Mutee'a Al-Fadi alikuwa ni Mwislamu mwenye msimamo mkali wa Wahabbi ambao alisomea kule Saudi Arabia. Lakini baada ya kukutana na upendo wa Yesu, moyo wake uligeuka kabisa na akaanza kuitafuta kweli iliko. Hatimaye alitambua kuwa Yesu ndiye Njia, Kweli na Uzima. Ufuatao ndio ushuhuda wake:
****************
Mimi nilikuwa Muislamu wa Wahabbi ambaye nilizaliwa na kulelewa kama Mwislamu nchini Saudi Arabia. Katika maisha yangu yote nilikuwa mfuasi mwaminifu wa Kiislamu ambaye nilifuata na kuishi mafundisho ya Uislamu katika kila eneo la maisha yangu. Mafundisho haya yalikuwa ni pamoja na imani:
- kwamba Uislamu ndio dini ya mwisho duniani;
- kwamba ndiyo dini pekee inayokubalika kwa Mungu;
- kwamba ndiyo njia ya kwenda Mbinguni;
- kwamba wale wasioukubali Uislamu wanakwenda jehanamu na kwamba matendo na ibada zao hazitawaokoa hadi watakapomkubali Allah kama Mungu wao na Muhammad kama mtume wake;
- kwamba wokovu kwa Mwislamu ni kwa njia ya matendo mema na hauna uhakika isipokuwa kwa wale walio tayari kufa kwa jina la Allah;
- kwamba Waislamu ni watu bora kuliko wengine;
- kwamba watu wote wasio Waislamu ni makafiri, ikiwa ni pamoja na Wakristo;
- kwamba Kristo alikuwa ni mwanadamu tu na nabii aliyetumwa na Allah;
- kwamba yeye si Mungu au Mwana wa Mungu;
- kwamba hakuwahi kusulubiwa, kufa msalabani au kufufuka kutoka kwa wafu;
- kwamba Yesu alipaishwa Mbinguni ili kuokolewa dhidi ya waliotaka kumuua na
- kwamba Yesu atakuja tena siku za mwisho ili kuujenga upya Uislamu kama dini ya kweli ya Allah, kuharibu msalaba, kumuua mpinga-Kristo, na kuwafanya Wakristo wawe Waislamu.
Lakini jambo lenye nguvu zaidi ambalo nilijifunza katika makuzi yangu ni kuwa na CHUKI dhidi ya wale wote wasiomwabudu Allah; wasiomfuata Muhammad; wasioamini Uislamu – ikiwa ni pamoja na Wakristo na Wayahudi. Kwa lugha rahisi ni kwamba, nilikuwa adui wa Kristo.
Katika umri wa miaka 12, nilikuwa nimeshakariri nusu ya Qur’an. Lengo langu lilikuwa kukariri kitabu chote; maana huwa tunafundishwa kwamba kukariri Qur’an kunasaidia kufunika baadhi ya dhambi zako na kuboresha matendo yako mema Siku ya Hukumu; pia kunakupandisha daraja mbinguni.
Mapema mwaka 1980, nilikuwa niko tayari kufa kwa ajili ya jina la Mungu pamoja na kundi kubwa la vijana waliokuwa wanakwenda Afughanistani kupigana na Umoja wa Kisovieti tukiwa upande wa Osama Bin Laden (ambaye kwao alikuwa ni mtu wa kuigwa). Kama asingekuwa mama yangu kunisihi nisiondoke, ningeenda, maana niliamini kuwa thawabu za wale Waislamu wanaokufa kwa jina la Allah ni bora zaidi ya zile za Waislamu wasiokuwa tayari kupigana na kufa kwa ajili ya Allah – kama watafika mbinguni – lakini wale wanaokufa kwa ajili ya Allah wamehakikishiwa kuingia mbinguni na kusamehewa dhambi zao.
Lakini kadiri nilivyoendelea kukua, nilianza kutafakari na kuelewa lugha ya Qur’an zaidi. Na ndani yake niliona ujumbe wa chuki dhidi ya wasioamini, jambo ambalo sikujisikia amani nalo na sikulipenda kamwe; na wala sikuweza kulielewa au kulihalalisha. Sikuweza kuelewa kwa nini Mungu awe na chuki kiasi hicho dhidi ya viumbe wake mwenyewe kwa kuwa tu hawamkubali. Niliamini kuwa huruma na upendo wa Mungu vinatakiwa kuwa vikubwa zaidi ya hapo. Lakini kuzungumza na wengine kuhusu mawazo na mashaka yangu juu ya imani yangu kungenisababishia matatizo makubwa sana na kuhatarisha usalama wangu (maana adhabu ya mashaka na kufuru dhidi ya Allah na kuuacha Uislamu ni Kifo).
