Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aaini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao (Waebrania 11:6).
Kama waaminio, imani yetu imejengwa kwenye msingi kwamba Mungu yupo, naye huwatendea watu wanaomtafuta kitofauti na wale wasiomtafuta. Tukiamini kweli kweli mambo hayo, tunaanza kumpendeza Mungu, kwa sababu mara moja tunaanza kumtafuta. Kumtafuta Mungu ni pamoja na (1) Kujifunza mapenzi Yake, (2) Kumtii, na (3) Kutumainia ahadi Zake. Hayo yote matatu yanapaswa kuwa sehemu ya mwenendo wetu wa kila siku.
Sura hii inatazama mwendo wetu wa imani. Ni bahati mbaya kwamba wengi wamekazia imani mpaka ikapita mipaka ya KiBiblia – hasa mkazo kuhusu mafanikio kimwili. Kwa sababu hiyo, kuna watu ambao wana hofu kulishughulikia swala hili kabisa. Lakini, kwa kuwa kuna watu wanaozama katika madimbwi yao ya kuogelea, si sababu kwetu kuacha kunywa maji. Tunaweza kuwa na msimamo na ukweli wa Maandiko. Biblia ina mengi sana inayofundisha kuhusu mada hiyo, na Mungu anataka tuitumie imani yetu kwa habari ya ahadi Zake nyingi sana.
Yesu aliweka mfano wa mwenye kuwa na imani katika Mungu, Naye anatazamia wanafunzi Wake kufuata mfano Wake. Vivyo hivyo, mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi hujitahidi kuweka mfano wa kumtumaini Mungu, naye huwafundisha wanafunzi wake kuziamini ahadi za Mungu. Hii ni muhimu sana sana. Sit u kwamba haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani, ni kwamba haiwezekani kupokea majibu ya maombi yetu pasipo imani (ona Mathayo 21:22; Yakobo 1:5-8). Maandiko yanafundisha wazi wazi kabisa kwamba wenye mashaka wanakosa baraka ambazo waamini hupokea. Yesu alisema hivi: “Yote yanawezekana kwake yeye aaminiye” (Marko 9:23, TLR).
Maana Ya Imani
Tafsiri ya KiBiblia ya imani inapatikana katika Waebrania 11:1, kama ifuatavyo:
Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyo-onekana.
Kutokana na tasiri hii, tunapata sifa kadhaa za imani. Kwanza – mtu mwenye imani ana uhakika. Hii ni tofauti na tumaini, kwa sababu imani ni “uhakika wa mambo yatarajiwayo.” Tumaini hutoa nafasi kwa mashaka. Tumaini kila wakati linasema, “labda”. Mfano: Ninaweza kusema hivi: “Natumaini leo mvua itanyesha ili shamba langu lipate maji.” Ni kwamba natamani mvua, lakini sina hakika kama itanyesha. Lakini imani ina uhakika wakati wote, “wa mambo yatarajiwayo.”
Kile ambacho watu wanaita imani mara nyingi si imani kwa tafsiri ya Biblia. Wanaweza kutazama mawingu meusi juu na kusema, “Naamini mvua itanyesha.” Ila, hawana hakika kwamba itanyesha – wao wanafikiri tu kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba pengine itanyesha. Hiyo si imani ya KiBiblia. Imani ya Biblia haina sehemu ya mashaka. Haitoi nafasi yoyote kwa chochote kingine isipokuwa kile ambacho Mungu ameahidi.
Imani Ni Uhakika Wa Mambo Yasiyo-onekana
Tafsiri ipatikanayo katika Waebrania 11:1 pia inasema kwamba imani ni “bayana ya mambo yasiyo-onekana.” Basi, kama tunaweza kuona kitu au kukitambua kwa hisia zetu tano, imani haitakiwi.
Hebu fikiri kwamba mtu hivi: “Kwa sababu ambayo siwezi kueleza, nina imani kwmaba kuna kitabu mikononi mwako.” Bila shaka ungedhani kwamba ana matatizo fulani. Ungemwambia hivi: “Ha! Huna haja ya kuaminikwamba nina kitabu mikono mwangu, maana unaweza kuona dhahiri kabisa kwamba nimeshika kitabu.”
