Thursday, September 19, 2013

Juhudi za Kupinga Ukristo za Mwanaharakati wa Kundi la Ahmadiah Kutoka Pakistani Zamfanya Aachane na Uislamu



Nusrat Aman alikuwa ni mwanaharakati wa kiislamu wa kundi la Ahmadiah kule Pakistani. Siku moja aliamua kuingia kanisani ili akamwulize mchungaji ni kwa nini hasa hataki kuwa mwislamu ilhali unabii wote umeshatimizwa ndani ya Muhammad? Nusrat aliishia kupata aibu, hasira na hatimaye wokovu …!


Je, ilikuwaje? Endelea kusoma ushuhuda wake wenye kichwa kisemacho "Kwa nini niliamua kuwa Mkristo?" ambao unafungua macho na mioyo kwa kuwa ni watu wengi walio katika kundi alimokuwa Nasrat hapo zamani.


*****************

Kwa nini niliamua kuwa Mkristo?

Na Nusrat Aman
Nilizaliwa katika familia halisi wa Kiislamu nchini Pakistani mwaka 1958. Nilisoma katika shule ya kimishenari ya Kiislamu na chuo kilichosimamiwa na Ahmadiah Movement in Islam, Pakistani. Wakati wa masomo yangu katika shule ya kimisionari na chuo cha Kiislamu vyenye mwamko mkubwa sana kuhusu Uislamu, nilijenga shauku kubwa ya kujifunza dini ya Kiislamu. Kwa hiyo, nilijiunga na Ahmadiah Movement, kundi ambalo lilitangazwa na Serikali ya Pakistani mwaka 1974 kuwa ni dini ya kizushi isiyo Kiislamu.

Mimi nilikuja kujua neno, "Kristo au Masihi" kwa mara ya kwanza katika maandiko ya Ahmadiah Movement yanayopinga Ukristo. Mwasisi wa harakati za Ahmadiah, Mirza Ghulam Ahmad alidai kuwa yeye ndiye "Masih Maud" (yaani Masihi aliyeahidiwa). Mimi nilikuwa na furaha sana na shauku ya kuhubiri mafundisho ya Ahmadiah Movement ambayo yalikuwa ni mapya na ya kuvutia sana kwangu. Nilikuwa nakumbuka aya zote kwenye Biblia zinazoongelea kuhusu ujio wa pili wa Kristo katika Biblia na Quran lakini bila kuwa na ufahamu wa kina kuhusiana na aya hizo.

Kosa nililofanya, likaniokoa
Siku moja nilikuwa napita mbele ya kanisa na nikafikiri kuwa hiyo ni fursa nzuri ya kumwuliza mchungaji ni kwa nini hasa yeye hawi Muislamu na mfuasi wa Muhammad wakati unabii wote umeshatimizwa ndani ya Muhammad?


Nilikwenda kanisani na nikamwambia mtu mmoja kwamba mimi nilitaka kukutana na mchungaji. Mtu huyo aliniongoza hadi kwa mchungaji na mimi nilijitambulisha kwamba ni Mwislamu na nataka kujua kwa nini hutaki kumwamini Mtume Muhammad wakati ambapo Yesu mwenyewe alisema kuwa yeye hastahili kubeba viatu vyake?

Mchungaji alinikaribisha kwenye kiti kisha akaenda kushughulika na watu wengine. Baada ya kumalizana nao, aliniuliza, “Unaweza kunionyesha mahali ambako Yesu alisema jambo hilo?”

Nilichukua Biblia kutoka kwa mchungaji na mara moja nilifungua kitabu cha Mathayo sura ya 3:11-12 na kuisoma mbele yake. Aliniambia nisome sura nzima kuanzia aya ya 1-17. Nilisoma, na nilipomaliza, hakukuwa na haja ya mtu kunieleza juu ya nani aliyezungumza maneno yale na yanamwongelea nani. Nilijisikia aibu na ghafla nilitoa andiko jingine ambalo lilikuwa ni Yohana 14:30 linalosema: “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”

Mchungaji aliniambia, "Siwezi kupingana na wewe kama unataka kusema kuwa andiko hili linamwongelea mtume wako, Muhammad." Alinifafanulia aya hii kutoka kwenye muktadha wa aya zingine kwenye kitabu hichohicho kwamba maneno “mkuu wa ulimwengu huu” yanamtaja Shetani kama anavyotajwa pia kwenye Yohana 12:32 na Yohana 16:11.