Baada ya kuhitimu chuo kule Saudi Arabia nilitamani kwenda kusoma nchi za magharibi. Lakini hili lilisababisha upinzani ndani yangu. Upinzani huo ni kwamba, Uislamu unafundisha wafuasi wake wasiwe na marafiki Wakristo au Wayahudi. Na ulimwengu wa Kiislamu unaamini kabisa kwamba nchi zote za magharibi ni Wakristo na Wayahudi.
Mwishoni mwa miaka ya 80, nilifika kwenye moja ya nchi za magharibi. Nilikuwa nimejawa na hofu sana na kukosa amani kwa kuwa sasa nilikuwa naenda kuwa karibu na Wakristo, hivyo ningeweza kupoteza matendo yangu mema (kama inavyosema Qur’an kwenye Sura 5:51 na 5:57). Lakini pamoja na hayo, nilikuwa natambua kwamba, ili kupata elimu bora kabisa, ni lazima niende kwenye nchi ya magharibi nikasome kwenye moja ya vyuo vyao vikuu.
Baada ya kukaa kwenye bweni kwa takribani mwezi mmoja, nilianza kujisikia haja ya kuufahamu utamaduni na maisha ya nchi ile. Pia, ingawaje nilikuwa nikidhani kuwa naweza kuongea Kiingereza vizuri, nilikuta kwamba Kiingereza cha kuzungumza cha magharibi ni kigumu zaidi kuelewa kuliko nilivyofikiri kutokana na matumizi ya nahau na misemo mbalimbali – jambo ambalo sikuwa nimedhania lingekuwa tatizo kwangu. Lakini kumbe huu ulikuwa ni mpango wa Mungu wa kunivuta kwake kupitia matukio yafuatayo:
Katika kipindi hicho nilisikia juu ya mpango wa kuwasaidia wanafunzi kutoka nje kujifunza zaidi juu ya utamaduni na namna ya maisha ya magharibi na pia kuepuka kikwazo cha lugha.
Sikujua kwamba shirika lililohusika na mpango huu lilikuwa la Kikristo, maana kama ningejua, KAMWE nisingeenda kwao. Kwa hiyo, nilijiandikisha – uamuzi ambao ulikuja kutikisa kabisa msingi wa maisha yangu na kubadili kabisa mwelekeo wake.
Karibu wiki mbili baada ya kujiandikisha, familia moja ya mtu na mkewe iliwasiliana nami na kunieleza kuwa walikuwa wameteuliwa kuwa karibu nami na kunisaidia kwa mahitaji ya msingi. Na kwa miezi saba iliyofuata, familia hii ILINIPENDA kwa namna ambayo sikutarajia kabisa – upendo ambao sikuwahi kuuona kamwe; hata kutoka kwa Waislamu wenzangu. Kulikuwa na hali ya amani iliyowazunguka ambayo iliwafanya wawe tofauti na watu wengine waliowazunguka, kiasi kwamba nilidhani kuwa hawa si Wakristo – maana kama kila mtu aliyenizunguka alikuwa Mkristo, kwa nini hawa wako tofauti?
Baadaye mwaka ule, familia hii ilinialika kwenye nyumba yao katika chakula cha jioni wakati wa sherehe za kutoa shukurani. Ni hapo ndipo nilipotambua kuwa wao nao ni Wakristo, maana waliuliza kama wanaweza kuomba, nami nikasikia maombi yao.
Ni lazima nikiri kwamba moyo wangu ulishuka sana wakati ule. Sikuwahi kujua kwamba Wakristo wana upendo mkubwa kiasi kile badala ya chuki kama ambavyo nilikuwa nikifundishwa kwenye imani yangu. Achilia mbali kwamba familia hii hata siku moja haikuwahi kunihubiria Injili; badala yake walinionyesha Kristo kupitia matendo yao na maisha yao (ulikuwa ni ushuhuda wa kimyakimya).
Siku hiyo, niliondoka kwenye nyumba yao huku nikiwa na mashaka mengi juu ya imani yangu na mafundisho yangu. Niliamua kuwa lazima nitafanya utafiti juu ya Ukristo ili nijue zaidi habari za huyu Yesu ambaye anaweza kuwafanya watu wawe na amani na furaha kubwa kiasi hiki – jambo ambalo kamwe sikuwahi kuliona au kulipata kabla – yule ambaye alikuwa chanzo cha nuru iliyokuwa inang’aa kutoka kwao.