Imani ni ya dunia isiyo-onekana na macho. Kwa mfano: Ninapoandika maneno haya, ninaamini kwamba kuna malaika karibu na mimi. Yaani, nina hakika kabisa. Ninawezaje kuw ana uhakika kiasi hicho? Je, nimemwona? Hapana. Je, nimehisi au kusikia malaika akiruka karibu? Hapana. Kama ningekuwa nimemwona au kumsikia au kuguswa na mmoja, nisingekuwa na haja ya kuamini kwamba kuna malaika karibu nami – ningejua kwamba yupo.
Basi, ni kitu gani kinachonifanya kuwa na hakika kwamba malaika yupo? Uhakika wangu unatokana na ahadi moja ya Mungu. Katika Zaburi 34:7, aliahidi hivi: “Malaika wa Bwana hufanya kituo karibu na wale wamchao, na kuwaokoa” (TLR). Sina ushahidi wa kile ninachoamini isiokuwa Neno la Mungu. Hiyo ndiyo imani ya kweli ya Biblia – ‘bayana ya mambo yasiyo-onekana’. Watu wa dunia mara nyingi wanatumia msemo huu: “Kuona ni kuamini.” Katika ufalme wa Mungu ukweli ni kinyume: “Kuamini ni kuona.”
Tunapofanyia kazi imani yetu kuhusu ahadi mojawapo ya Mungu, mara nyingi tunakabiliana na mazingira yatakayotujaribu kuwa na mashaka, au kupitia kipindi ambapo inaonekana kana kwamba Mungu hatimizi ahadi yake kwa sababu mazingira yetu hayabadiliki. Kwa hali hiyo, tunachohitaji kufanya ni kupinga mashaka, kudumu katika imani, na kuendelea kuamini mioyoni mwetu kwamba Mungu siku zote hutimiza Neno Lake. Yeye hawezi kudanganya kamwe (ona Tito 1:2).
Tunapataje Imani?
Kwa kuwa imani imejengwa kwenye ahadi za Mungu tu, kuna mahali pamoja tu pa kupata imani ya KiBiblia – Neno la Mungu. Warumi 10:17 inasema hivi: “Basi, imani huja kwa kusikia, Neno la Kristo (TLR, maneno mepesi kutilia mkazo). Neno la Mungu hufunua mapenzi Yake. Tunapoyajua mapenzi ya Mungu ndipo tunapoweza kuyaamini.
Basi, ukitaka kuwa na imani, lazima usikie (au usome) ahadi za Mungu. Imani haiji kwa maombi, kwa kufunga, au kwa mtu kukuwekea mikono ili uipate. Inakuja kwa kusikia Neno la Mungu. Na, ukiisha kulisikia, bado inakubidi ufanye uamuzi kuliamini.
Zaidi ya kupata imani, imani yetu pia inaweza kuwa na nguvu. Biblia inataja viwango kadhaa vya imani – kutoka imani ndogo hadi imani yenye kuhamisha milima. Imani hukua na kupata nguvu sana inapolishwa na kufanyiwa kazi, sawa tu na musuli ya kibinadamu. Tunapaswa kuendelea kuilisha imani yetu kwa kutafakari Neno la Mungu. Tunapaswa kuifanyisha kazi kwa kutenda na kuitikia kila kitu kulingana na Neno la Mungu. Hata nyakati zile tunapokabiliana na matatizo, wasiwasi na mambo yanayotusumbua. Mungu hataki watoto Wake kuwa na wasiwasi kuhusu lolote, bali kumtumaini katika kila hali (ona Mathayo 6:25-34; Wafilipi 4:6-8; 1Petro 5:7). Kukataa kuwa na wasiwasi ni njia moja ya kufanyia kazi imani yetu.
Kama kweli tunaamini aliyosema Mungu, tutatenda na kusema kana kwamba ni kweli. Ukiamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, utasema na kutenda kama mtu anayeamini hayo. Kama unaamini kwamba Mungu atakupa mahitaji yako yote, utasema na kutenda hivyo. Ukiamini kwamba Mungu anataka uwe mwenye afya, utatenda nakuzungumza hivyo. Biblia imejaa mifano ya watu ambao wakiwa katikati ya mazingira magumu, walifanyia kazi imani yao katika Mungu na wakapata miujiza. Tutawatazama baadhi yao katika sura hii baadaye, na katika sura inayofuata kuhusu uponyaji wa Mungu. (Ukitaka mifano mingine mizuri, tazama 2Wafalme 4:1-7; Marko 5:25-34; Luka 19:1-10 na Matendo 14:7-10).
Imani Ni Kitu Cha Moyo
Imani ya KiBiblia haifanyi kazi katika akili zetu – ni moyoni. Paulo aliandika hivi: “Maana kwa moyo mtu huamini” (Warumi 10:10a, TLR). Yesu naye alisema hivi:
Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng’oka ukatupwe baharini’, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake (Marko 11:23. Maneno mepesi kutilia mkazo).
Yawezekana kabisa kuwa na mashaka kichwani mwako na ukawa bado na imani moyoni mwako na kupokea kile ambacho Mungu ameahidi. Ukweli ni kwamba mara nyingi tunapojaribu kuamini ahadi za Mungu, aili zetu, zikishawishiwa na hisia zetu za kimwili na uongo wa Shetani, hushambuliwa na mashaka. Katika nyakati hizo tunahitaji kuondoa mawazo yenye mashaka na kutia ahadi za Mungu mahali pake, na kudumu katika imani bila ya kusita au kuyumba.
Makosa Ya Kawaida Kuhusu Imani
Tunapojaribu kuwa na imani katika Mungu, wakati mwingine tunashindwa kupokea tunachotaka kwa sababu hatufanyi kulingana na Neno la Mungu. Kosa moja la kawaida sana hutokea wakati tunapojaribu kuamini kupata kitu ambacho Mungu hajatuahidi.
Kwa mfano: Ni halali KiMaandiko kwa wenye ndoa kumwamini Mungu kupata watoto kwa sababu Neno la Mungu lina ahadi ambayo wanaweza kuisimamia. Ninajua wana ndoa ambao wameambiwa na daktari kwamba hawatapata watoto. Wao waliamua kumwamini Mungu, wakisimama kwenye ahadi mbili zinazofuata hapo chini, na leo hii ni wazazi wa watoto wenye afya nzuri sana.
Nanyi mtamtumikia BWANA Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba wala aliye tasa katika nchi yako; na hesabu ya siku zao nitaitimiza (Kutoka 23:25-26).
Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo (Kumbu. 7:14).
Ahadi hizi ziwatie moyo wana ndoa wasiokuwa na watoto! Lakini, kujaribu kuamini kwamba lazima mtoto awe mvulana au msichana ni jambo lingine. Katika Biblia hakuna ahadi zinazosema tutachagua jinsia ya watoto tutakaozaa. Lazima tukae katika mipaka ya Neno la Mungu kama tunataka imani yetu itende kazi. Tunaweza kumwamini Mungu kwa kile alichotuahidi tu.
Hebu tuone ahadi nyingine ya Neno la Mungu, kisha tuamue tunachoweza kuamini kutokana na ahadi hiyo.
Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza (1Wathes. 4:16).
Kutokana na andiko hilo, tunaweza kuamini kabisa kwamba Yesu atarudi. Lakini je, tuombe na kuamini kwamba Yesu atarudi kesho? Hapana, kwa sababu andiko hili halituahidi hivyo, wala lingine lolote. Tena, Yesu mwenyewe alisema hakuna ajuaye saa wala siku ya kurudi Kwake.
Ila, tunaweza kuomba tukitumaini kwamba Yesu anaweza kurudi kesho, lakini hatuna uhakika kwamba itatokea kama tunavyoomba. Tunapoomba kwa imani, tuna hakika kwamba kile tunachokiomba kitatokea kwa sababu tuna ahadi ya Mungu kuhusiana nacho.
Kwa andiko hilo hilo, tunaweza kuamini kwamba miili ya wale waaminio waliokufa itafufuliwa wakati Yesu atakaporudi. Lakini je, sisi tulio hai wakati wa kurudi kwa Kristo tuamini kwamba tutapokea miili ya ufufuo wakati huo huo kama “waliokufa katika Kristo”, au hata kabla yao? Hapana, maana andiko hili linatuambia tofauti kabisa, kwamba: Wale “waliokufa katika Kristo” watafufuliwa kwanza.” Mstari unaofuata unaendelea hivi: “Kisha sisi tulio hai tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu” (1Wathes. 4:17). Basi, hakuna uwezekano kwamba “waliokufa katika Kristo” hawatakuwa wa kwanza kupokea miili yao ya ufufuo wakati Yesu atakaporudi. Neno la Mungu limeahidi kwamba watakuwa wa kwanza.
Hivyo – kama tunatakiwa kumwamini Mungu kwa habari ya kitu fulani, lazima tuwe na uhakika kwamba ni mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu kupokea tunachotaka. Mapenzi ya Mungu yanaweza kujulikana vizuri sana kwa kutazama ahadi Zake zilizoandikwa katika Biblia.
Imani inafanya kazi hivyo hivyo katika dunia ya kawaida. Utakuwa mjinga kuamini kwamba nitakutembelea nyumbani kesho mchana kama sikuwa nimekuahidi hivyo.
Imani bila ahadi ya kuisimamia, si imani kweli – ni upumbavu. Kwa hiyo – kabla hujamwomba Mungu chochote, kwanza jiulize swali hili – ni andiko gani katika Biblia linaloniahidi kile ninachotaka? Kama huna ahadi, huna msingi wa imani yako.
Kosa La Pili La Kawaida
Mara nyingi Wakristo hujaribu kutegemea ahadi moja ya Mungu kutimizwa maishani mwao bila ya kutimiza masharti yote yenye kuambatana na ahadi yenyewe. Kwa mfano: Nimesikia Wakristo wengi wakirejea maneno ya Zaburi 37 na kusema hivi: “Biblia inasema Mungu atanipa matakwa ya moyo wangu. Ninamwamini kwa hilo.”
Tatizo ni kwamba, Biblia haisemi tu kwamba Mungu atatupa matakwa ya mioyo yetu. Angalia inachosema:
Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini BWANA ukatende mema, ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa BWANA, naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya (Zaburi 37:1-5).
Kuna masharti kadha ambayo lazima tutumize ikiwa tunataka kumwamini Mungu atupe matakwa ya moyo. Ukihesabu utaona masharti nane katika ahadi hiyo. Tusipotimiza masharti hayo, hatuna haki ya kupokea baraka zilizoahidiwa. Imani yetu inakuwa haina msingi.
Pia, Wakristo wanapenda kureje ahadi inayopatikana katika Wafilipi 4:19, kwamba “Mungu wangu atanipa mahitaji yangu yote kulingana na utajiri Wake katika utukufu.” Sawa – je, kuna masharti katika ahadi hiyo? Bila shaka.
Ukichunguza mantiki ya ahadi ya Wafilipi 4:19, utaona kwamba si ahadi itolewayo kwa Wakristo wote. Ila ni ahadi itolewayo kwa Wakristo ambao ni watoaji. Paulo alijua Mungu angewapa Wafilipi mahitaji yao yote kwa sababu walikuwa wamemtumia sadaka. Kwa kuwa walitafuta kwanza ufalme wa Mungu kama Yesu alivyoagiza, Mungu angewapa mahitaji yao yoe, kama Yesu alivyoahidi (Mathayo 6:33). Ahadi nyingi katika Biblia zinazohusu Mungu kutupa mahitaji yetu ya kawiada zina sharti kwamba sisi tuwe watoaji kwanza.
Kweli hatuna haki ya kumtumaini Mungua kutane na mahitaji yetu kama hatutii amri Zake kuhusu fedha yetu. Katika agano la kale, Mungualiwaambia watu Wake kwamba walikuwa wamelaaniwa maana hawakuwa wanatoa zaka zao. Ila, aliahidi kuwabariki kama wangetoa zaka na sadaka zao kwa uaminifu na kwa utii (ona Malaki 3:8-12).
Baraka nyingi zilizoahidiwa kwetu katika Biblia zinategemeana na sisi kumtii Mungu. Basi, kabla ya kujaribu kumwamini Mungu kwa kitu fulani, tujiulize kwanza hivi: “Je, ninatimiza masharti yanayoambatana na ahadi hiyo?”
Kosa La Kawaida La Tatu
Katika Agano Jipya, Yesu aliweka sharti ambalo linafanya kazi kila wakati tunapo-omba kuhusu kitu.
Mwaminini Mungu. Amin nawaambia, ‘Yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu (Marko 11:22-24, maneno mepesi kutilia mkazo).
Sharti ambalo Yesu alitaja ni kuamini kwamba tumekwisha pkea tunapoomba. Wakristo wengi hukosea kwa kujaribu kufanyia kazi imani yao kwa kuamini kwamba wamepokea wanapo-ona jibu la maombi yao. Wanaamini kwamba watapokea, si kwamba wamekwisha pokea.
Tunapomwomba Mungu kitu ambacho ametuahidi, tunatakiwa kuamini kwamba tunapoikea jibu wakati tunapo-omba, kisha tuanze kumshukuru Mungu kwa jibu wakati huo. Lazima tuamini kwamba tumejibiwakabla ya kuona, si baada ya kuona. Tunatakiwa kumjulisha Mungu haja zetu pamoja na shukrani, kama anavyoandika Paulo.
Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu (Wafilipi 4:6).
Kama tulivyokwisha ona, tukiwa na imani mioyoni mwetu, maneno yetu na matendo yetu vitalingana na kile tunachoamini. Yesu alisema hivi: “Mdomo hunena yale yaujayazo moyo” (Mathayo 12:34).
Kuna Wakristo wengine wanaofanya kosa la kurudia kuomba kitu kile kile. Hiyo inadhihrisha kwamba hawajaamini bado kwamba wamekipokea. Kama tunaamini kwamba tunapokea tunapoomba, hakuna haja ya kurudia kuomba ombi lile lile. Kurudia kuomba kitu kile kile ni kuonyesha mashaka kwamba Mungu hakutusikia tulipomwomba mara ya kwanza.
Je, Yesu Hakurudia Ombi Zaidi Ya Mara Moja?
Yesu alirudia ombi moja mara tatu, alipokuwa anaomba katika Bustani ya Getsemane (ona Mathayo 26:39-44). Lakini kumbuka hakuwa anaomba kwa imani kulingana na mapenzi ya Mungu. Alipoomba mara hizo tatu ili ikiwezekana asiende msalabani, alijua kwamba ombi Lake lilikuwa kinyume na mapenzi ya Mungu. Ndiyo sababu alijinyenyekeza kwa mapenzi ya Baba Yake mara tatu pia katika sala hiyo hiyo.
Hiyo sala mara nyingi hutumiwa kimakosa kwamba ni mfano wa maombi yote, maana kuna wengine wanaofundisha kwamba kila sala inapaswa kumalizika kwa kusema hivi: “Kama ni mapenzi Yako” au “Si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi Yako yatendeke.”
Hapa tena tunapaswa kukumbuka kwamba Yesu alikuwa anaomba kitu alichojua kwamba si mapenzi ya Mungu. Kufuata mfano Wake wakati sisi tunaomba kitu kulingana na mapenzi ya Mungu ni kosa, na kutokuwa na imani. Kwa mfano: Kuomba hivi: “Bwana! Naungama dhambi yangu kwako, nami naomba unisamehe ikiwa ni mapenzi Yako” ni kuonyesha kwamba yawezekana si mapenzi ya Mungu kusamehe dhambi yangu. Tunajua kwamba Biblia inaahidi Mungu atatusamehe tunapoziungama dhambi zetu (ona 1Yohana 1:9). Hivyo, sala kama hiyo itadhihrisha kutokuwa na imani kwa mtu, kuhusu mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa wazi.
Yesu hakumaliza kila sala kwa kusema, “Si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi Yako yatimizwe.” Kuna mfano mmoja tu wa Yeye kuomba hivyo, na ni wakati alipokuwa anajitolea kufanya mapenzi ya Baba Yake, akijua mateso ambayo angepitia kwa sababu hiyo.
Kwa upande mwingine, kama hatujui mapenzi ya Mungu katika hali fulani kwa sababu hajayafunua, basi inafaa kumalizia maombi yetu kwa maneno haya: “Kama ni mapenzi yako.” Yakobo aliandika hivi:
Haya basi ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya (Yakobo 4:13-16).
Tufanye nini tukiisha omba kulingana na ahadi ya Mungu, na kutimiza masharti yote? Tuendelee kumshukuru Mungu kwa majibu ambayo tumeamini kwamba tumeyapokea mpaka tupokee tulichokiomba. Tunapokea na kurithi ahadi za Mungu kwa imani na subira (Waebrania 6:12). Shetani atajaribu kutushinda kwa kuleta mashaka, nasi lazima tutambue kwamba akili zetu ndiyo uwanja wa mapambano. Wakati mawazo ya mashaka yanaposhambulia akili zetu, tunahitaji kuyabadilisha kwa mawazo yenye msingi kwenye ahadi za Mungu na kulitamka Neno la Mungu kwa imani. Tukifanya hivyo, Shetani lazima akimbie (ona Yakobo 4:7; 1Petro 5:8-9).
Mfano Wa Imani Katika Matendo
Mfano mmoja maarufu sana katika Biblia kuhusu imani katika matendo ni habari ya Petro akitembea juu ya maji. Hebu tusome habari yenyewe, tuone tutajifunza nini.
Mara [Yesu] akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi, maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari wakafadhaika wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi, msiogope. Petro akamjibu akasema, Bwana! Ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu! (Mathayo 14:22-33).
Kabla ya hapa, wanafunzi wa Yesu walikuwa wamenaswa katika dhoruba nyingine kali wakiwa mtumbwini katika Bahari ya Galilaya (ona Mathayo 8:23-27). Wakati wa tukio hilo, Yesu alikuwa nao, na baada ya kutuliza dhoruba kwa neno lake, aliwakemea wanafunzi Wake kwa kutokuwa na imani kwao. Kabla ya kuanza safari alikuwa amewaambia kwamba ni mapenzi Yake wavuke hadi ng’ambo ya pili ya ziwa (Marko 4:35). Lakini, dhoruba ilipotokea, walishawishika zaidi na mazingira yao, na kuna wakati waliamini watakufa wote. Yesu alitazamia haidhuru wasiogope basi.
Safari hii, Yesu aliwatuma wavuke ng’ambo ya ziwa wakiwa peke yao. Hakika aliongozwa na Roho kufanya hivyo, na hakika Mungu alijua kwamba upepo wa mbisho ungetokea usiku huo. Kwa hiyo Bwana aliwaruhusu wakabiliwe na changamoto ndogo tu kwa imani yao. Kwa sababu ya hizo pepo za mbisho, safari ambayo ingechukua masaa machache tu ilichukua usiku kucha. Kweli tunastahili kuwasifu wanafunzi kwa jitihada zao, lakini hatuachi kushangaa ikiwa kuna mmoja wao aliyejaribu hata kuwa na imani kwamba hizo pepo zitulie – kitu ambacho walikuwa wamemwona Yesu akifanya siku chache kabla ya hapo. Cha ajabu ni kwamba, katika Injili ya Marko, tunasoma kwamba wakati Yesu alipowaendea akitembea juu ya maji, “akataka kuwapita” (Marko 6:48). Alikuwa anataka awaache wakabiliane na tatizo lao peke yao, huku yeye anapita hapo kimuujiza! Hii inaonyesha kwamba hawakuwa wanaomba au kumtazama Mungu. Changamoto kwetu ni kwamba Mtenda Miujiza hutupita mara ngapi tunapong’ang’ana na maisha dhidi ya upepo wa matatizo.
Kanuni Za Imani
Yesu aliitikia wito wa Petro kwa neno moja tu: “Njoo.” Kama Petro angejaribu kutembea juu ya maji kabla ya neno hilo, angezama mara moja, maana asingekuwa na ahadi ya kutegemeza imani yake. Angekuwa anajitokeza kwa kudhania badala ya imani. Vile vile hata baada ya Yesu kusema neno Lake, kama mwanafunzi mwingine yeyote angejaribu kutembea juu ya maji, angezama mara moja, kwa sababu Yesu alimpa Petro tu ahadi. Hakuna mwingine ambaye angeweza kutimiza masharti ya ahadi hiyo, maana hawakuwa Petro. Basi, kabla yeyote kati yetu hajajaribu kutegemea ahadi moja ya Mungu, lazima kuhakikisha kwamba ahadi hiyo ni yetu na kwamba tunatimiza masharti yake.
Petro akaweka mguu kwenye maji. Hapo ndipo alipoamini, japo hakuna shaka kwamba yeye aliyekuwa anapiga kelele kwa kuogopa mzuka muda mfupi kabla ya hapo, pia alikuwa na mashaka ichwani mwake alipopiga hatua ya kwanza. Lakini ili aweze kupokea muujiza, ilibidi afanyie kazi imani yake. Kama angeshikilia mlingoti wa mtumbwi na kutia dole gumba la mguu ndani ya maji aone kama maji yana uwezo wa kumbeba, asingepata muujiza. Vivyo hivyo na sisi – kabla ya kupokea muujiza wowote, lazima tujitolee kuamini ahadi ya Mungu, kisha tutende kama tunavyoamini. Kila mara kuna wakati ambapo imani yetu lazima ipimwe. Wakati mwingine kipindi ni kifupi, wakati mwingine kirefu. Lakini kuna muda ambapo itabidi tupuuze ushahidi wa hisia zetu na kutenda kulingana na Neno la Mungu.
Petro aliendelea vizuri mwanzoni. Lakini alipotafakari jinsi hicho alichokifanya kisivyowezekana, akikumbuka upepo na mawimbi, aliogopa. Pengine aliacha kutembea, akihofia hatua inayofuata. Sasa – yeye aliyekuwa anapokea muujiza akajikuta anazama. Twahitaji kuendelea katika imani tukiisha anza – kuendelea kutenda kulingana na imani yetu. Tuzidi kusonga mbele.
Petro alizama kwa sababu alikuwa na mashaka. Mara nyingi watu hawapendi kujilaumu wenyewe kwa kukosa imani kwao. Wanaona ni afadhali kumlaumu Mungu. Lakini, unadhani Yesu angeitikiaje kama angemsikia Petro, baada ya kurudi mtumbwini salama, akiwaambia wanafunzi wenzake hivi: “Kweli, mpango wa Mungu kwa ajili yangu ilikuwa kufika hapo nilipofika?”
Petro alishindwa kwa sababu aliogopa, akapoteza imani. Huo ndiyo ukweli. Yesu hakumlaumu, bali alinyosha mkono wake mara moja kumpa Petro kitu thabiti zaidi cha kushika. Na mara moja akamhoji Petro kwa nini aliona shaka. Petro hakuwa na sababu yoyote nzuri ya kuwa na shaka, kwa sababu neno la Mwana wa Mungu ni thabiti kuliko kitu chochote. Hakuna yeyote kati yetu mwenye sababu nzuri ya kutilia shaka Neno la Mungu, au kuogopa, au kuwa na wasiwasi.
Maandiko yamejaa ushindi ambao ulitokana na imani, na kushindwa kulikotokana na mashaka. Yoshua na Kalebu waliingia Nchi ya Ahadi kwa sababu ya imani yao. Wenzao wengi walikufa jangwani kwa sababu ya mashaka yao (ona Hesabu 14:26-30). Wanafunzi wa Yesu walipata mahitaji yao waliposafiri wawili wawili kuhubiri Injili (Luka 22:35), lakini waliwahi kushindwa kutoa pepo kwa sababu ya kutokuamini kwao (ona Mathayo 17:19-20). Wengi walipokea miujiza ya uponyaji katika huduma ya Kristo, lakini wagonjwa wengi katika mji wa Nazareti – nyumbani Kwake – walibakia wagonjwa kwa sababu ya kutoamini kwao (Marko 6:5-6).
Kama wote, hata mimi nimepata mafanikio na kushindwa kulingana na imani yangu au mashaka yangu. Lakini sitaskia uchungu kwa kushindwa kwangu au kumlaumu Mungu. Sitajihesabia haki kwa kumlaumu Yeye. Sitatafuta maelezo yasiyoeleweka kirahisi, yenye kutengeneza upya mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa wazi. Najua Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo, ninaposhindwa, ninatubu kutokuamini kwangu na kuanza kutembea juu ya maji tena. Nimeona kwamba Yesu kila mara ananisamehe na kuniokoa nisizame!
Tunamalizia hivi: Waamini hubarikiwa; wenye mashaka hawabarikiwi! Mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi hufuata mfano wa Yesu. Yeye mwenyewe amejaa imani, na anawashauri wanafunzi wake hivi: “Mwaminini Mungu!” (Marko 11:22).
No comments:
Post a Comment