Nilijisikia aibu ndani ya nafsi yangu na nikajawa na hasira sana dhidi ya kundi lile (la Ahmadiah) na dhidi ya yule anayeitwa eti ni Masihi wa Pili, ambaye yeye mwenyewe alikuwa akitumia nukuu hizi katika vitabu vyake alivyofunuliwa. Niliondoka kwenye ofisi ya mchungaji kimyakimya bila hata kusema asante kwa msaada wako.

Niliamua kujifunza Qur'an pamoja na Biblia kwa undani na kwa kina. Kwa lengo hili, mimi nilijiunga na kozi kwa njia ya posta iliyotolewa na na Shule ya Biblia kwa Njia ya Posta iliyoko Pakistani. Huku nikiwa ni mhubiri wa Uislamu mwenye bidii sana, kiu yangu ya kuwa na welewa wa kutosha kuhusu Quran na Biblia, ilinisukuma kutafuta ufahamu juu ya neno, "Masihi" na ujio wa pili wa yule aliyeahidiwa. Kadiri nilivyosoma Biblia, nilipata shauku ya kujua kuhusu unabii juu ya ujio wa kwanza wa Masihi na kutimizwa kwake.

Mimi nilikuwa mjuzi katika Qur'an na lugha yake, hivyo wakati nikisoma Biblia akili yangu iliweza kulinganisha moja kwa moja kati ya vitabu hivi viwili. Lugha ya picha katika maandiko ya Kikristo ya Kigiriki (Agano Jipya) yalinigusa sana na nilitambua kuwa huu haukuwa tu wasifu (biography) bali katika kila simulizi kuna tukio kubwa linalooonyesha kwamba Mungu alikuwa akitembea pamoja na mwanadamu.

Lakini unaposoma Qur'an hauoni kitu maalumu, badala yake zaidi ya theluthi mbili yake ni kutoka kwenye hadithi  za kipagani au upotoshaji wa Torati (vitabu tano vya kwanza vya Biblia). Haiwezekani ukawa na umakini pale unaposoma Qur'an kwa maana mambo yake yanabadilikabadilika mara kwa mara na kwa ghafla kila baada ya mistari miwili au mitatu.

Nilitambua kwamba Yesu katika huduma yake hapa duniani alionyesha mamlaka makuu. Alikuwa na ujasiri, mhalisia na aliwakabili moja kwa moja wakosoaji wake. Wakosoaji wake daima walikwepa kukabiliana naye. Tunasoma katika Yohana 6:41, 43 kwamba wakati Yesu alipokuwa akihutubia makutano ya watu kando ya ziwa, watu walianza kunung’unika dhidi yake kwa sababu Yeye alisema, "Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni,” lakini hawakuthubutu kumkosoa waziwazi. Badala yake Yesu akajibu, "Msinung'unike ninyi kwa ninyi."

Katika tukio lingine, Yesu alisema, "Niliyoyaona kwa Baba ndiyo ninenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo .... Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda.” (Yohana 8:38, 44). 

Kwa kulinganisha, kinyume chake kwa Mtume Muhammad, wakosoaji wake ndio waliokuwa wakeraji na wenye kujiamini.

Walisema, "Hatutokuamini hadi utakapofanya chemchemi ya maji itoke katika ardhi kwa ajili yetu; au hadi upate bustani ya miti na mitende na mizabibu, na ufanye mito ipite katikati yake; au ufanye vipande vya mbingu vituangukie kama unavyodai kwamba unaweza; au mlete Mungu na malaika wawe wadhamini; au umiliki nyumba iliyojaa dhahabu, au upae hadi mbinguni; japokuwa hatutakuamini kuwa umepaa hadi ulete kitabu kwa ajili yetu ambacho tunaweza kukisoma." (Sura 17:90-93).

Katika kujibu haya yote Mtume Muhammad alisema tu kwamba, "Mimi ni mwanadamu na mjumbe tu." (Sura 17:93).