Miaka kadhaa baadaye (karibu miaka 6), na baada ya kuhitimu chuo, nilijiunga na kampuni fulani. Humo nilikutana na Mkristo mwingine, ambaye kwa kweli alionyesha namna Mkristo anayeishi maisha ya Kikristo alivyo! Nilivutiwa sana na imani yake, mwenendo wake, furaha yake, amani yake, na nuru iliyong’aa kutokea kwake. Hakika alikuwa tofauti na kila mtu aliyemzunguka. Na aliponikaribisha kwenye chakula cha Krismasi nyumbani kwake, niligundua kuwa mke wake na watoto wake nao walikuwa kama yeye. Walifanana sana na ile familia niliyokutana nayo mwanzo nikiwa chuoni, ambako mbegu ya kwanza ilipandwa moyoni mwangu.
Ilikuwa ni pale ndipo niliposhindwa kuzuia shauku yangu ya kutaka kujua, na nikaanza kumuuliza kwa nini alikuwa tofauti hivyo na watu wengine? Akaanza kunielezea ushuhuda wake na akanieleza kuwa yeye ni Mkristo aliyeokoka (kitu ambacho sikukielewa kwa wakati ule). Aliniambia kwamba, kwa sababu alimpokea Kristo kama Bwana na Mwokozi wake binafsi, ndiyo maana yuko namna hiyo bila kutumia nguvu au juhudi zozote kwa upande wake; kwamba alikuwa ni Roho wa Bwana aliye ndani yake ndiye aliyesababisha matunda niliyokuwa nayashuhudia kwake. Pamoja na kwamba, kama ilivyokuwa kwa ile familia ya kwanza, hakunihubiria Injili moja kwa moja, ilikuwa ni dhahiri kwamba Yesu alikuwa ndiye chanzo cha amani na upendo ndani yake.
Kwa mara nyingine, nilimpenda Kristo ambaye ana nguvu kubwa kiasi hicho cha kubadili maisha ya watu hawa; nguvu kubwa kuliko hata ya mtume wangu ambaye nilimheshimu kama muhuri wa mitume wote na kipenzi zaidi cha Mungu. Lakini licha ya uaminifu wangu mkubwa, sikuwahi kuwa na amani kama watu hawa. Kusema kweli nilijisikia fedheha. Walikuwa ni kama kioo kilichoweka wazi ubovu wa maisha yangu ya ndani.
Kuanzia hapo na kuendelea, Bwana ameniruhusu kupita kwenye majaribu na hali mbalimbali katika maisha yangu, ambazo zilinifanya nitake kujua zaidi kuhusu Yeye, Mungu wa kweli – maana nilianza kubaini waziwazi kwamba Mungu wangu alikuwa hayupo popote.
Ndipo mapema kwenye miaka ya 2000, niliamua kwenda kwenye Kanisa la Kikristo (kinyume kabisa na yale niliyofundishwa na imani yangu ya Kiislamu, maana Mwislamu hawezi kamwe kwenda kwenye Kanisa kwa kuwa ni dhambi kubwa ambayo inaweza kunipotezea wokovu wangu). Kwa muda wa miezi 6 na kupitia kusoma Injili ya Yohana Kanisani kila Jumapili, nilijifunza Kristo ni nani hasa. Na polepole, Uungu wake ulianza kufunuka mbele za macho yangu, na ujumbe wa wokovu ukawa wazi kwangu; na nikajiona jinsi ambavyo sina uwezo na jinsi ambavyo ninauhitaji sana wokovu.
Mwishowe, bila hata ya mashaka yoyote, nilimpokea Kristo na Ukristo. Nikawa Mkristo niliyeokoka ambaye yuko tayari kufanya lolote kwa ajili ya kumtumikia Bwana na Mwokozi Yesu Kristo.
Miezi michache tu baada ya kumpokea Kristo, nikaja kujua maana ya kuwa na uhusiano binafsi na Bwana wangu mpendwa; na kumtegemea Yeye kikamilifu na kupokea uzima wake ndani yangu. Na katika kipindi hiki, alifunua utukufu wake wa ajabu kwangu kwa njia za ajabu kiasi kwamba siwezi kabisa kukana au kutilia shaka utukufu wake na kazi yake kwenye maisha yangu.
Tangu hapo, maisha yangu yamebadilika kabisa, na siko kama nilivyokuwa kabla. Hivi sasa mimi si tena mtu mwenye kiburi, si tena mtu ninayejihesabia haki. Nilipewa moyo laini, na nikawa kweli kiumbe kipya ambacho hata kila anayeniona anatambua hilo; kama ambavyo Biblia inasema juu ya wale wanaokuja kwa Bwana na kumkubali kuwa Mungu wao wa kweli:
Nami nitawapa moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa kijiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama; ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. (Ezekieli 11:19-20).
Inashangaza jinsi ambavyo kila kitu kilichosemwa kwenye mstari huo zaidi ya miaka 2500 iliyopita kilinitokea mimi na kinamtokea kila mtu anayemfuata Bwana. Kama ambavyo nilitambua kuwa waamini wote wa Bwana wana moyo MMOJA na Roho MOJA hivyo kuwafanya wawe tofauti na watu wengine, na wote wanafanana katika ukweli kwamba Bwana amebadili mioyo yao kutoka kuwa migumu kama jiwe na kuwa laini na yenye upole. Huo pekee ulikuwa ni ushuhuda mkubwa kwangu, kwamba kile kinachonitokea, hata kama si jambo kubwa kama baadhi watakavyosema, ni badiliko la KWELI na HALISI.
Mbali na hivyo, tafadhali kumbuka kile nilichotaja wakati wa ushuhuda wangu kwamba, ujumbe wa Injili haukuwahi kuhubiriwa kwangu wakati wote wa kumtafuta Kristo; au kuusikia kikamilifu hadi pale nilipompokea. Hivyo ndivyo nilivyompenda Kristo. Kubadilika kwa maisha yangu kulitokea kwa sababu ya matendo rahisi tu ya UPENDO yaliyoonyeshwa kwangu na familia mbili ambazo zilikuwa nuru ya kweli ing’aayo, kama ambavyo wameamuriwa na Bwana wetu katika Mathayo 5:14-16:
Ninyi ni nuru ya ulimwengu … nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Kupitia matendo haya ya kawaida kabisa ya upendo, niliweza kumjua mpendwa wangu Yesu Kristo; na kupitia upendo wao, Baba yetu wa mbinguni alitukuzwa, na ataendelea kutukuzwa. Mara nyingi huwa hatutilii maanani urahisi wa ujumbe wa Injili, kwamba upendo ndiyo amri kuu tuliyopewa na Kristo. Tunasau kwamba ujumbe ni KRISTO na si UKRISTO; kwamba sisi ni ujumbe na vyombo vyenye wajibu wa kumuwakilisha kwa wengine wanaotuzunguka; na jinsi uwakilishi huu unavyoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wale wanaotutazama, kama ilivyokuwa kwangu nilipokuwa nikiwatazama wale.
Tangu nilipomwamini Kristo, mimi si kipofu tena bali naiona kweli yote. Niliweza kuutambua uongo ambao niliuishi maisha yangu yote kama Mwislamu; uongo ambao Uislamu unafundisha; uongo ambao ndugu zangu Waislamu niwapendao bado wanauishi na kuuamini, kama nilivyokuwa mimi.
Uongo huu ni pamoja na madai kwamba: Muhammad ni nabii aliyetajwa kwenye Biblia, jambo ambalo nimelithibitisha kwamba hajatajwa popote kamwe. Uongo kwamba Qur’an ina miujiza ya kisayansi, jambo ambalo nalo nimelithibitisha kwamba ni udanganyifu. Hakuna hata kimoja kati ya yale yanayodaiwa kuwa ni miujiza kilicho karibu na sayansi. Uongo kwamba Biblia imepotoshwa, ilhali mimi nimethibitisha kwamba Qur’an haijawahi kuituhumu Biblia kama KITABU kuwa kimepotoshwa. Kiukweli, Qur’an inaitaka Biblia na watu wa Kitabu wathibitishe kwamba Qur’an inatoka kwa Mungu. Inawezekanaje Qur’an iwatake Waislamu waikague Biblia na kuiamini iwapo imepotoshwa? Na kwa vile Biblia haijapotoshwa, basi kile ambacho Biblia inafundisha ni cha kweli. Na Biblia inafundisha kwamba Yesu ni Mungu aliyekuja duniani kunikomboa mimi kutoka kwenye utumwa wa dhambi na shetani; kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu (badala yangu), na kunipa uzima wa milele na uhakika wa kusamehewa dhambi zangu ZOTE. Yesu alisema:
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. (Yohana 3:16).
AMINA.
Rafiki yangu, kama bado haujafanya uamuzi maishani mwako wa kumjua Kristo na kumpokea kama Bwana na Mwokozi wako; kama Mungu wa kweli aliye hai, basi ninaomba ufanye hivyo leo. Mara utakapofanya hivyo, utaingia kwenye safari itakayobadili kabisa mwelekeo wa maisha yako; lakini njia pekee ya kupokea hilo ni kumpokea Yesu Kristo sasa; maana maisha ni mafupi mno na hatuna mamlaka na udhibiti juu ya kile kinachoweza kutokea katika sekunde ijayo.
Nakukaribisha kuwasiliana nami kama una maswali au maoni yoyote.
Mungu wa Amani akubariki wewe pamoja na uwapendao.
Mutee’a Al-Fadi
***************
[Angalizo: Kwa kuwa ushuhuda huu ni tafsiri kutoka Kiingereza, ukiamua kuwasiliana na Mutee’a Al-Fadi, tafadhali tumia lugha ya Kiingereza, si Kiswahili.]
Pia, unaweza kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza kwa kubofya kwenye HAPA.
No comments:
Post a Comment