwa ni kukaa tu na kusema, “Kila mtu anayefanya mema, atakwenda mbinguni.” Hapana! Sasa kulikuwa na suala la kwamba, watu wanahitaji kujua Mungu ni nani; na nini amefanya. Watu wanahitaji kujua nafasi yetu ni nini kwa habari ya uhusiano wetu na Mungu; wanatakiwa kujua kuwa tunatakiwa kumwabudu Mungu mmoja wa kweli na Mwanawe, Yesu Kristo ambaye alikuja kufa kwa ajili ya dhabi zetu.
Tunatakiwa kuwaambia watu kuwa, ndiyo, Mungu ni mmoja. Hata hivyo, Yeye ni mmoja katika Utatu, na Utatu katika mmoja. Iwe tunaweza kuelewa hilo au hatuwezi, ni jambo lililo nje ya uwezo wetu. Si lazima tuelewe. Cha msingi ni kujua tu kuwa Yesu ni Mungu; kwamba Mungu aliamua kuja duniani kama mtu.
Waislamu wanaona kuwa hilo haliwezekani. Hakuna sababu ya hilo kutowezekana. Mungu anaweza kuamua kuja duniani kama mtu. Nionyeshe kwenye Quran panaposema kwamba Mungu hawezi. Badala yake, Quran inaonyesha kuwa Mungu anaweza kufanya chochote atakacho.
Siku ya mwisho, ya kiama kama Quran inavyosema, tutahukumiwa. Hakuna mtu anayeweza kwenda mbinguni, hata Waislamu, kwa juhudi zake mwenyewe. Ni lazima iwe kwa neema ya Mungu. Hata mtume wa Uislamu alisema watu waombe msamaha kwa Mungu mara nyingi kwa siku maana hajui kama ataingia mbinguni au la. Ni kwa neema ya Mungu pekee.
Hiyo neema sasa, ambayo hata Waislamu nao wanaitegemea siku ya mwisho ili kuingia mbinguni, ni neema ileile ambayo Wakristo wanaitegemea. Tofauti tu ni kwamba, Wakristo wanaamini kuwa neema hiyo tayari ilishatolewa kwenye msalaba miaka 2000 iliyopita Mungu aliitoa hiyo neema kwa ajili yetu. Ni neema ileile, si nyingine tofauti, tunatakiwa tu kutafuta kwa mioyo yetu yote. Naamini kwamba yeyote anayemwomba Mungu kwa moyo ulio wazi aonyeshwe kweli, ataonyeshwa kweli!
…………………………………..
Mpendwa msomaji, umemsikia Nabeel jinsi alivyokuwa na shauku ya kumjua Mungu wa kweli. Mungu si kiziwi. Yeye hujibu haja na shauku za mioyo yetu za kutaka kumjua na kumpendeza. Kwa nini usimwambie akuonyeshe njia ya kweli? Yesu ni njia, kweli, na uzima. Hakuna mtu anayeweza kwenda mbinguni – hata kama ni Mkristo – kama hajamkaribisha Yesu kuwa Bwana na Mwokozi maishani mwake na moyoni mwake.
Tafakari.
Jihoji.
Chunguza mambo.
Kweli imo ndani yako.
No comments:
Post a Comment