Wakati wa mabadiliko

Nilisoma Quran na Biblia kwa nguvu sana. Mstari mmoja wa Quran ukawa umenikaa zaidi akilini kuliko mingine yote, na matokeo yake imani yangu yote na kujitoa kwangu kote kuliparaganyika kabisa. Hiyo ni aya katika Qur'ani, Sura 46 "Al-Ahqaf" aya ya 9:

"Say: "I am not a new Messenger to come, nor do I know what is to be done to me or you. I only follow what is revealed to me. My duty is only to warn you clearly."

Yaani:
"Sema:"Mimi si Mjumbe mpya ajaye, na wala mimi sijui ni kile nitakachotendewa mimi wala mtakachotendewa ninyi. Ninafuata tu kile kinachofunuliwa kwangu. Wajibu wangu tu ni kuwaonya kwa uwazi."

Sikuweza kuwa na ujasiri wa kusubiri (uharibifu) bila kufanya uamuzi mpaka Siku ya Kiama. Nawezaje kumfuata mtu ambaye hajui mambo yanayomhusu yeye mwenyewe na hajui mambo kuhusu watu wanaomwamini?

Kubadili dini
Nikiwa Pakistani, kubadili dini na kuwa Mkristo ilikuwa ni changamoto ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kwangu; mahali ambapo 95% ya watu ni Waislamu. Wakristo ni wachache sana na kubadili dini ina maana kutengwa kutoka katika mahusiano yote ya jamii. Hofu ya kudumu ya kuhukumiwa na umma nayo haondoki. Umati wa Waislamu unaweza kufanya lolote dhidi ya Wakristo kwa jina la Uislamu. Hata ndugu na marafiki wa karibu wanapokuwa na migogoro ya kibinafsi na Wakristo na inayohusu mali, watu hao huweza kuwatuhumu kwamba wamesema kitu dhidi ya Uislamu au Mtume Muhammad.

Wakristo wanaweza kuhukumiwa kifo chini ya sheria ya kukufuru. Na kundi la Waislamu wenyewe nalo linaweza kuwahukumu ilhali tuhuma za uongo zinazotolewa kwa jina la Uislamu zenyewe hazina adhabu yoyote.

Ni katika mazingira haya, ndipo mimi nilimkubali Yesu Kristo kama Mwokozi wangu binafsi na kubatizwa kwa siri mwaka 1979 bila mzazi na ndugu zangu kujua. Kwa miaka 10 nilikuwa Mkristo katikati ya Wakristo na Waislamu kabla ya mzazi wangu kujua. Shinikizo kutoka kwa mzazi wangu la kunitaka nioe kutoka kwenye familia ya kiislamu lilinilazimisha kufichua imani yangu kwamba siwezi kuoa msichana wa Kiislamu (maana ndoa kati ya mwanamume Mkristo na mwanamke Mwislamu haitambuliwi na Sheria za Pakistan).

Nafurahi kwamba Mwokozi wangu, Yesu Kristo anajua Yeye ni nani (Yohana 17:14, 21) na kile anachoweza kufanya Yeye kwa ajili yangu. (Yohana 17:02). Nina imani katika Yeye.
Alisema: "Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi." (Yohana 14:06).

Sasa, ni mzigo wangu kuihubiri Kweli kama alivyoamuru Yesu (Mathayo 28:20); na ole wangu nisipoihubiri Injili (1 Kor 9:16)

Nilifanya kazi Pakistan kama meneja wa mradi wa maendeleo ya jamii hadi 2001 na kisha nilihamia Kanada katika kundi huru.

Mimi ni wa kujitolea na niko tayari kukaribisha maswali yoyote, lawana au mazungumzo kuhusu Ukristo.

Nusrat Aman
E-mail: naman@gosonic.ca
E-mail: nusrat04@hotmail.com

 
***************

[Angalizo la blogger: Kwa kuwa ushuhuda huu umetafsiriwa kutoka kwenye Kiingereza, tafadhali kama unapenda kuwasiliana na Nusrat, fanya hivyo kwa lugha ya Kiingereza, na si Kiswahili.


Kama pia ungependa kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza, bofya HAPA.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW